Aya ya Kibla
Aya ya Kibla (Kiarabu: آية القبلة) ni Aya ya 144 katika Surat al-Baqarah ambayo inatoa amri ya kubadilisha kibla cha Waislamu kutoka Masjidul Aqsa na kuelekea Masjidul Haram huko Makka. Baada ya Hijra ya Waislamu (kugura) kutoka Makka na kuelekea Madina, wakazi wa Kiyahudi wa mji huo walikuwa wakitaja hatua ya Waislamu ya kuelekea Msikiti wa al-Aqswa kuwa, ni hoja ya Uislamu kutokuwa na asili. Hilo lilipelekea na kumfanya Mtume (s.a.w.w) atamani Kaaba iwe Kibla cha Waislamu.
Baadhi ya wafasiri wamezitambua Aya za 142-144 za Surat al-Baqarah kwamba, ni Aya za kubadilisha kibla na baadhi ya wengine wamelitambua suala la kubadilishwa kibla cha Waislamu kuwa linazungumziwa katika Aya ya 150 ya Surat al-Baqarah. Wafasiri wa Qur’an wanasema kuwa, Aya ya Kibla ilishuka katika kipindi cha baina ya miezi saba mpaka 19 baada ya Mtume kuhajiri na kuhamia Madina. Sehemu iliposhuka kuna nukuu mbalimbali kuhusiana na sehemu iliposhuka Aya hii ambapo kwa mujibu wa nyaraka za historia ni moja kati ya sehemu hizi tatu: Masjid Qiblatein, Masjid Qiblah (Salim bin Auf) na Masjid al-Nabi.
Andiko la Tarjuma
قَدْ نَرَى تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاءِ فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنْتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ وَإِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ لَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِنْ رَبِّهِمْ وَمَا اللَّهُ بِغَافِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ
Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso wako mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo; na hakika wale walio pewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda.
(Surat al-Baqarah: 150)
Aya hii ambayo ina hukumu ya kubadilisha kibla, imeondokea kuwa mashuhuri kwa Aya ya kibla. [1] Baadhi ya wafasiri wameitaja Aya ya 150 ya Surat al-Baqarah kwamba, nayo ni Aya ya Kibla. [2] Kadhalika Tantawi, mmoja wa wafasiri wa Kisuni amezitambua na kuzitaja Aya za 142 hadi 144 kuwa ni Aya za kubadilisha Kibla. [3]
Sababu ya kushuka
- Makala asili: Kubadilishwa Kibla
Kwa mujibu wa nukuu ya Muhammad bin Jarir Tabari, mmoja wa wafasiri wa Qur’an wa Ahlu-Sunna ni kuwa, Mayahudi wa Madina walikuwa wakiona kuwa ni aibu na mapungufu kwa Mtume kuswali ilihali anaelekea Masjid al-Aqswa na walikuwa wakisema: Muhammad (s.a.w.w) anapinga dini yetu lakini anaswali Sala zake kwa kuelekea katika kibla chetu; ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Mtume (s.a.w.w) alikuwa akitaka na kutamani Waislamu wawe na kibla chao peke yao na kuswali kuelekea Kaaba; [4] ni kwa msingi huo, ndio maana Mtume (s.a.w.w) akaangalia mbinguni na kusubiri amri ya Mwenyezi Mungu ya kubadilishwa kibla ambapo Aya hii ikashuka na kutoa amri ya kubadilishwa kibla kutoka katika Msikiti wa al-Aqswa Palestina na kuelekea Kaaba katika mji wa Makka. [5]
Zama na mahali iliposhuka
Wafasiri wa Qur’an Tukufu wanasema kuwa Aya ya Kibla ilishuka katika kipindi cha baina ya miezi saba [6] mpaka miezi 19 [7] baada ya Mtume kuhajiri na kuhamia Madina. Allama Muhammad Hussein Tabatabai anasema katika kitabu chake cha Tafsir al-Mizan: Kwa kuzingatia kwamba, kubadilishwa kibla kulifanyika katika mwezi Rajab mwaka wa pili Hijria, kipindi sahihi zaidi ni miezi 17 baada ya Hijra ya Mtume (s.a.w.w). [8] Ayatullah Makarim Shirazi anasema katika tafsiri yake ya Nemooneh (Tafsir al-Amthal) kwamba, kibla kilibadilishwa wakati wa kutekelezwa Sala ya Adhuhuri kiasi kwamba, wanaume na wanawake walibadilishana sehemu zao. [9]
Sehemu ya kutekelezwa hukumu ya kubadilishwa kibla kwa mujibu wa nukuu mbalimbali za kihistoria ni moja kati ya maeneo haya matatu.
- Msikiti wa kitongoji cha Bani Salimah [10] kaskazini magharibi mwa Madina [11] ambao ni mashuhuri kwa jina la Masjid Qiblatein (Msikiti wa vibla viwili]. [12]
- Masjid Qiblah "Bani Salim bin Auf", eneo ambalo Mtume (s.a.w.w) alisali Swala ya kwanza ya Ijumaa hapo. [13]
- Masjid al-Nabi. [14]
Kufutwa Aya
Fadhl bin Hassan Tabarsi ameandika katika kitabu chake cha Tafsri cha Maj’maa al-Bayan: Baadhi wamedai kuwa, Aya ya kibla, imefutwa na Aya ya 115 Surat al-Baqarah inayosema: ((فَأَيْنَمَا تُوَلُّواْ فَثَمَّ وَجْهُ اللَّهِ ; Basi kokote mnako elekea, huko Mwenyezi Mungu yupo)). Hata hivyo, mwanazuoni huyu yeye ameukataa mtazamo huu na kusema kuwa, kwa mujibu wa hadithi, Aya ya 115 ya Surat al-Baqarah inahusiana na suala la kusali Sala za mustahabu mtu akiwa safarini. [15]
Rejea
Vyanzo
- Abū l-Futūḥ al-Rāzī, Ḥusayn b. ʿAlī. Rawḍ al-Jinān wa rawḥ al-Janān. Edited by Yāḥaqī & Nāṣiḥ. Mashhad: Āstān-i Quds-i Raḍawī, 1375 Sh.
- Fakhr al-Rāzī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Al-Tafsīr al-kabīr. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1415 AH.
- Ibn Kathīr al-Dimashqī, Ismāʿīl b. ʿUmar. Tafsīr al-Qurʾān al-ʿaẓīm. Edited by Marʿashlī. Beirut: Dār al-Maʿrifa, 1409 AH.
- Ibn Saʿd, Muḥammad b. Manīʿ al-Basrī. Al-Ṭabaqāt al-kubrā. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Qādir ʿAṭāʾ. Beirut: Dār al-Kutub al- ʿIlmīyya, 1418 AH.
- Ibn Syyid al-Nās, Muḥammad b. Muḥammad. ʿUyūn al-athar. Edited by Ibrāhīm Muḥammad. Beirut: Dār al-Qalam: 1414 AH.
- Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
- Qāʾidān, Aṣghar. Tārikh wa Āthār-i Islāmī Mecca wa Medina. Tehran: Mashʿar, 1386 Sh.
- Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Edited by Jazāʾirī. Qom: Dār al-Kutub, 1404 AH.
- Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Jāmiʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Edited by Ṣidqī Jamīl. Beirut: Dār al-Fikr, 1415 AH.
- Ṭabāṭabāyī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī Tafsīr al-Qurʾān. Translated by Mūsawī Hamidānī. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.
- Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al. Iʿlām al-warā bi-Iʿlām al-Hudā. Qom: Āl al-Bayt, 1417 AH.
- Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Tehran: Nāṣir khusru, 1372 Sh.
- Ṭanṭāwī, Sayyid Muḥammad. Al-Tafsīr al-wasīṭ. Cairo: Dār al-Maʾārif, 1412 AH.
- Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Tibyān. Edited by Aḥmad Ḥabīb Qaṣīr al-ʿĀmulī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1412 AH.
- Zamakhshrī, Maḥmūd b. ʿUmar al-. Al-Kashshāf ʿan ḥaqāʾiq qwāmiḍ al-Tanzīl. Qom: Nashr al-Balāqa, 1415 AH.