Aya ya Hijabu
Jina la Aya | Aya ya Hijabu |
---|---|
Sura Husika | Surat al-Nuur |
Namba ya Aya | 31 |
Juzuu | 18 |
Mahali pa Kushuka | Madina |
Maudhui | Kifiqhi |
Mada Yake | Wajibu wa Hijabu |
Mengineyo | Aya ya Jilbab |
Aya ya Hijabu (Kiarabu: آية الحجاب) (Surat Nur: 31) inabainisha na kueleza ulazima wa wanawake kuvaa hijabu. Aya hii ni hoja inayotumiwa na mafakihi kwa ajili ya kuonyesha kuwa vazi la hijabu ni wajibu kwa wanawake. Kadhalika baadhi ya mafakihi kwa mujibu wa ibara «اِلّا ما ظَهَر مِنها ; isipo kuwa unao dhihirika» iliyokuja katika Aya ya Hijabu wamesema kuwa, sio wajibu kwa mwanamke kufunika uso na mikono na kuanzia kifundo cha miguu mpaka chini.
Kuna Aya zingine ambazo nazo zinatambuliwa kwa jina la Aya ya Hijabu. Miongoni mwazo ni Aya ya 59 ya Surat al-Ahzab ambayo inafahamika kwa jina la Aya ya Jilbab.
Aya ya Hijabu na Tarjumi yake
Aya ya 31 katika Surat Nur inatambuliwa kwa jina la Aya ya Hijabu. [1] Inaelezwa kuwa, hijabu iliwajibishwa kwa wanawake baada ya kushuka Aya hii. [2]
وَقُلْ لِلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَى جُيُوبِهِنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَى عَوْرَاتِ النِّسَاءِ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِنْ زِينَتِهِنَّ وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ
Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.
(Surat Nuur: 31)
Matumizi ya Kifikihi
Katika vitabu vya fiqhi, Aya hii imetajwa na kutumiwa ili kueleza wajibu wa wanawake kuvaa hijabu na baadhi ya hukumu zake, ikiwa ni pamoja na mipaka ya hijabu.[3] Kwa mujibu wa mafaqihi, maneno ya «وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ» yaani "wala wasionyeshe uzuri wao" yanaashiria faradhi ya hijabu kwa wanawake. [4] Pia, kwa mujibu wa baadhi ya Mafakihi wa Kishia, kama vile Sheikh Ansari, Shahid Thani na Allama Hilli ni kwamba, ibara ya «Arabic|اِلّا ما ظَهَر مِنها}}» (isipo kuwa unao dhihirika) iliyokuja katika Aya ya Hijabu haijumuishi uso na mikono (kuanzia katika vifundo vya mikono kuelekea chini) katika wajibu wa hijabu. Kwa maana kwamba, viungo hivyo sio wajibu kwa mwanamke kuvifunika.[5]
Sababu ya Kushuka Aya
Kuhusiana na kisa cha kuteremshwa kwa Aya hii, imepokewa kutoka kwa Jabir bin Abdullah al-Ansari kwamba, siku moja, kundi la wanawake lilikwenda kwenye Asma bint Murshida hali ya kuwa hawajavaa vizuri kwa namna ambayo vifundo vyao vya miguu, shingo na uvimbe wa matiti vilikuwa dhahiri. Alikasirishwa na kitendo hiki na akawalaumu. Baada ya hayo, Aya hii ikateremshwa.[6] Tabarsi, mfasiri wa Qur'ani, naye ameandika katika muktadha huu kwamba, kabla ya kuteremka Aya hii, wanawake walikuwa wakivaa hijabu kwa namna ambayo mkia wake uliangukia nyuma, kwa hiyo shingo zao na kifua vilikuwa vikionekana.[7]
Nukta za Kitafsiri
Kwa mujibu wa wafasiri, maana ya: «وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ» yaani "wala wasionyeshe uzuri wao" ni kutoonyesha sehemu za mwili ambazo kwa kawaida hupambwa (kama masikio na shingo), na sio kutoonyesha mapambo hayo peke yake; kwa sababu haikatazwi kuonyesha vito peke yake kama pete.[8] "Khumur" ni wingi wa khimar, ambayo ina maana ushungi ambao wanawake hufunika vichwa vyao.[9] Katika ibara ya: «وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ» ; Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, inaamrishwa wanawake washushe shungi zao juu ya vifua vyao ili nywele, masikio na shingo zao zisionekane.[10] Tafsir Nur al-Thaqalayn inanukuu hadithi kutoka kwa Imam Muhammad Baqir katika kutafsirii Aya hii: «وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا» yaani "wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika: Kumetambulishwa mapambo matatu:
- Uzuri na mapambao ya watu: Kama wanja, pete, bangili na hina ambayo hupakwa katika kiganja cha mkono.
- Uzuri na mapambo kwa ajili ya maharimu: Cheni ya shingoni, mapambo ya sura na mapambo ya mikono.
- Mapambo kwa ajili ya mume: Mapambano hay ni ya mwili wote. [11]
Vazi la Jilbab
- Makala Asili: Aya ya Jilbab
Aya ya Jilbab ni Aya ya 59 ya Surat al-Ahzab[12]. Aya hii inawataka wanawake wajiteremshie Jilbab zao ili wasiudhiwe na wanaume.[13] Katika Aya hii limetumika neno “Jalabib” ambalo ni wingi wa Jilbab. Jilbab inaelezwa na wataalamu wa lugha kuwa maana yake ni nguo ambayo ni kubwa zaidi kuliko mtandio (kitambaa cha kichwa). Kwa hakika, Jilbab ni vazi ambalo ni kubwa zaidi ya mtandio na dogo kuliko juba na joho na huvaliwa na wanawake na hufunika kuanzia kichwani mpaka katika vifua vyao.[14]
Rejea
- ↑ Tazama: Markaz farhangi va Ma'rifa Al-Qur'an, Dar Ma'rifa Al-Qur'an karim, juz. 1, uk. 381, 1382 S; Jam'i az Muhaqiqin, Farhang nameh Ulum Al-Qur'an, uk. 129, 1394 S.
- ↑ Sa'idi, «Hijab (1)» uk. 604
- ↑ Tazama: Khui, Mawsu'at al-Imam al-Khui, juz. 32, uk. 36-47, 1418 H; Hilli, Tadhkirat al-fuqaha', juz. 2, uk. 446-447.
- ↑ Khui, Mawsu'at al-Imam al-Khui, juz. 32, uk. 36, 1418 H.
- ↑ Sheikh Ansari, Kitab al-nikah, uk. 46-47, 1415 H; Shahid al-Thani, Masalik, juz. 7, uk. 47, 1413 H; Hilli, Tadhkirat al-fuqaha, juz. 2, uk. 446-447.
- ↑ Ibn Abi l-Hatam, Tafsir al-Qurʾan al-ʿadhim, juz. 8, uk. 2573, 1419 H.
- ↑ Tabrisi, Majma' al-bayan, juz. 7, uk. 217, 1372 S.
- ↑ Tabrisi, Majma' al-bayan, juz. 7, uk. 217, 1372 S; Tabatabai, al-Mizan, juz. 15, uk. 111, 1417 H.
- ↑ Tabrisi, Majma' al-bayan, juz. 7, uk. 217, 1372 S; Tabatabai, al-Mizan, juz. 15, uk. 111, 1417 H.
- ↑ Tabrisi, Majma' al-bayan, juz. 7, uk. 217, 1372 S.
- ↑ Huizi, Tafsir al-nur al-thaqalain, juz. 3, uk. 529, 1415 H.
- ↑ Jami' az Muhaqiqina, Farhangnama-yi ulum Qur'ani, uk. 126, 1394 S.
- ↑ Tabatabai, Al-Mizan, juz. 16, uk. 339, 1417 H; Tabrisi, Majma' al-bayan, juz. 8, uk. 581.
- ↑ Turahi, Majma' al-bahrayn, juz. 2, uk. 24, 1375 S.
Vyanzo
- Ibnu Abi Hatim, Abdurrahman bin Muhammad. Tafsir al-Qur'an al-'Adhim. Tahqiq: As'ad Muhammad al-Tib. Arab Sa'udi: Maktabah Nizar Mustafa al-Baz, juz. 3, 1419 H.
- Jami' az muhaqiqin. Farhang Ulum Qur'ani. Qom: Pazuheshgah 'Ulum wa Farhang-e Islami, 1394 S.
- Hur 'Amili, Muhammad bin al-Hassan. Wasa'il al-Shiah ila Tahsil al-Shari'ah. Tahqiq: Muhammad Ridha Husseini Jalali. Qom: Muasasah Ali al-Bait Li Ihya' al-Turath, 1416 H.
- Huizi, 'Abd 'Ali bin Jum'a, Tafsir al-nur al-thaqalain, Qom: Nashr 'Ismailiyan, juz. 4, 1415 H.
- Sa'idi, Faride. «Hijab» dar daneshname jahan islami. Tehran: Bunyad Dairah al-Ma'arif Islami, 1387 S.
- Shahid Thani, Zain al-Din bin Ali. Masalik al-Afham ila Tanqih Shari'ah al-Islami. Tahqiq va Tas-hih: Pazuhesh Muasasah Ma'arif Islami. Qom: Muasasah al-Ma'arif al-Islamiyah, juz. 1 1413 H.
- Sheikh Ansari, Murtadha. Kitab al-Nikah Qom: Konfrensi jahan buzurge dosht Sheikh A'dham Ansari, 1415.
- Tabatabai, Sayid Muhammad Hussein, Al-Mizan fi Tafsir Al-Qur'an, Qom: Daftar intesharat Islami, Juz. 5, 1417 H.
- Tabarsi, Fadhl bin Hasan. Majma' al-Bayan fi Tafsir al-Quran. Tehran: Nasir Khusru, juz. 3, 1372 S.
- Tarihi, Fakhr al-Din. Majma' al-Bahrain. Tahqiq: Sayyid Ahmad Husseini, Tehran: Kitab Furushi Murtadhawi, 1375 S.
- Alamah Hilli, Hassan bin Yusuf. Tadhkirah al-Fuqaha. Tahqiq va Tas-hih: Guruh Pazuhesh Muasasah Ali al-Bait. Qom: Muasasah Aali al-Bait. juz. 1, 1414 H.
- Markaz Farhang wa Ma'arif Qur'an. Dairah al-Ma'arif Qur'an Karim. Qom: Bustan Kitab, 1382 S.