Ali bin Abi Rafi’
Ali bin Abi Rafi’ (Kiarabu: علي بن أبي رافع) alikuwa mwandishi na msimamizi wa Beitul Maal (Hazina ya Dola) katika utawala wa Imamu Ali (a.s). Yeye ni mtoto wa Abu Rafi’ sahaba wa Mtume (s.a.w.w) na kaka wa Abdallah bin Abi Rafi’.[1]
Ali bin Abi Rafi’ alikuwa miongoni mwa tabiina (watu waliokutana na mmoja au masahaba kadhaa wa Mtume) na mmoja wa masahaba wa Imamu Ali (a.s) ambaye kwa mujibu wa Sayyid Muhsin Amin alikuweko katika vita vya Jamal, Siffin na Nahrawan na alikuwa katika jeshi la Imamu Ali.[2] Kadhalika Sayyid Muhsin Amin amemtambua Ali bin Abi Rafi’ kwamba, mtu wa kwanza ambaye aliandika kitabu cha Fiqhi katika Uislamu.[3] Ahmad bin Ali Najashi mtaalamu wa wasifu wa wapokezi wa hadithi wa Kishia anasema kuwa, kitabu chake kinajumuisha milango ya udhu, Sala na maudhui zingine.[4] Kwa mujibu wa Sayyid Muhsin Amin ni kwamba, yeye alikuwa ni katika mafakihi wa Kishia na alijifunza fikihi kwa Imamu Ali bin Abi Twalib (a.s).[5]
Ali bin Abi Rafi’ mwandishi na msimamizi wa Beitul-Maal (Hazina ya Dola) katika utawala wa Imamu Ali (a.s). Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwake ni kwamba, kwa ombi la binti yake Imamu Ali (a.s), Ibn Abi Rafi, ambaye alikuwa msimamizi wa hazina ya Waislamu, alimpa mkufu uliokuwa kwenye hazina hiyo kwa muda wa siku tatu kama mkopo, kwa sharti kwamba aurudishe kwenye hazina hiyo baada ya siku tatu kwa matumizi ya sikukuu ya Eidul Adh’ha.[6] Imamu alipojulishwa kuhusu hilo, akamwita na kumwambia: Vipi ulimpa binti yangu mkufu ule bila ya idhini yangu na ridhaa ya Waislamu? Irudishe leo na usiruhusu jambo hili litokee kwako tena kwani nitakuadhibu. Lau isingekuwa kuchukua mkufu huo kulifanyika kwa makubaliano na muamala wa kuazima na dhamana ya kulipa endapo utaharibika, basi angekuwa mwanamke wa kwanza wa Kihashimi ambaye ningemkata mkono kwa sababu ya kuiba.