Hukumu ya Kifiqhi Juu ya Uharamu wa Kuunda na Kutumia Silaha za Nyuklia
Hukumu ya Kifiqhi Juu ya Uharamu wa Kuunda na Kutumia Silaha za Nyuklia: Hukumu hii ya kifiqhi ni hukumu inayohusiana na mtazamo wa kisheria wa Sayyid Ali Khamenei, ambaye ni Marja' al-Taqlid (mujitahid) wa Kishia, ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hukumu hii ilitolewa katika muktadha wa kujibu tuhuma juu ya azma ya Iran ya kuunda silaha za nyuklia. Sayyid Ali Khamenei anazitafsiri silaha za maangamizi ya halaiki kamani tishio kwa ulimwengu naye anaharamisha uundaji pamoja na matumizi yake.
Baadhi ya watafiti wamehusisha uharamu wa hukumu hii na Aya za Qur'ani pamoja na Riwaya zinazokataza mashambulizi dhidi ya raia wa kawaida (wasio wapiganaji). Kulingana na kauli ya Abolqasim Alidoust, ni kwamba; chimbuko la hukumu hii ya uharamu wa matumizi ya silaha zenye uwezo wa maangamizi makubwa miongoni mwa mafaqihi wa Kishia lina historia ya kipindi cha takriban milenia moja.
Fatwa hii ilizua mijadala na aina mbali mbali za uchambuzi kwenye taasisi za kimataifa za tafakuri na vituo vya uchanganuzi wa kisiasa, na inadaiwa kuwa ilirikodiwa kama ni waraka rasmi katika Umoja wa Mataifa. Vitabu kiitwacho Fiqhi Hastei (Fikih ya Nyuklia), ambacho ni kazi ya waandishi kadhaa, pamoja na kitabu Fatwai Hastei Az Manzare Huquuqe Bainal Milal (Fatwa ya Nyuklia kwa Mtazamo wa Haki za Kimataifa) cha Jaber Sivanizad, ndiyo miongoni mwa vitabu muhimu vilivyofanya uchunguzi wa kina kuhusiana na hoja za kisheria pamoja na nyanja mbalimbali za uharamu wa kuunda na kutumia silaha za nyuklia.
Umuhimu wa Fatwa Hii
Fatwa ya kuharamisha uzalishaji na matumizi ya silaha za nyuklia ilitolewa na Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ambaye ni Marjaa wa Waislamu wa Kishia na Kiongozi Muadhamu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. [1] Fatwa hii ilitolewa ili kubainisha msimamo wa Sharia kuhusu madai ya njama za Iran juu ya kutengeneza silaha hizo za maangamizi. Tamko hili la kidini lilitangazwa rasmi katika Mkutano wa Kimataifa wa Upokonyaji wa Silaha za Nyuklia Pamoja na Umarufuku wa Kueneza Silaha Hizo Angamizi, uliofanyika nchini Iran mwaka 1389 Hijria Shamsia. [2]
Kiongozi wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Ali Akbar Salehi, akijibu tuhuma za Kimagharibi zinazoitumu Irani kwa kuwa na harakati zenye mwelekea azma ya kutengeneza Silaha za Nyuklia, alithibitisha akisema kwamba; Lenye umuhimu mkubwa zaidi kwa Iran, ni kuendelea kulinda heshima ya fatwa hii pamoja na kushikamana na amri hii ya Mwenye Ezi Mungu iliyotolewa kupitia Marjaa wake (Kiongozi wake mkuu wa Kidini). [3] Viongozi wa Marekani kama vile Hillary Clinton (aliyekuwa waziri mkuu wa Marekani) na Rais Barack Obama waliirejelea fatwa hii katika kauli zao za hadhara, wakikiri uzito wa msimamo wa kidini wa Kiongozi Muadhamu wa Iran kama msingi wa kujenga uaminifu na amani. Wao walijaribu kutumia kauli zao hizo kama ni chachu maalumu za kuelekea kwenye majadiliano kati yao na Iran, kuhusiana na mradi wa nyuklia wa Iran. [4] [5]
Mwitikio wa Kimataifa Kuhusiana na Fatwa
Inasemekana kwamba tamko la kimaadili la Sayyid Ali Khamenei, lilipokelewa vyema na kuungwaji mkono katika medani za kimataifa [6] na hatimae likawa na mwitikio mkubwa katika vituo vya uchambuzi wa kisiasa na taasisi za kimataifa za tafakuri ulimwenguni. [7] Aidha, kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Kayhan, ujumbe wa Sayyid Ali Khamenei kwa Mkutano wa Kimataifa wa Uondoaji wa Silaha, uliobeba fatwa ya uharamu wa kutengeneza na kutumia silaha za nyuklia, ulisajiliwa kama hati rasmi katika Umoja wa Mataifa. [8] Jonathan Granoff, rais wa Taasisi ya Usalama wa Dunia nchini Marekani, katika moja ya mahojiano yake, alimtaka Kiongozi wa Iran kuitangaza fatwa yake hii juu ya umarufuku wa kutumia kuzalisha na kutumia silaha za nyuklia, kupitia barua maalumu kwa ajili ya viongozi wengine wa kidini duniani, ili nao waweze kuungana naye mkono katika msimamo wake huo. [9]
Mnamo mwaka 2013 (1392 Hijria Shamsia), ujumbe wa watu sita kutoka Marekani, uliowajumuisha viongozi wa dini na wataalamu, ulifunga safari hadi Iran ili kukutana na kufanya mazungumzo na wanazuoni wa Kishia katika mji wa Qom. Madhumuni ya ziara hiyo ilikuwa ni kutathmini uhalali na uzito wa mtazamo huo wa kisheria (fiqhi) juu ya uhalali wa kutengeneza na kutumia silaha za nyuklia. Baadae ujumbe huo uliwasilisha ripoti zake kwa serikali ya Marekani kuhusiana uharamu wa silaha za nyuklia katika fiqhi ya Kishia, pamoja na matokeo ya safari hiyo, ili mambo hayo yazingatiwe katika mazungumzo ya nyuklia kati ya mataifa ya Magharibi na Iran. [10]
Aidha, mnamo mwaka 2021 (1400 Hijria Shamsia), kituo cha televisheni cha BBC Persian, kilirusha hewani kipindi maalumu kilichoitwa Yek Fatwa Hastei "Fatwa Moja ya Nyuklia". Kipindi hicho kilijadili uwezekano wa fatwa ya Sayyid Ali Khamenei kubadilika au kupitiwa na muda. [11] Hata hivyo, watafiti wa fiqhi walikanusha uwezekano wa kubadilika kwa fatwa hiyo, pia walikaa uwezekano wa kugeuka kwake kulingana na mabadiloko ya nyakati au mazingira fulani. [12]
Misingi ya Kihistoria ya Hukumu Hii
Silaha za nyuklia zinahisabiwa kuwa ni miongoni mwa silaha za maangamizi ya halaiki na ni kielelezo cha silaha hizo. [13] Kulingana na kauli ya Abulqasim Alidoust, ni kwamba; kwa takriban milenia moja hivi sasa, mafaqihi (wanazuoni wa sheria) wa Kishia, wamekuwa wakitoa fatwa zinazoharamisha utumiaji wa silaha angamizi, pamoja na zana zinazosababisha mauaji ya halaiki, uangamizaji wa viumbehai, na zinazopelekea uharibifu wa mfumo wa ikolojia (mazingira). [14] Tangu tarehe 19 Februari 2010, mara kadhaa Sayyid Ali Khamenei, ameonekana kukariri fatwa yake ya kupinga uundaji na utumiaji wa silaha za nyuklia. [15]
Matini ya Fatwa ya Sayyid Ali Khamenei na Kuungwa Mokono Kwake na Viongozi Wengine Wakuu wa Kidini (wanajitihadi)
Matini ya fatwa ya Sayyid Ali Khamenei, mmoja wa viongozi wakuu wa kidini, ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilisomwa na Ali Akbar Wilayati tarehe 17 Aprili 2010, mbele ya wajumbe rasmi wa "Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Uondoaji wa Silaha za Nyuklia na Kuzuia Usambaaji wake duniani." [16] Ujumbe wa fatwa hii, ulielezwa kama ifuatavyo:
"Kwa mtazamo wetu, mbali na kuharamisha silaha za nyuklia, bali pia ni haramu kuzalisha na kutumia aina zote za silaha za maangamizi ya halaiki, kama vile silaha za kemikali na za kibayolojia, silaha ambazo ni tishio kubwa kwa maisha ya binadamu... " [17]
Imeripotiwa kwamba katika nusu ya kwanza ya miaka ya 2010, kulitoka wanazuoni kadhaa wakuu waliounga mkono fatwa ya Sayyid Ali Khamenei. Miongoni mwa viongozi wakuu wa kidini waliotoa fatwa ziungazo mkono fatwa hiyo, ni pamoja na; Nassir Makarim Shirazi, Hussein Nuri Hamadani, Jafar Sobhani, na Abdullah Jawadi Amoli. [18] Pia kuna wanazuoni wengine kadhaa wanaohusiana na baraza la mchakato wa sheria waliounga mkono fatwa hii, wanazuoni hawa ni; Abulqasim Alidust, mwanasheria wa Kishia na katibu wa kongamano la kitaifa kuhusiana na sheria za Kiislamu za nyuklia, na Ahmad Muballighi, mwanasheria wa Kishia na mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Sheria. Kwa kuzingatia ushahidi wa vielelezo vya kisheria, wanazuoni haya wameitaja nadharia hii, kuwa ni amri ya Kimungu na ya kudumu isiyoweza kubadilishwa wala kujadiliwa. 19
Hoja na Dalili
Kuna hoja na dalili kadha wa kadha za kifiqhi zilizowasilishwa katika kujadili suala la uhalali au uharamu wa uzalishaji, urundikaji na utumiaji wa silaha za nyuklia. Sayyid Ali Khamenei akiwasilisha nadharia yake, anasema kwamba; uharamu wa silaha hizi, unatopkana na kutowiana na kutokubaliana kwake na misingi ya kiitikadi ya Uislamu, kwani itikadi za Kiislamu ni zenye kupingana wazi na dhana ya utumiaji wa silaha za maangamizi ya umma. Akiendelea na hoja zake anaeleza kwamba; matumizi ya silaha hizo ni miongoni mwa vielelezo vya uharibifu wa 'harth' (rasilimali za kilimo) na 'nasl' (vizazi vya binadamu), dhana inayorejelewa katika Qur'ani, kupitia Suratu ya Al-Baqara, Aya ya 205. [20] Katika muktadha huu, Abulqasim Alidust, ambaye faqihi wa madhehebu ya Shia, anabainisha mtazamo wake akisema kuwa; mojawapo ya madhumuni makuu ya Sharia (Maqasidu al-Shari'ah) ni kustawisha maslahi baina ya waja wenyewe kwa wenyewe na yale mahusiano yaliopo baina yao na Mola wao. Hivyo, yeye anasisitiza kwamba; Ustawi huu hauwezi kufikiwa kupitia njia ya uharibifu (ifsad) na kwa kutumia silaha za maangamizi ya umma. [21]
Ufuatao ni uchambuzi wa kina wa hoja zilizowasilishwa kuhusiana na mjadala huu:
Nukuu za Qur'ani
Ahmad Muballighi, faqihi wa Kishia, anaamini kwamba; kuna dalili nyingi za kifiqhi kuhusiana na uharamu wa kuzalisha na kutumia silaha za nyuklia. Akisisitiza mtazamo wake huu, amejaribu kurejelea kanuni tatu muhimu zilizoko ndani ya Qur'ani, nazo ni kama ifuatavyo: [22]
· Qā'idatu al-Wizr (Kanuni ya Mzigo): Kanuni hii inatokana na ibara ya Qur’ani isemayo «ولا تَزِرُ وازرةٌ وزرَ أُخری» (Wala hakutatokea mbebaji atakayebeba mzigo wa mwengine) (Surat al-Israa Aya15). Kanuni hii inasistizakuwa; haiwezekani watu wasio na hatia kushirikishwa na kuadhibiwa pamoja na wahalifu. Kiuhalisia ni kwamba; matumizi ya silaha za nyuklia, husababisha mauaji ya umma na kupelekea adhabu kwa wasio na hatia na kuathiri hata vizazi vijavyo.
· Qā'idah Hurmat al-Sa'ayu Bil-Fasād (Kanuni ya Uharamu wa Kueneza Ufisadi). Hii ni kaida iliochukuliwa kutoka katika Surat al-Baqarah, Aya ya 205. Kwa mujibu wa kanuni hii; ni marufuku kwa mtu fulani kutenda au kushiriki kitendo chochote kile kinachopelekea ufisadi ardhini, na kusababisha uangamizaji wa rasilimali za kilimo, mifugo na kuhatarisha vizazi vijavyo.
· Qā'idatu al-Ithm (Kanuni ya Dhambi/Madhara): Kulingana na ile ibara ya Qur’ani iseyo; «إثمُهُما اَکْبَرُ مِنْ نَفْعِهِما» (Madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake) (Surat al-Baqarah, Aya ya 219). Kanuni hii imekuja kuharamisha tendo lolote lile lenyo uovu na ufisadi, ambalo uovu wake unazidi na kupindukia manufaa yake. Kwa mujibu wa mawazo ya Muballeghi, ni kwamba; hakuna shaka kuwa matumizi ya silaha za nyuklia unaweza kusababisha ufisadi kubwa mno ulimwenguni humu, na madhara yake ni makubwa zaidi kupindkuia manufaa yake.
Naser Qurbannia akitoa mtazamo wake kupitia tafsiri ya Aya ya 190 na 205 za Suratu Al-Baqara, na Aya 8 na ya 32 za Suratu Al-Maida, anasema kwamba; Aya hizi zinasimama kama ni hoja rasmi ya kuharamisha moja kwa moja suala la uzalisha pamoja na utumiaji wa silaha za kinyuklia. [23]
Nukuu za Riwaya
Kuna hoja kadhaa zilizotolewa kutoka kwenye Riwaya mbalimbali, kuhusiana na mjadala wa kifikihi juu ya uharamu wa matumizi ya silaha za kinyuklia, huku silaha hizo zikihisabiwa kama ni kielelezo cha silaha za maangamizi ya halaiki. Miongoni hoja hizo ni kama ifuatavyo:
Miongoni mwa Hadithi na Riwaya zilizotumika kama ni vielelezo vya kuharamisha matumizi ya silaha hizi, ni zile Hadithi zinazohusiana na uharamu wa kutia sumu kwenye vyanzo vya maji vya adui. Riwaya hizi ndiyo nguzo muhimu ilitumiwa na baadhi ya wanazuoni katika kuharamisha silaha za nyuklia, akiwemo Abulqasim Alidoust na Mohammad Jawad Fadhil Lankarani. [24]
Baadhi ya watafiti wamejaribu kujenga hoja zao juu ya zile Riwaya zinazokataza uvamizi dhidi ya raia wa kawaida (wasio wapiganaji) wakiwemo; watoto, wanawake, wazee, watu wasio na akili timamu, na hata wanyama. [25]
Bibliografia
Kuna vitabu kadhaa vilivoandikwa juu ya fatwa inayoharamisha utengenezaji na utumiaji wa silaha za nyuklia, miongoni mwavyo ni:
Kitabu Fatwae Hastei Az Manzare Huquuqe Bainal Milali (Fatwa ya Nyuklia kwa Mtazamo wa Sheria za Kimataifa), kilichoandikwa na Jabir Siwani-Zad, kitabu hichi kimechapishwa na kampuni ya uchapishaji ya Marekani, iitwayo "Supreme Century." Inasemekana kwamba; kitabu hichi kinachambua hadhi na vipimo vya kisheria vya fatwa ya nyuklia ya Sayyid Ali Khamenei kwa mtazamo wa sheria za kimataifa. [26]
Kitabu Fiqh Hastei (Sheria za Kifiqhi za Nyuklia), kilichokusanywa na Abulqasim Alidust, kitabu hichi kilichapishwa mnamo mwaka 2013. Nacho ni kitabu chenye makala kumi za kisheria, zinazoelezea uharamu wa kutengeneza na kutumia silaha za nyuklia pamaoja na zenye maangamizi makubwa ya halaiki. Maudhui ya kitabu hichi ni mkusanyiko wa mada zilizowasilishwa kwenye kongamano la sheria za Kiislamu za nyuklia lililofanyika Tehran na Qom mano mwaka 2013. [27]
Kitabu Fatwae Hastei (Fatwa ya Nyuklia; Siasa na Madhehebu katika Mkakati wa Iran Juu ya Kuzuia Usambaaji Silaha za Nyuklia), ni kitabu kilichoandikwa na Michael Eisenstadt akishirikiana na Mehdi Khalaji. Waandishi wawili hawa wameandika kitabu chao hichi wakitoa uchambuzi juu ya mtazamo na mwelekeo wa Iran juu ya dhamira mikakatiti ya uzuiaji wa silaha hizi hatari. Kitabu hiki kilichapishwa na Taasisi ya Washington ya Masuala ya Mashariki ya Karibu. [28]