Vita vya Hamra al-Asad (Kiarabu: غزوة حمراء الأسد) ni miongoni mwa Ghazwa za Mtume (s.a.w.w) (vita ambavyo Mtume alishiriki). Vita hivi vilitokea mwaka wa 3 Hijria na siku moja baada ya Vita vya Uhud. Inaelezwa kuwa, wakati Mtume (s.a.w.w) alipofahamu nia ya Washirikina wa Makka ya kutaka kushambulia tena mji wa Madina baada ya Vita vya Uhud, alitoa amri ya kufuatiliwa maadui. Katika vita hivi kwa amri ya Mtume nyakati za usiku kila Muislamu alikuwa akiwasha moto ili kuonyesha kwamba, idadi ya jeshi la Waislamu ni kubwa na hivyo kuzusha wasiwasi miongoni mwa maadui. Kitendo hiki kilipelekea kukimbia wanajeshi wa Makka na baada ya siku tatu Mtume alirejea Madina.

Vita vya Hamra al-Asad

Wafasiri wa Qur'ani tukufu wanasema kuwa, Aya ya 140, 172 mpaka 174 ya Surat al-Imran na vilevile Aya ya 104 ya Surat al-Nisaa zimeshuka kuhusiana na vita hivi.

Sababu ya Kutokea Kwake

Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria, wakati wa kutokea Vita vya Hamra al-Asad ilikuwa katika mwaka wa tatu wa Hijria,[1] na siku moja baada ya vita vya Uhud.[2] Sababu ya vita hivi kuitwa kwa jina la Vita vya Hamra al-Asad ni kwa sababu vilitokea katika eneo lenye jina hilo, ambalo lilikuwa maili nane (kilomita ishirini) kutoka Madina.[3] Imekuja katika vyanzo vya kihistoria kwamba, siku moja baada ya kushindwa Waislamu katika Vita vya Uhud, Mtume (s.a.w.w) alifahamishwa kwamba washirikina wa Makka walikuwa wanapanga kuishambulia tena Madina.[4] Kwa mujibu wa kile kilichokuja katika Tafsir Qummi ni kwamba: Malaika Jibril alimjuza Mtume kuhusiana na lengo na nia ya Makureshi ya kuushambulia tena mji wa Madina.[5] Kuna nadharia mbili kuhusiana na akina nani walishiriki katika vita hivi. Kwa mujibu wa Tafsir Qummi, Malaika Jibril alimfahamisha Mtume (s.a.w.w) kwamba wale tu waliojeruhiwa katika vita vya Uhud ndio wana haki ya kushiriki katika vita hivi.[6] Imeelezwa katika kitabu cha A'yan al-Shia kwamba, kwa amri ya Mtume (s.a.w.w), Bilal alitangaza baada ya Sala ya asubuhi kwamba, wale walioshiriki katika vita vya Uhud waanze harakati ya kushiriki katika vita hivi na kuwafuata maadui.[7] Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria, harakati ya Mtume (s.a.w.w) kuelekea upande wa washirikina wa Makka ilikusudiwa kuleta hofu miongoni mwa maadui na kuwafahamisha washirikina kwamba Waislamu bado wana nguvu.[8]

Matukio ya Vita

Kwa mujibu wa ripoti ya Waqidi katika kitabu cha al-Maghazi, Mtume (s.a.w.w) alipoamuru kusonga mbele kuelekea eneo la Hamra al-Asad, majeruhi waliokuwa wakitibiwa pia walikuwa tayari kuelekea huko.[9] Inaelezwa kuwa, kulikuwa na watu 40 kutoka katika kabila la Bani Salama waliokuwa wamejeruhiwa ambao walishiriki katika vita hivi[10] na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Mtume akawaombea dua.[11]

Kwa mujibu wa vitabu vya kihistoria, Mtume (s.a.w.w) alimteua Ibn Umm Maktum kuwa mrithi wake huko Madina[12] na licha ya majeraha mengi aliyokuwa nayo kutokana na vita vya Uhud, Mtuume alikwenda pamoja na Waislamu kushiriki katika vita hivyo. [13] Imekuja katika kitabu cha Qasas al-Anbiya cha Qutbuddin Ravandi kwamba, Mtume (s.a.w.w) alimpa Imam Ali (a.s) bendera ya Muhajirina na akamtanguliza mbele ya jeshi mpaka kufika Hamra al-Asad.[14]

Kwa mujibu wa Waqidi, katika vita hivi Mtume (s.a.w.w) alimuahidi Talha ushindi wa vita vyote hii na kwamba Mwenyezi Mungu atatufungulia Makka.[15] Inanukuliwa kwamba, Saad Ibn Ubadah alileta mizigo 30 ya tende iliyobebewa na ngamia. Aidha alileta ngamia kadhaa ambapo alikuwa akichinja ngamia wawili hadi watatu kwa siku.[16]

Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo vya kihistoria, Mtume (s.a.w.w) alituma watu watatu kupata taarifa kutoka katika kambi ya adui; lakini wawili kati yao walitekwa na Maquraishi na kuuawa shahidi[17] na Waislamu wakawazika wote wawili katika kaburi moja.[18]

Kuzusha Woga Katika Kambi ya Mushirikina

Kwa mujibu wa wanahistoria wengi, jeshi la Uislamu lilipofika eneo la Hamra al-Asad, Mtume (s.a.w.w) aliwaamuru Waislamu kukusanya kuni na inapofika usiku, kila mtu anapaswa kuchoma kuni zake. Kuwashwa kwa mioto mia tano usiku na kuonyesha nguvu ya hali ya juu ya Waislamu kulisababisha hofu kubwa katika kambi ya washirikina[19]. Washirikina wa Makka walipofika eneo la Rauha na wakiwa katika kupanga kushambulia tena, walikutana na mtu mmoja aitwaye Ma'bad.[20] Wakamuuliza Ma'bad kuhusu habari za jeshi la Waislamu, naye akazungumza kuhusu Waislamu kufanya njama ya kulipiza kisasi, na kwa kusoma mashairi yaliyoashiria nguvu ya jeshi la Kiislamu, kuliibuka hofu katika moyo wa Abu Sufyan na kumfanya abadilishe uamuzi na kuacha kuishambulia tena Madina.[21] Kwa mujibu wa Ravandi, Ma'bad alipokutana na Abu Sufyan katika eneo la Rauha alisema: “Ewe Abu Sufyan, huyu ni Ali ambaye amekuja mbele ya jeshi”, na maelezo haya yalimfanya Abu Sufyan aache nia yake ya kushambulia.[22]

Katika baadhi ya vyanzo, imeelezwa kwamba baada ya washirikina wa Makka kuacha kupigana na Waislamu, walimtuma Ma'bad mtu kutoka kabila la Khuza'a aende kwa Mtume (s.a.w.w) na kutuma ujumbe kwamba Abu Sufyan na masahaba zake walikimbilia Makka.[23] Kwa mujibu wa nukuu ya Tafsir Qummi, baada ya washirikina kukimbia, Jibril alimteremkia Mtume (s.a.w.w) na akamwamrisha arejee Madina na kusema: Mwenyezi Mungu ameweka khofu katika nyoyo za Makureshi na wakaondoka.[24]

Imekuja katika kitabu cha Tarikh Tabari kwamba, Abu Sufyan, baada ya kuacha vita, alituma ujumbe kwa Mtume (s.a.w.w) kupitia kundi lililokuwa likienda Madina kwamba tumeamua kurejea kwako popote pale ulipo. Kisha akafunga safari kuelekea Makka. Mtume (s.a.w.w) na Waislamu waliposikia ujumbe wa Abu Sufyan, walisema: Hasbuna Allah wa Ni’ma al-Wakil (Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa).[25] Kwa mujibu wa Tabari, vita hivi vilidumu kwa muda wa siku tatu.[26]

Kushuka Aya Kuhusu Vita vya Hamra al-Asad

Imekuja katika vyanzo kadhaa vya tafsiri na historia kwamba, Aya ya 172 hadi 174 ya Surat al-Imran zimeshuka kuhusiana na vita hivi.[27] Villevile imeelezwa kuwa, Aya ya 140 ya Surat al-Imran na Aya ya 104 ya Surat al-Nisaa zimeshuka kuhusiana na vita hivi.[28]

Rejea

Vyanzo