Aya ya 139 ya Suratu ya Aal-Imran
![]() | |
Sura Husika | Surat ya al-Imran |
---|---|
Namba ya Aya | 139 |
Juzuu | 4 |
Mahali pa Kushuka | Madina |
Maudhui | Itikadi |
Mada Yake | Ahadi ya ushindi kwa waumini. |
Aya Zinazofungamana Nayo | Aya ya 35 ya Surat Muhammad |
Aya ya 139 ya Surat ya Al-Imran (Kiarabu: الآية 139 من سورة آل عمران) ni Aya iliyobeba ujumbe wa matumaini kwa waumini wa mwenye Ezi Mungu. Nayo ni Aya yenye kuwaahidi waumini ya kwamba; mwishowe wao ndiwo watakaokuwa washindi dhidi ya wapinzani wao. Zaidi ya hayo, lililo muhimu zaidi katika Aya hii, ni utumiaji wake wa lugha njema ya kuwatia moyo waumini hao, na kuwataka wasikate tamaa na waendelee kuwa imara, popote pale wanapokabiliwa na upinzani fulani dhidi yao.[1]
وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنْتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ
Wala msilegee katika mapambano yenu, wala msihuzunike (msihuzunishwe na yaliyopita), kwani nyinyi ndiwo mlio juu (washindi), ikiwa nyinyi ni waumini.
(Qu'ran: 3: 139)
Maelezo ya kihistoria yanaonesha kuwa Aya hii ilishuka katika wakati mgumu mno. Inaanza kwa kuwakutaka Waislamu wasikate tamaa au kuhuzunika kwa sababu tu walipata pigo fulani vitani.[2] Mchambuzi (mfasiri) mashuhuri wa upande wa madhehebu ya Shia wa karne ya sita Hijria, ajulikanaye kwa jina la Fadhlu bin Hassan al-Tabarsi, akifasiri Aya ya 139 ya Surat Al-Imran katika tafsiri yake iitwayo Majma’u Al-Bayan, anasema; Aya hii ilikuwa ni ujumbe wa faraja na matumaini kwa Waislamu, uliowajia baada ya vita vya Uhud, vita ambavyo viliwaacha na majeraha na simanzi ya kuwapoteza wenzao kadhaa vitani humo.[3] Mfasiri huyu akiendelea na uchambuzi wake, ananukuu ripoti isemayo kwamba; Aya hii iliteremshwa huko Hamra al-Asad, wakati Mtume (s.a.w.w) alipoongozana na kikosi cha askari wake waliojeruhiwa ili kukabiliana na tishio kutoka Makka amabalo lilitarajiwa kuuvamia tena mji wa Madina.[4] Kwa ufupi, Aya hii inatafsiriwa kama wito wenye nguvu unaowataka waumini wasimame imara na kutetea imani yao mbele ya upinzani kutoka kwa wale wasioamini Mungu mmoja (washirikina).[5]
Ufafanuzi wa Aya hii umepitia mabadiliko kadhaa ya kimuktadha, kama inavyodhihirika katika kazi za wanazuoni wakuu mbali mbali. Mwanafalsafa na mfasiri wa Qur’ani, Sayyid Muhammad Hussein Tabataba'i, akitafsiri neno (تَهِنُوا) lenye maana ya ulegevu uliokatazwa na Mwenye Ezi Mungu, anasema; Ulegevu na udhaifu uliokatazwa hapa, sio ulegevu wa kijeshi peke yake, bali lilikusudiwa hapa, ni ule mmomonyoko wa azma ya jihadi pamoja na kutojali umuhimu wa kuimarisha dini.[6] Ama kuhusiana na uchambuzi wa kifafanuzi juu ya semi usemao (وَأَنْتُمُ الْأَعْلَوْنَ) Nanyi ndio bora, usemi huu umeelekeza kwenye hitimisho lisemalo kwamba; hii ni kauli ya kitheolojia yenye lengo la kujenga taswira ya ushindi usioepukika kwa waumini, na kwamba inagawaje safari inaweza kuwa ni ngumu, lakini hatimaye, wale walio na imani ndio watakaosherehekea ushindi.[7] Katika mchango wake wa kifafanuzi, Muhammad Jawad Mughniyyah anatumia mbinu ya uhusiano-matini (intertextuality) ulipo baina ya na Hadithi za Mtume (s.a.w.w), ili kuipa Aya uzito wa ziada. Katika uchambezi wake juu ya Aya hii, Mughniyyah anarejelea Hadithi mashuhuri ya al-I'tila (Ukuu au Utukufu wa Waislamu). Kwa mujibu wa Hadithi hiyo, Uislamu utabaki kuwa ndiyo umfumo wa juu zaidi usioweza kupikuliwa au kupinduliwa na mfumo mwengine wowote ule dhidi yake.[8] Aidha, dhana ya imani ndani ya kifungu kisemacho; «إِنْ کنْتُمْ مُؤْمِنینَ» "ikiwa nyinyi ni waumini", imefafasiriwa kwa maana ya kumtegemea Mungu na kuamini ahadi Zake.[9] Pia Ayatollah Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliisoma Aya hii ya 139 katika hotuba yake kwa taifa la Iran, kufuatia shambulizi la kijeshi la Israeli dhidi ya Iran, pamoja na utekelezaji wa mauaji ya maafisa wakuu kadhaa wa jeshi la nchi hiyo.[10] Baada ya yeye kuisoma Aya hii, aliendelea akisema kwamba; Kwa mujibu wa Aya hii, yeye anaamini kwamba, endapo waumini watatimiza masharti ya imani, basi katu hasimu wao hatakuwa na mamlaka ya kutekeleza jambo lolote katika uwanja halisi wa mapambano.[11]
Kadhalika, Mwanazuoni Sayyid Muhammad Taqi al-Modarresi, katika tafsiri yake ya Aya hii tukufu, anagusia Sunna ya Mwenye Ezi Mungu (utaratibu wa Mwenyezi Mungu). Kwa msingi wa Sunna au desturi hiyo, ushindi na nusura havipatikani kwa njia ya sadfa wala bila ya kujitolea, bali vinahitaji maandalizi maalumu pamoja na kustahimili mitihani na mashaka mbali mbali; kwani adui naye amejiandaa vya kutosha kwa ajili ya mapambano.[12]
Pia Aya ya 35 ya Surat Muhammad, ni yenye kuwasilisha dhana inayofanana na ile ya Aya ya 139 ya Surat Al-Imran. Aya hii ya 35 imekuja na malezo yasemayo: "Hivyo basi, msilegee na kuitisha suluhu, kwani nyinyi ndiwo mlio juu, na Mungu yu pamoja nanyi, Nayue kamwe hatapunguza (hatakupunjeni) thamani ya amali zenu".
Rejea
- ↑ Tayyib, Atib al-Bayan, 1378 S, juz. 3, uk. 366.
- ↑ Makarim Shirazi, Tafsir Nemune, 1374 S, juz. 3, uk. 108.
- ↑ Tabrasi, Majma al-Bayan, 1372 S, juz. 2, uk. 843.
- ↑ Tabrasi, Majma al-Bayan, 1372 S, juz. 2, uk. 843.
- ↑ Tha'labi Niyshaburi, Al-Kashf wa al-Bayan, 1422 AH, juz. 3, uk. 172.
- ↑ Tabataba'i, Al-Mizan, 1417 AH, juz. 4, uk. 26-27.
- ↑ Fakhru Razi, Mafatih al-Ghayb, 1420 AH, juz. 9, uk. 371.
- ↑ Mughniyah, Tafsir al-Kashif, 1424 AH, juz. 2, uk. 163.
- ↑ Tabrasi, Majma al-Bayan, 1372 S, juz. 2, uk. 843.
- ↑ «Dovomin Payam Televisioni Ayatullah Khamenei Khitab Be Milat Iran Dar Pi Tahajum Rizhim Suhyuni.», Tovuti Rasmi ya Ayatullah Khamenei.
- ↑ «Bayanat Dar Didor Mas-ulan Nidham», Tovuti Rasmi ya Ayatullah Khamenei.
- ↑ Mudarisi, Min Huda al-Qur'an, 1419 AH, juz. 1, uk. 666.
Vyanzo
- «Bayanat Dar Didor Mas-ulan Nidham», Tovuti Rasmi ya Ayatullah Khamenei, Tarikh Darj Matlab: 16 Tir 1393 S, Tarikh Bozdad: 1 Tir 1404 S.
- Tha'labi Niyshaburi, Ahmad ibn Ibrahim, Al-Kashf wa Al-Bayan An Tafsiri al-Qur'an, Beirut, Dar Ihya' Al-Turaht Al-Arabi, Chapa ya kwanza, 1422 AH.
- «Dovomin Payam Televisioni Ayatullah Khamenei Khitab Be Milat Iran Dar Pi Tahajum Rizhim Suhyuni.», Tovuti Rasmi ya Ayatullah Khamenei, Tarikh Darj Matlab: 28 Khordad 1404 S, Tarikh Bozdad: 1 Tir 1404 S.
- Taliqani, Sayyid Mahmoud, Partwi Az Qur’an, Tehran, Sharikat Sahami Intishar, Chapa ya Nne, 1362 AH.
- Tabataba’i, Sayyid Muhammad Hussein, Al-Mizan Fi Tafsir al-Qur’an, Qom, Daftar Intisharat Islami, Chapa ya Tano, 1417 AH.
- Tabrasi, Fadhlu ibn Hassan, Tafsir Jawami’ al-Jami’i, Tehran, Intisharat Daneshghah Tehran, Mudiriyat Hawze Ilmiye Qom, Chapa ya Kwanza, 1377 AH.
- Tabrasi, Fadhlu ibn Hassan, Majma’ al-Bayan Fi Tafsir al-Qur’an, Muqadimat Muhammad Jawad Balaghi, Tehran, Nasser Khusruw, Chapa ya Tatu, 1372 AH.
- Tayyib, Sayyid Abdul Hussein, Atib al-Bayan Fi Tafsir al-Qur’an, Tehran, Intisharat Islami, Chapa ya Pili, 1378 AH.
- Fakhr Razi, Muhammad ibn Omar, Mafatih al-Ghayb, Beirut, Dar Ihya’a al-Turath al-Arab, Chapa ya Tatu, 1420 AH.
- Mudarrisi, Sayyid Muhammad Taqi, Min Huda al-Qur’an, Tehran, Dar Mahabba al-Hussein, Chapa ya Kwanza, 1419 AH.
- Mughniyeh, Muhammad Jawad, Tafsir al-Kashif, Tehran, Dar al-Kutub al-Islamiyyah, Chapa ya Kwanza, 1424 AH. Makarim Shirazi, Nasser, Tafsir Nemune, Tehran, Dar al-Kutub al-Islamiyyah, Chapa ya Kwanza, 1374 AH.