Abdullah al-Dahdouh

Kutoka wikishia
Abdullah al-Dahdouh

Abdullah al-Dahdouh (Kiarabu: عبد الله الدهدوه أو الدحدوح) (1966-2012) alikuwa mmoja wa viongozi wa kidini na mubalighi wa Kishia nchini Ubelgiji. Baada ya kuingia katika madhehebu ya Ahlul-Bayt (Shia) alielekea katika mji wa Qom, Iran kwa ajili ya msomo. Baada ya kusoma masomo ya dini katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Qom na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha al-Mustafa (al-Mustafa International University) alirejea nchini Ubelgiji na kuasisi kituo cha Kiislamu na msikiti wa Imam Ridha (a.s) katika mji wa Brussels na kujishughulisha na ufundishaji na uenezaji wa mafundisho ya Kiislamu. Kuendesha shughuli za kiibada na kidini, kuandika vitabu kadhaa na kulea wanafunzi zaidi ya 200 ni miongoni mwa zilizokuwa harakati za msomi huyu. Abdullah al-Dahdouh aliuawa shahidi 13 Machi 2012 na magaidi wa kitakfiri.

Historia Yake

Abdullah al-Dahdouh (1966 mwafaka na 1344 Hijiria Shamsia) katika mji wa Tangier nchini Morocco. Abdullah ambaye asili yake ni Morocco aliathirika na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s) na hivyo akaingia katika madhehebu ya Kishia. Mwaka 1980 alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) katika mji wa Qom, Iran kwa ajili ya masomo.[1]

Kuhamia Ubelgiji

Abdullah al-Dahdouh baada ya kukamilisha hatua fulani ya masomo na kupata misingi ya kwanza kabisa ya maarifa ya Kiislamu, alifunga safari na kuhajiri kuelekea Ubelgiji kwa ajili ya kufanya tablighi na kueneza mafundisho ya Kiislamu. Sambamba na harakati hizo aliendelea na masomo ya Chuo Kikuu katika moja ya vyuo vikuu vya Ubelgiji na kufanikiwa kupata shahada ya kwanza katika taaluma ya Sayansi Asilia.[2]

Kusoma Tena Qom

Sheikh Abdullah al-Dahdouh baada ya kuishi kwa miaka kadhaa nchini Ubelgiji alikata shauri kurejea tena Iran katika mji wa Qom kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Baada ya kukamilisha duru ya masomo ya fiqhi na maarifa ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha al-Mustafa (al-Mustafa International University) alirejea nchini Ubelgiji na kuanza harakati za kuhubiri na kueneza mafundisho ya dini. Hatua ya kwanza aliyoichukua ilikuwa ni kuasisi kituo cha Kiislamu na kujenga msikiti wa Imam Ridha (a.s) katika mji wa Brussels, ambao ni mji mkuu wa Ubelgiji.[3]

Harakati za Kitablighi

Sheikh Abdullah al-Dahdouh katika kipindi chake chote cha harakati zake, alifanya mambo yenye taathira nzuri mno katika kueneza utamaduni wa Ahlul-Bayt (a.s) na mafundisho yao adhimu na yenye thamani, ambapo miongoni mwazo ni kuendesha shughuli za kiibada na kidini, kuandika vitabu kadhaa kama “al-Hurriyah min wajhat nadhar al-Islam wal-maghrib) sambamba na kufundisha na kulea wanafunzi zaidi ya 200. Aidha hatua nyingine ya Sheikh Abdullah al-Dahdouh ilikuwa ni kuanzisha Taasisi ya Madinat al-Ilm.[4]

Alikuwa pia miongoni mwa watu muhimu katika kuchapisha na kusambaza jarida lililokuwa likichapishwa kwa lugha ya Kifaransa lililojulikana kwa jina la “Shua’a al-Hikmah”. Maudhui kuu za jarida hili zilikuwa ni makala kuhusu fiq’h na itikadi. Jarida hili liliondokea kupendwa na kuwa na wafuasi wengi miongoni mwa Waislamu wa Ulaya.[5] Alikuwa pia mjumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) na alifanya safari katika mataifa mbalimbali ya Ulaya kwa ajili ya kutoa mawaidha na kueneza mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s). Kadhalika Sheikh Abdullah al-Dahdouh alikuwa na ushiriki amilifu katika mikutano ya kimataifa.[6]

Katika kipindi chote cha harakati zake nchini Ubelgiji alifanikiwa kuwafanya mamia ya wananchi wa Ubelgiji na wa Morocco kuwa na ufahamu kuhusiana na madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s) na baadhi ya wanafunzi wake walikuwa wahadhiri katika vyuo vikuu vya Ubelgiji na katika mataifa mengine barani Ulaya.[7]

Sheikh Abdullah al-Dahdouh alihudhuria kikao cha 50 cha Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Ahllu-Bayt (a.s) kilichofanyika Septemba 2011 mjini Tehran na alifanikiwa pia kukutana na Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran.[8]

Kuuawa Shahidi

Abdullah al-Dahdouh aliuawa shahidi 13 Machi 2012 katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels.[9] Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali magaidi wa kitakfiri walishamnbulia msikiti wa Imam Ridha (a.s) na kuuchoma moto. Sheikh Abdullah al-Dahdouh alikufa shahidi katika tukio hilo la kuchomwa moto msikiti wa Imam Ridha (a.s). Mshukiwa mkuu alisema katika vikao vya kesi hiyo mahakamani kwamba, alitaka kulipiza kisasi cha Wasyria wanaouawa na Mashia.[10]

Mwili wa shahidi Sheikh Abdullah al-Dahdouh ulisafirishwa na kuzikwa Tangie, Morocco eneo alilozaliwa.[11] Mahakama ya Ubelgiji ilimhukumu mshukiwa mkuu wa mauaji hayo miaka 27 jela.[12]

Filamu ya Matukio Halisi

Filamu ya matukio halisi iliyokuwa na anuani ya «Phoenix» ilionyeshwa mwaka 2015 katika Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Filamu hii ya matukio halisi ilikuwa ikieleza maisha ya Sheikh Abdullah al-Dahdouh na Mashia wa Ubelgiji.[13] Hadi sasa filamu hii imepata tuzo mbalimbali.

Rejea

  1. Majmau Jahan Ahlul-bayt, Vijyaname Shahadat Hujat al-islam wal-muslimiin Abdullah Dahduh, 1391 SH, Uk. 11.
  2. Zindeginame Shahid Abdullah Dahduh، Shirika la habari la Abna.
  3. Majmau Jahan Ahlul-bayt, Vijyaname Shahadat Hujat al-islam wal-muslimiin Abdullah Dahduh, 1391 SH, Uk. 11.
  4. Majmau Jahan Ahlul-bayt, Vijyaname Shahadat Hujat al-islam wal-muslimiin Abdullah Dahduh, 1391 SH, Uk. 11.
  5. Majmau Jahan Ahlul-bayt, Vijyaname Shahadat Hujat al-islam wal-muslimiin Abdullah Dahduh, 1391 SH, Uk. 11.
  6. Zindeginame Shahid Abdullah Dahduh، Shirika la habari la Abna.
  7. Zindeginame Shahid Abdullah Dahduh، Shirika la habari la Abna.
  8. Zindeginame Shahid Abdullah Dahduh، Shirika la habari la Abna.
  9. Zindeginame Shahid Abdullah Dahduh، Shirika la habari la Abna.
  10. Limadha yanhadir aghalabu al-shia al-mugharabah al-muqimina bibiljika mina-riif؟، Site nadurusity.
  11. Janazah al-Shahid al-Sheikh Abdullah al-Dahduh Taswil Madinah Twanjah al-Maghribiah Site wikalah Abna Buratha
  12. 27 Sanah Sajna Nafidha lil Bukhari Qatil al-Sheikh Abdullah Dahduh Imam Masjid al-Ridha Site chichaouapress
  13. Terur Shahid Abdullah Dahduh Ruhani Shiah dar Beljik Mustanad shud Shirika la habari la Mizani

Vyanzo