Mu’jam Rijal al-Hadith (kitabu)
Mu’jam Rijal al-Hadith wa Tafsir Tabaqat al-Ruwat (Kiarabu: مُعْجَمُ رجالِ الْحَدیث وَ تَفْصیلُ طَبَقاتِ الرُّواة) ni kitabu cha Sayyid Abul-Qassim al-Khui kinachozungumzia elm al-rijal – sayansi ya hadithi- (elimu inayochambua hali na wasifu wa wapokezi wa hadithi). Kitabu hiki kina zaidi ya wapokezi 15,000 wa hadithi za upande wa Mashia ambao wamepangwa kwa mujibu wa alfabeti na kumetolewa maoni na mitazamo kuhusiana na kuwa na itibari au kutokuwa na itibari nakili zao za hadithi.
Katika utanguzi wa kitabu hiki, kumejadiliwa kwa mapana na marefu maudhui sita kuhusiana na elm al-rijal; maudhui kama udharura wa elimu ya rijal, vigezo vya uamuinifu vya mpokezi wa hadithi na itibari ya hadithi za kutub al-Arbaa vya Kishia. Sehemu nne za kitabu hiki ni: Majina, lakabu, kuniya na wanawake. Kitabu cha Mu’jam Rijal al-Hadith kina juzuu 24.
Kukusanya majina ya wapokezi wote wa vitabu vya Rijal mahali pamoja na kuzingatia suala la "kupotoshwa" kwa majina ya wapokezi na kuyasahihisha zinahesabiwa kuwa miongoni mwa sifa za kitabu hiki.
Mwandishi
- Makala Kuu: Seyyid Abulqasim Khui
Seyyed Abul-Qassim Musawi Khui (1278-1371) ni mmoja wa Marajii Taqlid wa Shia alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Mirza Naini na Muhaqqiq Isfahani. [1] Aliondokea kuwa Marajaa Taqlidi wa juu kabisa nchini Iraq baada ya kifo cha Sayyid Muhsin Tabatabai Hakim. [2]
Seyyed Abul-Qasim Khui ameandika vitabu kuhusu fiqhi, misingi ya fiqhi (Usulul Fiq’h), rijaal, teolojia na sayansi ya Qur'ani. Kazi zake zimekusanywa katika mkusanyo wa juzuu hamsini unaoitwa "Ensaiklopidia ya al-Imam al-Khui". [3]
Nafasi ya Kitabu Hiki
Mu'jam Rijal al-Hadith kinatambuliwa kuwa kitabu jumuishi na chenye thamani zaidi miongoni mwa vitabu vya rijaal vya Kishia na inaelezwa kwamba, kitabu hiki kina sifa chanya ambazo hazipatikani katika vitabu vingine vya Rijal. Kuwachunguza wasimuliaji kutoka pembe tofauti na mkabala wa kukosoa mitazamo ya wakati uliopita, hasa vitabu vya mwanzo vya Rijali na kurekebisha maoni hayo ni mojawapo ya sifa hizo. [4]
Pia, kitabu hiki kimezingatiwa kuwa mojawapo ya vitabu bora zaidi vya rijal kwa sababu kimewachunguza wapokezi wa hadithi katika pembe mbalimbali na kutoa habari muhimu kuwahusu ambazo haziwezi kupatikana popote au hazionekani kwa urahisi. [5]
Msukumo na Namna Kilivyoandikwa
Kwa mujibu wa mwandishi wa kitabu katika utangulizi wake, elm rijal kwa muda mrefu ilikuwa ikizingatiwa na wanachuoni na mafaqihi; lakini kwa wakati wa sasa inapuuzwa; katika hali ambayo, ijtihad na kupatikana kwa hukumu za Sheria (kunyambua hukumu) kunategemea hilo. Kwa hivyo, aliamua kuandika kitabu cha kina na kamili katika uwanja huu ambacho kina faida na sifa zote za elimu hii [6].
Khui alikuwa na wasaidizi katika utungaji wa ensaiklopidia ya Rijal al-Hadith ambao walimsaidia katika kuhariri, kunakili, kusahihisha, kulinganisha na kurejelea kitabu. [7] Kundi hili linajumuisha: Mohammad Mozafari, Haydar Ali Hashimian, Yahya Araki, Seyed Morteza Nakhjavani, Seyed Abdul-Aziz TabatabaiYazdi, Sayyid Javad Golpaygani, Mohammad Kadhim Khansari, Fakhruddin Zanjani, Muhammad Tabrizi, Ghulamridha Rahmani, na Sayyid Murtadha Hakami. [8]
Maudhui na Muundo wa Kitabu
Kitabu kina utangulizi wa kina na sehemu nne. Katika utangulizi, masuala sita ya utangulizi katika elm rijal yamezungumziwa na kujadiliwa. Katika sehemu kuu nne, majina ya wapokezi yametajwa na kuchunguzwa itibari na uaminifu wao:
Utangulizi
Maudhui sita zilizozungumziwa katika utangulizi wa kitabu hiki ni:
- Udharura wa elimu ya rijal, kukataa maoni ya wale wanaokanusha haja ya elimu ya rijal na maoni ya wale wanaozingatia vitabu vya Kutub al-Arbaa kuwa ni vya yakini au vinapelekea kupatikana yakini; [9]
- Vigezo vya kuainisha uaminifu au uzuri wa hali ya mpokezi; [10]
- Itibari ya uaminifu wa namna fulani; [11]
- Kutokuwa na itibari suala la uaminifu jumla, kama kuwa miongoni mwa as’hab Ij’maa (kundi la wapokezi wa hadithi ambalo kwa mujibu wa wanazuoni wa erlimu ya rijal lina daraja ya juu ya uaminifu), kuwa miongoni mwa masheke wanaotoa ijaza na idhini ya kunukuu hadithi, kuwa na uwakala kutoka kwa Imamu Ali (as), kusuhubiana na Imamu Ali (as); [12]
- Kuchunguza hadithi za Kutub al-Ar’baa (vitabu vinne vya hadithi vyenye itibari vya Waislamu wa Kishia) na kupinga hoja za kuthibitisha kwamba, hadithi zote zilizomo katika vitabu hivyo ni sahihi; [13]
- Kutambulisha vyanzo muhimu kabisa vya wapokezi wa hadithi wa Kishia na kutilia shaka asili ya kitabu cha Rijal ibn Ghadhairi. [14]
Mgawanyo wa Kitabu
Sehemu nne za kitabu hiki ni mjumuiko wa: Majina, lakabu, kuniya na wanawake. Katika sehemu hizi, kumetajwa majina 15,676 na kufanyiwa uchunguzi ingawa baadhi yanashirikiana; yaani yanaashiria mtu mmoja. Katika kila sehemu tatu za kwanza, kunajadiliwa watu ambao majina, kuniya au lakabu zao zimekuja katika vitabu vya rijal au katika mapokezi ya wapokezi. Sehemu ya nne inahusiana na wanawake ambao wametajwa katika vitabu vya rijaal au mapokezi ya hadithi. [15]
Sifa Maalumu za Kitabu Hiki
Kitabu cha Mu’jam rijal al-Hadith kina sifa maalumu ikilinganishwa na vitabu vingine vya taalumna na fani hii. Baadhi ya sifa hizo maalumu ni:
- Majina yote ya wapokezi wa hadithi za Kutub al-Arbaa yametajwa; hata wale ambao majina yao hayajatajwa katika vitabu vya kuchambua majina na wasifu wa wapokezi wa hadithi (Elm rijal).
- Majina ya wapokezi wote wa hadithi ambao ni maarufu na wasiokuwa maarufu yameyajwa katika kitabu hiki.
- Katika kitabu hiki, inawezekana kwa urahisui kabisa kutambua tabaka la wapokezi wa hadithi; kwani katika kumtambulisha mpokezi wa hadithi, kumetajwa na kubainishwa majina ya watu wote waliopokea kutoka kwake au yeye amepokea kutoka kwao.
- Ufafanuzi wa hali ya mpokezi wa hadithi imeelezwa kwa sura kamili kabisa.
- Mbali na mtazamo wa wataalamu wengine wa elimu ya rijaal, mwandishi wa kitabu hiki amebainisha vigezo vyake maalumu na mtazamo wake kuhusiana na mpokezi wa hadithi. Kwa maneno mengine ni kuwa, amechambua na kujadili sambamba na kuchunguza wasifu wa mpokeaji juu ya uadilifu na kuaminika kwake (Jarh wataadil). [16]
Machapisho
Kitabu cha Mu’jam rijal al-Hadith awali kilichapishwa mwaka 1403 Hijria kikiwa na juzuu 23. [17] Mwaka 1413 Hijria kikachapishwa tena kikiwa na masahihisho mapya na kikiwa katika juzuu 24. [18]
Miongoni mwa mabadiliko yaliyofanyika katika chapa hiyo ni kuongezea baadhi ya nukta katika sehemu mbalimbali za kitabu na kadhalika. [19]
Athari Zinazo Husiana
Baadhi ya athari zinazohusiana na Mu’jam rijal al-Hadith ni:
- Dalil Mu’jam rijal al-Hadith, mwandishi Muhammad Said Tarihi;
- Al-Muin ala mu’jam rijal al-hadith, mwandishi: Sayyid Muhammad Jawad Husseini Baghdadi;
- Al-Mufid min Mu’jam rijal al-hadith, mwandishi Muhammad Jawahiri. Katika kitabu hiki kumebainishwa mitazamo ya karibuni kabisa ya Ayatullah Khui kuhusiana na kila mpokezi wa hadithi kwa mukhtasari. [20]
- Dar omadi bar elm rejal, tarjuma ya utangulzi wa kitabu cha Mu’jam rijal al-Hadith, mwandishi Abdul-Hadi Fiq’hzadeh.