Abu Jahl

Kutoka wikishia

Amr bin Hishām bin Mughīra al-Makhzūmi mashuhuri kwa jina la Abu Jahl (aliaga dunia mwaka wa 2 Hijiria) alikuwa mmoja wa wapinzani wa Mtume (s.a.w.w) na Uislamu katika mji wa Makka . Kupanga njama za kumuua Mtume (s.a.w.w), kuwatesa na kuwatisha watu waliokuwa wakisilimu na ambao ni wageni katika Uislamu, kuwazuia watu wasisikilize Aya za Qur'an, kumtusi na kumvunjia heshima Bwana Mtume (s.a.w.w), kufanya njama za kukatwa uhusiano wa Quraishi na Bani Hashim na kuandaa mazingira ya kutokea vita vya Badr ni miongoni mwa mambo yaliyofanywa na Abu Jahl dhidi ya Uislamu na Waislamu. Wafasiri wamemzungumzia Abu Jahl takriban katika Aya 30 wakati wakitoa maelezo na tafsiri. Kwa maana kwamba, kuna Aya zisizopungua 30 ambazo zimemzungumzia adui huyu wa Mtume na Uislamu.

Abu Jahl alikuwa na nafasi na mchango mkubwa na wa asili wa kutokea vita vya Badr na aliuawa katika vita hivyo hivyo akiwa katika jeshi la washirikina.


Nasaba, kuniya na lakabu

Amr bin Hisham bin Mughira au Abu Jahl kama anavyojulikana zaidi alikuwa miongoni mwa wapinzani wa Mtume na daima alikuwa akimfanyia uadui Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu. [1] Baba yake ni Hisham bin Mughira anayetokana na kabila la Bani Makhzum na maqureshi walifanya kifo chake kuwa mwanzo wa kalenda yao. [2] Mama yake ni Asma' binti Mukhriba bin al-Jandal al-Handhali kutoka kabila la Bani Tamim. [3] Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana alikuwa akifahamika pia kama Handhaliya. [4]

Kuniya ya Abu Jahl ilikuwa Abul-Hakam lakini alimuita kwa kuniya ya Abu Jahl. [5] Sababu ya kupewa jina hili imetajwa kuwa ni ujahili na ujinga aliokuwa nao pamoja na uadui wake dhidi ya Uislamu. [6] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (saww) ni kwamba, Firauni wa umma wa Kiislamu ni Abu Jahl. [7] Kwa mujibu wa ripoti ya Waqidi katika kitabu cha Maghazi ni kuwa, kabla ya kuanza vita vya Badr, baada ya kuswali Swala ya Suna aliwalaani namna hii makafiri akiwemo Abu Jahl: ((أَللّهُمَّ لَايُفْلِتَنَّ فِرْعَوْنُ هذِهِ الاُمَّةِ أَبُوجَهْلُ بْنُ هِشَامٍ ; Ewe Mola! Nakuomba Firauni wa umma huu, Abu Jahl bin Hisham asifanikiwe kukimbia)). Haukupita muda, Abuu Jahl akauawa na jeshi la Waislamu. [8]

Ikrima bin Abi Jahl, mtoto wa Abu Jahl ambaye alikuwa akimfanyia uadui Mtume (saww), baada ya kukombolewa Makka aliachana na ukafiri na kusilimu. [9]

Upinzani dhidi ya Uislamu

Abu Jahl alikuwa akimfanyia uadui Mtume Muhammad (saww) na alikuwa akimtusi Mtume kwa mbinu na njia mbalimbali [10] na akimvunjia heshima. [11] Kadhalika sababu ya kushuka baadhi ya Aya zimetambuliwa kuwa ni kutokana na mwenendo wa Abu Jahl pamoja na upinzani wake dhidi ya Uislamu na Mtume wa Allah. [12] Katika Dairat al-Maarif (tabu kubwa la maarifa yaani insaiklopidia kumetajwa Aya 32 ambazo wafasiri wamezitambua kuwa, zinamhusu Abu Jahl. [13] Abu Jahl alichukua hatua na kufanya mambo mbalimbali ili kuzuia kuenea na kupata nguvu Uislamu ambapo baadhi ya hatua hizo ni:

Kuzuia watu wasisikilize Aya za Qur'an

Muhammad ibn Ahmad Qurtubi anasema katika tafsiri ya Aya ya: ((وَ قَالَ الَّذِینَ کَفَرُواْ لَا تَسْمَعُواْ لهَذَا الْقُرْءَانِ وَ الْغَوْاْ فِیهِ لَعَلَّکمُ‌ْ تَغْلِبُون‌ ; Na walio kufuru walisema: Msiisikilize Qur'an hii, na timueni zogo, huenda mkashinda)) [14] ya kwamba imenukuliwa kutoka kwa Ibn Abbas akisema kuwa, kila mara Mtume alipokuwa akisoma Qur'an, Abu Jahl alikuwa akisema, timueni zogo ili watu wasifahamu na kuelewa anachokisema. [15]

Mpangaji wa mkakati wa kuuawa Mtume

Kwa mujibu wa nukuu ya Abdul Malik ibn Hisham ni kwamba, washirikina wa Makka walikusanyika Dar al-Nadwa kwa ajili ya kuchukua uamuzi kuhusiana na namna ya kukabiliana na Mtume (s.a.w.w) ambapo kila mmoja alitoa pendekezo lake. Abu Jahl alitoa pendekezo lake kwa kusema: Tumuue Mtume, lakini mauaji yake yanapaswa kuyashirikisha makabila yote, ili Bani Hashim wasiweze kupigana vita na makabila yote kwa ajili ya kulipiza kisasi na hivyo kulazimika kukubali dia. Hatimaye pendekezo lake hilo lilikubaliwa na kwa msingi huo wakakubaliana kutekeleza mpango wao usiku na kila kabila litoe mtu mmoja. Abu Jahl alikuwa miongoni mwa hadhirina na alikuwa akiwashajiisha walioteuliwa kutekeleza mpango huo. Hata hivyo kuondoka Mtume na Imam Ali kulala sehemu yake, ni hatua ambayo ilipelekea kufeli mpango wao huo. [16] Abu Jahl alikuwa amefanikiwa kuwa mjumbe katika Dar al-Nadwa akiwa na umri wa miaka 30. Hii ni katika hali ambayo, katika zama hizo, wajumbe wa Dar al-Nadwa ukiacha kabila la Bani Qusay walipaswa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 40. [17]

Kuwatesa na kuwatisha watu waliokuwa wakisilimu

Abu Jahl alikuwa akiwazuia watuu kuingia katika Uislamu. [18] Ikitokea mtu amesilimu alikuwa akimtisha na kumtesa ili aachane na Uislamu. [19] Miongoni mwa watu waliokuwa wakiteswa na Abu Jahl kutokana na kusilimu kwao na kumuunga mkono Mtume (s.a.w.w) ni Bilal Habashi, [20] Yasir bin Ammar na Sumayyah bint Khabbat. Sumayyah bint Khabbat aliyekuwa mama wa Ammar bin Yasir alikufa shahidi kutokana na mateso ya Abu Jahl. [21] Kadhalika Iyash bin Abi Rabia, kaka wa mama yake Abu Jahl (mjombake) aliyekuwa amefunga safari kuelekea Madina kwa ajili ya kuungana na muhajirina alichukua hatua ya kumrejesha Makka akiwa amefika Quba na kisha akamtia jela. [22] Kwa mujibu wa nyaraka za historia, Abu Jahl alikuwa na mipango na mikakati mbalimbali dhidi ya Waislamu wapya; kama mtu akisilimu na kuingia katika Uislamu na akawa ana nafasi na cheo katika jamii alikuwa akifanya kila awezalo kumdhalilisha na kumfanya akose hadhi na itibari katika jamii. Kama mtu huyo alikuwa mfanyabiashara alikuwa akitishia kumuwekea vikwazo na kumkwamishia biashara yake na hivyo kusambaratisha mali na mtaji wake, na kama alikuwa mtu dhaifu basi Abu Jahl alikuwa akimpiga na kumuweka chini ya mashinikizo na mbinyo. [23]

Kuandaa mazingira ya vita vya Badr

Makala asili: Vita vya Badr

Vyanzo mbalimbali vya historia vinaonyesha kuwa, Abu Jahl alikuwa na mchango mkubwa katika kutokea vita vya Badr. Kabla ya kutokea vita hivyo, Mtume (saww) alimlaani Abu Jahl pamoja na Zam'a ibn al-Aswad kutokaana na kung'ng’ania vita. [26] Katika mwaka wa pili Hijria, msafara wa makureshi uliokuwa ukiongozwa na Abu Sufiyan ulikabiliwa na vitisho kutoka kwa Waislamu. Abu Sufiyan akaomba msaada kutoka kwa makureshi. Abu Jahl alifunga safari akiwa na jeshi na kutoka Makka kwa ajili ya kwenda kutoa msaada. Pamoja na kuwa, msafara ule ulipita salama salmini, lakini Abu Jahl aling'ang'ani kulipeleka jeshi la Makka katika visima vya Badr [27 na hapo vikatokea vita baina yao na jeshi la Waislamu. Jeshi la Makka likashindwa na Waislamu na Abu Jahl pamoja na idadi kadhaa ya viongozi wa Kureshi waliuawa. [28] Abu Jahl aliuawa na Muadh bin Amr na watoto wa Afraa na Abdallah bin Mas'ud akatenganisha akatenganisha na mwili kichwa cha Abu Jahl. [29]


Vyanzo

  • Balādhurī, Aḥmad b. Yaḥyā al-. Ansāb al-ashrāf. Edited by Muḥammad Ḥamīd Allāh. Cairo: Dār al-Maʿārif, 1959 CE.
  • Ibn Athīr, ʿAlī b. Muḥammad. Usd al-ghāba. Beirut: Dār al-Kitāb al-ʿArabī, [n.d].
  • Ibn ʿAbd al-Barr, Yūsuf b. ʿAbd Allāh. Al-Istīʿāb fī maʿrifat al-aṣḥāb. Edited by ʿAlī Muḥammad al-Bajāwī. Beirut: Dār al-Jīl, 1412 AH.
  • Ibn Durayd, Abūbakr Muḥammad b. Ḥasan. Kitāb al-ishtiqāq. Edited by ʿAbd al-Salām Muḥammad Hārūn. Baghdad: 1399 AH.
  • Ibn Ḥabīb, Muḥammad b. Ḥabīb b. Umayya. Kitāb al-muḥabbar. Edited by Elza Lichten Stetter. Beirut: Dār al-Āfāq al-Jadīda, [n.d].
  • Ibn Hishām, ʿAbd al-Malik. Al-Sīra al-nabawīyya. Edited by Muṣṭafā al-Saqā, Ibrāhīm Ābyārī and ʿAbd al-Ḥafīz Shalbī. Cairo: 1355 AH/1936.
  • Ibn Isḥāq, Muḥammad. Al-Sīyar wa al-maghāzī. Edited by Suhayl Zakar. Beirut: 1398 AH.
  • Ibn al-Jawzī, ʿAbd al-Raḥmān b. ʿAlī. Al-Muntaẓam fī tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Qādir ʿAṭāʾ. Beirut: [n.n], 1412 AH.
  • Ibn Saʿd, Muḥammad b. Manīʿ al-Ḥāshimī al-Baṣrī. Al-Ṭabaqāt al-kubrā. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Qādir ʿAṭā. Beirut: Dar al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1410 AH, 1990.
  • Markaz-i farhang wa maʿārif-i Qurʾān. Aʿlām-i Qurʾān az dāʾirat al-maʿārif-i Qurʾān-i karīm. Qom: Būstān-i Kitāb, 1385 SH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Jāmiʾ al-bayān fi tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār al-Maʾrifa, 1412 AH.
  • Qurṭubī, Muḥammad b. Aḥmad al-. Tafsīr al-Qurtubī. Edited by Muḥammad Muḥammad Ḥasanayn. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1405/1985.
  • Wāḥidī, Alī b. Aḥmad. Asbāb al-nuzūl al-Qurʾān. Edited by Kamāl Basyūnī Zaghlūl. Beirut: Dār al-Kutub al-Ilmiyya, 1411 AH.
  • Wāqidī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Al-Maghāzī. Edited by Marsden Jones. 3rd edition. Beirut: [n.n], 1409 AH/1989.