Kumsaidia Yatima
Kumsaidia Yatima ni kumpa himaya na msaada wa kifedha na kimaanawi. Jambo hili limekokotezwa na kutiliwa mkazo mno katika Uislamu. Qur’ani tukufu inamthamini yatima na imewataka watu kuchunga haki za mayatima na kuwatendea wema. Katika Qur’ani kumeusiwa na kuagizwa kuwakirimu mayatima, kuwatendea wema, kuwalisha na kutoa kwa ajili ya mayatima.
Katika hadithi pia suala la kuwafanyia upendo na kuwajali mayatima limezingatiwa na limepewa umuhimu wa aina yake. Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w): Kila ambaye atamhurumia yatima na kumuweka katika huba na huruma yake madhali angali mhitaji, basi pepo itakuwa wajibu kwake. Kuwasaidia na kuwajali mayatima ni jambo ambalo lilikuwa na umuhimu sana katika sira ya Ahlul-Bayt (a.s) Kwa mfano inanukuliwa kwamba Imamu Ali bin Abi Twalib (a.s), alikuwa akizipa umuhimu mno haja na mahitaji ya mayatima na alikuwa akijiita baba wa mayatima.
Katika kipindi chote cha historia, katika ulimwengu wa Kiislamu suala la kuwajali mayatima limekuwa likizingatiwa na kupewa umuhimu mno na kuliasisiwa vituo vingi vilivyojulikana kwa jina la Dar al-Aitam ambavyo vina jukumu la kuwatunza na kuwalea mayatima. Hata hii leo kuna vituo vingi katika maeneo mbalimbali ambavyo vinawatunza na kuwalea mayatima. Mwaka 1392 Hijria Shamsia nchini Iran kulipasishwa katika Bunge (Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu) sheria ya kuwaunga mkono watoto na mabarobaro wasio na walezi na wenye walezi wabaya.
Udharura wa Kumsaidia Yatima Katika Dini
Wasomi na wanazuoni wa dini wamesema kuwa, Uislamu umeusia na kuagiza juu ya kuwaheshimu na kuwapa hifadhi mayatima,[1] na umeitambua jamii kwamba, inabeba dhima na jukumu mkabala wa mayatima.[2] Kadhalika waumini wametakiwa wajihusishe na mambo ya mayatima ili madhara na hasara yasiwapate mayatima.[3] Hussein Ansariyan, mwanazuoni na khatibu wa Kishia anasema: Kusaidia yatima ni katika ibada kubwa kabisa.[4]
Yatima ni nani?
- Makala kuu: Yatima
Katika istilahi na msamiati wa kifikihi yatima ni mtoto ambaye ameondokewa baba yake (baba yake amefariki) kabla ya kufikisha umri wa kubaleghe.[5] Katika Qur'ani na hadithi neno yatima limetumiwa pia kwa maana isiyo ya kisheria na kilugha ambayo ni mtoto ambaye ambaye ameondokewa na mmoja wa wazazi wake wawili (baba au mama).[6]
Amri ya Qur’ani ya Kumthamini Yatima
Qur’ani Tukufu imemthamini yatima na imewataka watu kuchunga haki za mayatima na kuwatendea wema.[7] Katika Qur’ani kumeusiwa na kuagizwa kuwakirimu mayatima (Aya ya 17 ya Surat al-Fajr), kuwalisha mayatima (Aya ya 8 ya Surat al-Insan na Aya ya 15 ya Surat Balad), kuwatendea wema na hisani mayatima[8] (Aya ya 83 ya Surat al-Baqarah na Aya ya 36 ya Surat al-Nisaa) na kutoa kwa ajili ya mayatima[9] (Aya ya 215 Surat al-Baqarah) [10]
Katika Aya ya 1 na 2 za Surat Maaun inaelezwa kuwa, watu ambao wanakadhibisha siku ya malipo (Kiyama) ndio wale wanaomsukuma yatima.[11] Katika Aya ya 9 ya Surat al-Dhuha, Mtume na Waislamu wote kwa ujumla wanahutubiwa na kutakiwa wasimuonee na kumdhalilisha yatima.[12] Kwa mujibu wa Aya ya 10 ya Surat al-Nisaa ni kwamba: Wanao kula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote watapewa adhabu kali kabisa[13] na wataingia Motoni.[14]
Imeelezwa kuwa, haki ya yatima ni kuchukua mali yake na kuianzishia biashara ili iwe na faida zaidi na wakati atakapobaleghe apatiwe.[15] Kwa mujibu wa Aya ya 17 ya Surat al-Fajr ni kwamba, sababu ya kudhalilika baadhi ya watu ni kwamba, hawakuwa wakiwakirimu mayatima na hawakuwa wakichunga na kutekeleza haki zao.[16] Tunastafidi na kunufaika kupitia Aya hii ya kwamba, kila ambaye atamkirimu yatima kisha akachunga na kutekeleza haki yake basi Mwenyezi Mungu atamkirimu na kumtukuza.[17] Ayatullah Ja’afar Subhani, mmoja wa wanazuoni na Marajii watajika katika ulimwengu wa Kishia anasema kuwa: Qur’ani imefanya hima ili kuuvuta mtazamo wa jamii kuelekea upande wa mayatima; kiasi kwamba, inatoa amri na maagizo kwamba, wakati wa kugawanya mali na urithi kama kutakuweko na yatima miongoni mwa watu wa karibu na maiti naye apewe fungu hata kama si miongoni mwa warithi.[18]
Sira ya Ahlul-Bayt (a.s)
Katika hadithi pia suala la kuwafanyia upendo na kuwajali mayatima limezingatiwa na limepewa umuhimu wa aina yake[19] na kuwakirimu na kuwajali mayatima ni jambo ambalo limetambuliwa kuwa sehemu ya sira ya Ahlul-Bayt (a.s).[20] Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w): «Kila ambaye atamhurumia yatima na kumuweka katika huba na huruma yake madhali angali mhitaji, basi pepo itakuwa wajibu kwake».[21] Kadhalika imenukuliwa kwamba, Imamu Ali bin Abi Twalib (a.s), alikuwa akizipa umuhimu mno haja na mahitaji ya mayatima na alikuwa akijiita baba wa mayatima.[22] Katika wasia wake, Imamu Ali (a.s) aliliweka suala la kuwajali Mayatima pamoja na suala la kujali na kuipa umuhimu Sala na Qur’ani: «Kuna wakati mayatima wameshiba na kuna wakati wana njaa, msiruhusu wapate shida na nyinyi mpo».[23]
Kituo cha Mayatima
Kutiliwa mkazo kwa namna tofauti tofauti kuhusiana na mayatima katika maandiko ya dini, kumewafanya Waislamu katika kipindi chote cha historia kuwa na mtazamo maalumu na uzingatiaji wa aina yake kuhusiana na mayatima. Katika jamii za Kiislamu suala la kuwalea na kuwatunza mayatima linapewa umuhimu mno na kumeasisiwa vituo vingi vilivyojulikana kwa jina la Dar al-Aitam ambavyo vina jukumu la kuwatunza, kuwasomesha na kuwalea mayatima. Jambo hili linashuhudiwa mno katika ulimwengu wa Kiislamu. Dar al-Aitam au nyumba za mayatima (vituo vya mayatima) viliasisiwa mwishoni mwa karne ya 13 Hijria na kisha katika karne ya 14 Hijria harakati hii iilishika kasi na kuchukua wigo mpana kwa haraka sana.[24]
Nchini Iran katika zama za utawala wa ukoo wa Safavi, kulijengwa vituo vya mayatima katika baadhi ya miji na miongoni mwavyo ni katika mji wa Mash’had kituo ambacho kiko kando ya Haram ya Imamu Ridha (a.s) na ambacho kilikuwa kikifanya shughuli zake hadi mwishoni mwa zama za utawala wa ukoo wa Qajar.[25]
Katika zama za utawala wa Qajar na Pahlavi wa pili pia kulitokea mageuzi makubwa katika uwanja wa kuanzisha vituo vya mayatima.[26]
Kituo cha Dar al-Aitam cha Mahdiyah katika mji wa Hamedan, Iran kilichoasisiwa 1351 Hijria Shamsia[27], Nyumba ya Vijana ya Muhammad Ali Mudhafari katika mji wa Tehran iliyoanzishwa 1326 Hijria Shamsia,[28] na Kituo cha Malezi cha Mozhdehi katika mji wa Rasht kilichoanzishwa 1328 Hijria Shamsia[29] vinahesabiwa kuwa vituo vikongwe na vya kale zaidi vya mayatima nchini Iran.
Baada ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 na kwa mujibu wa muswada uliopasishwa na serikali 1358 Hijria Shamsia, vituo vyote ambavyo kwa namna moja au nyingine vilikuwa na jukumu la kutunza, kulea na kuhudumia watoto wasio na walezi na mayatima, vilihamishiwa na kuwekwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya na Ustawi. Kuna baadhi ya vituo vya mayatima pia ambavyo vimejengwa na wahisani na wafadhili wa masuala ya kheri.[30]
Mipango ya Himaya Kwa Ajili ya Kuwakirimu Mayatima Iran
Ili kuheshimu, kuthamini na kutatua matatizo ya mayatima katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sheria ya kuwalinda watoto mayatima na mabarobaro wasio na walezi na wenye walezi wabaya iliidhinishwa na Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) mwaka 1392 Hijria Shamsia na baada ya kuidhinishwa na Baraza la Kulinda Katiba, sheria hiyo ilipatiwa serikali ili iitekeleze.[31]
Kamati ya Misaada ya Imamu Khomeini kuanzia mwaka 1378 Hijria Shamsia ilianzisha mpango uliojulikana kwa jina la “Kuwakirimu Mayatima” ambao lengo lake ni kuwasaidia na kuwapa himaya watoto mayatima na kudhamini na kukidhi mahitaji yao.[32] Katika mpango huu, wafadhili na wahisani hujitokeza na kukubali kuchukua jukumu la kumsaidia kifedha yatima au mayatima kadhaa katika kipindi cha mwaka mzima na kumtatulia au kuwatatulia matatizo yao ya kimaada na kimaanawi. Inaelezwa kuwa, kuna wahisani takriban milioni moja katika maeneo mbalimbali ya Iran ambao wamechukua jukumu la kuwa wasimamizi na watoaji huduma kwa watoto mayatima katika kivuli cha Kamati ya Misaada ya Imamu Khomeini.[33]
Rejea
- ↑ Modarresi, Tafsir Hedayat, juz. 18, uk. 353, 1377 S.
- ↑ Subhani, Manshur Javid, Qom: juz. 13, uk. 153.
- ↑ Ansariyan, Zibayiha-e Akhlaq, Qom: uk. 325.
- ↑ Ansariyan, Zibaha-e Akhlaq, Qom: uk. 320.
- ↑ Sheikh Tusi, al-Mabsut, juz. 2, uk. 281, 1387 H; Rawandi, Fiqh al-Qur'an, juz. 1, uk. 245, 1405 H.
- ↑ Jasas, Ahkam al-Qur'an, juz. 2, uk. 12, 1405 H; Mishkini, Mustalahat al-Fiqh, uk. 576.
- ↑ Subhani, Manshur Javid, Qom: juz. 13, uk. 153; Ansariyan, Zibaha-e Akhlaq, Qom: uk. 320; Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, juz. 3, uk. 379, 1371 S.
- ↑ Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, juz. 1, uk. 328, 1371 S
- ↑ Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, juz. 2, uk. 104, 1371 S
- ↑ Ansariyan, Zibaha-e Akhlaq, Qom: uk. 320
- ↑ Tabatabai, al-Mizan, juz. 20, uk. 368, 1390 H.
- ↑ Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, juz. 27, uk. 106, 1371 S
- ↑ Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, juz. 3, uk. 280, 1371 S; Subhani, Manshur Javid, Qom: juz. 13, uk. 161.
- ↑ Qiraati, Tafsir Nur, juz. 2, uk. 27, 1388 H; Muhsini, Naqsh-e Islam dar Asr Hadhir, uk. 89, 1387 S.
- ↑ Muhsini, Naqsh-e Islam dar Asr Hadhir, uk. 89, 1387 S.
- ↑ Ansariyan, Zibaha-e Akhlaq, Qom: uk. 320
- ↑ Abu al-Futuh Razi, Raudh al-Jinan wa Ruh al-Jinan, juz. 20, uk. 271, 1408 H; Ansariyan, Zibaha-e Akhalq, Qom: uk. 320.
- ↑ Subhani, Manshur Javid, Qom: juz. 13, uk. 160.
- ↑ Makarim Shiarzi, Tafsir Nemuneh, juz. 26, uk. 463, 1371 S; Makarim Shirazi, Anvar-e Hedayat, uk. 388, 1390 S.
- ↑ Ansariyan, Zibaha-e Akhlaq, Qom: uk. 321.
- ↑ Allamah Majlisi, Bihar al-Anwar, juz. 74, uk. 58, 1403 H; Modarresi, Tafsir Hadayat, juz. 18, uk. 354, 1377 S.
- ↑ Makarim Shirazi, Payam-e Emam Amir al-Mu'minin, juz. 10, uk. 272, 1386 S.
- ↑ Makarim Shiarzi, Tafsir Nemuneh, juz. 27, uk. 113, 1374 S; Makarim Shirazi, Az tu Sual Mikunan, uk. 131.
- ↑ Ma'sumi, «Dar al-Aitam»
- ↑ Ma'sumi, «Dar al-Aitam»
- ↑ Ghafarirad, «Mururi bar Sabeqe Dar al-Aitamha-e Ghair Daulati dar Dure-e Qajar» uk. 67.
- ↑ «Muarrefi va Tarikhche», Tovuti, darolaytam.ir.
- ↑ «Tarikhche», Tovuti, mozaffarikids.com
- ↑ «Muarrefi Pazuheshgah Mojdehi», Tovuti, itam-mojhdehi.ir.
- ↑ Ma'sumi, «Dar al-Aitam».
- ↑ «Qanun-e Hemayat az Kudakan va Nujavanan bi Sarparast va bad Sarparast», Tovuti, rc.majlis.ir.
- ↑ «Tarh-e Ikram», Tovuti, ekram.emdad.ir.
- ↑ «Tarh-e Ikram», Tovuti, ekram.emdad.ir.
Vyanzo
- Abu al-Futuh Razi, Hussein bin Ali. Raudh al-Jinan wa Ruh al-Jinan fi Tafsir al-Qur'an. Mashhad: Bunyad Pajuheshha-e Islami, 1408 H.
- Ansariyan, Hussein. Zibaha-e Akhlaq. Qom: Dar al-Irfan, Bita.
- Jasas, Ahmad bin Ali. Ahkam al-Qur'an. Tahqiq: Muhammad Sadiq Qumhawi. Beirut: Dar Ihya al-Turath al-Arabi, 1405 H.
- Hur 'Amili, Muhammad bin Hassan. Wasail al-Shiah, Qom: Muasasah Alulbait 'Alaihimusalam li Ihya al-Turath, Bita.
- Rawandi, Qutub ad-Din. Fiqh al-Qur'an fi Sharh Ayat al-Ahkam. Tas-hih: Sayid Ahmad Husseini. Qom: kitab khane Ayatullah Mar'ashi Najafi, juz. 2, 1405 H.
- Subhani, Ja'far. Manshur Javid. Qom: Muasasah Imam Sadiq (a.s), Bita.
- Sheikh Tusi, Muhammad bin Hassan. al-Mabsut fi Fiqh al-Imamiah. Tahqiq: Sayid Muhammad Taqi Kashfi. Tehran: Al-maktaba al-Murtadhawiyah li Ihya al-Athar al-Ja'fariyah, juz. 3, 1387 H.
- Tabatabai, Sayid Muhammad Hussein. al-Mizan fi Tafsir al-Qur'an. Beirut: Muasasah al-A'lami li al-Matbu'at, 1390 H.
- Site ekram.e,dad.ir. «Tarh-e Ikram». Samane Akram Bazdid: 8 Urdibehesht 1403 S.
- Allamah Majlisi, Baqir bin Muhammad Taqi. Bihar al-Anwar. Tahqiq: Sayid Ibrahim Miyanji, Muhammad Baqir Bahbudi. Beirut: dar Ihya al-Turath al-Arabi, 1403 H.
- Site rc.majlis.ir. «Qanun-e Hemayat az Kudakan va Nujavanan bi Sarparast va bad Sarparast». Markaz pajuheshha-e Majlis Shuraye Islami, Bazdid: 8 Urdibehesht 1403 S.
- Ghafarirad, Firuzeh. «Mururi bar Sabeqe Dar al-Aitamha-e Ghair Daulati dar Dure-e Qajar». Tarikh Revai, juz. 20 & 21, Mwaka wa 6, Bahar va tabestan 1400 S.
- Qiraati, Muhsin. Tafsir-e Nur. Tehran: Markaz Farhanggi Dars-hayi az Qur'an, 1388 S.
- Muhsini, Sheikh Muhammad Asif. Naqsh-e Islam dar Asr-e Hadhir. Kanal: Bina, 1387 S.
- Modarresi, Sayid Muhammad Taqi. Tafsir-e Hedayat. Mashhad: Bunyad Pajuheshha-e Islami, 1377 S.
- Mishkini, Ali. Mustalahat al-Fiqh, Bita.
- Misbah Yazdi, Muhammad Taqi. Payam-e Maula az Bastar-e Shahadat. Tadvin va nagaresh: Muhammad Mahdi Naderi. Qom: Intisharat Muasasah Amuzeshi va Pajuheshi Emam Khomeini.
- Site itam-mojhdehi.ir. «Muarrefi Pajuheshgah Mujdahi». Muasasah jami'iyat hemayt Aitam, Bazdid 18 Urdibehesht, 1403 S.
- Site darolaytam.ir. «Muarrefi va Tarikhche». 18 Urdibehesht, 1403 S.
- Makarim Shirazi, Nasir. Anvar-e Hedayat. Majmue-e Mabahis-e Akhlaqi. Qom: Imam Ali bin Abi Talib (a.s), 1390 S.
- Makarim Shirazi, Nasir. Payam-e Emam Amir al-Mu'minin. Tehran: Dar al-Kutub al-Islamiah, 1386 S.
- Makarim Shirazi, Nasir. Tafsir Nemuneh. Tehran: Dar al-Kutub al-Islamiah, juz. 32, 1374 S.
- Makarim Shirazi, Nasir. Az Tu Sual Mikunan. Tahiye va Tanzim: Abu al-Qasim Aliyan Nejadi. Qom: Imam Ali bin Abi Talib Alaihisalam, 1387 S.