Nyakati za Swala
Nyakati za Swala (Kiarabu: أوقات الصلاة) ni moja ya masharti ya kusihi Sala za kila siku. Kila Sala miongoni mwa Swala za kila siku inapaswa kuswaliwa katika wakati ulioainishwa kwani kinyume na hivyo wadhifa utakuwa haujatekelezwa. Kwa mujibu wa Fat'wa za mafakihi ni kwamba; wakati wa Sala ya Asubuhi, huanzia kuchomoza kwa alfajiri na hukomea wakati wa kuchomoza jua. Wakati wa Sala ya Adhuhuri, huanzia wakati jua linapopinduka wakati wa mchana mpaka kabla ya jua kuzama, kwa kiwango cha muda utoshao kuswali Sala ya Alasiri. Wakati wa Sala ya Alasiri, huanzia baada ya kupinduka jua baada tu ya kiasi cha kuweza kuswali Sala ya Adhuhuri na hukomea wakati wa kuzama jua kisheria. Wakati wa Sala ya Magharibi, huanza baada ya kuzama jua kisheria mpaka kabla ya nusu ya usiku na kabla ya kwisha muda unaotosha kusali Sala ya faradhi ya Isha. Wakati wa Sala ya Isha, huanza tangu kuzama jua kisheria pale unapopita muda utoshao kusali Sala ya Magharibi, na hukomea nusu ya usiku. Kuna hitilafu baina ya Maulamaa kuhusiana na suala la nyakati za Sala.
Lililo mashuhuri baina ya mafakihi kuhusiana na Swala ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na Isha ni kuweko wakati maalumu kwa ajili ya Swala hizi; kwa maana kwamba, wakati wa mwanzo ni ule ambao unatosha kuswali Swala ya Adhuhuri na Magharibi. Wakati huu unatambuliwa kuwa mahususi kwa ajili ya Swala hizi na haiwezekani kuswali katika wakati huu Swala za Alasiri na Isha. Kadhalika mwisho wa wakati ambao unatosha kuswali Swala za Alasiri na Ishaa unatambuliwa kama wakati maalumu kwa ajili ya Swala hizi mbili.
Ni mustahabu mtu kuswali Swala mwanzo wa wakati na jambo hili limetiliwa mkazo mno katika hadithi na riwaya mbalimbali. Kila Swala miongoni mwa Swala za kila siku ina wakati wake maalumu uliobainishwa ambapo kuswali ndani ya wakati huo ni bira na unatambuliwa kama «wakati wa fadhila».
Nafasi ya Kifikihi
Swala za kila siku (Swala Tano) zina masharti yake na miongoni mwayo ni kuchunga na kuzingatia wakati wa Swala; kwa maana kwamba, mukallaf anapaswa kuiswali kila Swala katika wakati maalumu ulioainishwa na endapo sharti la kila Swala kuswaliwa katika wakati wake halitazingatiwa wadhifa utakuwa haujatekelezwa. Kwa maana kwamba, wadhifa na wajibu huo utakuwa ungalipo. Njia ya kuthibitisha wakati wa Swala ni mtu mwenyewe kuwa na yakini juu ya kuingia wakati wa Swala au watu wawili waadilifu wampe khabari juu ya kuwa tayari wakati wa Sala. [1]
Nyakati za Sala za Kila Siku
Kwa mujibu wa fat'wa za mafakihi wakati wa Sala za kila siku ni:
- Sala ya Alfajiri: Ni baina ya kuchomoza kwa alfajiri na hukomea wakati wa kuchomoza jua. [2]
- Sala za Adhuhur na Alasiri: Mwanzo wa wakati wa Sala ya adhuhuri ni adhuhuri ya kisheria au zawali ya jua na hakuna hitilafu baina ya mafakihi kuhusiana na mas’ala haya. [3] Baadhi ya mafakihi wanaona kuwa, mwisho wa Sala ya Adhuhuri na Alasiri ni Magharibi; [4] lakini baadhi ya wengine kama Muhaqiq Hilli wanasema kuwa, mwisho wa wakati wake ni kuzama jua. [5] Kwa mujibu wa Sahib al-Jawahir na Boroujerdi ni kwamba, kauli ya kuzama jua ni mashuhuri au mashuhuri zaidi. [6] Baadhi ya Maulamaa kama Muhaqiq na Sayyid Yazdi ambao wanakubaliana na nadharia ya wakati maalumu na wa pamoja, [7] wanasema kuwa, lahadha za awali za kupinduka/zawali kwa jua ni wakati maalumu wa Sala ya adhuhuri kwa kiwango cha kutosha kusali Sala ya adhuhuri na vilevile lahadha na wakati wa mwisho kabisa kwa kiwango cha kutosha kusali Sala ya adhuhuri ni muda maalumu kwa ajili ya Sala ya alasiri na muda uliopo baina ya Sala hizi mbili ni wakati wa pamoja (wa kushirikiana) baina ya Sala ya adhuhuri na alasiri. [8]
- Sala za Magharibi na Isha: Baadhi ya mafakihi wanatambua wakati wa Sala ya Magharibi na Isha kuwa ni kuanzia kuzama jua mpaka nusu ya usiku; [9] lakini baadhi wanaona kuwa, mwanzo wa wakati ni Magharibi. [10] Kwa mujibu wa nadharia ya mafakihi ambao wanakubali kuweko wakati maalumu na wa kushirikiana akiwemo akiwemo Muhaqqiq Hilli na Sayyid Yazdi ni kwamba, muda wa kutosha kusali Sala ya Magharibi ndio wakati maalumu wa Sala hiyo na lahadha na wakati wa mwisho kabla ya kuingia nusu ya usiku kwa kiwango cha kutosha kusali Sala ya Isha huo ni muda maalumu wa Sala ya Isha na alasiri na muda uliopo baina ya Sala hizi mbili ni wakati wa pamoja (wa kushirikiana) baina ya Sala ya Magharibi na Isha. [11]
Baadhi ya mafakihi wanasema: Watu ambao kutokana na kulala, kusahau au wanawake ambao wako katika siku zao za hedhi na hawakuweza kusali Sala ya Magharibi na Isha mpaka ukawadia wakati wa nusu ya usiku, wanaweza kusali mpaka kabla ya kuchomoza jua kwa nia ya adaa; [12] lakini baadhi ya wengine kama Sayyid Hussein Boroujerdi, Imamu Khomeini na Ahmad Khansari hawakubaliani na nadharia hii na badala yake wanasema, katika hali kama hii, ni kufanya ihtiyat ambayo ni kusali Sala kwa nia ya lililoko katika dhima. [13]
Wakati Maalumu na wa Kushirikiana
Wakati maalumu maana yake ni kwamba, katika Sala za Adhuhuri na Alasiri na Magharibi na Isha, wakati wa kwanza (mwanzo) wa kiwango na muda wa kutosha kusali Sala ya adhuhuri au magharibi ni makhsusi na maalumu kwa ajili ya Sala hizi na haiwezekani kuzisali Sala hizi katika wakati wa Sala za Alasiri na Isha na vilevile wakati wa mwisho ambao ni wa kiwango cha kusali Sala ya alasiri na Magharibi ni wakati maalumu kwa ajili ya Sala hizi. [14] Baadhi ya maulamaa kama Muhaqqiq Hilli na Sayyid Yazdi wanaamini nadharia ya wakati makhsusi na maalumu. [15] Ayatullah Khui ameinasibisha nadharia hii na mafakihi mashuhuri. [16]
Lakini mkabala na hao, kuna mafakihi wengine akiwemo Sayyid Abul-Qassim Khui hawakubaliani na nadharia hii na wanaamini mtazamo wa wakati wa pamoja (wa kushirikiana) na wamaeinasibisha nadharia na mtazamo huu na Sheikh Saduq na Maulamaa wengine. [17] Kwa mujibu wa nadharia hii, wakati wa Sala kuanzia mwanzo mpaka mwisho ni wa kushirikiana baina ya Sala; lakini kutokana na kuwa ni lazima kuchunga utaratibu, inapasa kusali Sala ya Adhuhuri kisha Alasiri na Magharibi kisha Isha. [18]
Wakati Wenye Fadhila
Mafakihi wanasema kuwa, ni mustahabu mtu kusali Sala mwanzo wa wakati na kumeusiwa na kutiliwa mkazo mno kuhusiana na hili. Na kadiri mtu anaposali karibu na wakati ni bora, isipokuwa kama kuchelewesha kwake kuna jambo bora kwa mfano anasubiri ili asali Sala ya jamaa. [20] Kwa mujibu wa fat’wa za mafakihi wakati wa fadhila yaani wakati bora ambao ni vyema Sala zikasaliwa katika wakati huo ni:
- Sala ya Afajiri: Kuanzia alfajiri mpaka kupatikana wekundu upande wa mashariki mwa mbingu ambayo kwa Kiarabu inajulikana kama “al-Humrat al-Mashraqiyyah”. [21]
- Sala ya Adhuhuri: Kuanzia zawali na kupinduka jua mpaka wakati kivuli kitakapokuwa na ukubwa wa mtu mwenyewe. [22]
- Sala ya Alasiri: Kuanzia wakati na muda wa kumalizika wakati wa fadhila wa adhuhuri mpaka kivuli cha alama kitakapokuwa na urefu mara mbili. [23]
- Sala ya Magharibi: Kuanzia Magharibi wakati wa kuondoka wekundu upande wa magharibi wa mbingu ambao Kiarabu unajulikana kama “al-Humrat al-Maghribiyyah”. [24]
- Sala ya Isha: Kuanzia wakati wa kumalizika wakati wea fadhila mpaka theluthi moja ya usiku. [25]
Baadhi ya Hukumu za Wakati wa Sala
Baadhi ya fat’wa za mafakihi kuhusiana na wakati wa Sala ni kama ifuatavyo:
- Kama rakaa moja ya Sala itakuwa ndani ya wakati, basi ni sawa na kwamba, Sala nzima imesaliwa ndani ya wakati. [26]
- Kama mukallaf atakuwa na kazi ya wajibu, kwa mfano mwenye deni amekuja, basi anapaswa kutekeleza kwanza kazi hiyo ya wajibu na kisha asali. Hata hivyo kama ataacha kufanya hivyo na akaswali kwa makusudi mwanzo wa wakati licha ya kuwa atakuwa amefanya dhambi, lakini Sala yake itakuwa sahihi. [27]
- Ni jambo jema na la kupendeza mtu kuwaamsha watu wengine kwa ajili ya Sala na baadhi ya wakati ni jambo la lazima kwani, kuamrisha mema ni kitendo cha wajibu; lakini haijuzu kumuamsha mgonjwa au mtu ambaye anataabika kwa hilo. [28]