Tahniki kwa mtoto mchanga
Tahniki kwa mtoto mchanga (Kiarabu تحنيك المولود): Ni mila maalumu ya Kiislamu inayotekelezwa kwa kuweka kiasi kidogo cha maji au chakula kwenye kinywa cha mtoto mchanga punde tu baada ya kuzaliwa kwake. Kwa mujibu wa mafundisho ya wanazuoni wa Kishia, tahniki inapaswa kufanywa kwa kutumia maji ya Mto Furati pamoja na udongo mtakatifu wa Imamu Hussein (a.s) (udungo wa Karbala), kwa mujibu wa maoni yao, kufanya hivyo ni miongoni mwa amali za sunna. Kuna Riwaya kadhaa zinabainisha kwamba; mtu aliyefanyiwa tahniki kwa kupitia maji ya Mto Furati atapata hatima njema ya kuwa mfuasi wa madhehebu ya Kishia na kuwa mpenzi wa Ahlul-Bayt (a.s).
Ufahamu wa Dhana ya Tahnik
Tahniki ni desturi inayohusisha zoezi la upakaji au uwekaji wa kiasi kidogo cha chakula chepesi kwenye kinywa cha mtoto mchanga kiwango ncha ya kidole, kisha kudidimiza kidole hicho kwenye sehemu ya juu ya kinywa cha mtoto huyo. [1] Kawaida, zoezi hili hufanywa na mkunga au mtu mwengine asiyekuwa yeye. [2] Katika tamaduni za jamii mbalimbali, desturi hii inajulikana kwa majina tofauti, ikiwa ni pamoja na; tahniki, kuondoa kinywa, [3] sunna ya kufungua au kupanua kinywa. [4] Katika muktadha wa imani za kidini na kijamii, zoezi la kufanya tahniki linaaminika kuwa na manufaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na; kuimarisha afya ya mtoto, kurahisisha unyonyaji au ufyonzaji wa maziwa ya mama, kuzuia matatizo ya kusema (ulimi), kama vile kigugumizi, pamoja na kuweka msingi wa malezi ya kidini katika maisha ya baadae. [5] Kulingana na mafundisho ya wanazuoni wa Kishia, yaliofafanuliwa katika fiqhi ya ndoa, tahniki ni amali inayofa nyiwa mtoto mchanga mara tu baada ya kuzaliwa. [6]
Umuhimu wa Tahniki Katika Wasa’il al-Shi‘a, ambacho ni mojawapo ya vitabu maarufu vya Hadithi za Kishia, kuna sehemu mahususi iliotengwa kwa ajili ya kufafanua umuhimu wa tahniki kwa watoto wachanga, pamoja na hukumu zake za kisharia kuhusiana na zoezi hilo. [7] Pia kuna Hadithi kadhaa zinathibitisha kwamba; mtoto anayefanyiwa tahniki kupitia maji ya Mto Furati atapata hatima ya kuwa Mshia na mwenye mapenzi thabiti kwa Ahlul Bayt (a.s). [8] Hata hivyo, zoezi la kuwanyia watoto tahniki, si desturi iliyobuniwa ndani ya Uislamu; bali mila hiyo ilikuwepo miongoni mwa mataifa mbalimbali hata kabla ya kuja kwa Uislamu. [9] Baadhi ya tafsiri za Kisunni katika kufasiri Aya ya 25 ya Suratu Maryam, zimeeleza kwamba; desturi ya tahniki kupitia tende ilianzishwa kutokana kule Bibi Maryam kula tende wakati wa kumzaa Nabii Isa (a.s). [10] Katika zama za mwanzoni mwa Uislamu, Masahaba walikuwa na ada ya kumchukua mtoto mchanga na kumpeleka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) mara tu baada ya kuzaliwa kwake, naye bwana Mtume (s.a.w.w) alikuwa akimpokea mtoto huyo na kumfanyia tahniki kwa kutumia tende, kisha kuhitimisha amali hiyo kwa kumwombea dua. [11] Desturi hii ilipata msisitizo wa kipekee katika enzi za Maimamu wa Kishia, ambapo ilihimizwa kufanya tahniki kupitia maji ya Mto Furati. Baada ya kuuawa kwa Imam Hussein (a.s), Mashia walisisitizwa kutumia turbah (udongo mtakatifu wa Karbala) katika zoezi hilo la tahniki, jambo ambalo lilisisizwa na kupewa kipau mbele na Maimamu hao. [12] Katika jamii ya Wairani, desturi hii imeingatiwa kwa kina katika imani na mila zao za kijamii, ikichuwa nafasi maalumu katika uwanja wa fasihi na tamaduni zao. [13] Kuna imani ya jadi isemayo kwamba: tahniki inastahili kufanywa na mtu mwenye uadilifu na nafasi maalumu na inayohimidiwa katika jamii, kwa kuwa inadhaniwa kuwa jambo hilo lina ushawishi wa moja kwa moja katika malezi na mustakabali wa mtoto mchanga. [14]
Adabu na Hukumu za Kifiqhi Kuhusu Tahniki Kuna Hadithi mbalimbali zinaonyesha jinsi tahniki ilivyotekelezwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w) pamoja na Maimamu wa kutoka upande wa Ahlul Bayt (a.s). Kulingana na moja ya Riwaya kutoka kwa Imamu Ali (a.s.), ni kwamba; bwana Mtume (s.a.w.w) alimfanyia tahniki Imamu Hassan (a.s.) na Imam Hussein (a.s.) kwa kutumia tende mara tu baada ya kuzaliwa kwao. [15] Vile vile, kuna Hadithi iliyomepokewa kutoka kwa Imamu Musa al-Kadhim (a.s.), ya kwamba; Baada ya kuzaliwa kwa Imamu Al-Ridha (a.s), Imamu Musa al-Kadhim (a.s) ndiye aliyemfanyia tahniki mwanawe huyo, kwa kutuia maji ya Mto Furati. [16] Kulingana na mafundisho mafaqihi wa upande wa madhehebu ya Kishia, tahniki ni sunna inayopendekezwa kufanywa mara tu baada ya kuzaliwa kwa mtoto na kabla ya kumpatia jina rasmi. [17] Sunna hii inastahili zaidi kufanywa kwa maji ya Mto Furati pamoja na turbah ya Imamu Hussein (a.s) (udongo mtakatifu wa Karbala). [18] Iwapo maji ya Furati hayapatikani, basi maji matamu (maji safi) ndiyo yanayopendekezwa kutumika badala yake. Endapo maji yaliyopo yatakuwa ni maji yenye chumvi nyingi, basi inashauriwa yachanganywe na kiasi kidogo cha tende au asali ili kupunguza athari zake. [19] Pia Katika madhehebu ya Kisunni, tahniki inachukuliwa kuwa ni sunna inayostahili kufanywa mara tu baada ya kuzaliwa kwa mtoto. Ibn Qayyim al-Jawziyya, mmoja wa wanazuoni maarufu wa Kisunni, ameitaja tahniki kama ni moja ya amali zinazopendekezwa wakati wa kuzaliwa kwa mtoto, akizingatia mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) pamoja na Masahaba zake katika suala hilo. [20]