Nenda kwa yaliyomo

Seyyid Muhammad Hassan Shirazi

Kutoka wikishia
Makala hii ni kuhusu Seyyid Muhammad Hassan Shirazi mashuhuri kwa jina la Mirza Bozorg. Ili kumtambua Mirzayi wa Pili angalia makala ya Muhammad Taqi Shirazi.
Sayyid Muhammad Hassan Hussein Shirazi

Sayyid Muhammad Hassan Husseini (1230-1312 Hijiria) mashuhuri kwa jina la Mirzayi Shirazi, Mirzayi Bozorg na Mirzayi Mujaddid ni mmoja wa Marajii Taqlid wa Kishia katika karne ya 14 Hijiria na ambaye alitoa fat’wa ya kuharamisha tumbaku.

Mirzayi Shirazi alichukua jukumu la Umarjaa baada ya kuaga dunia Sheikh Murtadha Ansari 1864 na alishikilia jukumu hilo kwa muda wa miaka 30 mpaka anaaga dunia. Alikuwa mwanafunzi maalumu na anayependwa na Sheikh Ansari. Miongoni mwa waliokuwa wanafunzi wake ni Sheikh Abdul-Karim Hairi, mwanzilishi wa Chuo Kikuu cha Kidini cha Qom (Hawza), Akhund Khorasani, Sheikh Fadhlullah Nuri, Mirza Naini na Muhammad Taqi Shirazi.

Mirzayi Shirazi ameandika vitabu mbalimbali katika taaluma ya fiq’h na usul. Mirzayi Shirazi anatambulika kuwa muasisi wa Chuo Kikuu cha Kidini na maktaba ya Samarra. Inaelezwa kuwa, alihajiri na kwenda Samarra kwa minajili ya kukurubisha Mashia na Masuni pamoja na akauchagua mji huo wa Iraq kuwa makazi yake. Miongoni mwa huduma za umma alizotoa ni kujenda Madrasa, Husseiniya, daraja, soko na mabafu ya umma.

Mwanazuoni huyu aliaga dunia huko Samarra akiwa na umri wa miaka 82 na kuzikwa katika Haram ya Imamu Ali bin Abi Twalib (a.s) katika mji wa Najaf, Iraq. Kumeandikwa athari mbalimbali kwa lugha ya Kiarabu na Kifarsi kumuhusu alimu na msomi huyu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Hadiyat al-Razi ilaa al-Imam al-Mujaddid al-Shirazi kilichoandikwa na Agha Bozorg Tehran na Hatyat al-Imam al-Mujaddid al-Shirazi kilichoandikwa na Muhammad Ali Gharawi Urdubadi ambacho kinamzungumzia Mirza Hassan Shirazi pamoja na wanafunzi wake.

Historia Yake

Seyyid Muhammad Hassan Husseini alizaliwa tarehe 15 Jumadi al-Awwal 1230 Hijiria katika mji wa Shiraz, Iran. [1] Baba yake, Mirza Mahmoud, alikuwa miongoni mwa wanachuoni wa kidini. [2] Mirza Muhammad Hassan alimpoteza baba yake alipokuwa mtoto na akalelewa chini ya usimamizi wa mjomba wake, Mirza Hussein Mousawi, anayejulikana kama Majd al-Ashraf. [3]

Wakati wa miaka yake ya kuishi Isfahan, Mirzayi Shirazi alifunga ndoa na binamu yake akiwa na umri wa kati ya miaka 17 na 20 na kupata binti na mtoto wa kiume aliyeitwa Ali. Mke wake wa kwanza alifariki mwaka 1303 Hijiria. Alioa tena na kuruzukiwa kwa mkewe huyo wa pili mtoto wa kiume aliyeitwa Muhammad na pia binti. [4]

Mwaka 1287 Hijiria alikwenda Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija. Katika safari hii, Sharif wa Makka alimtembelea Mirzayi Shirazi na kumpeleka nyumbani kwake. Wakati wa safari hii, Mirza Hassan alipanga kuishi mjini Madina, na wakati alipoona hilo haliwezekani, alikata shauri kwenda kuishi jirani na mji wa Mash’had. Lakini hatimaye alielekea Samarra na kuishi huko hadi mwisho wa maisha yake. [5]

Mirza Bozorg alifariki dunia tarehe 24 Shaban 1312 Hijiria (Februari 8, 1895) akiwa na umri wa miaka 82 na kuzikwa katika Haram ya Imam Ali (a.s) huko Najaf. [6] Baadhi ya watu walihusisha kifo chake na maradhi ya kifua kikuu [7] au mkamba (ugonjwa wa mapafu unaomfanya mtu apumue kwa shida). Wengine wanaona kuwa, kifo chake kilitokana na kupewa sumu na mamluki wa serikali ya Uingereza. [8]

Masomo

Mirza Hassan Shirazi akiwa na umri wa miaka 4 alienda maktaba (madrasa za wakati huo) na akafanikiwa katika kipindi cha miaka miwili kukamilisha usomaji Qur’an na vitabu vya kawaida vya fasihi ya lugha ya Kifarsi. Akiwa na umri wa miaka 6 alianza kujifunza sarf na nahau ya Kiarabu na alipofikisha umri wa miaka 8 alikuwa amekamilisha masomo ya msingi. [9] Baada ya hapo alifundishwa na Mirza Ibrahim Shirazi Aya, hadithi, khutba na utoaji mawaidha. [10] Akitekeleza agizo la mwalimu wake, Mirza Hassan Shirazi akiwa na umri wa miaka minane alipanda mimbari baada ya Sala ya Adhuhuri na Alasiri katika msikiti wa Wakil huko Shiraz na kuwasomea watu kwa hifadhi sehemu ya kitabu cha akhlaq cha Abwab al-Jinan. [11]

Baada ya hapo akaanza kusoma elimu ya Fiqhi na Usul na akiwa na miaka 12 alianza kuhudhuria masomo ya Sheikh Muhammaq Taqi Shirazi msomeshaji mkubwa kabisa wa kitabu cha sherh ya Lum’a katika mji wa Shiraz wakati huo. Alipofikisha umri wa miaka 18 alielekea katika mji wa Isfahan kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu baada ya kushauriwa kufanya hivyo na mwalimu wake. [12] Mirza Muhammad Hassan kabla ya kuhajiri na kuelekea Isfahan, kipindi fulani alijihusisha kuandika diwani badala ya baba yake. [13] Kadhalika alipokuwa na umri wa miaka 15 alikuwa akifundisha kitabu cha sherh ya Lum’a katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) katika mji wa Shiraz. [14]

Masomoni Isfahan

Mirzai Shirazi aliwasili Isfahan tarehe 17 Safar 1248 Hijiria [15] na kukaa katika Shule ya Sadr. [16] Katika kipindi hiki, alihudhuria masomo maalumu ya Muhammad Taqi Isfahani, mwandishi wa kitabu Hidaya al-Mustarshidin. Baada ya mwalimu wake kufariki dunia mwishoni mwa mwaka wa 1248 Hijiria, alimchagua Seyyed Hasan Bidabadi, aliyejulikana kama Mir Sayyid Hassan Modarres, kuwa mwalimu wake na kabla hajafikisha umri wa miaka 20, alipata idhini ya ijtihadi kutoka kwake. [10] Alikaa Isfahan kwa miaka 10 ambapo mbali na masomo ya Bidabadi alikuwa akishiriki pia katika masomo ya Muhammad Ibrahim Kalbasi. [18]

Masomoni Iraq

Akiwa na umri wa miaka 29, Mirza Hassan alifunga safari na kuelekea Iraq. Hiyo ilikuwa mwaka 1259 Hijiria na akahudhuria masomo ya wanazuoni kama vile Muhammad Hassan Najafi (Sahib Jawahir), Hassan Kashif al-Ghita' (mtoto wa Jafar Kashif Al-Ghita') [19] na Sheikh Ansari. [20]

Alikuwa mmoja wa wanafunzi maalum wa Sheikh Ansari na alikuwa na uhusiano maalumu na mwalimu wake. [21] Sheikh Ansari alimkabidhi masahihisho ya kitabu chake cha Faraid al-Asul. [22] Ni mashuhuri kuwa Sheikh Ansari mara kwa mara alisema, “Mimi nafundisha somo langu kwa watu watatu: Muhammad Hassan Shirazi", Mirza Habibullah Rashti na Hassan Najmabadi. [23] Ni mara chache sana alizungumza katika darsa za Sheikh Ansari na inajulikana kuwa alipozungumza, sauti yake ilikuwa tulivu kiasi kwamba Sheikh alilazimika kuegemea upande wake ili aweze kusikia na alikuwa akiwataka wanafunzi wengine wanyamaze na alikuwa akisema: “Bwana Mirza anazungumza.” [24]

Umarjaa

Baada ya kifo cha Sheikh Ansari mwaka 1281 Hijiria, Mirzayi Shirazi akachukua jukumu la Umarjaa. Kwa mujibu wa Agha Bozorg Tehrani, baada ya kifo cha Sheikh Ansari, wanafunzi wake mashuhuri waliafikiana kuhusiana na Umarjaa wa Mirza, isipokuwa kikundi cha wanazuoni wa Azerbaijan ambao walipendekeza jukumu la Umarjaa liende kwa Sayyid Hussein Kuhkamarai, mwanafunzi mwingine wa Sheikh Ansari. Baada ya kifo cha Kuhkamarai mwaka wa 1299 Hijria, Mirzayi Shirazi akawa Marjaa mmoja na pekee wa Mashia. [25]

Wanazuoni wa fiq’h na Usul wamelinganisha hadhi na daraja ya kielimu ya Mirza Shirazi na mwalimu wake Sheikh Ansari, na wengine wamemwona kuwa ni bora kuliko Sheikh. [26]

Kuasisi Hawza ya Samarra

Makala Kuu: Hawza ya Samarra

Mnamo mwaka 1291 Hijiria, Hawza ya Samarra iliundwa sambamba na kuwasili na kuanza kuishi huko Mirza Shirazi na kuwepo kwa wanafunzi wake katika mji huu. [27] Chuo hiki cha kidini kilikuwa na harakati kwa takribani miaka 20 na kwa kuaga dunia Mirza Shirazi mwaka 1312 Hijiria na kuhajiri wanazuoni na wasomi na kuelekea Karbala na Najaf, kikapoteza hali yake ya ustawi. Seyyid Hassan Sadr, Seyyid Mohsen Amin, Sharafuddin Amili, Muhammad Javad Balaghi, Sheikh Mohsen Sharare, Agha Bozorg Tehrani, Allama Amini na Muhammad Reza Mozafar walikuwa miongoni mwa shakhsia kubwa wa Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Samarra. [28] Mtindo na namna ya ufundishaji na uandishi wa Fiqhi na Usul wa Mirza Shirazi na wanafunzi wake unajulikana kama maktaba ya Samarra. [29] Seyyid Ridha Shirazi, ambaye ni katika wajukuu wa Mirzayi Shirazi anasema kuwa, sababu muhimu ya kukaa kwake Samarra ilikuwa ni kuwaleta Mashia na Masuni pamoja. [31]

Kuharamisha Tumbaku

Makala Kuu: Harakati ya tumbaku

Moja ya matukio yaliyotokea wakati wa uongozi wa Mirza Shirazi ni harakati ya kupiga marufuku tumbaku. Mirza Shirazi alitoa fat'wa maarufu ya kuharamisha tumbaku ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu. Fat'wa hiyo ilitolewa baada ya Mfalme Naser al-Din Shah Qajar wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni ya Regie ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku ya Iran katika miji minne ya Iran. Watu walianza maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi wanne wa Mirzayi Shirazi.

Sheikh Fadhlullah Nouri huko Tehran, Agha Najafi Isfahani huko Isfahan, Seyyid Ali Akbar Falasiri huko Shiraz na Mirza Jawad Mujtahid Tabrizi huko Tabriz walikuwa viongozi wa harakati hii. [32] Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fat'wa hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fat'wa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fat'wa hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni. Fat'wa yake iliwafanya watu wajitokeze kuipinga kiasi cha kumlazimisha Naser al-Din Shah Qajar, kufuta mkataba huo wa tumbaku. [33]

Wanafunzi Wake

Mirza Shirazi alikuwa na wanafunzi wengi. Agha Bozorg Tehrani amewataja wanafunzi wake wapatao 500 katika kitabu chake cha Hadiyat al-Razi ilaa al-Imam al-Mujaddid al-Shirazi. [34] Baadhi yao ni:

Hatua za Kisiasa na Kijamii

Mirzayi Shiirazi mbali na kuharamisha tumbaku, alichukua pia hatua nyingine za kisiasa na kijami:

  • Kutuma ujumbe wa telegrafu kwa Malkia wa Uingereza kwa ajili ya kuzuia mauaji ya umati ya Abdulraham (aliyetawala 1880-1901), dhidi ya Mashia wa Hazara nchini Afghanistan, ujumbe ambao aliutuma 1309 Hijiria. [43].
  • Kufanya juhudi za kuleta umoja baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni kupitia kuimarisha Chuo cha Kidini cha Kishia (Hawza) katika mji wa Masuni wa Samarra, Iraq, ambapo alifanya hima mtawalia na kuwasaidia kimali wanafunzi na Maulamaa wa Kisuni sambamba na kukabiliana na vikali na watu waliokuwa wakizusha mifarakano baina ya Mashia na Masuni. [44]
  • Kulea na kuwatuma Mubalighina maalumu kwa ajili ya maeneo nyeti na yaliyokuwa chini ya utawala na udhibiti kama India, Kashmir, Afghanistan, Caucasus na Iraq. [45]
  • Kujenga madrasa (vyuo) mbili katika mji wa Samarra. [46]
  • Kujenga daraja kwa ajili ya kuunganisha sehemu mbili za pwani ya Mto Tigris. [47]
  • Kujenga soko. [48]
  • Kujenga nyumba za wageni kwa ajili ya wafanyaziara na wasafiri.
  • Kujenga Husseiniya.
  • Kujenga mabafu ya umma kwa ajili ya wanawake na wanaume. [49]

Vitabu

Mirzayi Shirazi ana vitabu alivyoandika katika nyanja za Fiqhi na usul. Agha Bozorg Tehrani ameorodhesha vitabu vifuatavyo katika kitabu chake cha Tabaqat A'lam al-Shiah ambapo baadhi ya vitabu hivyo ni:

Baadhi ya fat'wa na mitazamo ya Mirza Shirazi imekuja katika baadhi ya vitabu au katika athari zenye kujitegemea. Athari na vitabu hiivyo ni:

  • Manhaj al-Nijat: ni kitabu cha sheria za Kiislamu ambazo zimechukuliwa kutoka katika fat'wa za Mirzayi Shirazi. Kitabu hiki kimeandikwa na Shekhe Ali Najafi Isfahani. Katika kitabu hiki ambacho kina muundo wa maswali na majibu na ambacho ni kwa lugha ya Kifarsi mwandishi ametosheka na kutaja majibu yaliyotolewa na Mirza Shirazi kwa hati yake mwenyewe au kwa saini yake. [53]
  • Majmaa al-Masail: Kitabu hiki kiliandikwa na Seyyid Asadullah Qazwini kwa amri ya Mirzayi Shirazi. [54]
  • Resaleh Sual va Pasukh: Katika kitabu hiki kuumekusanywa maswali 236 kutoka kwa Sheikh Fadhlullah Nuri sambamba na majibu ya Mirzayi Shirazi. [55]
  • Majmaa al-Masail: Kitabu hiki kiliandikwa na Muhammad Hassan bin Muhammad Ibrahim Jazi Isfahani kwa mujibu wa Fat'wa za Mirzayi Shirazi. Aidha Akhund Khurasani, Seyyid Muhammad Kadhim Yazdi, na Sayyid Isma'il al-Sadr wameandika maelezo ya ziada kuhusiana na kitabu hiki. [56]

Monografia

Kumeandika athari na vitabu mbalimbali kuhusiana na Mirzayi Shirazi:

  • Kitabu cha Hadiyat al-Razi ilaa al-Imam al-Mujaddid al-Shirazi kilichoandikwa na Agha Bozorg Tehran kinazungumzia maisha ya mirza Shirazii na wanafunzi wake. [57] Kwa mujibu wa Nasser al-Din Ansari ni kuwa, kitabu hiki ndio kamili zaidi kuhusiana na Mirzayi Shirazi. [58] Kitabu hiki kimetarjumiwa kwa lugha ya Kifarsi na Muhammad Dezful.
  • Hayat al-Imam al-Mujaddid al-Shirazi kimeandikwa na Muhammad Ali Gharawi Urdubadi (aliaga dunia 1380 Hijria) na kinazungumzia historia na maisha ya Mirza Shirazi na baadhi ya wanafunzi wake pamoja na watu walioishi naye zama moja. [59]
  • Saba'ik al-tibr fi-ma qila fi l-Imam al-Shirazi min al-shi'r, kimeandikwa na Muhammad Ali Gharawi Urdubadi. [60] Kwa mujibu wa Agha Bozorg Tehrani, athari hii ni juzuu ya pili ya kitabu cha Hayat al-Imam al-Mujaddid al-Shirazi. [61]
  • Mirza Shirazi Ihyagar Qudrat Fat'wa, mwandishi Seyyid Mahmoud Madani. [62]

Rejea

Vyanzo

  • Amīn, al-Sayyid Muḥsin al-. Aʿyān al-Shīʿa. Edited by Ḥasan Amīn. Beirut: Dār al-Taʿāruf li-l-Maṭbūʿāt, 1403AH.
  • Anṣārī, Nāṣir al-Dīn. Āthār wa taʿlīfāt Mīrzā-yi Shīrāzī. Ḥawza 50,51 (1371 Sh).
  • Āqā Buzurg al-Tihrānī, Muḥammad Muḥsin. Al-Dharīʿa ilā taṣānīf al-shīʿa. Beirut: Dār al-Aḍwāʾ, 1403 AH.
  • Āqā Buzurg Tihrānī, Muḥammad Ḥasan. Ṭabaqāt aʿlām al-Shīʿa wa huwa nuqabāʾ al-bashar fī qarn al-rābiʿ ʿashar. Mashhad: Dār al-Murtaḍā, 1404 AH.
  • Arbāb Qummī, Muḥammad. Al-Arbaʿīn al-Ḥusaynīyya. Tehran: Intishārāt-i Uswa, 1379 Sh.
  • Iṣfahānī Karbalāyī, Ḥasan. Tārīkh-i dukhānīyya: yā tārīkh-i waqāyiʿ-i taḥrīm-i tanbākū. Qom: Nashr-i al-Hādī, 1377 Sh.
  • Dārābī, Bihnām. Ḥawza-yi ʿilmīyya-yi taqrīb girā-yi Sāmarrā wa naqsh-i Mīrzā-yi Shīrāzī. Muṭāliʿat-i Taqrībī-yi Madhāhib-i Islāmī 31 (1392 Sh).
  • Ḥusaynī, Sayyid ʿAlī. Nigāhī ṭaṭbīq bih madrasa-yi Qum wa Najaf. Rahnāma-yi Pazhūhish 7 (1390 Sh).
  • Madanī Bajistānī, Sayyid Maḥmūd. Mirzā-yi Shīrāzī: iḥyāgar-i qudrat-i fatwā. In Gulshan-i Abrār, volume 1. Qom: Nashr-i Maʿrūf, 1385 Sh.
  • Muʾassisa-yi Farhangī Hunarī-yi Qadr-i Wilāyat, Dar Mashrūṭah chih gudhasht?. Tehran: Qadr-i Wilāyat, 1389 Sh.
  • Muṭallibī, Sayyid Abu l-Ḥasan. Nujūm-i ummat: Ḥaḍrat-i Āyat Allāh al-ʿuẓmā Ḥāj Mīrzā Sayyid Muḥammad Ḥasan Shīrāzī. Nūr-i ʿilm 33, 34 (1370-1371 Sh).
  • Shubayrī Zanjānī, Sayyid Mūsā. Jurʿaʾī az daryā. Qom: Muʾassisa-yi Kitābshināsī Shīʿa, 1389 Sh.
  • Ṣiḥḥatī Sardrūdī, Muḥammad. Guzīda sīmā-yi Sāmarrā sīnā-yi sih Mūsā. Tehran: Nashr-i Mashʿar, 1388 Sh.