Dua ya Kufungua Saumu

Kutoka wikishia

Dua ya Kufungua Saumu: ni dua iliyopokewa kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w) na Imam Ali (a.s), [1] ambayo husomwa wakati wa kufungua saumu. [2] Katika dua hii, mja huzungumza na Mola wake akimwambia: “(Ewe Mwenye Ezi Mungu), sisi tumeifunga saumu (hii) kwa ajili yako tu, na tunafungua (saumu hii) kwa riziki yako.” [3] Baada ya hapo, mtu huwomba Mwenye Ezi Mungu amkubalie ibada hii. [4]

Kwa mujibu wa baadhi ya wafasiri na wachambuzi wa Hadithi, dhana kuu ya dua hii ni kuonesha kuwa; sisi tumefunga saumu zetu kwa nia safi na ikhlasi, na kwa ajili ya Mwenye Ezi Mungu peke yake, na kwa kuwa sisi tunafaidika na rizki zake, kutokana na kwamba Yeye ndiye mtoaji wa riziki pekee ulimwenguni, basi sisia tunamwabudu Yeye peke yake." [5]

Dua hii imetajwa katika vyanzo vya Hadithi mbali mbali, na inapatikana ndani ya mlango wenye orodha ya matendo ya mwezi wa Ramadhani. Hata hivyo, Hadithi zinazoinukuu dua hii hazijaifunga dua kwa ajili ya mwezi wa Ramadhani peke yake. [6] Katika baadhi ya Riwaya, imeelezwa kwamba; Pale bwana Mtume (s.a.w.w), alipomaliza kusoma dua hii, alikuwa akisema: “Kiu kali na ugumu wa kufunga vimeondoka, ila thawabu zake zingalipo”. [7] Aidha, katika baadhi ya masimulizi, dua hii huanzwa kwa “Bismillahi”. [8]

Matini ya Dua na Tafsiri Yake

[9]  بِسْمِ اللَّه اللَّهُمَ‏ لَكَ‏ صُمْنَا وَ عَلَى رِزْقِكَ أَفْطَرْنَا فَتَقَبَّلْ [فَتَقَبَّلْهُ] مِنَّا إِنَّكَ أَنْتَ السَّمِيعُ الْعَلِيم

“Ewe Mwenye Ezi Mungu, (hakika sisis) tumefunga kwa ajili yako na tumefungua kwa riziki yako; (basi) tutakabalie funga zetu, hakika Wewe ni Msikivu na Mjuzi!”.

Pia dua hii imenukuliwa kutoka kwa Imamu Ridha (a.s), ambayo ni tofauti kidogo na dua ya mwanzo, kwani ndani yake kuna ongezeko la maneno na tofauti ya aina fulani katika ibara zake. [Maelezo 1: اللَّهُمَ‏ لَكَ‏ صُمْنَا بِتَوْفِيقِكَ وَ عَلَى رِزْقِكَ أَفْطَرْنَا بِأَمْرِكَ فَتَقَبَّلْهُ مِنَّا وَ اغْفِرْ لَنَا إِنَّكَ أَنْتَ الْغَفُورُ الرَّحِيم] Dua nyingine inayofanana na hii, miongoni mwa Dua zinazosomwa wakati wa kufungua saumu, iliyo nukuliwa na Imamu Kadhim (a.s) kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w). Ama kuhusiana na sifa na malipo ya dua hii, imeelezwa kwamba; mtu yeyote atakayesoma dua hii atapata thawabu sawa na thawabu za wale wote walio funga siku hiyo aliyofunga na kuomba dua hii ndani yake. Matini ya dua hii ni kama ifuatavyo:

اللَّهُمَ‏ لَكَ‏ صُمْتُ‏ وَعَلَى رِزْقِكَ أَفْطَرْتُ وَعَلَيْكَ تَوَكَّلْت‏.

Ewe Mwenye Ezi Mungu! Nimefunga kwa ajili yako, nimefuturu kwa riziki yako, na ninakutegemea Wewe (ninatawakali kwako Wewe)”.