Aya ya Israa

Kutoka wikishia

Aya ya Israa ni Aya ya kwanza ya Surat al-Israa ambayo ilishuka kuhusiana na safari ya miraji ya Mtume (saww). Kwa mujibu wa Aya hii, Mtume (saww) alichukuliwa usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu (Msikiti wa Makka) mpaka Msikiti wa mbali (Masjdul al-Aqswa) na lengo la safari hii ya lilikuwa ni kuonyeshwa ishara za Mwenyezi Mungu. Kupitia Aya hii inafahamika kwamba, Mtume (saww) alifanya safari hii kimwili na kwamba, jambo hili lilikuwa ni muujiza.

Utambulisho

Aya ya kwanza ya Surat al-Israa ambayo inaashiria tukio la Mtume (saww) kusafiri usiku mmoja kutoka Masjid al-Haram mpaka Masjid al-Aqswa inajulikana kwa jina la Aya ya Israa. [1]

سُبْحَانَ الَّذِی أَسْرَی بِعَبْدِهِ لَیْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَی الْمَسْجِدِ الأَقْصَی الَّذِی بَارَکْنَا حَوْلَهُ لِنُرِرِیَهُ مِنْ آیَاتِنَا إِنَّهُ هُوَ السَّمِیعُ البَصِیرُ﴿۱﴾

Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.

Sababu ya kushuka Makala kuu: Miraji

Aya hii ilishuka kuhusiana na safari ya Mtume kutoka Makka na kuelekea katika Masjid al-Aqswa huko Baytul-Muqaddas. [2] Kwa mujibu wa Shekhe Tabarsi, mmoja wa wafasiri wa Qur’an wa karne ya 6 Hijria ni kuwa, Mtume (saww) alianza safari yake ya Miraji baada ya kukamilisha kuswali Sala ya Magharibi na Isha katika msikiti wa Makka na alirejea usiku huo huo na akaswali Sala ya Alfajiri pia katika Msikiti wa Makka. Waislamu wote wanaafikiana kuhusiana na jambo hili na limenukuliwa na baadhi ya masahaba kama Ibn Abbas, Ibn Mas’ud, Jabir bin Abdillah na Hudhaifa. Wafasiri wa Qur’an wamebainisha kwa undani kuhusiana na tukio hili chini ya Aya hii kama vile wakati, sehemu na jinsi lilivyofanyika. [4]

Tukio la Miraji ni muujiza

Baadhi ya wafasiri wanaitaja Aya ya Israa kuwa moja ya miujiza ya Mtume (saww). [5] Ja’afar Sobhani anasema katika Tafsiri Manshur Javid kwamba, safari ya Mtume kutoka Masjid al-Haram mpaka Masjid al-Aqswa ni moja ya miujiza ya Bwana Mtume (saww), safari ambayo ilifanyika bila ya suhula na vyombo vya leo na nje ya uwezo wa mwanadamu. [6] Murtadha Mutahhari (aliaga dunia 1358 Hijria Shamsia), msomi na mwanafikra wa Kishia anasema kuwa, katika Aya hii kumebainishwa wazi na bayana kuhusiana na kufanyika safari isiyo ya kawaida ya kimwili iliyofanywa na Mtume (saww); kwani safari kama hii haiwezi kuwa kitu kingine ghairi ya muujiza hasa katika zama ambazo suhula za safari ilikuwa ngamia. [7] Hata hivyo, Ayatullah Makarim Shirazi anaamini kwamba, Aya hii peke yake haijaweka wazi na kubainisha suala la muujiza; bali hilo limebainishwa kwa kuunganisha na hadithi na sababu ya kushuka Aya hii wakati wa kufasiri Aya hii ya kwamba, ni katika miujiza ya Bwan Mtume (saww) [8]

Safari ya Miraji ilikuwa ya kimwili

Chini ya Aya hii, wafasiri wamezungumza kuhusu kupaa kuwa ni kimwili au kwa kiroho. Kwa mujibu wa Allama Tabatabai (aliyefariki: 1360 Hijria), wengi wao wanaamini kwamba kupaa huko kulikuwa ni kwa kimwili. [9] Hata hivyo Allama Tabatabai mwenyewe anaamini kwamba, kupitia Aya hii na Aya za Surah Najm, inapatikana natija hii kwamba safari ya Mtume kutoka Masjid al-Haram kwenda Masjid al-Aqsa ilikuwa ya kimwili, lakini kupaa kwake kutoka Msikiti wa Al-Aqsa kwenda mbinguni kulikuwa kwa kiroho. [10] Ayatullah Makarim Shirazi anasema kuwa, kupitia neno «بِعَبْده» inapatikana natija hii kwamba, safari ya Miraji ya Mtume ilikuwa ya kimwili, kwani neno hili linaonyesha kuwa, mwili wa Mtume ulikuwa pamoja naye katika safari hii. [11] Kadhalika Ja’far Sobhani amesema, kama safari hii ingekuwa ni ya kimaanawi (kiroho) basi badala ya neno «بِعَبْده» Mwenyezi Mungu ange kutumia neno “بِروحه " [12]

Lengo la Miraj ya Mtume

Wafasiri wameashiria ibara ya «لنریه من آیاتنا» yaani ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu, kwamba ndio lengo la Miraji. [13] Lengo la Miraji lilikuwa ni kumuonyesha Mtume (saww) adhama ya ishara za Mwenyezi Mungu ili roho yake ipate adhama na iwe na maandalizi zaidi kwa ajili ya kuongoza watu. [14]

Tabarsi katika Majmaal al-Bayan anaitambua safari ya usiku ya Mtume (saww) kutoka Makka hadi Baytul-Muqaddas, kupaa mbinguni na kuwaona Mitume kuwa ni miongoni mwa ishara hizo. [15] Kadhalika, kutokana na neno “مِنْ “ katika Aya hiyo, inafahamika kwamba, Nabii Muhammad (saww) aliona baadhi ya ishara za adhama ya Mwenyezi Mungu katika safari hiyo na sio zote. [16]