Nenda kwa yaliyomo

Zainul-Abidin (Lakabu)

Kutoka wikishia
Makala hii fupi inahusiana na lakabu ya Zainul-Abidin.

Zainul-Abidin ina maana ya “Pambo la Wafanya Ibada”. Hii ni moja ya lakabu mashuhuri kabisa ya Imam Ali bin Hussein Sajjad (as) ambaye ni Imam wa Nne katika mlolongo wa Maimamu 12 wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala na kuipa kwake mgongo dunia (zuhdi).[1]

Imenukuliwa kutoka kwa Anas bin Malik fakihi na mpokezi wa hadithi wa Ahlu Suuna kwamba: Imam Zainul-Abidin kwa usiku mmoja alikuwa akiswali rakaa 1,000 na kutokana na kufanya kwake ibada namna hii alikuwa akiitwa kwa lakabu ya Zainul-Abidin yaani Pambo la Wafanya Ibada.[2] Aidha katika vitabu vya hadithi Imam huyu ametajwa kama Sayyid al-Abidin yaani Bwana wa Wafanya Ibada.[3] Inaelezwa kuwa, katika historia ya Uislamu hakuna mtu aliyewahi kupewa lakabu ya Zainul-Abidin ghairi ya Imam huyu wa nne wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia.[4]

Kwa mujibu wa hadithi zilizokuja katika kitabu cha Ilal al-Sharayi ni kuwa, Imam Sajjad alikuwa akiitwa kwa lakabu hiyo kuanzia karne ya pili Hijria.[5] Ibn Shahab Zuhri, faqihi na mpokezi wa hadithi wa Ahlu Sunna alikuwa akinakili mara kwa mara hadithi kutoka kwa Ali bin Hussein na alikuwa akimtaja kwa lakabu ya Zainu-Abidin. Siku moja Sufiyan bin Uyainah (107-198 Hijria) alimuuliza, kwa nini unamuita Ali bin Hussein kwa lakabu ya Zainul-Abidina? Katika kujibu swali hilo, Zuhri aliashiria hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (saww) ambayo inasema: Katika Siku ya Kiyama mwenye kunadi atanadi, Zainul-Abidin yuko wapi? Nitamuona mwanangu Ali bin Hussein akija akipiga hatua baina ya safu na mkusanyiko wa watu.[6]

Katika kitabu cha Kashful-Ghummah bila ya kutajwa sanadi (mapokezi) ya hadithi yenyewe, imekuja maudhui kuhusiana na kupewa Imam wa Nne lakabu ya Zainul-Abidin ya kwamba: Usiku mmoja alikuwa akiswali Swala za Usiku katika mihrabu, akasikia sauti ikimuita na kukariri mara tatu: أنْتَ زَینُ الْعابدین (Wewe ni “,Pambao la Wafanya Ibada”), baada ya hapo akaondokea kuwa mashuhudi baina ya watu kwa lakabu hii.[7]

Rejea

  1. Qurashi, Hayat al-Imam Zainul-Abidin, 1409 Hijria, Jz 1, uk 145 na 146.
  2. Dhahabi, al-Ibar, Darul-Kutub al-Ilmiyah, Jz.1, uk. 83.
  3. Kama mfano angalia: Sheikh Swaduq, Ilal al-Sharayi, 1385 Hijria Shamsia, Jz. 1, uk. 132.
  4. Qurashi, Hayat al-Imam Zainul-Abidin, 1409 Hijria, Jz. 1, uk. 187.
  5. Sheikh Swaduq, Ilal al-Sharayi, 1385 Hijria Shamsia, Jz. 1, uk. 229-230.
  6. Sheikh Swaduq, Ilal al-Sharayi, 1385 Hijria Shamsia, Jz. 1, uk. 229-230.
  7. Ardabili, Kashful-Ghummah, 1421 Hijria, Jz. 2, uk. 619.

Vyanzo

  • Ardabili, Kashful-Ghummah Fi Maarifat al-Aimah, Radhii, 1421 Hijria.
  • Dhahabi, Muhammad bin Ahmad, al-Ibar Fi Khabar Man Ghabar, mhakiki: Abu Hajar Muhammad Said bin Zaghlul, Beirut, Darul-Kutub al-Ilmiyah, Bita.
  • Sheikh Swaduq, Muhammad bin Ali, Ilal al-Sharayi, Qum, Duka la Vitabu la Davari, 1385 Hijria/1966 Miladia.
  • Al-Qurashi, Baqir Sharif, Hayat al-Imam Zainul-Abidin, Beirut, Darul-Adh’waa, 1409 Hijria.