Qassim bin Habib al-Azdi
Qassim bin Habib bin Abi Bishr al-Azdi (Kiarabu: القاسم بن حبيب بن أبي بشر الأَزْدِيّ) ni mmoja wa mashahidi wa Karbala. Sheikh Tusi katika kitabu chake cha Rijaal al-Shia amemtaja kuwa mmoja wa masahaba wa Imamu Hussein (a.s). [1]
Katika kitabu cha Ibsar al-Ain fi Ansar al-Hussein, Muhammad Samawi amemtaja Qassim kuwa mmoja wa Mashia na wapiganaji shupavu wa mji wa Kufa. [2] Kwa mujibu wa Samawi ni kuwa, Qassim aliondoka pamoja na Omar bin Sa’d kuelekea Karbala, lakini alipowasili Karbala alijiunga na Imamu Hussein na kuwa pamoja naye mpaka Siku ya Ashura alipouawa shahidi katika shambulio la kwanza. [3] Wakati wa Qassim kujiunga na Imamu Hussein umetajwa kuwa ni siku ya tano Muharram au ya siku ya sita Muharram. [4] Umri wake wakati anaaga dunia umetajwa kuwa ni miaka 40. [5]
Shahidi huyu anasalimiwa na kutolewa salamu katika Ziyarat al-Shuhadaa [6] na Ziyarat Rajabiyah ya Imam Hussein (a.s) [7] kwa ibara ya:«السَّلَامُ عَلَى قَاسِمِ بْنِ حَبِیبٍ الْأَزْدِی» Amani (ya Mwenyezi Mungu) iwe juu ya Qassim bin Habib al-Azdi.
Qassim alikuwa akitokana na kabila la Azd. [8] Katika Ziyara ya Rajabiyah [9] kuna mtu ametajwa kwa jina la Qassim bin Harith ambapo inaelezwa kuwa kuna uwezekano mkusudiwa ni Qassim bin Habib. [10] Kadhalika katika kitabu cha Tasmiya Man Qutila Maa al-Hussein (kiliandikwa karne ya 2 Hijiria) kuna mtu ametajwa kwa jina la Qassim bin Bishr kwamba, ni mmoja wa mashahidi wa Karbala [11] ambapo inaelezwa kwamba, mkusudiwa ndio huyo huyo Qassim bin Habib. [12] Jina lake limetajwa pia kwamba, ni Qassim bin Bashir. [13]