Nenda kwa yaliyomo

Al-Mahdi al-Abbasi

Kutoka wikishia

Muhammad Ibn Mansur (Kiarabu: محمد بن المنصور) mashuhuri kwa jina la Al-Mahdi Al-Abbasi (126-169 AH) ni khalifa wa tatu wa ukoo wa Bani Abbas na alitawala baada ya Mansour Dawaniqi na alikuwa katika zama moja na Imamu Musa Kadhim (a.s). Alitawala akiwa khalifa kuanzia mwaka 158-169 AH. Baadhi wanaamini kwamba, suala la itikadi ya Umahdi na malengo yaliyokuwa na muelekeo wa ahadi ya baba yake Mansour yalikuwa na mchango katika kupewa lakabu ya Mahdi. Mwaka 159 Hijiria Al-Mahdi al-Abbasi alitoa amri ya kupelekwa Baghdad Imamu Mussa al-Kadhim (a.s) na akamfunga jela.

Mwanzoni mwa ukhalifa wake, Mahdi Abbasi alizuia kuuawa na kuteswa kwa Mashia. Aliwaachia huru Mashia waliokuwa jela na kuwawekea masharti na sheria fulani, lakini taratibu akabadili sera yake katika kushughulika na Mashia. Katika zama zake kulikuwa na uasi ambao ulikandamizwa na serikali. Mara kadhaa alituma majeshi Roma na India.

Historia ya Maisha yake

Muhammad bin Abdallah bin Muhammad bin Ali bin Abdallah bin Abbas, aliyepewa lakabu ya Mahdi [1] ni Khalifa wa tatu wa Bani Abbas baada ya Safah na Mansour Dawaniqi. [2] Alizaliwa mwaka wa 126 Hijiria huko Humaima karibu na Makka. [3] Baba yake alikuwa Mansour Dawaniqi na alijali sana malezi yake na alikuwa akimkabidhi vyeo muhimu tangu akiwa mdogo.[4]

Katika mwaka 147 Hijiria, Mansour alimfanya kuwa mrithi wa kiti cha chake cha ufalme wake. [5] Alikuwa maarufu kwa akili, kusamehe na upole, [6] na baada ya kifo cha baba yake mnamo tarehe 17 Dhuli-Hijja mwaka wa 158 Hijiria [7] au 159 AH [8] alirithi ukhalifa.

Mahdi Abbasi aliwafanya wanawe wawili, Hadi na Harun, kuwa warithi wa kiti cha ufalme wake kwa utaratibu. [9] Hata hivyo mwishoni mwa umri wake alijuta kumfanya mwanawe Hadi kuwa mrithio wa kiti cha utawala, hata hivyo hakufanikiwa kubadilisha hilo. [10]

Kusifiwa kwa Lakabu ya Mahdi

Kwa mujibu wa watafiti wa zama hizi, Muhammad bin Mansour alipatiwa lakabu ya Mahdi kwa lengo la kudhamini uungaji mkono wa watu kwake [11] na kwa minajili ya kukabiliana na madai ya Umahdi ya Nafs Zakiyah. [12] Kwa msingi huo inasemekana kwamba, Bani Abbasiyya walifanya juhudi za kumtambulisha Mahdi Abbasi kuwa ndiye Mahdi Muahidiwa aliyetajwa katika hadithi za Mtume (s.a.w.w) ili kupata kuungwa mkono na watu na kuihifadhi serikali ya Bani Abbas. [13]

Kifo

Mahdi Abbasi alikufa katika mwaka 166 AH [14] au 169 AH [15] baada ya miaka 10 ya ukhalifa katika eneo la Masbadhan [16] (Ilam ya kisasa) katika kijiji cha Rudh. [17] Kuna hitilafu kuhusiana na kifo cha Mahdi Abbasi ya kwamba, aliuawa kwa sumu au alikufa katika hali ya kufanya mazoezi ya kuwinda Swala. [18]

Muamala wake kwa Imamu Kadhim (a.s)

Mwaka 159 Hijiria Al-Mahdi al-Abbasi alitoa amri ya kutolewa Imamu Kadhim (a.s) huko Madina na kupelekwa Baghdad na kisha akamfunga jela. [19] Baada ya muda, na baada ya Imamu kula kiapo kwamba, hataanzisha harakati na mapinduzi dhidi ya utawala wa wakati huo alimuachilia huru. Hata hivyo Imamu Kadhim alikuwa chini ya uangalizi hadi mwishoni mwa utawala wa Mahdi Abbasi. [20] Baada ya hayo, Imamu Kadhim (a.s) aliwausia masahaba zake kufanya taqiyyah [21].

Baadhi ya watafiti wa zama hizi wamezingatia kuuawa shahidi Imamu SWadiq (a.s) na mgawanyiko wa Mashia kuwa ndio sababu ya kudhoofika nafasi ya Imamu Kadhim (a.s) na kwa sababu hiyo, alilazimika kuchagua taqiyyah. [22] Ni kutokana na hilo ndio maana, utawala wa wakati huo wa Bani Abbas haukuchukua hatua dhidi ya Imamu Kadhim (a.s) na wafuasi wake. [23] Hata hivyo, taratibu wafuasi wa makundi mengine ya Shia walijiunga na masahaba wa Imam Kadhim na Shia Imamiyyah wakawa na nguvu zaidi kuliko makundi mengine ya Kishia, na kwa ajili hiyo Mahdi Abbasi aliwawekea mipaka na akawabana Mashia na kumfunga jela Imamu Kadhim (a.s). [24]

Muamala wake kwa Mashia

Mwanzoni Mahdi Abbasi alijaribu kuwaridhisha watu. [25] Alirudisha kwa wamiliki wake sehemu kubwa ya mali iliyobaki kutoka kwa utawala wa baba yake, ambayo ilipatikana kwa mabavu na kunyang'anywa mali za watu, hasa Mashia, na hilo likawa sababu ya watu kuridhika. [26] Mwanzoni, alizuia kuuawa na kuteswa kwa Mashia na akawatoa gerezani [27] na akawawekea masharti na sheria fulani. [28] Hata hivyo khalifa huyo wa tatu wa Bani Abbas hatua kwa hatua alianza kuwabinya na kuwabana Mashia na kutekeleza sera na siasa za vitisho, mateso na maudhi dhidi yao. [29].

Baada ya kupata madaraka, Mahdi Abbasi alichukua hatua katika uwanja wa siasa za ndani ambazo zilipelekea kupatikana amani na usalama wa jamii kwa namna fulani katika zama za utawala wake. [30] Ni kwa muktadha huo, ndio maana baadhi wanaamini kwamba, utawala huo, kilikuwa kipindi cha kuhama kutoka katika utumiaji mabavu na ukandamizaji cha khalifa wa kwanza na kuingia katika zama za wastani na upole cha makhalifa wa baadaye. [31]

Kukandamiza Waasi na Kutuma Majeshi Roma na India

Wakati wa utawala wa Mahdi Abbasi, kuliibuka harakati na uasi dhidi ya serikali. Katika hatua ya awali, alikabiliana na vuguvugu la wazandiki lililokuwa katika hali ya kuenea na kupanuka wigo wake.[32]

Uasi wa Muqanna’, [33] uasi wa Yusuf Baram mwaka wa 160 Hijiria huko Khorasan, [34] uasi wa Abdullah bin Marwan mwaka wa 161 AH katika ardhi ya Syria, [35] na uasi wa Khawarij chini ya uongozi wa Abdul Salam Yashkuri, mwaka wa 162 Hijiria, [36] ni matukio yaliyotokea katika zama za utawala wa Mahdi Abbasi na yote yalikandamizwa na kusambaratishwa. [37]

Mahdi Abbasi alituma majeshi mara kadhaa huko Roma. Mnamo mwaka wa 159 Hijiria, alimtuma Abbas bin Muhammad kwenda katika ardhi ya Roma na jeshi kubwa na akasonga mbele mpaka Ankara. [38] Pia mwaka 165 Hijiria alituma jeshi kubwa chini ya uongozi wa mwanawe Harun kwenda Roma na kufanikiwa kuelekea mpaka katika Ghuba ya Constantinople. [39] Pia alituma jeshi kwenda India kwa njia ya bahari mwaka wa 160 AH na kuuteka mji wa Barbad baada ya kuuzingira. [40]

Vyanzo

  • Dīnawarī, Aḥmad b. Dāwūd al-. Al-Akbār al-ṭiwāl. Edited by ʿAbd al-Munʿim ʿĀmir. Qom: Manshūrāt al-Raḍī, 1368 Sh.
  • Ḥusayn Jāsim. Tārīkh-i sīyāsī-yi ghaybat-i imam dawāzdahum. Translated to Farsi by Muḥammad Taqī Āyatollāhī. Tehran: Amīr Kabīr, 1376 Sh.
  • Ibn Athīr, ʿAlī b. Muḥammad. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār Ṣādir, 1965.
  • Ibn al-Jawzī, Sibṭ. Tadhkirat al-khawāṣṣ. Qom: Manshūrāt al-Raḍī, 1418 AH.
  • Ibn Kathīr, Ismāʿīl b. ʿUmar. Al-Bidāya wa l-nihāya. Beirut: Dār al-Fikr, [n.d].
  • Ibn Ṭaqṭaqī, Muḥammad b. ʿAlī. Al-Fakhrī. Edited by ʿAbd al-Qādir Muḥammad Mātū. Beirut: Dār al-Qalam al-ʿArabī, 1418 AH.
  • Khiḍrī, Sayyid Aḥmad Riḍā. Tārīkh-i khilāfat-i ʿAbbāsī. Tehran: Samt, 1383 Sh.
  • Maqdisī, Muṭahhar b. Ṭāhir al-. Al-Bidaʾ wa l-tārīkh. Beirut: Maktabat al-Thiqāfa al-Dīnīyya, [n.d].
  • Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Tanbīh wa l-ishrāf. Edited by ʿAbd Allāh Ismāʿīl al-Ṣāwī. Cairo: Dār al-Ṣāwī, [n.d].
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-.Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad Abū l-Faḍl Ibrāhīm. Beirut: Dār al-Turāth, 1387 AH.
  • Ṭabāṭabāyī, Sayyid Muḥammad Kāẓim. 1392 Sh. "Gūnahā-yi chālish āfarīnī-yi ʿabbāsīyān-i nukhustīn dar masīr-i imāmat." Pazhūhishhā-yi Iʿtiqādī Kalāmī 9:123-142.
  • Ṭaqūsh, Muḥammad Suhayl. Dawlat-i ʿabbāsīyān. Translated to Farsi by Ḥujjat Allāh Jūdakī. Qom: Pazhūhishkada-yi Ḥawza wa dānishgāh, 1383 Sh.
  • ʿUmar, Fārūq. 1383 Sh. "Farhang-i mahdawīyyat dar laqabhā-yi khulafā-yi ʿAbbāsī." Translated to Farsi by Ghulām Ḥasan Maḥramī. Tārīkh-i Islām Dar Āyina-yi Pazhūhish 1:157-184.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. Beirut: Dār Ṣādir, [n.d].