Nenda kwa yaliyomo

Mausu'ah Tabaqat Al-Fuqaha (Kitabu)

Kutoka wikishia

Mausu'ah Tabaqat Al-Fuqaha ni kitabu kilichoandikwa kwa lugha ya Kiarabu ambacho kina orodha ya watu 5,976 miongoni mwa mafakihi wa madhehebu za Kiislamu hadi mwishoni mwa karne ya 14 Hijria. Kitabu hiki kilikuwa moja ya vitabu vilivyoteuliwa kushinda katika tamasha la vitabu la mwaka katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kitabu hiki kimeandikwa na Ayatullah Ja'far Sobhani mmoja wa Marajii Taqlidi wa Kishia kwa ushirikiano na jopo la waandishi.

Kubainisha hali, harakati za kielimu na vilevile matukio ya kihistoria ya zama za kila fakihi, kutofautisha baina ya majina na lakabu zenye kushirikiana baina ya mafakihi, kubainisha kwa lugha nyepesi na kujiepusha na kuandika mambo mengi, ni miongoni mwa sifa maalumu zinazotajwa kuhusiana na kitabu hiki. Kitabu hiki kinajumuisha utangulizi katika juzuu mbili na maudhui asili ya kitabu hiki, nayo inajumuisha juzuu 14 ambapo Juzuu ya Kwanza inaeleza mafakihi na wanazuoni wa elimu ya fikihi walioishi pamoja na Bwana Mtume(s.a.w.w) na tabiina. Baada ya hapo katika Juzuu ya Pili mpaka ya kumi na nne, kinawatambulisha mafakihi walioishi katika karne ya pili hadi ya kumi na nne Hijria. Kwa msingi huo katika kila juzuu wametambulishwa mafakihi wa karne moja.

Umuhimu wa kitabu hiki

Kitabu cha Mausu'ah Tabaqat Al-Fuqaha mwaka 1378 kiliteuliwa kuwa kitabu bora katika maudhui ya dini katika duru ya 17 ya uteuzi wa kitabu cha mwaka katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. [1] Kitabu hiki kimeandikwa na Sheikh Ja’far Sobhani mmoja wa Marajii na mwanachuoni mahiri wa Kishia akishirikiana na baadhi ya waandishi. [2] Ayatullah Ja’far Sobhani anasema, kinyume na athari na vitabu vingine vilivyoandikwa kuwatambulisha mafakihi na wanazuoni wa Kiislamu ambavyo vimejihusisha na maisha ya wanazuoni wa kundi na mrengo fulani tu, [3] kitabu hiki kinajumuisha maisha na taarifa za mafakihi na wanazuoni wa madhehebu zote za Kiislamu, [4] na kwa upande wa zama pia kinazungumzia mafakihi kuanzia katika zama za mwanzo za Uislamu mpaka karne ya 14 Hijria. Kitabu hiki kina juzuu 14 na kila juzuu imewazungumzia mafakihi na wanazuoni wa karne moja. [5]

Waandishi

Kitabu cha Mausu'ah Tabaqat Al-Fuqaha kimeandikwa na jopo la waandshi wa jopo la kielimu la Taasisi ya Imam Swadiq (as) katika mji wa Qom, Iran [6] ambao ni: Sayyid Muhammad Hussein Modarresi Yazdi, Sayyid Muhammad Kadhim Modarresi Yazdi, Sayyid Muhammad Kadhim Hakimzadeh, Haidar Muhammad Baghdadi, Ahmad Fadhili Biyar Jamandi, Yahya Sadeghi, Qassim Shirzadeh na Muhammad Shuwaili.[7] Utangulizi mrefu wa kitabu hiki umeandikwa na Sheikh Ja’far Sobhani kama ambavyo mwanazuoni huyu mkubwa alikuwa na jukumu la kusimamia uandishi wa kitabu hiki. [8]

Sifa maalumu

Baadhi ya sifa maalumu za kitabu hiki ni:

  1. Wanazuoni na mafakihi wa madhehebu zote za Kiislamu hata mafakihi wa madhehebu ambazo baada ya muda zilisambaratika na kutoweka, wameorodheshwa katika kitabu hiki.
  2. Kumebainisha na kutofautishwa baina ya majina na lakabu za pamoja za mafakihi ambapo hili limebainishwa na kuashiriwa kwa kutaja hoja za baadhi ya makosa ya waandishi wa vitabu vya historia ya watu.
  3. Kitabu hiki kinabainisha hali ya mafakihi, harakati zao za kielimu na vilevile matukio ya kihistoria ya zama za kila fakihi.
  4. Utaratibu na mpangilio wa mafakihi katika kila juzuu umefanyika kwa mujibu wa herufi za alfabeti na mwishoni mwa kila juzuu mbali na kuweko faharasa ya alphabeti kuna orodha ya majina ya mafakihi sambamba na miaka ya kuaga kwao dunia.
  5. Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha nyepesi huku waandishi wakijiepusha na kuandika mambo mengi na ya ziada. [9]

Maudhui

Kitabu hiki kinajumuisha utanguzli ambao uko katika juzuu mbili [10] na juzuu 14 [11] ambazo ndani yake kunabainishwa hali na historia ya mafakihi 5,976 wa Kiislamu mpaka katika karne ya 14 Hijria [12]. Utangulizi wa kitabu hiki umeandikwa na Ayatullah Ja’far Sobhani [13] na mambo yaliyozungumziwa ndani yake ni:

  • Juzuu ya Kwanza ina utangulizi ambao una faslu 6:
  1. Faslu ya Kwanza: Vyanzo vyenye itibari vya utungaji sheria ambapo ndani yake kumejadiliwa nafasi ya Qur’an, Sunna, Ijmaa (makubaliano ya wanazuoni), akili, ada (kitu kilichozoeleka) na sira.
  2. Faslu ya Pili: Vyanzo vya utungaji sheria kwa Waislamu wa Kisuni.
  3. Faslu ya Tatu: Taathira ya zama na sehemu katika kunyambua hukumu za kisheria (hatua zipitiwazo kufikia natija ya hukumu ya kisheria ya kitu).
  4. Faslu ya Nne: Turathi za kihadithi kwa Shia na Suni.
  5. Faslu ya Tano: Turathi za Kifikihi kwa Shia na Suni.
  6. Faslu ya Sita: Historia ya Usulul-Fiqh kwa Shia na Suni. [14]
  • Juzuu ya Pili mbali na kuwa na utangulizi inajumuisha masomo ya fikihi kwa mujibu wa Shia na Suni. [15] Juzuu ya kwanza ina maudhui asili ya kitabu kuhusiana na wanazuoni wa fikihi walioishi katika zama za masahaba na zama za tabiina (watu waliowaona, kuwadiri au kuishi na masahaba). [16] Kuanzia Juzuu ya Pili mpaka ya 14 pia katika kila juzuu wanatambulishwa wanazuoni wa fikihi wa karne moja; yaani wametambulishwa maulamaa wa fikihi walioishi katika karne ya pili hadi ya 14. [17]

Kuchapishwa na kusambazwa

Kitabu hiki kimechapishwa na Taasisi ya Imam Swadiq(a.s) katika mji wa Qom, Iran mwaka 1418 Hijria. [18] Kadhalika kitabu hiki kilichapishwa na kusambazwa mwaka 1420 Hijria nchini Lebanon na Taasisi ya Dar al-Baydha. [19]