Nenda kwa yaliyomo

Al-Tibyan fi Tafsir al-Qur’an (kitabu)

Kutoka wikishia

Al-Tibyan Fi Tafsir al-Qur’ani (Kiarabu: التبيان في تفسير القرآن (كتاب))ni kitabu cha tafsiri ya Qur’ani na kimeandikwa na Abu Jafar Muhammad Ibn Hassan Tusi mashuhuri zaidi kwa jina la Sheikh Tusi (385-460 Hijria). Kitabu hiki kinafahamika kama, tafsiri ya kwanza ya Qur’ani iliyokuwa jumuishi na kamili ya Kishia. Kitabu cha At-Tibyan kilikuwa na taathira kubwa mno katika tafsiri za Kishia na wafasiri wengi wa Kishia waliokuja baadaye waliifanya tafsiri hiyo kama dira, muongozo na kiigizo chao. Kitabu hiki kinajumuisha tafsiri za Aya zote za Qur’ani Tukufu. Moja ya sifa inayotambuliwa kama ya kipekee ya kitabu hiki ni kwamba, kitabu hiki kina mtazamo jumla na mfasiri wake alistafidi na kunufaika na elimu mbalimbali. Katika kitabu hiki Sheikh Tusi ameleta mitazamo na maoni ya wafasiri na wanateolojia wa madhehebu zingine za Kiislamu na kisha akayachambua na kuyakosoa maoni yao hayo. Ibn Idris Hilli na Ibn Kal miongoni mwa Maulamaa wa Kishia katika larne ya 6 Hijria walifanya kazi ya kukifupisha na kukifanyia mukhtasari kitabu hiki na kukipa anuani ya “Talkhis al-Tibyan”

Mwandishi

Muhammad Ibn Hassan Tusi (385-460 Hijria) mashuhuri zaidi kwa jina la Sheikh Tusi ni fakihi na msomi mkubwa Kishia aliyeishi katika karne ya 5 Hijria. [1] Yeye ndiye aliyechukua jukumu la uongozi wa kidini wa Mashia baada ya kuaga dunia Sayyid Murtadha. Mwanazuoni huyu amelea wanafunzi wengi ambao baadaye waliondokea kuwa wasomi na wanazuoni wakubwa. Sheikh Tusi hakuwa nyuma pia katika uandishi wa vitabu, kwani amevirithisa vizazi vilivyokuja baada yake makumi ya vitabu vyenye thamani kubwa. [2] Sheikh Tusi ni mwandishi wa vitabu viwili kati ya vitabu vinne (Kutub al-Ar’baa) ambavyo ni vyanzo muhimu zaidi vya hadithi vya Waislamu wa madhehebu ya Shia: Vitabu hivyo viwili ni: Tahdhib al-Ahkam na al-Isbsar. [3]


Msukumo wa Kuandika Kitabu Hiki

Kama alivyosema mwenyewe Sheikh Tusi katika utangulizi wa kitabu hiki ni kwamba: Mpaka katika zama hizo hakukuwa kumefasiriwa Qur’ani yote au vitabu vya tafsiri ya Qur’ani vilivyokuweko havikuwa vimetafsiriwa kwa kuwa na mtazamo wa kujumuisha elimu zote; bali vilikuwa vikijumuisha elimu moja tu kwa mfano utambuzi na maana ya maneno au sarf na nahw. Katika baadhi ya tafsiri pia waandishi walikuwa wakitosheka tu na kutaja hadithi na hawakuwa wakizichambua na kuzifanyia tahmini.[4] Hata tafsiri za Qur’ani ambazo zilikuwa jumuishi, zilikuwa zikifafanua mambo kupita kiasi na zilikuwa zikijumuisha mambo yasiyo na mpangilio. [5] Kwa muktadha huo Sheikh Tusi aliandika tafsiri hii akizingatia na kutilia maanani mapungufu yaliyokuweko na lengo lake lilikuwa ni kuja na tafsiri ya Qur’ani ambayo itajumuisha humo elimu zote; kama vile: Qiraa (usomaji), maana, irabu, teolojia na vilevile kujibu shubha na utata wa itikadi za madhehebu mengine. Na kiwe ni kitabu chenye uwiano (wastani wa mambo) na sio kirefu kwa namna ambayo kitamchosha msomaji, kama ambavyo kisiwe kifupi na cha mukhtasari kiasi kwamba, kisifikishe maana sahihi. [6]


Daraja na Nafasi Yake

Al-Tibyan fi tafsir al-Qur’an kinatambulika kuwa kitabu cha kwanza cha tafsiri kamili na jumuishi. [7] Muhammad Hadi Maarifat anasema: Al-Tibyan ni kitabu cha tafsiri ambacho kiliviacha nyuma vitabu vyote vya tafsiri katika zama zake; kwani kinyume na vitabu vingine, kitabu hiki hakikutosheka na upande mmoja tu bali kimezingatia mitazamo ya wafasiri wa kabla yake. [7] Sheikh Tusi ameandika kitabu hiki kikiwa ni “tafsiri ya kati na kati na wakati huo huo jumuishi, kamili na iliyo na mambo yote mazuri ya tafsiri za hapo kabla”. [9] Kadhalika mwandishi wa makala anasema: “Kuchunguza utendaji wa kukurubisha baina ya tafsiri mbili za al-Tibyan na Majma’ al-Bayan katika kunukuu riwaya na hadithi za Ahlul-Beiti (as), al-Tibyan ni tafsiri ya kwanza ya kiijtihadi ya Kishia ambayo ina chimbuko la muelekeo ya kiakili, na anga iliyokuwa ikitawala katika karne ya 4 na ya 5 inashuhudiwa wazi ndani yake. [10] Kwa mujibu wa mwandishi: Katika kuandika tafsiri hii, Sheikh Tusi alistafidi na kunufaika na athari za Kishia na Kisuni. [11] Muhammad Ali Mahdavi Rad (aliyezaliwa 1334 Hijria Shamsia) na ambaye ni mhakiki na mtafiti wa masuala ya Qur’ani wa Kiirani ameandika: Kitabu cha al-Tibayn fi tafsir al-Qur’an kilikuwa na taathira kubwa mno kwa wafasiri waliokuja baadaye. Miongoni mwao ni Fadhl ibn Hassan ibn Fadhl Tabarsi ambaye amekisifu kitabu hiki na kuifanya mbinu na mtindo wa kitabu hiki kuwa dira na kiigizo chake katika kuandika tafsiri yake ya Majma’ al-Bayan. [12]

Sifa za Kipekee

Katika kitabu hiki Sheikh Tusi alikuwa na mtazamo jumuishi na ametumia elimu zote za Qur’ani (Ulumul Qur’an) katika tafsiri yake hii ya Qur’ani; elimu kama utambuzi wa lugha, qiraa, irabu, asbab al-nuzul (sababu za kushushwa Aya za Qur’ani), nasikh na mansukh, na kuwa Aya fulani imeshuka Makka (Makki) au Madina (Madani). [13] Kadhalika ndani ya tafsiri hiyo amebainisha masuala mengine kama taawili, muhkam na mutashabiha, uchambuzi kuhusiana na majina ya Qur’ani na majina ya sura zake. [14] Sifa nyingine ambayo imetajwa kuwa ni ya kipekee ikilinganishwa na vitabu vingine vya tafsiri ya Qur’ani: Ni kufasiri Qur’ani kwa Qur’ani, [15], kuweka kando hadithi dhaifu na kutumia hadithi sahihi kwa sharti kwamba, zisiwe zinapingana na Qur’ani na akili [16] sambamba na kuzungumzia kwa mapana na marefu masuala ya kiitikadi. [17] Katika kitabu hiki baada ya kutajwa kila Aya, kwanza kabisa hujadiliwa neno ambalo ni gumu na lisiloeleweka vyema na kisha kubainishwa tofauti za Qiraa (namna ya usomaji). Kisha baada ya hapo, kunafanyika uchunguzi na uhakiki kuhusiana na mitazamo na nadharia mbalimbali za kitafisiri kuhusiana na Aya husika. Katika hatua inayofuata ni kuzingatia mafuhumu na maana ya Aya sambamba na kuchambua sababu za kushuka kwake pamoja na masuala mengine ya kiitikadi, kifikihi. Aidha jambo jingine ni kukosoa fikra za wapinzani lakini kwa lugha ya adabu na heshima. [18]

Vitabu Teule

Agha Bozorg Tehran (aliyeaga dunia 1389 Hijria), msomi na mtambuzi wa vitabu wa Kishia amevitambulisha vitabu viwili vya tafsiri vya Maulamaa wa Kishia katika kitabu chake cha al-Dhariah kwa anuani ya Mukhtasar al-Tibyan ambavyo ni mukhtasar wa kitabu cha al-Tibyan fi tafsir al-Qur’an: • Moja ya vitabu hivyo kimeandikwa na Ibn Idris Hilli (aliyeaga dunia takribani 548 Hijria). [19] • Kitabu kingine ni cha Abu Abdallah Muhammad ibn Harun mashuhuri zaidi kwa jina la Ibn Kal (aliyeaga dunia 597 Hijria). [20]

Nakala za Hati na Machapisho ya Awali

Agha Bozorg Tehran ameandika kuwa, yeye hajaona katika maktaba yoyote ile nakala ya hati (iliyoandikwa kwa mkono) iliyo kamili ya kitabu cha al-Tibyan na nakala mbalimbali za hati (zilizoandikwa kwa mkono) ambapo kila moja ina juzuu moja zimetawanyika katika maktaba mbalimbali. [21] Mahdavi Rad anasema: Kwa mara ya kwanza na kwa juhudi za Sayyid Muhammad Hojjat Kooh Kamari (aliyeaga dunia 1372 Hijria), juzuu mbalimbali zilizokuwa zimetawanyika za kitabu hiki zilikusanywa kwa ajili ya kuchapishwa. [22] Chapa ya kwanza ya al-Tibyan ilichapishwa kwa juhudi za Mirza Ali Agha Shirazi na Sayyid Abdul-Rasul Roghanizadeh Isfahani katika juzuu mbili; Juzuu ya Kwanza ilichapishwa 1362 Hijria na Juzuu ya Pili ikachapishwa baada ya miaka mitatu yaani 1365 Hijria. [23]. Chapa ya pili, ilikuja kuchapishwa baina ya mwaka 1376 na 1382 Hijria huko Najaf, Iraq ikiwa katika juzuu kumi ambapo sehemu kubwa ya kazi ya kusahihisha na kufanya uhakiki ilifanywa na Ahmad Habib Qasir al-Amili. [24].


Rejea

Vyanzo