Ghaiba ya Imam Mahdi (a.t.f.s)

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Ghaiba kubwa)

Ghaiba ya Imam Mahdi (a.t.f.s) (Kiarabu: (عج)غيبة الإمام المهدي) ni katika imani na itikadi maalumu za Waislamu wa madhehebu ya Shia Imamiya (Shia Ithnaasharia) ambayo inaashiria maisha ya kujificha na yasiyo ya dhahiri ya Imam Mahdi (a.t.f.s) ambaye ni Imam wa 12 katika mlolongo wa Maimamu wa watu wa nyumba ya Bwana Mtume (s.a.w.w).

Kwa mujibu wa mafundisho ya madhehebu ya Kishia, Imam Mahdi(a.t.f.s) ana ghaiba mbili: Moja ni Ghaibat al-Sughra (Ghaiba Ndogo) ambayo ilidumu kwa miaka 69 na nyingine ni Ghaibat al-Kubra (Ghaiba Kubwa) ambayo ingali inaendelea mpaka siku atakapodhihiri mtukufu huyu kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kuja kuujaza ulimwengu uadilifu na usawa baada ya kuwa umejaa dhulma na uonevu.

Mashia wanaamini kwamba, katika zama za Ghaiba ndogo, Imam Mahdi alikuwa akiwasiliana na Mashia kupitia kwa baadhi ya watu ambao wanatambulika kama Manaibu wanne. Lakini katika kipindi cha Ghaiba Kubwa, mawasiliano ya kidhahiri ya Imam Mahdi na watu yamekatika na Mashia wanapaswa katika masuala ya kidini kuwarejea wapokezi wa hadithi na Maulamaa na wanazuoni wa Kishia. Hata hivyo, katika hadithi za Shia, Imam Mahdi katika zama zake za Ghaiba amefananishwa na jua lililoko nyuma ya mawingu ambapo daima watu hunufaika na uwepo wake. Kuhusiana na kwa nini uweko na ghaiba na Imam atoweke na kutoonekana katika upeo wa macho ya watu kumenukuliwa nukta mbalimbali katika hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ambapo miongoni mwazo ni kutahiniwa Mashia. Wanazuoni wa Kishia wameandika vitabu mbalimbali ili kubainisha suala la ghaiba ambapo kitabu mashuhuri zaidi miongoni mwavyo ni kitabu cha al-Ghaiba kilichoandikwa na Nu’mani na kitabu cha al-Ghaiba kilichoandikwa na Sheikh Tusi.

Utambuzi wa Maana

Kuamini ghaiba ya Imam wa 12 ni katika itikani na imani ambazo ni makhsusi kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia mkabala na Waislamu wa Kisuni. Kwa itikadi ya Mashia ni kwamba, ghaiba maana yake ni maisha ya siri na ya kificho ya Imam Mahdi (a.t.f.s) ambaye ni Imam wa 12 wa Waislamu wa Kishia. [1] Mashia wanaamini kwamba, Imam Mahdi (a.t.f.s) ameendelea kuwa ghaiba na kutoonekana katika upeo wa macho ya watu kwa amri ya Mwenyezi Mungu kwa muda usiojulikana na atakuja kudhihiri kwa amri na matakwa ya Mola Muumba. [2]

Namna ya Ghaiba

Kuhusiana na mbinu ya kughibu ya Imam Mahdi (a.t.f.s) kuna nukta kadhaa zimebainishwa kama mambo ya uwezekano:

  1. Kutoonekana mwili (kutoweka): Mwili wa Imam Mhadi (a.t.f.s) hauonekani katika macho ya watu na hii hali ya kujificha na kutoonekana katika upeo wa macho ya watu imetimia kupitia miujiza. [3] Kwa mujibu wa mtazamo huu, Imam wa kumi na mbili wa Mashia, anawaona watu, lakini wao hawamuoni yeye. Sayyid Muhammad Sadr anasema: Nadharia hii ni nadharia nyepesi zaidi inayoweza kukubalika kuhusiana na kwenda mafichoni na kuepukana na madhalimu. [4] Sadr kadhalika anasema, ufahamu wa hapo juu unaendana na maana ya kilugha ya ghaiba na hadithi zilizomshabihisha [5] Imam Mahdi katika kipindi cha kuwa kwake ghaiba kwamba, ni mithili ya jua lililoko nyuma ya mawingu. [6]
  2. Kujificha kianuani (kutotambuliwa): Sayyid Ridha Sadr anaamini kwamba, ghiab haina maana kwamba, Imam Mahdi (a.t.f.s) yupo mlimani au amejificha katika sehemu nyingine, bali makusudio ya ghaiba ni kutotambuliwa yeye na watu. Kwa maana kwamba, anaishi miongoni mwa watu lakini watu hawamtambui. [7]
  3. Kujificha mwili na kianuani: Katika baadhi ya wakati, mwili wa Imam Mahdi hauonekani katika upeo wa macho ya watu na wakati mwingine unaonekana na watu, lakini hatambuliwi kama ndiye. Lotfullah Safi Golpaygani, mmoja wa wanazuoni na marjaii wa Kishia anaamini kwamba, kwa mujibu wa hadithi na vilevile simulizi za watu waliobahatika kukutana na Imam Mahdi (a.t.f.s) inawezekana kupata natija hii kwamba, ghaiba imetokea kwa sura zote mbili (kutoweka na kuweko lakini kutotambuliwa), bali kuna wakati katika zama moja sura zote hizi za ghaiba zimetokea. [8]

Ghaibat-us-Sughra na Ghaibat-e-Kubra (Ghaiba ndogo na kubwa)

Ghaiba (kutoweka Imam Mhadi) imegawanyika katika sehemu mbili: Kipindi ambacho Imam alighibu kwa muda fulani kinatambulisha kama Ghaibat Sughra na kipindi ambacho ameghibu na kutoonekana katika upeo wa macho ya watu kwa muda mrefu kinatambulika kama Ghaibat-e-Kubra. Sheikh Mufid amevitaja vipindi viwili hivyo vya kughibu na kutoweka Imam Mahdi (a.t.f.s) kwa majina ya Ghaibat Qusra (fupi zaidi au ndogo) na Ghaibat Tulaa (ndefu zaidi au Kubra). [9] Imam Mahdi (a.t.f.s) katika barua yake aliyomuandikia naibu na mwakilishi wake wa mwisho Ali bin Muhammad Samuri siku sita kabla ya kifo chake alikitaja kipindi cha Ghaiba Kubwa kwa anuani ya "al-Ghaibat al-Tammah na akafasiri kwamba, hiyo ni ghaiba ambayo hakuna kudhihiri tena mpaka Mwenyezi Mungu atakapotoa idhini. [10]

Ghaibat-us-Sughra

Makala Asili: Ghaibat-us-Sughra

Ghaibat-us-Sughra ni hatua ya kwanza ya maisha yaa kujificha na kutooneka ya Imam wa 12 wa Mashia, kipindi ambacho kilifikia ukomo mwaka 329 Hijria. Kipindi hiki kwa mujibu wa hitilafu kuhusiana na zama za kuanza kwake kilidumu kwa muda wa miaka 69 au 74. Kundi la Maulamaa wa Kishia kama vile Sheikh Mufid (aliyeaga dunia 413 Hijria) katika kitabu chake cha al-Irshad [11], na Tabrasi (aliyefariki dunia 548 Hijria) katika kitabu chake cha Ilam al-Wara wametambua kipindi cha Ghaiba Ndogo kwamba ni miaka 74 na kwamba, kilianza mwaka 255 Hijiria (mwaka aliozaliwa Imam Mahdi a.s). [12] Hata hivyo, kundi jingine la Maulamaa linasema kuuwa, Ghaibat-us Sughra ilianza mwaka 260 Hijria (mwaka aliokufa shahidi Imam Hassan Askary na mwaka wa kuanza Uimamu wa Imam Mahdi) na kwamba, kipindi hiki kilidumu kwa muda wa miaka 69. [13]

Katika kipindi cha Ghaibat-us-Sughra Imam Mahdi alikuwa akiwasiliana na Mashia kupitia manaibu na wawakilishi wake. [14] Mashia walikuwa wakiandika barua na kueleza matakwa yao na barua zao ziliwasilishwa kwa Imam Mahdi kupitia manaibu wake na kupata majibu ya maswali na matakwa yao kupitia njia hiyo hiyo. [15] Kufanya juhudi za shakhsia wakubwa kupenya katika vyombo vya utawala vya Bani Abbas, kupambana na maghulati (watu wanaowatuuuza Maimamu na kuwapa sifa ya uungu) na wanaodai kwa uongo kwamba, ni manaibu na wawakilishi na kuratibu Shirika la Uwakala zimetajwa kuwa ni miongoni mwa zilizokuwa kazi na harakati za manaibu wa Imam Mahdi. [16]

Ghaibat-e-Kubra

Makala za Asili: Ghaibat-e-Kubra na Uwakala Jumuishi

Ghaibat-e-Kubra (Ghaiba Kubwa) ni hatua ya pili ya maisha ya kujificha na kutoonekana Imam Mahdi (a.t.f.s), kipindi ambacho kilianza mwaka 329 Hijria baada ya kuaga dunia Ali bin Muhammad Samuri naibu wanne wa Imam huyu na kitaendelea mpaka atakapodhihiri. Katika kipindi hiki Imam Mahdi (a.t.f.s) hana mawasiliano ya kidhahiri na Mashia na hakumchagua na kumuainisha pia mtu maalumu au mwakilishi wake. Pamoja na hayo, kwa mujibu wa imani na itikadi ya Mashia, wapokezi wa hadithi na Maulamaa wa Kishia ndio wawakilishi na manaibu wa kiujumla wa Imam Mahdi (a.t.f.s). Kwa mujibu wa tawqi' (barua na maandiko) ya Imam Mahdi (a.t.f.s) kwa Is'haq bin Yaqub, Mashia wanapaswa kuwarejea mafakihi wa Kishia katika masuala mapya. [17] Pamoja na hayo, kuna hitilafu za kimitazamo kuhusiana na uga na uwanja wa mamlaka ya fakihi katika kipindi cha zama za Ghaibat-e-Kubra. [18] Imam Ruhullah Khomeini akitegemea maandiko na barua hii amesema, katika kipindi cha ghaiba masuala yote ya jamii ya Kiislamu yanapaswa kukabidhiwa kwa mafakihi. [19] Tofauti ya Ghaibat-e-Kubra na Sughra ni uwepo wa manaibu wanne ambao walikuwa ni kiunganishi cha mawasiliano katika zama za Ghaiba Ndogo na watu waliokuwa na jukumu la kubeba na kuchukua ujumbe wa Imam Mahdi na kuwafikishia watu na baada ya hapo mawasiliano ya kidhahiri ya Imam wa 12 na watu yakawa yamekatwa kabisa. [20]

Hali ya Jamii ya Kishia Mwanzoni mwa Ghaiba

Katika zama za Imam Hassan Askary (a.s) ilikuwa mashuhuri kwamba, Mashia wanasubiri mapinduzi na harakati ya mawanawe. [21] Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana vyombo vya utawala wa Bani Abbas vilikuwa vikimtafuta mtoto wa Imam huyo. Imam Hassan Askary (a.s) alikuwa amemtambulisha mwanawe kwa watu wachache mno miongoni mwa masahaba zake na watu wake wa karibu [22] na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana wakati wa kufa shahidi Imam Askary, watu wengi hawakuwa na habari ya kuweko mtoto wake. [23] Katika upande mwingine, Imam Hassan Askary (a.s) kutokana na mazingira ya kisiasa katika wasia wake alitaja jina la mama yake tu na hilo likapelekea katika kipindi cha mwaka mmoja au miaka miwili ya baada ya kufa kwake shahidi Mashia waamini kwamba, mama wa Imam Hassan Askary ndiye mwenye jukumu la wadhifa wa Uimamu kwa niaba katika zama za ghaiba. [24]

Baada ya kuuawa shahidi Imam Askary (a.s), baadhi ya masahaba zake wakiongozwa na Uthman bin Said Umri (aliyefariki dunia baina ya 260 na 267 Hijiria) walitangaza kwa umma wa Shia kwamba Imam Askary ameacha nyuma mtoto wa kiume ambaye sasa ndiye mrithi wake na mwenye kuchukua jukumu la Uimamu. [25] Pamoja na hayo Ja'far ndugu wa Imam Hassan Askary (a.s) licha ya kuwa, mama wa Imam Askary alikuwa hai, alidai urithi wa mtukufu huyo. [26] Mama wa Askary na Hakima shangazi yake walikuwa wakiunga mkono Uimamu wa mtoto wa Imam Hassan Askary, lakini dada wa Imam Askary, alikuwa akiunga mkono Uimamu wa Ja'far kaka yake. [27] Kadhalika familia ya Naubakht, Othman bin Said na mwanawe walikuwa wakitambua rasmi jukumu la uniaba wa Imam Mahdi (a.t.f.s). [28] Hali hii iliwachanganya baadhi ya Mashia. [29] Baadhi wakajiunga na makundi mengine ya Kishia. [30] Baadhi ya makundi hayakukubali kifo cha Imam Askari na kumuona kuwa ni Mahdi, wakati kundi liliukubali Uimamu wa Sayyid Muhammad, mtoto wa Imam Hadi (a.s) na kuukana Uimamu wa Imam Askary. [31] Aidha kundi jingine miongoni mwao lilikuwa likimtambua Ja'far Kadhab (muongo) kuwa ndiye Imam. [32] Hata hivyo hatimaye akthari ya Mashia wakaelekea upande wa Uimamu wa Imam Mahdi (a.t.f.s), na harakati hii baadaye ikashika uongozi asili wa Mashia Imamiya. [33]

Falsafa na Sababu ya Ghaiba

Watafiti wa Kishia wanaamini kwambaa, siri na sababu zote za ghaiba ya Imam, haiko wazi kwetu; kama ambavyo katika baadhi ya hadithi, hekima kuu ya kughibu Imam na kutoonekana katika upeo wa macho ya watu imetajwa kuwa ni siri katika siri za Mwenyezi Mungu ambayo itabainika baada ya kudhihiri Imamu Mahdi (a.t.f.s). [34] Pamoja na hayo katika hadithi kuna maudhui kadhaa zimekokotezwa na kutiliwa mkazo:

  1. Kulinda uhai na roho ya Imam Mahdi (a.t.f.s). [35]
  2. Kuwatihini na kuwatia majaribuni watu [36]. Imekuja katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Mussa bin Ja'far al-Kadhim (a.s) ya kwamba, Mwenyezi Munguu anawatia majaribuni waja wake kupitia ghaiba. [37]

Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi mtihani na majaribu ya kipindi cha ghaiba ni katika mitihani migumu zaidi ya Mwenyezi Mungu. [38] na ugumu huu ni kutokana na mambo mawili:

  1. Kudumu kwa muda mrefu ghaiba kutapelekea watu kuingiwa na shaka na hali ya kusitasita kiasi kwamba, kundi miongoni mwa watu watatilia shaka juu ya kuzaliwa na wengine wataingia na shaka katika suala zima la kudumu kwa muda mrefu umri wa Imam Mahdi (a.t.f.s) na watabakia baadhi ya watu tu katika imani ya Uimamu wa mtukufu huyo, watu ambao kimsingi wamefanikiwa kufaulu mtihani huu ambao kimsingi wana ikhlasi, wana utambuzi wa kina. [39]
  2. Ugumu na kutokea mambo yasiyotarajiwa katika zama za ghaiba yatawageuza watu kiasi kwamba, kulinda na kubakia na imani na kusimama kidete katika dini litakuwa jambo gumu na imani ya watu itakabiliwa na hatari kali. [40]
  3. Kutotoa baia na kiapo cha utii Imam kwa mtawala yoyote dhalimu mpaka kudhihiri [41]. Baadhi ya hadithi zinasema, Imam wa kumi na mbili hatautambua utawala wowote ule dhalimu hata kwa taqiyya (kuficha imani). Yeye hajaamrishwa kufanya taqiyya kwa mtawala yeyote yule na katu hatokuwa chini ya utawala wowote ule dhalimu na atatekeleza sheria za dini ya Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu na bila kufumbia macho hata kidogo au kuwa na woga na wasiwasi. [42]
  4. Kutoa malezi kwa watu. [43]
  5. Kutokuweko mazingira na anga ya kisiasa na kijamii kwa ajili ya Uislamu kuwa dini ya ulimwengu.

Suala la ghaiba katika zama zilizopita lilikuweko kuhusiana na baadhi ya Mitume. [44] Kwa mujibu wa Aya za Qur’an Mitume kadhaa kama Saleh, Yunus, [45] Mussa, [46] Issa na mtukufu Khidhr (a.s) kwa sababu mbalimbali kama kutahiniwa umma zao, walipotea katika upeo wa macho ya watu. Katika baadhi ya hadithi, ghaiba na kutoonekana Mitume katika upeo wa macho ya watu kumetajwa kuwa ni katika sunna na mipango ya Mwenyezi Mungu ambayo ilitokea katika umma na jamii mbalimbali. [47] Sheikh Tusi anasema, watu pia walikuwa na nafasi na mchango katika ghaiba. Watu (ambao ni mukalafu) kwa miamala yao, kumuogopesha Imam, kumkosesha amani na kutosalimu kwake yeye ni mambo ambayo yaliandaa uwanja na mazingira ya ghaiba na wao wenyewe wakawa wamejinyima fursa ya kunufaika na Imam na kuwa na mahusiliano naye ya kimahudhurio na kidhahiri. [48] Khawaja Nasir al-Din Tusi mwanafalsafa mkubwa na mwanateolojia wa Kishia pia amenasibisha na watu katika kitabu chake cha Tajrid al-I’tiqad suala ghaiba ya Imam. [49]

Athari na Maandiko Kuhusu Ghaiba

Kuna vitabu mbalimbali vilivyoandikwa kuhusiana na Imam Mahdi (a.t.f.s). Vitabu kama al-Ghaibah kilichoandikwa na Nu’mani (kiliandikwa mwaka 342 Hijiria), Kamal al-Din kilichoandikwa na Sheikh Tusi (aliaga dunia 3781 Hijria) na al-Ghaibah kilichoandikwa na Shekhe Tusi vinahesabiwa kuwa vitabu vikongwe kabisa katika maudhui hii. [50] Baadhi ya athari nyingine zilizoandikwa katika uga huu ni:

  • The Occultation of the Twelfth Imam, A Historical Background cha Jassim Hussein. Muhammad Taqi Ayatullahi amekiweka katika lugha ya Kifarsi kwa anuani ya Tarikh Siyasi Ghaibat Imam Davazidahom.
  • Ar’baa Risalat fi Ghaibat: Kitabu hiki kimeandikwa na Sheikh Mufid na kinajumuisha risala nne kwa mtindo wa maswali na majibu kuhusiana na Imam Mahdi (a.t.f.s) ambapo katika risala ya nne kumejadiliwa sababu ya ghaiba ya Imam Mahdi (atfs).
  • Al-Fusul al-Ashara fi al-Ghaibah au al-Masail al-Asharh fil Ghaibat, kilichoandikwa na Sheikh Mufid. Katika kitabu hiki, mwandishi ametoa majibu ya mambo kumi ambayo ni shubha (tata) kuhusiana na ghaiba ya Imam Mahdi (a.t.f.s).
  • Mausuah al-Imam al-Mahdi ni majimui ya kitabu cha juzuu nne kuhusiana na imani ya Mahdi kitabu ambacho kimeandikwa na Sayyid Muhammad Sadr ((aliaga dunia 1377 Hijiria Shamsia) mmoja wa wanazuoni na Maulamaa wa Iraq. Juzuu ya kwanza ya kitabu hiki ina jina la Tarikh al-Ghaibah al-Sughra na juzuu ya pili ina jina la Tarikh al-Ghaibah al-Kubra. Juzuu mbili nyingine zinahusiana na kipindi cha baada ya ghaiba.

Rejea

Vyanzo