Nenda kwa yaliyomo

Al-Tamhid fi Ulum al-Qur’ani (Kitabu)

Kutoka wikishia
Al-Tamhid fi Ulum al-Qur’ani

Al-Tamhid fi Ulum al-Qur’ani (Kiarabu: اَلتّمْهید فی عُلومِ الْقُرْآن) ni kitabu cha Kiarabu kilichoandikwa na Muhammad Hadi Ma'rifat (1309-1385 A.H.). Kitabu hiki, ambacho kinachukuliwa kuwa ndiyo kazi kubwa zaidi andishi kwa zama za hivi sasa kuhusiana fani ya elimu za Qur’ani, kitabu hichi kimeandikwa katika mfumo wa juzuu sita. Hichi ni kitabu kinacho zungumzia masuala mbalimbali ya fani za Elimu ya Qur'ani, ikiwemo wahyi, kuteremshwa kwa Qur'ani, historia yake, njia tofauti za usomaji (qira'at), Aya zilizofutwa au zilizokuja kufuta hukumu ya Aya za wali (nasikh na mansukh), Aya dhahiri na Aya kanganyifu (muhkam na mutashabih), [pamoja na miujiza ya Qur’ani. Tatu kati ya juzuu zake, zimejikita hasa katika kuelezea misingi na sifa za miujiza ya Qur’ani Tukufu. Muhammad Hadi Ma'rifat ametumia vyanzo mbalimbali vya Kisunni na Shia katika kuandika kitabu chake hichi cha "Al-Tamhid". Utafiti wake ulitegea mada tofauti kutoka katika vyanzo hivyo kama vile; elimu ya Qur'ani, tafsiri, pamoja na historia. Al-Tamhid ni moja ya vyanzo muhimu kinachotumiwa katika utafiti wa Nyanja tofauti, nacho pia hutumiwa kama ni vitabu cha kusomeshea katika vyuo vikuu na Hawza za Kielimu mbali mbali.

Baadhi ya sifa za "Al-Tamhid" ni pamoja na kuepuka maelezo ya ziada yasiyo na mwelekeo na kuweka wazi mada inayojadiliwa, la pili ni kutumia Hadithi zitokazo pande zote mbili za Ahlul-Sunna na Shia, pia kutumia mfumo dadisi katika kuwasilisha muktadha wa mada zake. "Al-Tamhid" inahisabiwa kuwa ni kikamilishi kinachokamilisha na kuziba pengo la mapungufu ya kutokuwepo kwa ensaiklopidia ya Qur’ani miongoni mwa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Juzuu tatu za awali za kitabu cha "Al-Tamhid" zilichapishwa mnamo mwaka 1367 (Shamsia) na Shirika la Intisharate Markaz Mudiriyyat Hawze Ilmiyye Qom. Baadaye, Ofisi ya Uchapishaji ya Intisharate Islamiy ilikitoa kitabu hichi katika juzuu sita. Hatimae, Taasisi ya Al-Tamhid ilichapisha toleo lenye idadi ya juzuu kumi, ambalo pamoja na juzuu sita za awali, lilikuwa limeambatanisha ndani yake vitabu vitatu vyengine ambavyo ni: Shubuhat wa Rudud, Siyaanat al-Qur’ani min al-Tahrif na Al-Tafsir wa al-Mufassirun. Hapo awali vitabu vitatu hivi vilikuwa vimechapishwa kwa kujitegemea. Kuna tafsiri na vitabu mbali mbali vya muhtasari wa "Al-Tamhid" vilivyo andikwa kwa lugha ya Kifarsi ambavyo tayari vimechapishwa kupiotia taasisi tofauti. Pia sehemu za kitabu hichi zimetafsiriwa na kuwa kama ni vitabu vyenye kujitegemea. Mfano wa vitabu hivyo ni kitabu kiitwacho Tanasub-e Ayat. Pia, kuna programu ya dijitali ya "Al-Tamhid" iliyo tolewa na Daftare Tablighat Islamiy Qom (Ofisi ya Uenezi wa Kiislamu ya Hawza ya Qom).

Misingi na Nafasi ya Kitabu

Al-Tamhid fi Ulum al-Qur’ani ni kitabu kilichoandikwa na Muhammad Hadi Ma'rifat, kilichozalishwa kutokana na hati zake za mkono alizokuwa amezikusanya kutoka katika dondoo zake mbali mbali za muda mrefu kuhusiana na fani ya elimu za Qur'ani, ambazo mwishowe ziliandikwa na kuhaririwa katika mfumo wa kitabu. Mwandishi alikitayarisha kitabu hichi na maudhui zake kama ni utangulizi wa tafsiri iliyoipa jina la "Al-wasit". [1]

Kitabu hiki kimegawanywa katika juzuu sita, zikijadili mada saba zinazohusiana na elimu ya Qur'ani: wahyi, kushushwa kwa Qur'ani, historia ya Qur'ani, visomo (qira'at) mbalimbali, Aya zilizofutwa (nasikh na mansukh), Aya zilizowazi na kanganyifu (muhkam na mutashabih), na miujiza ya Qur'ani. [2] Maudhui ya Juzuu za Kitabu:

  • Juzuu ya kwanza ya kitabu hichi inashughulikia masuala matatu, nayo ni: Wahyi, kushushwa kwa Qur'ani, na historia ya Qur’ani.
  • Juzuu ya pili inajadili qira'at (visomo) mbalimbali pamoaj na Aya za nasikh na mansukh.
  • Juzuu ya tatu inatafiti Aya za muhkam (za wazi) na mutashabih (kanganyifu). [3]
  • Juzuu ya nne, ya tano, na ya sita zinajadili miujiza ya Qur'ani, ikijumuisha misingi ya miujiza, miujiza ya binafsi ya Qur'ani, miujiza ya kisayansi, miujiza ya kutoa habari za ghaibu, na miujiza ya kisheria iliyomo ndani ya Qur'ani Tukufu. [4]

Al-Tamhid kimeelezewa kama ni kitabu kamilifu na cha kina kinachojumuisha sehemu kubwa ya mada za elimu za Qur'ani. [5] Tofauti na kazi zilizotangulia kabla yake, ambazo mara nyingi zilikuwa zinakariri maneno ya waliopita, kitabu hichi kimepiga hatua na kusonga mbele kwa kufafanua makosa na mapungufu ya kazi zilizo tangulia kabla yake. [6] Baada ya Ayatullah Ma'rifat kufanya mapitio na maboresho kwenye toleo lake la awali, alikuja kuchapisha tena juzuu tatu za kwanza za kitabu chake hicho mnamo mwaka 1358 Shamsia. [7]

Muhammad Hadi Ma'rifat, alitumia vyanzo vingi kutoka pande zote mbili; Ahlul-Sunna pamoja na Shia katika uandishi wa kitabu chake kiitwacho “Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'ani”, miongoni mwavyo ni pamoja na; vyanzo vinavyo husiana na elimu za Qur'an, tafsiri, vyanzo vya Hadithi, historia na rokodi zinazohusiana na maisha ya wanazuoni fulani, vvyanzo vya theolojia, vyanzo vya fiqhi, usulu al-fiqhi, na fasihi. [8] Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'ani imekuwa ndiyo mojawapo ya vyanzo vikuu vya utafiti kuhusiana na elimu za Qur'ani. Kwa mujibu wa ripoti zilizopo, tasnifu na kazi nyingi zimeandikwa kwa kutegemea kitabu hichi, na vitabu mbali mbali vimeandikwa kama ni muhtasari wa kitabu hichi, ambavyo hutumika kwa ajili ya kusomesha katika vyuo vikuu mbali mbali vikiwemo vyuo vya kidini. [9]

Kuhusu Mwandishi

Muhammad Hadi Ma'rifat (1309 -1385 Hijiria Shamsia/ 1930 – 2006 Miladia) alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kishia, mtaalamu wa Hadith, na mtafiti wa elimu za Qur'ani na tafsiri. [10] Ma'rifat alisoma katika vyuo vya kidini vya Karbala, [11] Najaf [12] na Qom. [13] Katika mji wa Qom, pamoja na kufundisha vitabu vya fiq-hi na usulu al-fiq-hi kama vile Rasa'il, Makāsib na Kifāya na baadaye kufundisha Fiqhi na Usulu al-Fiq-hi katika ngazi za ijitihadi, aliendelea pia kufundisha elimu za Qur'ani katika chuo cha Haqqani. [14] Katika harakati hizi, hadi mwaka 1358 Hijiria Shamsia / 1979 Miladia, juzuu tatu za kitabu "Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'an" ziliweza kukamilika na zilichapishwa rasmi. [14] Baada ya masomo ya tafsiri na elimu za Qur'ani kuwa ni sehemu rasmi ya masomo ya kidini, Hadi Ma'rifat alijihusisha na kufundisha watu na kuwatayarisha kama ni walimu wa kufundisha masomo hayo, na kwa kuongezea, alianzisha vyuo 14 vya elimu za Qur'ani katika maeneo mbalimbali ya Iran. [15]

Ma'rifat pia aliandika vitabu vingine kama vile katika juhudi zake za kuikuza jamii, ambavyo ni; Al-Tafsir al-Athari al-Jami'i, [16] Siyanat al-Qur'an min al-Tahrif [17] na kitabu Shubuhat wa Ruduud, ambacho kilijibu shaka na ukosoaji wa wanatafiti Kimagharibi na baadhi ya wasomi wa ulimwengu wa Kiarabu kuhusiana na Qur'ani Tukufu. [18] Aidha, aliandika kitabu chenye juzuu mbili kiitwacho Al-Tafsir wa al-Mufassirun [19] ambacho, pamoja na kuchapishwa kama ni kitabu binafsi na huru, pia kilichapishwa kwa kuambatanishwa na kitabu “Al-Tamhid fi Ulumi al-Qur'an”. [20] Ma'rifat alifanya kazi nyingi andishi katika mada tofauti za fiqhi, kama vile; “Tamhid al-Qawaid”, “Hadith al- Itti’aad”, “Wilayat al-Faqih: Ab'aduha wa Hududuha”, “Maalikiyyatu al-Ardh” na “Masailu fi al-Qadha”, vyote vikiwa vimeandikwa kwa lugha ya Kiarabu. [21]

Sifa na Mbinu za Uandishi

Ayatullah Ma'rifat, katika kitabu chake “Al-Tamhid”, alijitahidi kufafanua dhana na istilahi mbali mbali kuhusiana na Qur'ani, ikiwemo Wahyi na Miujiza. Pia mara nyingine ameonekana kugusia maudhui zinazohusiana na sababu za kushuka kwa Aya za Qur'ani (Asbab al-Nuzul). [22]

Kitabu “Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'an” kimejitahidi kuepuka utoaji maelezo ya kusambaratika ya kuchosha akili, badala yake kimetumia mbinu ya kuanzisha maswali yanayohusiana na mada husika katika kila moja ya sura za kitabu hicho. Mbinu hii emelenga kufafanua suala linalojadiliwa kwa umakini ili kulifanya lieleweke haraka bila ya kutumia juhudi za ziada. [23] Katika kitabu hiki, Ma'rifat ametumia Hadithi za upande wa Ahlul-Sunna na Shia katika kuwasila kwake mada mbalimbali za elimu za Qur'ani, ikiwemo namna ya kushuka kwa Wahyi, Aya za mwanzo na mwisho, na sababu za kushuka kwa Aya (Asbab al-Nuzul) mbali mbali. [24]

Mwandishi wa “Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'ani”, katika utangulizi wa kitabu hichi, amesisitiza kwamba; katika kazi yake hii, amejumuisha tu yale aliyokuwa na uhakika nayo juu ya usahihi wake, katika uwakilishaji wa dhana mbali mbali kitabuni humo. [25] Madhumuni hayo ndiyo yaliyomfanya yeye, kuzigawanya maudhui za kitabu hicho katika mfumo wa kijitabu na kuwapa wanafunzi wake kukipitia kabla ya kuchapisha kwake rasmi. Wanafunzi wake walipitia maandishi hayo na kuelekeza maswali yao kwa mwalimu wao huyo, kwa nia ya kuondoa dosari zinazoweza kujitokeza baadae. Mwalimu naye hakuwa na ajizi katika kusikiliza mawazo ya wanafunzi wake, ambapo pia alifaidika na maoni pamoja na na ukosoaji wa wanazuoni hao, ambao walikuwa na wanafunzi wake katika fani hiyo. Alifanya hizvyo kwa moyo mkunjufu kwa ajili ya kukamilisha na kuboresha yaliyomo ndani ya kitabu chake. [26]

Sifa nyengine zilizotajwa kuhusiana na “Al-Tamhid” ni pamoja na: kuziba pengo la ukosefu wa ensaiklopedia za Qur'ani miongoni mwa wafwasi wa madhehebu ya Shia, [27] kuiarifisha nafasi Mashia na mchango wao katika uwanja wa elimu za Qur'ani, [28] pamoja na sifa ya kutumia njia ya ukosoaji kitaalamu katika katika uwasilishaji wa nadharia zake mbali mbali. Ma'rifat ameendelea na mwenendo huo kwa kiasi kikubwa, hadi wakati mwengine ameonekana kusoa nadharia na maoni ya Ayatullah Khui na Allama Tabatabai bila ya kujali nafasi zao katika jamii za wanazuoni wa zama hizo. [29]

Muhtasari wa Yaliyomo

Mada ya kwanza ya kitabu, baada ya utangulizi, imepewa jina la "Wahyi na Qur'ani" (الوحی و القرآن) mada ambayo inashughulikia masuala kadhaa yanayohusiana na Wahyi, kama vile; maana ya Wahyi kilugha, matumizi yake katika Qur'ani, mtazamo wa wanafalsafa watafiti wa Kimagharibi kuhusiana na Wahyi, aina za Wahyi wa mitume, hoja za kuthibitisha uwepo wa nafsi, na Hadithi ya Gharaniq. [30] Wahyi kilugha unamaanisha ujumbe wa haraka na wa siri, iwe kwa njia ya ishara, mnong’ono, kusema kwa sauti ya chini, au kuandika kwa siri. Neno hili katika Qur'ani, linatumika kwa maana hizo hizo, kama ilivyo katika Aya ya 11 ya Surat ya Mariam. Mwenye Ezi katika Aya hiyo anasema: (فَخَرَجَ عَلَىٰ قَوْمِهِ مِنَ الْمِحْرَابِ فَأَوْحَىٰ إِلَيْهِمْ أَنْ سَبِّحُوا بُكْرَةً وَعَشِيًّا, "Hivyo basi akatoka kwenye chumba chake cha ibada, akawapa ishara watu wake ya kuwambia wamdhukuru Mwenye Ezi Mungu asubuhi na jioni". Zaidi ya maana ya msamiati huo kilugha, pia kuna matumizi mengine matatu ya neno Wahyi yanayo patikana katika Qur'ani, ambayo ni:

  1. Muundo wa maumbile asili uliyojificha ndani maumbile na asili ya viumbe mbali mbali, ambapo hisia ya ndani na maelekezo ya kiasili ni mfano wa aina hii ya Wahyi. Kuhusiana na hili Aya ya 68 ya Surat An-Nahli inasema: (وَأَوْحَىٰ رَبُّكَ إِلَى النَّحْلِ أَنِ اتَّخِذِي مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا وَمِنَ الشَّجَرِ وَمِمَّا يَعْرِشُونَ ; Na Mola wako alimtuma nyuki, Kuchukua baadhi ya milimani na baadhi ya miti kama ni makazi yake, na kutokana na kile wanachojenga). Aya Hii inaonyesha mfano wa Wahyi katika maumbile nyuki. Pia, Aya ya 12 ya Surat Fussilat inasema: (وَ أَوْحی فِی کُلِّ سَماءٍ أَمْرَها ; Na akaimrisha kila anga kazi zake).
  2. Uhamasishaji wa kiroho au hisia ya ndani ya moyo, pia ni aina nyingine ya Wahyi katika Qur'ani. Aya ya 7 ya Surat Al-Qasas ni mfano wa aina hii ya Wahyi, Mwenye Ezi Mungu katika Aya hii anasema:(وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ أُمِّ مُوسَىٰ أَنْ أَرْضِعِيهِ ۖ فَإِذَا خِفْتِ عَلَيْهِ فَأَلْقِيهِ فِي الْيَمِّ وَلَا تَخَافِي وَلَا تَحْزَنِي ۖ إِنَّا رَادُّوهُ إِلَيْكِ وَجَاعِلُوهُ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ; Na tukamwambia mama ya Musa, Mnyonyeshe (mwanao), ama ikiwa utamwogopea (kuawa), basi mmweke kwenye mto, hivyo usiogope wala usihuzunike. Hakika, tutamrudisha (tena) kwako na tutamfanya kuwa miongoni mwa mitume).
  3. Wahyi wa utume ni ule aupokeao mtume fulani kutoka kwa Mola wake (kwa njia ya malaika au bila ya malaika), Wahyi ambao malengo yake huwa ni kwa ajili ya kueneza ujumbe wa Mwenye Ezi Mungu. [31] [Maelezo 1]Sehemu ya mwisho ya kitabu inamalizia kwa mada ya "Uhuru na Usawa Katika Uislamu". Mwandishi, katika muhtasari wa tafiti kuhusiana na mateka wa vita, anasisitiza ya kwamba; mateka wa vita ambavyo vita bado vinaendelea wanastahili kuuawa. Hata hivyo, ikiwa vita vimeisha, kiongozi wa Waislamu ana haki ya kuchukua hatua anayoona ni muwafaka kwa ajili yao, kama vile kuwaachia huru -ikiwa hawana hatari kwa Waislamu-, kuwatumia katika kubadilishana mateka, au kuchukua fidia kwa ajili ya uhuru wao au mali fulani inayokubaliwa na pande zote. Ikiwa hatua hizi haziwezekani, kuwaweka kama ni mateka ni bora kuliko kuuawa kwao, kwani wanaweza kuongoka kupitia tabia njema za Waislamu na huruma yao. [32]

Matoleo Tafsiri na Mafupisho

Kitabu cha “At-Tamhid fi Ulum al-Qur’an” kimechapishwa na vitengo vitatu tofauti. Kwanza, kilichapwa na Markaz Mudiriyyat Hauze Ilmiyye Qom, chapa hii ilikuwa ni ya juzuu tatu za mwanzo za kitabu hichi. Hadi kufikia mwaka 1367 Hijria Shamsia sawa na mwaka 1988, kitengo hicho kiliweza kufikia toleo lake la tatu la kitabu hichi. [33] Kitengo cha pili ni Daftare Intishaarate Islamiy, kilioko chini ya Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qom (chuo kikuu cha kidini cha Qom). Wao walichapisha juzuu sita za kitabu hichi katika matoleo kadhaa, baadhi ya juzuu zake ziliendelea kuchapishwa hadi kufikia toleo la tano. [34] Mwishowe kitabu hichi kilikuja kuchapishwa na Taasisi ya At-Tamhid ilichapisha kitabu hichi katika juzuu kumi. [35] Toleo la juzuu kumi, kama alivyoeleza Muhammad Hadi Ma'rifat, linajumuisha juzuu sita za kitabu At-Tamhid, toleo ambalo limeambatanishwa na vitabu vyengine vitatu, ambavyo ni Shubuhat wa Rudud, Siyanat al-Qur’an min al-Tahrif na At-Tafsiru wa al-Mufassiruna. [36] Vitabu vitatu hivi hapo awali vilikuwa ni vitabu huru vilivyo mechapishwa kwa kujitegemea wenyewe bila ya kuambatanishwa na vikitabu vyengine. [37]

Kitabu cha juzuu mbili kiitwacho “Talikhs al-Tamhid” ni muhtasari wa toleo la juzuu sita za kitabu “Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'an”. Mukhtasari huo uliandaliwa kwa ajili ya kutumika kama ni kitabu cha kusomeshe masomo ya fani ya sayansi za Qur’ani katika vyuo vya kidini. [38] Kitabu hiki kimechapishwa kwa matoleo kadhaa na mashirika mawili ya uchapishaji ya Kiislamu; Intishaarete Islamiy na Intishaarete Al-Tamhid. [39] Aidha, kitabu cha “Tareekh al-Qur'an”, ambacho ni mavuno yatokayo katika juzuu mbili za mwanzo za “Al-Tamhid”, kilichapishwa kwa lugha ya Kifarsi kwa ajili ya kufundisha fani ya Elimu za Qur'ani katika vyuo vikuu, kikiwa na ongezeko la maudhui nyengine ndani yake. [40] Vilevile, kuna muhtasari na uandishi mpya kwa ajili ya kitabu “Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'an”, pamoja na kitabu “Siyanat al-Qur'an min al-Tahrif”, uliofanyika na kuchapishwa katika kitabu maalumu kilicho tolewa kwa lugha ya Kifarsi chiuni ya jina la “Ulum al-Qur'an”. [41]

Kitabu kiitwacho “Tanasub Ayat”, ambacho ni tafsiri ya Kifarsi ya sehemu ya juzuu ya tano ya kitabu “Al-Tamhid”, ni kazi iliyo fanywa na Izzatullah Maulainia Hamadani iliochapishwa mnamo mwaka 1373 Hijiria Shamsia/1994 Miladia. [42] Maudhui ya “Tanasub Ayat /Uhusianao Kati ya Aya”, katika kitabu “Al-Tamhid” inatajwa kama moja ya ishara za muujiza wa Qur'an Tukufu. [43] Kuna tafsiri nyingi za Kifarsi za “Al-Tamhid” zililzochapishwa na kusambazwa, zikiwemo: “Amuuzesh Ulumu Qur'an” ikazi ya Abu Muhammad wakiliy. Miongoni mwa tafsiri nyengine maarufu za Kifarsi za kitabu “Al-Tamhid”, ni “Muqaddimeye Ulume Qur’an”, ya Jawad Irawani, na “Tarjume Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'an”, ambayo ni kazi Mirza Alizadeh aliyo ifanya kwa kushirikiana na Mujtaba Khatat. [44]

Programu ya Kidijitali ya Al-Tamhid

Programu ya kidijitali ya “Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'ani” imetolewa na “Markaze Ittilaat wa Madaarike Islami” (Kituo cha Taarifa na Nyaraka za Kiislamu), kinachohusishwa na Daftare Tabliighaat Islamiy Hauzeye Ilmiyye Qom (Ofisi ya Tablighi ya Kiislamu ya Hawza ya Qom). [45] Programu hii imekusanya ndani yake matini (maandiko) kamili ya juzuu kumi za kitabu “Al-Tamhid fi Ulum al-Qur'ani”, ikiwapatia watumiaji wake zaidi ya istilahi elfu nane zinazohusiana na fani ya Elimu za Qur'ani. Vilevile, programu hii ina uwezo wa kuwapa watumiaji wake zaidi ya mafupisho elfu tano kutoka kwenye maandiko asili ya kitabu “Al-Tamhid”. [46]

Mada Zinazo Husiana

Maelezo

  1. ما یلقیه الله الی نبیّ من أنبیائه بواسطة ملک أو بغیر واسطة لأجل تبلیغ رسالة الله

Rejea

Vyanzo