Kalenda ya Hijria
Kalenda ya Hijiria au mwaka wa Hijiria (Kiarabu: التاريخ الهجري أو التقويم القمري، أو السنة الهجرية القمر) ni mwaka ambao unahesabiwa kulingana na mzunguko wa mwezi, na Waislamu hufanya ibada zao na hafla au minasaba ya kidini kwa kutegemea kalenda hii ya Hijiria. Asili na mwanzo wa kuhesabiwa ya kalenda ya Hijiria ni kugura na kuhama kwa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) kutoka Makka kwenda Madina, ambako kulitokea mwaka 622 Miladia. Kwa mujibu wa kauli mashuhuri, mwaka wa Hijria uliamuliwa na kuainishwa kuwa mwaka wa kalenda ya Waislamu kwa pendekezo la Imam Ali (a.s) kwa aliyekuwa Khalifa wakati huo yaani Omar bin al-Khattab.
Mwaka wa Hijiria una siku 354 au 355 na una siku kumi au kumi na moja pungufu ikilinganishwa na mwaka unaohesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa jua au mwaka wa Miladia. Kalenda hii huanza na mwezi wa Muharram na kuishia na mwezi wa Dhul-Hijja. Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, Ramadhani ni mwezi wa kwanza wa mwaka wa Hijiria, na kwa hiyo, katika baadhi ya vitabu vya dua, amali na matendo ya mwaka wa Hijiria Qamaria huanza na matendo na amali za Ramadhani na kuishia na matendo na amali za Sha'abani. Sayyid Ibn Tawus, mwanazuoni wa Kishia katika karne ya 7 Hijiria, amesema kuna uwezekano kwamba, mwezi wa Ramadhani ni mwanzo wa mwaka wa kiibada na mwezi wa Muharram ni mwanzo wa mwaka minasaba. Miezi ya mwaka wa Hijiria au kalenda ya Kiislamu ya Hijiria ni: Muharram, Safar, Rabi al-Awwal, Rabi al-Thani, Jumadi al-Awwal, Jumadi al-Thani, Rajab, Sha'ban, Ramadhan, Shawwal, Dhul-Qa'dah na Dhul- Hijja.
Nafasi na Umuhimu
Mwaka wa kalenda ya Hijria ni mwaka ambao unahesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa mwezi na kwa sababu asili yake na mwanzo wa kuhesabiwa kwake ulikuwa ni kuhama kwa Mtume (s.a.w.w.) mnamo 622 Miladia, unaitwa mwaka wa Hijiria. [1] Waislamu hufanya ibada zao za kidini kwa mujibu wa mwaka wa Hijiria. Ni kwa msingi huo ndio maana, kalenda ya mwezi ya Hijiria inaitwa pia kwa jina la kalenda ya Kiislamu. [2]
Kuhesabu siku kwa mujibu wa kalenda ya Hijiri ilikuwa msingi wa tarehe rasmi katika nchi za Kiislamu hadi kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia (1918-1914), na matukio yalikuwa yakirekodiwa kwa msingi wake. [3] Katika nchi ya Iran, sheria ya kubadili kalenda na kuhesabiwa kwa mujibu miezi ya Kifarsi na kwa mujibu wa mzunguko wa jua ilibadilishwa rasmi 31 Machi 1925 katika kipindi cha utawala wa Kipahlavi. [4] Kadhalika huko Afghanistan mwaka 1922 kalenda ya Shamsia ilichukua nafasi ya kalenda ya Hijiria. [5] Nchini Saudi Arabia pia kuanzia mwaka 1439 Hijiria kalenda ya Miladia ilichukua nafasi ya kalenda ya Hijiria. [6]
Mwanzo wa Tarehe ya Hijiria
Kwa mujibu wa ripoti za kihistoria, asili na mwanzo wa tarehe ya Hijria ni mwaka aliogura na kuhama Mtume wa Uislamu kutoka Makka kwenda Madina, lakini ripoti zinatofautiana kuhusu na lini uamuzi huu ulifanywa. Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, kuhama kwa Mtume kwenda Madina kufanywa kuwa asili na chimbuko la kuhesabu kalenda ya Kiislamu kuliainishwa na kupasishwa wakati wa ukhalifa wa Omar bin al-Khattab katika mwaka wa 17 au 18 Hijiria. [8] Kwa kuzingatia ripoti za kihistoria, Abu Musa Ash'ari alilalamika kuhusu ukosefu wa tarehe thabiti katika barua aliyomuandikia Omar ibn al-Khattab. Kwa sababu alipokea barua kutoka kwa khalifa wa pili, na kutokana na ukweli kwamba tarehe hiyo haikutajwa, alipata shida katika kutofautisha baina ya barua ya mwanzo na ya baada yake. [9] Kwa hiyo, Omar bin al-Khattab aliunda baraza la kuainisha tarehe ya Kiislamu [10] ambalo lilipendekeza mambo matatu kuwa mwanzo na kigezo cha kuhesabu kalenda ya Kiislamu. Mambo hayo yalikuwa, mab'athi (siku ya kupewa Utume Mtume Muhammad), siku aliyoaga dunia na siku aliogura na kuhama Makka na kwenda Madina. [11] Pendekezo la Ali bin Abi Twalib (a.s) la kujaaliwa tarehe ya kuhama kwake kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu lilikubaliwa, na hivyo huo ukawa mwanzo wa tarehe ya Kiislamu au kalenda ya Kiislamu ya Hijiria. [12]
Kwa mujibu wa riwaya na ripoti nyingine, baada ya Mtume kuhama Makka na kwenda Madina, alitoa amri hijra yake hiyo iwe mwanzo wa kalenda ya Kiislamu. [13]. Kwa mujibu wa Sheikh Ja'afar Sobhani, fakihi, mwanateolojia na mwandishi wa hitoria wa Kishia, kuna barua zilizokuwa zikiandikwa katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w) ambazo zinaonyesha zikiwa zimeandikwa tarehe ya Hijiria; miongoni mwa barua na maandiko hayo ni pamoja na barua ya mapatano ya amani baina ya Mtume (s.a.w.w) na Wakristo wa Najran, ambayo ni mwaka wa tano wa Hijiria [14] na wasia wa Mtume (s.a.w.w) kwa Salman Farsi, ulioandikwa kwa hati ya Ali (a.s), mwaka wa tisa wa Hijiria.[15]
Mwezi wa Kwanza wa Hijiria
Mwaka wa Hijiria huanza na mwezi wa Muharram na kumalizika kwa mwezi wa Dhu al-Hijja. [16] Kabla ya kuainishwa kuhama kwa Mtume kuwa mwanzo wa tarehe na kalenda ya Kiislamu, mwaka wa Hijria lilikuwa jambo la kawaida na lililokuwa limeenea miongoni mwa Waarabu na Wayahudi na ulikuwa ukianza na mwezi wa Muharram. [17] Kwa hiyo, baada ya kuamuliwa na kuafikiwa kwamba, kugura na kuhama Mtume kuwe ndio kigezo cha mwanzo wa tarehe na kalenda ya Kiislamu, ikapendekezwa kwamba, mwezi wa Ramadhani na Muharram iwe mwanzo wa mwaka mpya wa Hijiria. Mapendekezo hayo yakawasilishwa kwa Khalifa wa pili (Omar ibn al-Khattab) na yeye akakubaliana na pendekezo la Muharram kuwa ndio mwanzo wa mwaka mpya wa Hijiria. [18]
Sheikh Tusi, fakihi na mwanazuoni wa hadithi wa Kishia wa karne ya tano Hijria anasema kwamba, kwa mujibu wa hadithi maarufu za Waislamu wa madhehebu ya Shia, mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kwanza wa mwaka wa Hijria, na kwa msingi huo ndio maana, katika kitabu Misbah al-al-Mujtahid, ameanza amali na matendo ya mwaka wa ibada na mwezi wa Ramadhani. [19] Pia aliuchukulia mwezi wa Rajab kuwa mwezi wa mwisho miongoni mwa miezi mitakatifu (miezi ambayo ndani yake kumeharamishwa baadhi ya mambo kama kupigana vita ndani yake na kadhalika) [20] na akahitimisha matendo na amali za mwaka kwa amali na matendo ya mwezi wa Sha'aban. [21]
Sayyid Ibn Tawus, mwanazuoni na mtaalamu wa elimu ya hadithi wa Kishia katika karne ya 7 Hijiria sambamba na kuashiria hitilafu za hadithi kuhusiana na mwezi wa kwanza wa Hijiria, amesema kuwa, kufanyia kazi idadi kubwa ya Maulamaa waliotangulia na vitabu vyao ni ishara ya wazi kwamba, mwezi wa Ramadhani ni mwanzo wa mwaka wa Hijria; hata hivyo, amesema inawezekana kwamba mwezi wa Ramadhani ndio mwanzo wa mwaka wa kidini na mwezi wa Muharram ndio mwanzo wa mwaka matukio na minasaba. [22]
Miezi ya Mwaka wa Hijiria
- Makala Kuu: Mwezi wa Hijiria
Mwaka wa Hijria Qamaria una miezi kumi na mbili [23] na kila mwezi una siku 29 au 30, lakini hakuna utaratibu maalumu na kanuni makhususi kuhusu ni mwezi gani una siku 29 na ambao una siku 30. [24] Idadi ya siku katika mwaka wa Hijiria ni pungufu kwa siku kumi au kumi na moja ikilinganishwa na mwaka wa Miladia (ambao una siku 365); kwa hiyo, idadi ya siku katika mwaka wa Hijria ni siku 354 katika miaka ya kawaida na siku 355 katika miaka mirefu. [25]
Kwa mujibu wa Ali bin Hussein Masoudi, mwandishi wa historia wa karne ya 4 Hijiria anasema, Waarabu katika zama za ujahilia walikuwa wakiongeza mwezi mmoja kwenye mwaka wa Hijiria, na Qur'an imekitaja kitendo hicho kuwa ni nasiu (kuakhirisha) na kukikemea na kukilaumu. [26]
Miezi ya Hijiria kwa utaratibu ni kama ifuatavyo:
Rejea
Vyanzo