Amin (Lakabu)

Kutoka wikishia
Faili:مسجد النبی (مدینه).jpg
Makala hii inahusiana na lakabu ya Amin (mwaminifu). Ili kujua kuhusiana na maisha na shakhsia ya Mtume (s.a.w.w) angalia makala ya Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Amin (Kiarabu: الأمين (لقب)) ni moja ya lakabu za Bwana Mtume (s.a.w.w) ambayo alikuwa akiitwa nayo kwa miaka mingi kabla ya kubaathiwa na kupewa Utume. Amin ni mtu mwaminifu na anayeaminiwa ambaye watu wengine wanasimilika na kutofanya kwake khiyana na usaliti. Moja ya sifa maalumu za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) ambayo ilikuwa ikipelekea aitwe amin yaani mwaminifu ni utunzaji wake wa amana. Katika hadithi za Maimamu watoharifu (a.s) kumesisitizwa juu ya kuwa kwake mwaminifu na katika visomo vya ziyara mbalimbali anatajwa kwa ibara ya: السَّلَامُ عَلَى أَمِينِ اللَّهِ عَلَى رُسُلِه)‏ ; Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya mwaminifu wa Allah kwa Mitume wake).

Maana na Daraja

Amin ni moja ya lakabu za Bwana Mtume (s.a.w.w) ambayo alikuwa akiitwa nayo kwa miaka mingi kabla ya kubaathiwa na kupewa Utume. [1] Amin ni mtu mwaminifu na anayeaminiwa ambaye watu wengine wanasimilika na kutofanya kwake khiyana na usaliti. [2] Ibn Sa’d, mwanahistoria wa karne ya tatu Hijiria anasema katika kitabu chake cha al-Tabaqat al-Kubra: “Kutokana na kuwa sifa njema za Mtume (s.a.w.w) zilikuwa zimefikia ukamilifu huko Makka hakuwa na jina lingine isipokuwa Amin.” [3] Kwa mujibu wa ripoti iliyokuja katika kitabu cha Tarikh Tabari (kilichoandikwa 303 Hijria) ni kwamba, makureshi walikuwa wakimuita Mtume kwa jina la Amin hata kabla ya kushushiwa Wahyi. [4]

Vile vile imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba, washirikina wa Kikureshi walikuwa wakimwita Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) Amin na walikuwa wakijua kwamba, kamwe yeye hasemi uwongo, lakini walimkadhibisha na kukataa ujumbe aliokuja nao kutoka kwa Mwenyezi Mungu. [5] Maadui wa Mtume (s.a.w.w) pia walikuwa wakikiri juu ya uaminifu wa Mtume na kuna visa vilivyonukuliwa katika historia vya kukiri kwa Abu Jahl juu ya suala hili. [6] Katika ripoti hizi, sababu ya wao kumkanusha Mtume (s.a.w.w) sio kwa sababu hawakuwa wakiamini maneno ya Mtume, la hasha, bali ni kwa sababu ya ushindani wa kifamilia na kikabila ambao ndio ulisababisha kukanusha utume wa Mtume (s.a.w.w). [7]

Muhammad Amin na Amin ni miongoni mwa majina ambayo Waislamu huwapatia watoto wao. Amin ni miongoni mwa majina 100 ya juu ya Wairani baina ya mwaka miaka 1297-1380 Hijiria Shamsia. [8]

Kutunza Amana za Watu

Moja ya sifa za Mtume (s.a.w.w) zilizomfanya ajulikane kama Amin ni uaminifu na utunzaji wake wa amana. [9] Kuna riwaya nyingi zilizonukuliwa katika vyanzo vya historia zinazoelezea uaminifu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w). Miongoni mwa mwazo ni pale, Mtume (s.a.w.w) alipofanya biashara kwa mtaji wa Bibi Khadija (a.s) na kurejea kwa mafanikio kutoka katika safari ya hiyo ya kibiashara ambapo, Bibi Khadija (a.s) alimwambia: “Ewe binamu; Najivunia baina ya kaumu yangu kutokana na nasaba yenye heshima, ukuruba, ukweli, tabia njema na uaminifu wako.” Ni baada ya hapo ambapo Bibi Khadija akatoa pendekezo la ndoa na Mtume. [10]

Pia, watu walikuwa wakikabidhi amana zao kwa Mtume. Wakati Mtume (s.a.w.w) alipoamua kuhamia Madina. Alimtaka Imam Ali (a.s) kuhama kutoka Makka kwenda Madina pale tu atakaporudisha amana ambazo watu walikuwa wameziacha kwa Mtume (s.a.w.w) kwa wamiliki wao. [11] Kwa maana kwamba, aungane na Mtume Madina baada ya kukamilisha kazi aliyopatiwa na Mtume ya kukabidhi na kurejesha amana za watu zilizokuwa kwa mbora huyo wa viumbe. Imeelezwa pia katika riwaya kwamba, Waislamu walikumbwa na upungufu na uhaba wa chakula wakati wa Vita vya Khaybar. Katika hali hii, mchungaji mmoja aliyekuwa akiwachungia Mayahudi alikuja kwa Mtume na baada ya kuzungumza naye, alisilimu na kumwambia Mtume (s.a.w.w) kwamba “kondoo wa Mayahudi nimekabidhiwa mimi na wapo kwangu kama amana, na sasa mimi nimekuwa Muislamu, jukumu langu ni nini?” Licha ya Waislamu kuhitaji chakula, Mtume (s.a.w.w) lakini alimtaka mchungaji huyo awakabidhi Mayahudi kondoo zao. [12]

Amin wa Wahyi

Utume wa Mtume (s.a.w.w) unaonyesha kuwa yeye ni mwaminifu, kwa sababu unabii ni amana ya Mwenyezi Mungu na inapasa kukabidhiwa kwa mtu mwaminifu. [13] Imepokewa kutoka kwa Imam Ali (a.s): “Mwenyezi Mungu alimtuma Mtume Muhammad (s.a.w.w) ili awe muonyaji kwa walimwengu na Amin (mwaminifu) wa Wahyi. [14] Katika kitabu cha Tafsir Qomi, neno "Amin" katika Aya: ([[Arabic|مُطَاعٍ ثَمَّ أَمِينٍ}}) yaani Anayetiiwa tena muaminifu limefasiriwa kuwa kwa maana ya amana ya Mtume na imepokewa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) kuhusu Aya hii kwamba maana yake ni “amri ina taathira kwa Mola Mlezi na Siku ya Kiyama.”[15] Kadhalika katika baadhi ya Ziyara zilizopokewa kutoka kwa Maimamu (as), Mtume (s.a.w.w) anatajwa kwa ibara ya: (السَّلَامُ عَلَى أَمِينِ اللَّهِ عَلَى رُسُلِه‏ ; Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya mwaminifu wa Allah kwa Mitume wake). [16]

Zimenukuliwa beti za mashairi kutoka kwa Abu Talib ami yake Mtume (s.a.w.w) ambazo ndani yake anamhutubu Mtume kuwa ni Aminullah (Mwaminifu wa Mwenyezi Mungu).

ٲنْتَ الأَمِينُ ٲَمِينُ اللهِ لَاكَذِبُ *** وَالصَّادِقُ الْقَوْلِ لَالَهْوٌ و َلا لَعِبُ


Wewe ni mwaminifu, mwaminifu wa Mwenyezi Mungu ambaye hajawahi kusema uwongo, na wewe [mtu] mkweli ambaye hajawahi kukujihusisha na mambo yasiyo na maana. [17]


Rejea

Vyanzo

  • Dihkhuda, ʿAlī Akbar. Lughatnāma. Tehran: Dānishgāh-i Tehran, 1377 Sh.
  • Faraj Allāhī, Faraj Allāh. "Amānatdārī-yi Payāmbar-i (s) raḥmat". Darshāyī az maktab-i Islām, no. 673, 1396.
  • Ibn Hishām, ʿAbd al-Malik b. Ayyūb. Al-Sīrat al-nabawīyya. Beirut: Dār al-Maʿrifa, nd.
  • Ibn Qūlawayh, Jaʿfar b. Muḥammad. Kāmil al-zīyārāt. Najaf: Dār al-Murtaḍawīyya, 1356 Sh.
  • Ibn Saʿd, Muḥammad. Al-Ṭabaqāt al-kubrā. Beirut: Dār Ṣadir, nd.
  • Ibn Shahrāshūb, Muḥammad b. ʿAlī. Manāqib Āl Abī Ṭālib. Qom: ʿAllāma, 1379 Sh.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad. Al-Irshād fī maʿfirat ḥujaj Allāh ʿala l-ʿibād. Qom: Kungira-yi Shaykh Mufīd, 1413 AH.
  • Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm. Tafsīr al-Qummī. Qom: Dār al-Kitāb, 1367 Sh.
  • Sharīf al-Raḍī, Muḥammad b. Ḥusayn. Nahj al-balāgha. Ed. Ṣubḥī Ṣāliḥ. Qom: Hijrat, 1414 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr. Ṭārīkh Ṭabarī. Beirut: Dār al-Turāth, 1387 AH.
  • Zamakhsharī, Maḥmūd. Al-Kashshāf ʿan haqāʾiq ghawāmiḍ al-tanzīl. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿArabī, 1407 AH.