Nenda kwa yaliyomo

Muujiza wa kisayansi wa Qur’an

Kutoka wikishia

Muujiza wa Kisayansi wa Qur’an (Kiarabu: الإعجاز العلمي للقرآن) ni nadharia inayotaka kuthibitisha kuwa Qur'an Tukufu ni Muujiza kwa kulinganisha (na kuyapima) yale yaliyomo ndani ya Aya za Qur’an Tukufu na matokeo ya Sayansi za Majaribio (Experimental Sciences). Maana ya Sayansi za Majaribio: Sayansi za Majaribio kwa ibara nyingine ni Elimu za majaribio, maana yake ni: Sayansi ya hakika na yakini inayothibitishwa na ambayo hupatikana kupitia uchunguzi wa kihisia na wa kina zaidi, pia kupitia uzoefu na majaribio ya mara kwa mara, yote hiyo itakuwa sehemu ya sayansi ya majaribio.

Sayansi za Majaribio au Elimu za Majaribio zimegawanywa katika matawi kadhaa ambayo ni kama ifuatavyo: Fizikia, Kemia, Biolojia, Jiolojia. Hiyo ni mifano hai ya Sayansi za Majaribio. Kwa mujibu wa nadharia hii (Yaani: Muujiza wa Kisayansi wa Qur’an), Qur’an Tukufu imezungumzia kuhusu (uhakika na) ukweli katika nyanja ya sayansi, hasa sayansi za majaribio, ambazo hazikuwa zimegunduliwa katika zama za kuteremshwa kwa Qur’an Tukufu, na kwa kuwa kutoa maelezo na kufafanua juu ya mambo hayo na uhakika (ukweli) huo wa kisayansi lilikuwa ni suala ambalo liko nje ya uwezo wa mwanadamu kwa wakati huo, basi kwa hakika Qur'an hii inapaswa kuchukuliwa kuwa ni Muujiza wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) na itambulike bayana kuwa ni Kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.).

Kurejelea (na kuashiria) kwa Qur'an Tukufu kuhusu masuala kama vile: Mzunguko wa ardhi (na matokeo yanayopatikana kutokana na harakati ya mwendo au mzunguko wa Ardhi / Dunia). Kuibuka kwa uhai kutokana na maji (kama inavyosemwa kuwa maji ni uhai). Nguvu ya mvutano wa ardhi: (Ufafanuzi: Nguvu hii ya uvutano ipo ndani na juu ya ardhi ya dunia, na inajulikana kama (gravity, kwa maana: Nguvu ya uvutano, nayo ni nguvu inayovuta vitu vyote vyenye uzito, nguvu hiyo ya uvutano ndio inayohusika pia kuweka miguu yako katika ardhi na ukaweza kutembea juu ya ardhi, bila nguvu hii ya uvutano ya ardhi mwanadamu hawezi kutembea juu ya ardhi, angelishuhudiwa akipepesuka angani, lakini kutokana na uwepo wa nguvu hii inayovuta vitu vyenye vyenye uzito kuja chini, ndio mwanadamu anaweza kuweka miguu yake na kutembea, na ukitaka kuihisi zaidi nguvu hii, jaribu kurusha kitu chochote juu angani, ni lazima kitu hicho kirudi chini ardhini kwa sababu ya nguvu hii ya uvutano wa ardhi, hata embe mtini litadondoka kwa kuja chini ya ardhi na kamwe haliwezi kwenda angani, sababu ni ni nguvu hii ya uvutano wa ardhi. Pia nguvu hii ya uvutano wa ardhi ndio inayohusika kuiweka Dunia pamoja na sayari zote katika mfumo wetu wa Jua katika njia zake (obiti) pindi zinapolizunguka Jua). Na Jozi ya Mimea na Wanyama: ((Ufafanuzi: Kama ilivyo kwa Mwanadamu, kuna jozi ya kiume na kike, kiasi kwamba wanaweza kuzaliana kutokana na kuumbwa kwao wakiwa ni jozi, kwa mfano: Chembeuzi (au kromosomu) X kutoka kwa Mwanamke ikikutana na Chembeuzi X kutoka kwa Mwanaume atapatikana mtoto wa Kike. Na Chembeuzi (au kromosomu) X kutoka kwa Mwanamke ikikutana na Chembeuzi Y kutoka kwa Mwanaume, atazaliwa mtoto wa kiume.Namna hiyo Wanadamu (au Wanyama) huzaliana kwa sababu wameumbwa wakiwa ni Jozi. Na vivo hivyo ndivyo ilivyo kwa Mimea, nayo iko katika mfumo wa jozi)). Yote hiyo (na mingine mingi) ni sehemu ya mifano ya miujiza ya kisayansi ya Qur'an Tukufu (na imetajwa na kuelezwa kwa uzuri kabisa ndani ya Qur’an, tena katika zama ambazo hakuna mwanadamu aliyekuwa na uwezo wa kutoa ufafanuzi juu ya uhakika huo kama ulivyoelezwa ndani ya Qur’an Tukufu, na hilo linaifanya Qur’an Tukufu kuwa Muujiza mkubwa wa Kisayansi).

Muhammad bin Ahmad Iskandarani, Rashid Reza na Tantawi walikuwa Waislamu wa kwanza kabisa kuandika katika uwanja huu (kuhusiana na Muujiza wa Sayansi ya Qur’an). Waanzilishi wa suala hili (la Muujiza wa Sayansi ya Qur’an) nchini Iran walikuwa ni hawa wafuatao: Mohammad Taqi Shariati, Sayyid Mahmoud Taleqani na Mahdi Bazargan.

Baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu, wanapinga Tafsiri ya Kisayansi ya Qur’an na wanaamini kwamba nadharia za kisayansi daima zinaweza kubadilika na kurekebishika na kupotoshwa, na iwapo nadharia hizo zitapotoshwa (au kubadilika au kurekebishika), basi Qur’an nayo pia itatiliwa shaka. Lakini wale wanaoafiki (na kukubaliana na Tafsiri ya Kisayansi ya Qur’an), wanaona kwamba utwabikishaji wa Aya za Qur'an kwa matokeo ya sayansi za majaribio ni kama njia tu ya kuthibitisha ukweli, uhakika na usahihi wa Qur'an Tukufu (na si vinginevyo).

Maana ya Nadharia hii

Kwa mujibu wa nadharia ya muujiza wa kisayansi wa Qur’an, Kitabu hiki (yaani: Qur’an Tukufu) kimezungumzia mambo ya hakika kabisa katika nyanja ya sayansi, hasa sayansi za majaribio, ambayo hayakugunduliwa katika zama za kuteremshwa Qur’an. Aidha, tofauti na vitabu vingi vya kisayansi ambavyo nadharia zake hubatilika baada ya muda, Qur'an ina maudhui za kisayansi ambazo hazijawahi kukiukwa (wala kubatilika). Kwa vile ufafanuzi na ubainishaji wa mambo hayo ya kisayansi wakati huo ulikuwa nje ya uwezo wa Mwanadamu, Qur'an inapaswa kuchukuliwa kuwa ni muujiza wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) na ni Kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu [1].

Kutambulisha nadharia

Tafsiri ya kisayansi ya Qur’an inayo historia ndefu katika ulimwengu wa Kiislamu. Imesemekana kwamba kwa mara ya kwanza, Ibn Sina (aliyezaliwa mwaka 370 A.H na kufariki mwaka 428 A.H) alijaribu kutoa Tafsiri ya Kisayansi ya baadhi ya Aya za Qur’an Tukufu, kwa kulinganisha (au kwa kutwabikisha na) baadhi ya mapendekezo ya Kifalsafa na Aya za Qur'an. Fakhrur Razi (aliyezaliwa mwaka 544 .AH na kufariki mwaka 606 A.H) pia alilinganisha (kwa maana: Alitwabikisha) maneno ya Qur'an Sab’a' Sama’wat (Mbingu saba) kwa Sayari Saba, kama ilivyothibitishwa katika Elimu ya nyota ya Ugiriki ya Kale [2]. Hata hivyo, uthibitisho wa Muujiza wa Kisayansi wa Qur'an ulianzia karne iliyopita, ambapo tafsiri ya kisayansi ya Qur'an ilipokea uangalifu mkubwa (kwa kuzingatiwa zaidi) kutokana na uvumbuzi mpya (uliopatikana) katika sayansi za majaribio [3].

Katika kipindi hiki, wafasiri na wanazuoni wengi wa Shia na Sunni walijaribu kuthibitisha Muujiza wa Kisayansi wa Qur'an [4]. Vitabu vingi viliandikwa katika uwanja wa Tafsiri ya Kisayansi ya Qur'an na Miujiza yake [5]. Mohammad bin Ahmed Iskandarani, Rashid Reza na Tantawi ni miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kuchapisha kazi zao katika uwanja huu [6]. Waanzilishi wa suala hili (yaani: Muujiza wa Kisayansi wa Qur'an) nchini Iran walikuwa ni: Mohammad Taqi Shariati, Sayyid Mahmoud Taleqani na Mahdi Bazargan [7].

Mifano ya Muujiza wa Kisayansi wa Qur'an

Wafasiri (wa Qur'an Tukufu), wamezihusisha maudhui nyingi za Kisayansi na Qur'an, na kuliona hilo kuwa ni Muujiza wa Kisayansi. Miongoni mwa maudhui hizo ni:

  • Harakati ya mzunguko wa mkao na mpito wa ardhi (dunia):
  • Kutokea kwa uhai kutoka kwenye maji.
  • Nguvu ya uvutano ya dunia.
  • Uwepo wa jozi kwa mimea na wanyama.
  • Na kuzunguka kwa tufe katika njia (obiti) fulani. [8]

Baadhi ya aya ambazo zimetumika kuthibitisha Muujiza wa kisayansi wa Qur'an ni hizi zifuatazo:

  • ((وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ کلَّ شَیءٍ حَی ; Tukajaalia kutokana na maji kila kitu kilicho hai)) (Surat al-Anbiyaa: Aya ya 30).

Wengine wameichukulia Aya hii kuwa moja ya Miujiza ya Kisayansi ya Qur’an, wakinukuu matokeo mapya ya Sayansi za Majaribio yaliyojengeka katika msingi wa uhai unatokana na maji. [9]

  • ((وَمِن كلِّ الثَّمَرَ اتِ جَعَلَ فِیهَا زَوْجَینِ اثْنَینِ ; Na katika matunda akafanya jozi (viwili viwili) ndani yake)) (Surat Ar-Raad: Aya ya 3).

Kwa mujibu wa Tafsiri ya Sampuli (au: Tafsir al-Amthal iliyoandikwa na Ayatollah Makarim Shirazi), suala la kuwepo kwa uwili au jozi katika baadhi ya mimea, lilijulikana katika siku za nyuma; lakini katikati ya karne ya 18 Miladia, Wanasayansi za Majaribio waligundua kwamba hii ni kanuni ya jumla na inatumika kwa mimea yote.[10]. (Kwa hiyo kitu ambacho wanasayansi hawakukijua – hali ya kuwa tayari Qur’an Tukufu tayari ilishakiongelea muda mrefu – ni suala hilo – la uwepo wa jozi kwa mimea – kuwa kwamba hiyo ni kanuni ya jumla kwa mimea yote, na wala sio kwa baadhi ya mimea).

  • ((ثُمَّ اسْتَوَیٰ إِلَی السَّمَاءِ وَهِی دُخَانٌ ; Kisha akaielekea mbingu)), na ilikuwa Moshi (Bukhari) (Surat Fussilat: Aya ya 11).

Baadhi ya wafasiri wa Qur’an Tukufu wanasema kwamba Aya hii inaeleza nadharia ya Mlipuko Mkubwa (Nadharia Big Bang), ambao ndio asili ya ulimwengu. Nadharia hii ya Big Bang au Mlipuko Mkubwa) ni nadharia ya kisayansi inayoelezea chanzo cha ulimwengu huu. Nukta ya msingi katika hili ni hii kwamba: Nadharia hii imethibitishwa na wanasayansi wengi baada ya kuashiriwa na kuzungumziwa kwa miaka mingi ndani ya Qur’an Tukufu. Na Aya hii Tukufu tuliyoitaja sehemu hii - hapo juu- inaashiria katika uhakika huo wa Big Bang - yaani - Mlipuko Mkubwa au Mlipuko wa Asilia, au Mlipuko Mkuu, ambao ndio chanzo au asili ya ulimwengu huu)). Wafasiri hao wanaamini kwamba bukhari (moshi) unaotajwa katika Aya hiyo, ni wingi uleule wa moshi ambao kulingana na kauli ya wanasayansi uliundwa kutokana na mlipuko mkubwa (Big Bang) [11].

  • ((وَمَن یُرِ‌دْ أَن یضِلَّهُ یجْعَلْ صَدْرَ‌هُ ضَیقًا حَرَ‌جًا کأَنَّمَا یصَّعَّدُ فِی السَّمَاءِ ; Na yule ambaye (Mwenyezi Mungu) anataka apotee, hufanya kifua chake kina dhiki kimebana.Kama kwamba anapanda mbinguni)) (Surat al-An’am: Aya ya 125).

Imesemwa kwamba leo hii imethibitishwa kwamba mtu anapoinuka juu ya uso wa dunia (akatoka juu ya uso wa dunia na kwenda -karibu au- nje kabisa ya uso wa dunia, ni vigumu zaidi kwake kupumua; kwa sababu huzidi kuteseka zaidi kwa kuikosa hewa ya oksijeni na kupoteza fahamu, na hii ni moja ya Miujiza ya Kisayansi ya Qur’an [12].

Wapinzani wa nadharia ya miujiza ya Kisayansi

Wapinzani wa tafsiri ya kisayansi ya Qur'ani Tukufu wanasema kuwa Qur'an ni Kitabu cha mwongozo na hakipaswi kutarajiwa kueleza nadharia za kisayansi na sheria za fizikia na kemia. Wanaamini kwamba nadharia za kisayansi daima zinaweza kubadilika na kupotoshwa au kubatilika, na iwapo nadharia hizo zitabatilika (au zitapotoshwa), basi Qur'an nayo itatiliwa shaka. Kwa upande mwingine, watetezi (wanaoafikiana na nadharia hii) wamesema kwamba ulinganisho wa matokeo ya kisayansi na Aya za Qur'an haupingani na kuwa kwake Kitabu cha Mwongozo; kinyume chake, kuonyesha mambo ya kisayansi yaliyomo ndani ya Qur'an Tukufu, kunathibitisha usahihi wake na husaidia zaidi Muongozo (kwa Mwanadamu) [13].

Pia kuna tofauti ya maoni kati ya wale wanaounga mkono Tafsiri ya kisayansi ya Qur'an: Baadhi wanaamini kwamba sayansi (au elimu) zote zipo katika Qur'an na wamejaribu kutoa maarifa kama vile tiba, hisabati, jiometri, aljebra na unajimu kutoka ndani yake [14]. Tantawi, Muhammad Abdul Naeem Al-Jamal, Muhammad bin Ahmed Iskandarani na Sayyid Ahmad Khan wa India, wanatoka katika kundi hili (linaloamini na kuthibitisha kwa dalili za wazi na bayana kuwa sayansi zote zipo ndani ya Qur’an Tukufu) [15].

Kundi jingine miongoni mwao linaamini kuwa kundi la kwanza limekwenda mbali zaidi (kwa maana: Limevuka mipaka) katika uga wa Tafsiri ya Kisayansi na limeweka nadharia za Sayansi za Majaribio juu ya Qur'an bila ya kuzingatia wala kujali njia (manhaji) za kisayansi za kutafsiri Qur’an. Kwa mujibu wao, Qur'an haikutaja sayansi zote; hata hivyo, katika baadhi ya Aya za Qur'an, ukweli na uhakika umeelezwa kiasi kwamba wanasayansi wa Sayansi ya Majaribio wamegundua baada ya karne nyingi kupita kuhusu ukweli na uhakika huo. Aya hizi zinaonyesha miujiza ya kisayansi ya Qur’an. [16] Sayyid Qutb, Rashid Reza, Mohammad Taqi Shariati, Sayyid Mahmoud Taleqa’ni na Mahdi Bazargan ni (wanafikra na wanachuoni) wa kundi hili [17] linaloamini kuwa Aya hizi zinaonyesha miujiza ya kisayansi ya Qur’an.

Allama Tabatabai, katika utangulizi wa Tafsiri ya al-Mizan, alichukulia tafsiri ya kisayansi ya Qur'an kuwa ni uwekaji wa nadharia za sayansi ya majaribio juu ya Qur'an (kwa maana: Ni kuibebesha Qur’an nadharia za kisayansi na kujaribu kuihukumu Qur’an kupitia nadharia hizo badala Qur’an iwe ndio yenye kuzihukumu nadharia hizo) na wala halitambui hilo kuwa ni aina fulani ya kutwabikisha nadharia za sayansi za majaribio kwa Qur’an. [18].

Bibliografia

Vitabu vingi, makala na machapisho ya kisayansi yamechapishwa katika uwanja wa Tafsiri ya Kisayansi ya Qur'ani [19]. Kitabu kiitwacho: “Kashfu al-As’rari al-Nura’niyyah al-Qur’aniyyah”, yaani: “Kufichua Siri Tukufu za Qur’ani”, Al-Barahinul Bayyina’ti Fi Bayan Haqaiqul Hayawana’ti yaani: “Uthibitisho wa wazi Katika kueleza Uhalisia Wa Wanyama”, na “Tibyan al-As’rari al-Rabba’niyyah Fi al-Naba’ta’ti wal Maadin wal khawa’si al-hayawa’niyyah” yaani: “Kueleza Siri za Ki_Mwenyezi Mungu katika Mimea, Madini na Tabia za Wanyama”, vilivyoandikwa na Muhammad bin Ahmed Iskandarani, na Al-Manar, kilichoandikwa na Rashid Reza, na Jawahir Al-Qur'an, kilichoandikwa na Tantawi, ni katika vya mwanzo vya Tafsiri za Kisayansi za Qur'an[20]. Tafsir Novin (Kwa maana: Tafsiri Mpya) iliyoandikwa na Mohammad Taqi Shariati pia inajulikana kama mojawapo ya vitabu mashuhuri kabisa katika uwanja huu (wa Tafsiri ya Sayansi ya Qur’an), ambao alijaribu (kupitia Tafsiri hii) kuonyesha mifano ya (wazi kabisa na inayoeleweka ya) Miujiza ya Qur'an Tukufu pasina kwenda mbali sana. [21] Mohammad Hadi Maarifat pia amezungumzia suala hili (sayansi ya Qur’an) katika juzuu ya sita ya kitabu chake al-Tamhid [22]. Baadhi ya vitabu vingine muhimu zaidi katika uwanja huu ni hivi vifuatavyo:

  • Pezhoheshi dar I’jaz Qur’an (Utafiti juu ya miujiza ya kisayansi ya Quran): Mohammad Ali Rezaei Esfahani.
  • Al-I’jaz Al-Tarbawi Lil-Qur'an: Mustafa Rajab.
  • Mausu’at al-I’jaz al-ilmiy fil Qur’an al-Karim was-Sunnat al-Mutahharat (Encyclopedia (Kamusi elezo) ya Muujiza wa Kisayansi ndani ya Qur’an Tukufu na Sunna Tukufu): Yusuf Al-Haj Ahmed.
  • Al-Mausu’at al-ilmiyyah fi Iijaz al-Qur’an al-Karim was-Sunnat al-Nabawiyyah ((Encyclopedia -kamusi elezo- ya kisayansi kuhusu miujiza ya Qur’an Tukufu na Sunnah za Mtume-s.a.w.w-)): Amjad Fat’hi na Hani bin Mar’a al-Qulainiy.
  • Mausu’at al-dhahbiyyah Fi Iijaz al-Qur’an Al-Karim was- Sunnat al-Nabawiyyah ((Encyclopedia -kamusi elezo- ya Al-Zahabiyyah juu ya maajabu ya Qur'ani Tukufu na Sunnah za Mtume-s.a.w.w-)) : Ahmad Mustafa Mutawalliy.
  • Minal I’jaz al-ilmi fil Qur'an al-Karim ((Miongoni mwa miujiza ya kisayansi katika Qur’an Tukufu)) : Hasan Abul-Ainain [23].

Sura au Mlango wa: "Muujiza wa Kisayansi katika Qur'an na Sunnah" Kitabu hiki, ni moja ya machapisho ya kisayansi ambapo, kimefanya utafiti katika masuala zaidi ya thelathini ya miujiza ya kisayansi ya Qur'an, katika nyanja mbalimbali kama vile nyanja za tiba, astronomia, jiolojia, biolojia, hisabati, uchumi, elimu na sosholojia [24].

Vyanzo

  • Burūmand, Muḥammad Ḥusayn. 1381 Sh. "Barrasī wa naqd-i tawjīh-i ʿilmī-yi Qurʾān." Maqālāt wa Barrasīhā 71:75-94.
  • Maʿārif, Majīd. 1385 Sh. "Jāygāh-i iʿjāz-i ʿilmī-yi Qurʾān dar tafsīr-i nuwīn." Saḥifa-yi Mubīn 37:82-92.
  • Makārim- Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1374 Sh.
  • Maʿrifat, Muḥammad Hādī. Al-Tamhīd fī ʿulūm al-Qurʾān. Qom: Daftar-i Nashr-i Islāmī, 1412 AH.
  • Pūrḥasan, Qāsim. 1384 Sh. "Naqd wa barrasī-yi rawish-i tafsīr-i ʿilmī-yi qurʾān." Payām-i Jāwīdān 6:87-106.
  • Riḍāyī Iṣfahānī, Muḥammad ʿAlī. 1389 Sh. "Chistī wa chālishhā-yi iʿjāz-i ʿilmī-yi Qurʾān." Qurʾān wa ʿIlm 7:11-44.
  • Riḍāyī Iṣfahānī, Muḥammad ʿAlī. Pazhūhishī dar iʿjāz-i ʿilmī-yi Qurʾān. Fifth edition. Rasht: Kitāb-i Mubīn, 1388 Sh.
  • Riḍāyī, Ḥasan Riḍā. 1389 Sh. "Manbaʿ shināsī-yi iʿjāz-i ʿilmī-yi Qurʾān." Qurʾān wa ʿIlm 7:197-220.
  • Ṭabāṭabāyī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Fifth edition. Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.