Al-Mus'haf al-Othmani

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Msahafu wa Othmani)
Picha ya nakala ya Qur'an huko Misri, ambayo inadaiwa kutoka katika maandishi ya Othmani

Mus'haf Othmani (Kiarabu: المصحف العثماني) ni nakala ya Qur'an Tukufu iliyoandikwa kwa amri ya Othman bin Affan. Baadhi wameiita kwa jina la Misahafu ya Othman na wengine wameiita kwa jina la Msahafu wa Imamu. Sababu ya kukusanywa msahafu huu ilitokana na kuweko nakala tofauti za Qur'an baina ya Waislamu na ambayo ilikuwa ikitofautiana. Baada ya msahafu wa Othman kukamilika, misahafu mingine iliteketezwa kwa amri ya Othman. Kwa mujibu wa mtazamo mashuhuri, wakusanyaji wa msahafu wa Othman walikuwa watu wanne ambao ni Zayd bin Thabit, Abdallah ibn Zubayr, Said bin A'as na Abdul-Rahman bin Harith.

Masahaba na Maimamu wa Waislamu wa madhehebu wa Shia hawakupinga suala la kufanywa msahafu kuwa mmoja kama ambavyo hawakupinga msahafu wa Othman; ingawa walikosoa kuhusiana na mbinu na mtindo wa kuandikwa kwake na baadhi ya maneno yake. Kwa mujibu wa wahakiki wa masuala ya Ulum al-Qur'an (Sayansi ya Qur'an) kuna makosa ya kiuandishi (kiimla) katika msahafu wa Othman. Hata hivyo wanaamini kwamba, hiyo haina maana ya kupotoshwa Qur'an; kwani maneno ya Qur'an yamehifadhiwa na kubakia (hayajapotoshwa).

Idadi ya misahafu ya Othman imetajwa kuwa nii nne hadi tisa. Kila moja kati ya misahafu hii ya Othnman ulitumwa katika moja ya miji muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu ili ukawe chanzo na marejeo ya usomaji wa Qur'an. Hii leo athari ya misahafu hiyo haipo; lakini kuna nakala ambazo zimeandikwa kwa kunakili nakala hizo ambapo ndio hii misahafu iliyoenea leo baina ya Waislamu. Kwa maana kwamba, misahafu ya leo imechapishwa kwa mujibu wa nakala hizo.

Kutokea Misahafu

Kadhalika angalia: Msahafu na uandikaji wa Qur'an

Mus'haf (msahafu) ni katika majina ya Qur'an ambapo kwa mujibu wa ripoti za vyanzo vya historia ilianza kuitwa hivyo kuanzia zama za Abu Bakr. [1] Kwa mujibu wa watafiti wa masuala ya Qur'an, uandikaji wa Qur'an na kuwa katika nakala moja hakukufanywa na Mtume (s.a.w.w). Mtume (s.a.w.w) alikuwa ameainisha Aya na majina ya sura za Qur'an; lakini kukusanya Qur'an katika maandiko ya kujitegemea, kupanga mpangilio wa Sura ni kazi iliyofanywa baada yake na kwa mtazamo wa masahaba; [2] kwa namna hii kwamba, baada ya kuaga dunia Bwana Mtume (s.a.w.w) kila mmoja wa masahaba zake alijihusisha na kukusanya sura za Qur'an. [3] Kwa utaratibu huo kukajitokeza misahafu mingi. [4] Msahafu wa Ali, msahafu wa Abdallah bin Mas'oud, msahahu wa Ubay bin Kaab, msahafu wa Abu Mussa al-Ash'ari na msahahu wa Miqdad As'wad ni katika misahafu mashuhuri zaidi ya Qur'an. [5]

Sababu ya Kuandika Msahafu wa Othman

Ni kwa sababu misahafu ya masahaba ilikuwa ikitifautiana katika mpangilio na usomaji, na hilo lingepelekea kuibuka hitilafu na tofauti kubwa miongoni mwa Waislamu katika suala la Qur'an. Ingekuwa kila kundi miongoni mwa makundi hayo lingedai kwamba, qiraa ya Qur'an yake ni sahihi na nyinginezo sio sahihi na ni za bandia. [6] Sayyid Muhammad Baqir Hujjati mtafiti wa Ulum al-Qur'an amenukuu kutoka kwa Tabari ya kwamba, mzozo wa Waislamu kuna wakati umepelekea kukufurishana. [7]

Ili kuondoa tatizo hilo, Othman bin Affan aliteua kundi fulani la masahaba na kulipa jukumu kuandika na kukusanya Qur'an moja kutoka katika nakala za Qur'an zilizopo. [8] Kadhalika alitoa amri ya kukusanywa nakala zote za Qur'an zilizoko katika maeneo mbalimbali ya Kiislamu na kuteketezwa. [9]

Wakati wa Kukusanywa

Kuna tofauti za kimitazamo kuhusiana na wakati na zama ambazo msahafu wa Othman ulikusanywa. Ibn Hajar al-Asqalani, mtaalamu na mpokezi wa hadithi mfuasi wa Shafii wa karne ya 8 na 9 Hijiria anasema kuwa, hilo lilifanyika mwaka wa 25 Hijiria; [10] lakini kwa mujibu wa Ibn Athir mwanahistoria wa karne za 6 na 7 Hijiria, msahafu wa Othman ulikusanywa mwaka wa 30 Hijria. [11] Baadhi ya watafiti wa Ulum al-Qur'an wakitumia ushahidi na nyaraka wanasema kuwa, madai kwamba, msahafu wa Othman ulikusanywa mwaka 30 Hijiria si sahihi. [12] Miongoni mwa ushahidi huo ni kwamba, Said bin A'as mmoja wa kundi lililokusanya msahafu huo wa Othman hakuweko Madina kuanzia mwaka 30-34. [13] Wao wanaamini kwamba, mwaka wa kuanza kazi ya kukusanya na kuandika msahafu wa Othman ulikuwa 25 Hijiria [14] au mwishonii mwaka wa 24 Hijria. [15] Kazi hiyo ilimaliizika mwaka wa 30 Hijria. [16]

Wakusanyaji

Kuhusiana na mtu au watu waliokuwa na jukumu la kukusanya na kuandika msahafu wa Othman kuna ripoti mbalimbali. Baadhi wanasema, Zayd bin Harith pekee ndiye aliyepewa jukumu la kazi hiyo. Baadhi wanasema, mbali na yeye Said in A's alishiriki pia katika kazi hiyo. Kundi jingine linasema Ubayy pia alishirikiana na masahaba hao wawili katika kazi hiyo, [17] na kundi jingine linataja majina ya watu watano kwamba, ndio waliofanya kazi hiyo, huku wengine wakisema walikuwa 12 kutoka miongoni mwa Makureshi na Ansari. [18]

Baadhi wanasema kuwa, ripoti yenye itibari zaidi ni nukuu ya Anas bin Malik na Aslam, kijakazi aliyeachiliwa huru wa Omar ibn al-Khattab ambao walikuwa wakishirikiana na kundi lililokuwa na jukumu la kukusanya na kuandika msahafu wa Othman. [19] Kwa mujibu wa ripoti hiyo, waliofanya kazi hiyo walikuwa watu wanne ambao ni Zayd bin Thabit, Abdallah ibn Zubayr, Said bin A'as na Abdul-Rahman bin Harith. [20] Muhammad-Hadi Maarefati, mtafiti wa Ulum al-Qur’an na mwandishi wa kitabu cha al-Tamhid fi Ulum al-Qur’an, akifafanua sababu ya kuweko hadithi ya watu 12 ameandika: Watu hawa wanne wasingeweza kufanya kazi hii na kwa msingi huo wakaomba msaada kutoka kwa watu wengine kama Abdallah bin Abbas na Anas bin Malik. [21]

Zayd ibn Harith alikuwa kiongozi wa kundi hilo. [22] Yeye anatokana na Ansari na mmoja wa watu wa kuaminika kwa Othman na alikuwa msimamizi wa Hazina ya Dola (Beit al-Mal). [23] Watu wengine watatu wa kundi hili wote walikuwa wanatokana na Makureshi na walikuwa wakwe wa Othman (walioa kwa Othman). [24] Abdallah bin Mas’oud mmoja wa masahaba mahiri wa Mtume (s.a.w.w) alilalamikia na kupinga mno kuchaguliwa watu hawa. Alikuwa akisema kuhusiana na kuchaguliwa Zayd bin Harith kuongoza kundi hilo ya kwamba: Uandishi na ukusanayaji wa Qur’an umekabidhiwa kwa mtu ambaye wakati mimi ninasilimu yeye alikuwa bado hajazaliwa. [25]

Mbinu ya Ukusanyaji

Kulingana na ripoti za kihistoria, Msahafu Othman ulikusanywa kwa kutegemea Msahafu ambao uliandikwa katika kipindi cha Abu Bakr. Hata hivyo kando na hilo, kulizingatiwa pia nakala za Surah za Qur'ani zilizoandikwa wakati wa Mtume (s.a.w.w) na pia ulizingatiwa Msahafu wa Ubayy. [26] Othman aliwaambia wajumbe wa kundi hilo kwamba, ikiwa kutaibuka hitilafu baina yao kuhusiana na neno fulani, fanyeni kwa mujibu wa lahaja ya Kikureshi; kwa sababu Qur’an iliteremshwa kwa lahaja ya Kikureshi. [27]

Kwa mujibu wa Mahmoud Ramyar, mwandishi wa kitabu Tarikh Qur’an (Historia ya Qur'an), ukusanyaji na uandishi wa msahafu wa Othman ulifanywa kwa uangalifu mkubwa. [28] Alimnukuu Malik bin Abi Amir kwamba, wakati wowote waandishi walipopata tofauti ya maoni katika Aya fulani, walikuwa wakiacha wazi sehemu yake katika msahafu mpaka wawapate watu ambao walisikia Aya hiyo kutoka kwa Mtume na wawe na uhakika wa kuandika Aya hiyo. [29] Régis Blachère mtaalamu mambo ya nchi za mashariki wa Kifaransa na mfasiri wa Qur'ani kwa Kifaransa; ameandika: Bila shaka, waandishi wa msahafu wa Othman walihisi kuwa na jukumu kubwa na waliandika kwa tahadhari, uangalifu mkubwa na usahihi. [30]

Ukosoaji

Pamoja na hayo yote, Muhammad-Hadi Maarefat amekosoa mbinu na mtindo uliotumika kuandika msahafu huu. Anasema kuwa, katika kazi hii hali ya kutokuwa makini ilijitokeza na kwa msingi huo katika misahafu ya Othamn kuna makosa mengi ya kiuandishi. [31] Kadhalika misahafu hii haikulinganishwa na kwa muktadha huo ina tofauti baina yao. [32] Ananukuu kutoka kwa Ibn Abi Dawud kwamba, wananchi wa Sham walikuwa wakitambua msahafu wao na wa Basra kuwa ni sahihi zaidi ya msahafu wa Kufa; kwani msahafu wa Kufa ulipelekewa wakazi wa mji huo pasi na kulinganishwa na kusahihishwa. [33] Kadhalika Muhammad-Hadi Maarefat ananukuu kutoka kwa Ibn Abi Dawud na kusema kuwa, baada ya Othman kushuhudia msahafu wa Othman aliona makosa ndani yake na kusema, kama mwandishi wa masuala ya kiimla angekuwa anatokana na kaumu ya Hudhayl na mwandishi kutoka katika kaumu ya Thaqif makosa haya yasingelitokea. [34]

Sifa Maalumu

Kwa mujibu wa Muhammad Hadi Marafet, katika Mus’haf Othman, kama misahafu mingine iliyoandikwa na masahaba kabla yake, Surah zilipangwa kutoka kubwa hadi ndogo zaidi. Bila shaka, kulikuwa na tofauti chache katika uwanja huu. Kwa mfano, katika Misahafu ya Masahaba, Surat Yunus ilikuwa mojawapo ya Surah ndefu, na kwa hiyo iliwekwa kama surah ya saba au ya nane. Lakini katika msahafu wa Othman, badala ya surah hii, kulikuwa na surah za Anfal na Tawbah; kwa sababu Othman aliziona Surah hizi mbili kuwa ni sura moja na kwa hiyo aliziona kuwa ndefu kuliko Sura Yunus. [35] Inaelezwa kwamba, Ibn Abbas alimpinga Othman kwa sababu ya kazi hii. [36]

Sifa nyingine ni kuwa, herufi za Kiarabu za msahafu wa Othman hazikuwa na nukta. [37] Kuweko makosa mengi ya kiimla kunahesabiwa kuwa moja ya sifa zingine za msahafu wa Othman. [38]Muhammad-Hadi Maarefat anasema, kulikuwa na zaidi ya makosa 7,000 ya kiuandishi katika msahafu wa Othman. [39] Hata hivyo ametoa ufafanuzi kwa kusema kwamba, makosa hayo hayakuwa yakitia dosari hadhi ya Qur’an. [40]

Idadi ya Misahafu ya Othman

Jalal al-Ddin al-Suyuti, mmoja wa wasomi wa elimu za Qur’an wa karne za 9 na 10 Hijria anasema kuhusiana na idadi ya nakala zilizokusanywa na kuandikwa na kundi la kuandika msahafu wa Othman kwamba, kuna mitazamo tofauti kuhusiana na hili. [41] Maulamaa wengi wanaamini kwamba, kuliandikwa nakala nne ambazo zilitumwa Madina, Basra, Kufa na Sham. ref>Ramiar, Historia ya Kurani, 1369, uk. 460.</ref> Suyuti anasema, mtazamo mashuhuri zaidi kuhusiana na idadi ya misahafu ya Othman ni nakala tano. [42] Kuna mitazamao ya nakala 6, 7, 8 na tisa ambayo pia ina wafuasi. [43]

Muhammad-Hadi Maarefat amekusanya ripoti ya Ibn Abi Dawud na Ya’qubi na kupata natija hii kwamba, idadi ya misahafu ya Othman ilikuwa nakala 9. [44]

Msahafu wa Imamu

Katika baadhi ya vyanzo vya Ulumul Qur’an baina ya misahafu ya Othamn, msahafu ambao ni wa Madina (ambao ulipelekwa Madina) unafahamika kwa jina la Msahafu wa Imamu; [45] hata hivyo kwa mujibu wa Ibn Jazari, mpokezi wa hadithi na fakihi wa Kishafii wa karne ya 8 na 9 Hijiria ni kwamba, msahafu wa Imamu kilikuwa kitu kingine ghairi ya msahafu uliokuwa baina ya watu na huo ni msafahu ambao ulikuwa kwa Othman mwenyewe. [46] Ibn Kathir mfasiri wa Qur’an wa karne ya 8 Hijiria anasema katika kitabu cha Fadhail al-Qur’an kwamba, misahafu yote ya Othman ni msahafu wa Imamu. [47] Kwa mujibu wa al-Tamhid, msahafu wa Imamu ulikuwa marejeo ya misahafu ya Othman katika miji mingine na katika sehemu ambazo misahafu ilitofautiana, basi marejeo yalikuwa ni msahafu wa Imamu. [48]

Msimamo wa Masahaba na Tabiina

Masahaba hawakuwa na tofauti na kimitazamo na Othman kuhusiana na suala la kufanya msahafu kuwa ni mmoja (kusiweko na misahafu ambayo inatofautiana). [49] Katika uga wa mbinu ya ukusanyaji na uandishi pia kumenukuliwa upinzani wa mtu mmoja tu naye ni Abdallah bin Mas’oud ambaye kutokana na hilo, kuliibuka mzozo mkubwa wa maneno baina yake na Othman. Yeye alikuwa akiwaona watu waliopewa jukumu la kukusanya na kuandika Qur’an kwamba, hawakuwa na tajiriba na uzoefu na hivyo hakuwa tayari kutoa msahafu wake na kumkabidhi Othman. [50]

Kadhalika kumenukuliwa mitazamo tofauti ya baadhi ya masahaba kuhusiana na baadhi ya maneno yaliyoko katika msahafu wa Othman. [51] Kwa mfano neno «هَذَانِ» (wawili hawa) katika Aya isemayo: «إنْ هٰذَانِ لَسَاحِرَان» (Hakika hawa wawili ni wachawi) [52], kwa mujibu wa kanuni za kawaida za fasihi ya lugha ya Kiarabu inapaswa kuwa katika sura ya «هَذَیْنِ» [53]» Kwa msingi huo baadhi ya watu kama Aisha na Said bin Jubayr walikuwa wakitambua kuwa hilo ni kosa na hivyo walikuwa wakitamka «هَذَیْنِ» .[54]» Kwa mujibu wa Tabarsi katika tafsiri yake ya Majmaa al-Bayan, baadhi ya wasomaji wa visomo saba pia walikuwa wakisoma «هَذَیْنِ» .[55] Kumenukuliwa kwamba, Othamn pia alikuwa akitambua kuwa hilo ni kosa; lakini kutokana na kosa hilo kutosababisha kuharamishwa au kuhalalishwa kitu, hakulibadilisha. [56]

Katika Majlmaa ali-Bayan imekuja nukuu pia kutoka kwa Imamu Ali (a.s) ya kwamba: «طَلْحٍ مَنْضُود» [57]» (Na migomba iliyo pangiliwa) [58] alikuwa akitambua kuwa ni: «طَلْعٍ مَنْضُود»; lakini hakuruhusu kubadilishwa hilo. [59]

Mtazamo wa Maimamu wa Kishia

Muhammad-Hadi-Maarefat anasema: Maimamu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia hawakuupinga msahafu wa Othman na kwa msingi huo, Mashia wote, wanautambua na kuukubali msahafu huu ulioenea hii leo baina ya watu kuwa ni sahihi na kamili. [60] Suyut amenukuu hadithi kutoka kwa Imamu Ali (a.s) ambayo kwa mujibu wake, Othman alishauriana na Imamu Ali kuhusiana na kukusanya na kuandika msahafu na yeye akaafiki hilo. [61] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha Wasail al-Shi’ah: Imam Swadiq (a.s) alimzuia bwana mmoja aliyekuwa akisoma Qur’an kinyume na kisomo rasmi na akamtaka aache kufanya hivyo. [62]

Hatima ya Misahafu

Kwa mujibu wa vyanzo vya historia misahafu ya Othman ilikuwa na utukufu maalumu baina ya Waislamu na ilikuwa ikichungwa mno; lakini pamoja na hayo na licha ya kuweko nakala nyingi zilizoandikwa zikikopi kutoka katika misahafu hiyo, [63] hakuna taarifa makini na za kuaminika kuhusiana na hatima ya misahafu hiyo. [64] Kwa msingi huo kuanzia huko nyuma mpaka leo, kumekuweko na madai yanayotolewa kwamba, nakala zilizopo ni msahafu wa Othman. [65] Hata hivyo wahakiki wanasema kuwa madai hayo si sahihi na wanaamini kwamba, hakuna athari iliyobakia ya misahafu hiyo. [66]

Kwa mfano kuna nakala ya Qur’an ambayo ni maarufu kwa jina la msahafu wa Samarqand huko Tashkent, Uzbekistan ambayo ilikuwa ikidaiwa kwamba, ni ule msahafu ambao Othman aliuawa nao na athari ya damu imebakia juu yake; [67] hata hivyo kwa mujibu wa Mahmoud Ramiyar ni kuwa. Licha ya ukongwe wa msahafu huo na kutokuwa na nukta katika herufi zake, ukale wake haufikii zama za Othman. [68] Kadhalika nakala ya Qur’an iliyoko katika makumbusho ya Istanbul Uturuki nayo inanasibishwa na Othman; lakini kutokana na kuwa na alama za uandishi wa kiimla (nukta juu au chini ya herufi) na kwa kuzingatia kwamba, misahafu ya Othman haikuwa na uandishi huo, madai haya hayatambuliwi kuwa ni sahihi. [69]

Kuchapisha Qur'an kwa Mujibu wa Mus’haf Othmani

Misahafu ya Othman ambayo ilitumwa katika ardhi tofauti za Kiislamu ilizingatiwa na kufanyiwa uangalizi maalumu kutoka kwa Waislamu. Muda mfupi baada ya kukusanywa kwa Mus’haf wa Othmani, uandishi wa nakala kutoka katika misafahafu hiyo ulienea na kupata umaarufu na nakala nyingi ziliandikwa kutoka katika misahafu hiyo. [70] Kulingana na Mahmoud Ramyar, kutoka karne ya pili Hijiria baadhi ya watu walijitolea na kuweka waqfu muda wao kwa ajili ya kuandika Qur'an. Kwa mfano Abu Amru Shaybani aliandika zaidi ya nakala 80 na kuziweka katika msikiti wa Kufa. [71] Nakala za Qur'an zikawa nyingi sana kiasi kwamba katika tukio moja mnamo 403 Hijiria, Al-Hakim Biamrillah, Khalifa wa Fatimiya katika ardhi ya Misri, alitoa nakala 1,298 za Quran kwa Msikiti mkuu wa Atiq na nakala 814 kwa Msikiti wa Touloni. [72].

Nakala za Qur’an zilizoko hii leo baina ya Waislamu zimechapishwa kutoka katika nakala za Qur’an zilizoandikwa kutoka katika misahafu ya Othman. Qur’an hii kwa mara ya kwanza ilichapishwa nchini Italia mwaka 1543; lakini kwa amri ya kanisa ikatokomezwa. Baada ya hapo, Qur’ani ikachapishwa mwaka 1692 na 1696 huko Ulaya. Qur’an ya kwanza iliyochapishwa na Waislamu ilikuwa mwaka 1200 Hijria na ilichapishwa na Mawla Othman huko Saint Petersburg nchini Russia.[73]

Iran ilikuwa nchi ya kwanza ya Kiislamu kuchapisha Qur’an. Baada yake zikafuata nchi nyingine za Kiislamu kama Uturuki, Misri na Iraq ambazo zilitoa chapa mbalimbali za Qur’an.[74]

Rejea

  1. Hujjat, utafiti juu ya historia ya Quran Tukufu, 1368, uk. 426.
  2. Siyuti, Al-Itqan, 1363, juzuu ya 1, uk.202; Marafet, Talmahid, 1412 AH, Juz. 1, uk. 272-282.
  3. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk.334.
  4. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk.334.
  5. Hujjat, utafiti juu ya historia ya Quran Tukufu, 1368, uk 448.
  6. Hujjat, utafiti juu ya historia ya Quran Tukufu, 1368, uk. 438.
  7. Hujjat, utafiti juu ya historia ya Quran Tukufu, 1368, uk. 438.
  8. Hojjat, utafiti juu ya historia ya Quran Tukufu, 1368, uk. 439 na 440; Marfat, Talmahid, 1412 AH, Juz. 1, uk. 338 na 339.
  9. Maaraft, Talmahid, 1412 AH, Juzuu ya 1, uk. 346; Hojjat, utafiti juu ya historia ya Kurani Tukufu, 1368, uk. 440.
  10. Maarifa, Talmahid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 343.
  11. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 433; Marafet, Talmahid, 1412 AH, Juz. 1, uk. 343.
  12. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 433; Marafet, Talmahid, 1412 AH, Juzuu 1, 344 na 345.
  13. Maaraft, Talmahid, 1412 AH, Juzuu 1, 344 na 345; Ramyar, Historia ya Kurani, 1369, uk. 433.
  14. Maarifa, Talmahid, 1412 AH, Juzuu 1, 345
  15. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 433 na 435.
  16. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 435.
  17. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 417.
  18. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 419.
  19. Angalia Ramyar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 417.
  20. Maraft, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk.339; Hojjat, utafiti juu ya historia ya Quran Tukufu, 1368, uk.439 na 440; Ramyar, Historia ya Kurani, 1369, uk. 417.
  21. Maraft, Talmahid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 339 na 340.
  22. Hojjat, utafiti juu ya historia ya Kurani Tukufu, 1368, uk. 440; Marafet, Talmahid, 1412 AH, Juz. 1, uk. 339.
  23. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 418.
  24. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 419.
  25. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 339.
  26. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 421 na 422.
  27. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 421 na 422.
  28. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 426.
  29. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 426.
  30. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 427.
  31. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 348.
  32. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 348.
  33. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 348 na 349.
  34. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 349.
  35. Meraft, Talmahid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 354 na 355.
  36. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 355.
  37. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 356.
  38. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 366.
  39. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 386.
  40. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 368.
  41. Siyuti, Al-Itqan, 1363, juzuu ya 1, uk. 211.
  42. Angalia Siyuti, Al-Itqan, 1363, juzuu ya 1, uk. 211.
  43. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 462.
  44. Angalia Marifat, Talmahid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 349 na 350.
  45. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk.350.
  46. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 462.
  47. Hujjat, utafiti juu ya historia ya Quran Tukufu, 1368, uk. 461.
  48. Marafet, Talmahid, 1412 AH, Juz. 1, uk. 350.
  49. Marafet, Talmahid, 1412 AH, Juz. 1, uk. 339.
  50. Marafet, Talmahid, 1412 AH, Juz. 1, uk. 343.
  51. Marafet, Talmahid, 1412 AH, Juz. 1, uk. 369-373.
  52. Surah Taha, aya ya 63.
  53. Marafet, Talmahid, 1412 AH, Juz. 1, uk. 369.
  54. Marafet, Talmahid, 1412 AH, Juz. 1, uk. 369.
  55. Tabarsi, Majmam al-Bayan, 1372, juzuu ya 7, uk.24 na 25.
  56. Thalabi, Al-Kashf na Al-Bayan kwenye Tafsir al-Qur'an, 1422 AH, juzuu ya 6, uk.250.
  57. Surah Al-Wakeh, aya ya 29.
  58. Imechukuliwa kutoka kwa tafsiri ya Fouladvand.
  59. Tabari, Jame al-Bayan, 1412 AH, juzuu ya 27, uk. 104.
  60. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 342.
  61. Maarifa, Talmhid, 1412 AH, juzuu ya 1, uk. 341.
  62. Har Ameli, Vasal al-Shia, 1409 AH, juzuu ya 4, uk.821.
  63. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk.471.
  64. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk.465.
  65. Ramiar, Historia ya Qur'an, 1369, uk.465 na 468 .
  66. Tazama Hojjat, utafiti juu ya historia ya Kurani Tukufu, 1368, uk. 460; Ramyar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 465 na 466.
  67. Ramyar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 467 na 466.
  68. Ramyar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 467.
  69. Angalia Hojjat, utafiti juu ya historia ya Kurani Tukufu, 1368, uk. 460.
  70. Ramyar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 471.
  71. Ramyar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 472.
  72. Ramyar, Historia ya Qur'an, 1369, uk. 472.
  73. Maarifat, «Pishine Chapa Qur'an Karim», Webgah Daneshname Maudhui Qur'an.
  74. Maarifat, «Pishine Chapa Qur'an Karim», Webgah Daneshname Maudhui Qur'an.

Vyanzo

  • Thaʿlabī, Aḥmad b. Muḥammad al-. Al-Kashf wa l-bayān ʿan tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1422 AH.
  • Ḥujjatī, Sayyid Muḥammad Bāqir. Pajūhishī dar tārīkh-i Qurʾān-i Karīm. Fifth edition. Tehran: Daftar-i Nashr-i Farhang-i Islami, 1368 Sh.
  • Ḥurr al-ʿĀmilī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Wasāʾil al-Shīʿa. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1309 AH.
  • Rāmyār, Maḥmūd. Tārīkh-i Qur'ān. Tehran: Amir Kabir, 1369 Sh.
  • Suyūṭī, ʿAbd al-Raḥmān b. Abī Bakr al-. Al-Itqān fī ʿulūm al-Qurʾān. Edited by Muhammad Abu al-Fadl Ibrahim. Qom: 1363 Sh.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Tehran: Naṣir Khusruw, 1372 Sh.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Jāmiʾ al-bayān fi tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār al-Maʾrifa, 1412 AH.
  • Maʿrifat, Muḥammad Hādī. Al-Tamhīd fī ʿulūm-i al-Qurʾān. Qom: Muʾassisa-yi Nashr-i Islāmī, 1412 AH.
  • Maʿrifat, Muḥammad Hādī, Pīshīna-yi Chāp-i Qurʾān-i Karīm