Niaba katika Hija
Niaba katika Hija: Ni dhana inayojulikana pia kwa jina la Hija ya niaba, nayo ni tendo la kutekeleza ibada ya Hija kwa niaba ya mtu mwingine. Kwa kufanikisha ibada hii kwa njia ahihi na kwa kufuata masharti yake maalumu ya kidini, wajibu wa amali ya Hija huondolewa kutoka kwa mtu anayefanyiwa ibada hiyo kwa njia ya niaba.
Katika muktadha wa amali ya Hija ya farḍhi (siyo umra), yaruhusiawa mtu fulani kutekeleza Hija ya mtu mwengina kwa niaba yake, hata kama mtu huyo atakuwa hai, ilimradi mtu huyo hana uwezo wa kutekeleza ibada hiyo yeye mwenyewe, kutokana na sababu za kimwili au sababu nyenginezo.
Endapo mtu atafariki kabla ya kutekeleza Hija ambayo ilikuwa ni wajibu wake kuitekeleza Hija hiyo, au kama yeye mwenyewe atakuwa ameusia kwamba ibada hiyo itekelezwe kwa niaba yake, basi warithi wake watawajibika kumchagua mwakilishi wa kutekeleza Hija hiyo kwa niaba yake. Hata hivyo, wajibu huu unazingatiwa tu pale ambapo mali ya marehemu huyo takuwa inatosha kugharamia Hija hiyo. Iwapo mali hiyo ni ya kiasi kidogo kuliko gharama za Hija, hapo hapatakuwa na ulazima wa kutekeleza jukumu.
Katika ibada ya Hija itekelezwayo kwa niaba, ni lazima pande zote mbili—yule anayefanyiwa ibada hiyo kwa niaba na yule wake mwakilishi—wawe ni Waislamu. Aidha, mwakilishi anatakiwa kuwa ni mtu mwenye akili timamu, asiye na wajibu wa kutekeleza Hija ya faradhi kwa niaba yake mwenyewe. Hata hivyo, kuna tofauti za maoni miongoni mwa mafaqihi kuhusu uhalali wa mwakilishi wa ibada hiyo ya Hija kwa nia ya niaba ya mwingine, hali ya kwamba yeye mwenyewe hajawahi kutekeleza wajibu wake wa amali ya Hija.
Iwapo mwakilishi atafariki baada ya kuvaa ihram na kuingia msikiti mkuu wa Makka, jukumu la Hija hiyo litaondoka juun ya shingo ya za wote wawili (mwakilishi pamoja na mwakilishwaji). Aidha, ni halali kwa watu kadhaa kutekeleza Hija kwa niaba ya mtu mmoja, lakini haikubaliki kwa mtu mmoja kuwa mwakilishi wa watu kadhaa katika kuwatekelezea amali Hija ya faradhi. Ila si tatizo kwa mtu huyo mmoja kufanya hivyo iwapo atakuwa anawatekelezea wawakilishwa wake amali ya Hija ya umra (Hija ya Sunna). Mwakilishi pia anapaswa kutekeleza Hija kulingana na maoni ya marja' taqlid wake yeye mwenyewe, yaani atekeleze Hija hiyo kulingana na fatwa za mwanazuoni anayemfuata katika utendaji wa amali zake mbali mbali.
Dhana na Umuhimu wa Hija kwa Niaba
Hija kwa niaba ni aina ya uwakilishi katika utendaji wa amali za kiibada, ambapo mtu mmoja hutekeleza ibada ya Hija kwa niaba ya mtu mwingine. [1] Dhana hii imeelezwa katika mbali mbali, vikiwemo vitabu vya Hadithi [2] na vitabu vya fiq’hi [3], ambavyo vimetenga sura maalum ndani yake zinazohusiana na masuala ya uwakilishi katika ibada ya Hija. Baadhi ya Hadithi zinaeleza kuwa; mtu anayetekeleza Hija kwa niaba ya mwingine hupata ujira mkubwa wa thawabu, ujira ambao unalingana na ujira wa amali tisa au kumi za Hija, hali ya kwamba yule anayefanyiwa Hija hiyo kwa niaba yake, hupata thawabu za Hija moja tu. [4] Mbali na uwakilishi wa Hija kwa ujumla, vitabu vya fiqh pia vinajadili juu ya suala la uwakilishi wa baadhi ya sehemu ya ibada maalum ndani ya Hija, zikiwemo amali ya tawafu, sala inayofuatia baada ya amali ya tawafu, pamoja na sa’y (kukimbia baina ya Safa na Marwa), ambapo uwakilishi wa kutenda amali hizi huwa unaruhusiwa kufanyika chini ya masharti fulani. [5]
Hukumu ya Hija kwa Niaba
Kwa mujibu wa maelezo ya Muhammad Hassan Sharif Isfahani, mjuzi wa sheria za Kiislamu wa karne ya 13 Hijria, ajulikanaye kwa jina la Sahib Al-Jawahir, ni kwamba; Hakuna tofauti kubwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu kuhusiana na uhalali wa amali ya Hija kwa niaba ya mtu fulani. [6] Kisheria, hakuna tatizo juu ya amali ya kutekeleza amali ya Hija kwa niaba ya mtu mwengine, iwe kwa hiari ya mtekeleza wa Hija hiyo, au kwa ombi la mtu mwenye kutekelezewa amali hiyo. [7] Hata hivyo, iwapo mtu atakubali kutekeleza amali ya Hija kwa niaba ya mwingine kwa malipo fulani, katika hali hiyo inakuwa ni wajibu kwake kutekeleza ibada hiyo kwa mujibu wa makubaliano waliokubaliana baina yao. [8]
Ni halali kwa mtu fulani kutekeleza amali ya Hija kwa niaba ya mtu aliyefariki dunia, iwe n ibada ya Hija ya wajibu (faradhi) au Hija ya Sunna ya tamattu'. Aidha, ni halali kutekeleza amali ya Hija Sunna kwa niaba ya mtu aliye hai. Hata hivyo, kumtekelezea mtu fulani amali Hija ya faradhi kwa niaba ya yake, hali yeye uwezo wa kutekeleza amali hiyo. Hivyo basi, ikiwa yeye mwenyewe hana uwezo wa kutekeleza Hija, kwa sababu ya matatizo ya kiafya au kifedha, basi hakutakuwa na tatizo juu ya mtu fulani kumtekelezea amali hiyo kwa niaba yake. [9]
Kulingana na mafaqihi wa madhehebu ya Shia, ni wajibu kwa mtu mwenye hali zifuatazo, kuweka wakili wa kumtekelezea amali zake za Hija:
1. Mtu aliye hai ambaye ana uwezo wa kutekeleza amali ya Hija kisha akawa hakutekeleza wajibu wake: Mtu yeyote mwenye uwezo wa kutelkeleza amali ya Hija kisha akawa hajakwenda kuitekeleza amali hiyo, [10] huku yeye mwenyewe akaelewa kwamba; yeye mwenyewe -kwa sababu za ugonjwa fulani au kwa sababu nyingine alizokuwa nazo- hataweza kwenda kuitekeleza ibada hiyo, hapo mtu huyo ni lazima aweke wakili fulani wa kumtendea amali zake za Hija. [11]
2. Mtu aliyefariki dunia ambaye alikuwa tayari amesha ambatwa na wajibu wa kufanya Hija: Ikiwa mtu aliyekufa alikufa huku akiwa ameelemewa na wajibu wa kufanya Hija, kisha kukawa hakuna mtu mwengine aliyefanya amali hiyo kwa niaba yake bila malipo, basi warithi wake watawajibika kumtafuta wakili kwa kutumia mali ya marehemu kwa ajili ya amali hiyo, isipokuwa tu iwapo mali ya marehemu itakuwa haitoshi kumlipa wakili wa kumtekelezea amali hiyo. [12]
3. Mtu aliyefariki dunia akiwa bado hajaambatwa na wajibu wa Hija ila aliagiza afanyiwe amali hiyo kwa niaba yake: Ikiwa mtu aliyefariki dunia aliagiza kufanyiwa amali ya Hija kwa niaba yake, na gharama za wakili zikawa hazizidi theluthi moja ya mali yake, warithi wa maiti huyo wanawajibika kufuata maagizo yake akama alivyotaka yeye mwenyewe. [13]
Masharti ya Mtu Anayetekeleza Hajj kwa Niaba na Mtu Anayetekelezewa
Kulingana na Mjuzi wa Sharia, al-Shaykh al-Jawahir, masharti ya mtu anayetekeleza Hajj kwa niaba ya mwingine ni kuwa Muislamu, mwenye akili timamu, na asiwe na wajibu wa kufanya Hajj mwenyewe. [14] Wataalamu wengine wa dini wanaongeza kuwa ni lazima awe baligh, mwenye imani, awe na uelewa wa hukumu za Hajj, na asiwe na udhuru wa kutofanya baadhi ya ibada za Hajj. [15]
Kwa mujibu wa maimamu wengi, mwanamume au mwanamke yeyote anaweza kuwa wakili wa mwanamume au mwanamke mwingine. [16] Hata hivyo, ikiwa Hajj inafanywa kwa niaba ya mtu aliye hai, mtu huyo lazima awe hana uwezo wa kufanya Hajj mwenyewe, lakini si lazima awe baligh au mwenye akili timamu. [17]
Masharti ya Pande Mbili Kati ya Mtekelezaji Hija kwa Niaba na Mtekelezewa
Kwa mujibu wa maelezo ya Sahibu al-Jawahir, masharti muhimu kwa mtu anayetekeleza Hija kwa niaba ya mwingine ni kama ifuatavyo:
1. Awe Muislamu.
2. Awe mwenye akili timamu.
3. Asiwe na wajibu wa kufanya Hija yake mwenyewe shingoni mwake. [14]
Wanazuoni wengine wa Kiislamu wameongeza masharti mengine zaidi, yakiwemo:
- Awe baligh (amefikia umri wa kubaleghe).
- Awe na imani kamili (awe Shia Ithnaasharia).
- Awe na uelewa wa hukumu za Hija.
- Asiwe na udhuru unaoweza kumzuia kutekeleza baadhi ya amali za Hija. [15]
Kwa mtazamo wa mafaqihi walio wengi, ni kwamba; mtu yoyote yule awe mwanamme au mwanamke anaweza kuchuwa uwakili wa mwanamume au mwanamke mwingine katika kutekeleza amali ya Hija kwa niaba yake. [16] Hata hivyo, endapo Hija hiyo inafanywa kwa niaba ya mtu aliye hai, sharti kuu la amali hiyo ni kwamba; mtu anayefanyiwa amali hiyo, ni lazima awe tayari ameshafariki, au kama akuwa bado yuhai, ni lazima awe hana uwezo wa kutekeleza Hija hiyo yeye mwenyewe, ima ni kwa sababu ya maradhi au kwa sababu nyenginezo. [17] Pia kuna wanazuoni wanaoamini kwamba; kuna uwezekano wa mtu fulani kumtekelezea ibada ya hija mtu fulani ambaye bado hajabalehe au hana akili timamu. [18]
Uwakili wa Sarurah
Sarura ni istilahi maalumu inayotumika ndani ya vitabu vya kifiqhi, ambayo humaanisha mtu ambaye bado hjawahi kwenda Hija, yaani hajawahi kutekeleza ibada ya Hija maishani mwake. [19] Kuna khitilafu za maoni kuhusiana na unaibu wa yule ambaye hajaelemewa na wajibu wa amali ya Hija shingoni mwake (Sarurah).
Mitazamo ya Wanazuoni Kuhusiana na Sarurah
1. Mtazamo wa Shaikh Tusi
Shaikh Tusi mwanazuoni wa Kishia wa karne ya tano Hijiria, anaeleza kwamba; mwanamke ambaye hajawahi kufanya Hija (Sarurah) hana sifa za kuwa wakili wa kufanyia mtu fulani amali hyo kwa niaba, iwe mwakilishwa huyo ni mwanamke au mwanamume. [20] [21]
2. Mitazamo Tofauti
Wanazuoni wengine wana mtazamo tofauti kuhusiana na suala hili, wengine wanasema kuwa; hakuna tatizo kwa mwanamke fulani ambaye hajawahi kwenda Hija, kuwa wakili wa kutekeleza amali Hija kwa niaba ya mtu mwingine. [22]
3. Uwakili kwa Mtu Aliye Hai
Kuna pia maoni kutoka kwa baadhi ya wanazuoni yasemayo kwamba; endapo mtu aliye hai atahitaji kumchagua wakili wa kumtendea amali ya Hija, kutokana na udhaifu wake wa kutoweza kutekeleza amali hiyo, basi ni lazima amchague wakili ambaye hajawahi kufanya amali ya Hija (Sirurah). [23]
Hukumu za Niaba Katika Hajj
Kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wengi wa fiqh, baadhi ya hukumu za Hajj ya niaba ni kama ifuatavyo:
1. Njia za Kufanya Amali ya Hija kwa Niaba:
Amali ya Hija itendwayo niaba, inaweza kufanyika; bila malipo, kwa mkataba wa malipo maalumu (ijara ambao unaweza kuwa si wa kifedha wali si wa kimali), au kupitia makubaliano maalum ya kifedha au mali maalumu (ja'ala). [24]
2. Kutekeleza Hajj kwa Usahihi:
Wajibu wa Hija hauwezi kuondoka juu ya shingo ya mtu mwenye kutekelezewa Hija hiyo, (manub 'anhu), isipokuwa baada ya kutekelezwa kwa usahihi ibada hiyo na yule aliye chukuwa jukumu la kuitekeleza ibadahiyo kwa niaba. Hii inamaanisha kwamba; mkataba wa malipo katika ya wahusika na mtekelezaji huyo, hauwezi kutosheleza katika kuundoa jukumu hilo juu ya shingo ya mtendewa amali hiyo. [25]
3. Kifo cha Mwajibikaji (Mwakilishi) Baada ya Ihram:
Endapo mwakilishi kwa niaba atafariki baada ya kuingia katika ihram na kuingia katika eneo takatifu la msikiti wa Makka, Hajj hiyo ya niaba inakubalika, na wajibu wa Hija utakuwa umeshaondoka juu ya shingo za wote wawili; mwakilishi pamoja na mwakilishwa wa amali hiyo. [26]
4. Kurejea kwa Uwezo wa Kuhiji Mtu Aliye Hai:
Iwapo mtu aliye hai alimteua mwakilishi fulani ili amhijie Hija yake kwa sababu ya udhaifu aliokuwa nao, kisha baadae hali yake ikarejea kuwa ni ya kawaida, kwa maoni ya wanazuoni wengi, mtu huyo ni lazima aitekeleze tena Hija yake hiyo iliyotendwa kwa niaba yake. Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wanasema kuwa; Hija iliyofanywa kwa niaba yake inatosheleza, na wala hakuna haja ya kurudia tena amali hiyo. [27]
5. Niaba ya Mtu Mmoja Kuwahijia Walio Wengi na Kinyume Chake:
Hakuna tatizo mtu mmoja kuwa naibu wa watu kadhaa katika amali ya Hija ya Sunna, ila jambo hili halikubaliki katika Hija ya wajibu. [28] Hata hivyo, hakuna tatizo unaibu wa watu kadhaa wa kumtekelezea amali ya Hija mtu mmoja, iwe ni Hija ya faradhi au ya Sunna, ili mradi masharti ya amali hiyo yawe yatimizwa. [29]
6. Kutoa Thawabu za Hija kwa Wengine:
Inawezekana mtu kutoa thawabu za Hija ya faradhi au ya Sunna kwa mtu mmoja au watu kadhaa, iwe aliweka nia za kutoa thawabu za Hija yake kabla au baada ya kutekeleza Hija hiyo. [30]
7. Kumwainisha Anayekusudiwa Kufanyia Hija kwa Niaba:
Ni lazima mtu anayefanyiwa amali ya Hija niaba (manub 'anhu) atajwe katika nia ya amali hiyo, lakini si lazima jina lake litajwe kwa matamshi katika kila sehemu ya ibada hiyo, bali ni vyema kufanya hivyo, na ni jambao linalopendekezwa (mustahab). [31]
8. Tofauti za Maraji' al-Taqlid:
Endapo mwakilishi na mtu anayefanyiwa Hija kwa niaba yake watakuwa wanafuata fatwa za marja' (Wanajitahidi) tofauti katika amali zao, mwakilishi anatakiwa kutekeleza Hija hiyo kwa mujibu wa maoni ya marja' (Mujitahidi) wake yeye mwenyewe. [32] Pia, kama kutatokea makosa au jambo fulani litakalosababisha kafara fulani katika kutekeleza ibada hiyo, gharama za kafara hiyo zitatakiwa kubebwa na mwakilishi wa Hija hiyo. [33]