Ilai

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na mafuhumu na hukumu ya Ilai. Ili kujua kuhusiana na Aya ya Qur’ani yenye jina kama hili angalia makala ya Aya ya Ilai.

Ilai (Kiarabu: الإيلاء) ni katika ada zilizokuwa enzi za Ujahilia na maana yake ni mwanaume kula kiapo cha kuacha kuwa na mahusiano ya tendo la ndoa na mkewe ambapo katika Uislamu ni haramu na jambo hilo limetengewa na kuainishiwa adhabu ya kafara. Endapo mwanaume afanya kitendo kama hicho, mwanamke anaweza kushtaki kwa mtawala wa Sheria (al-Hakim al-Shar’i) au mahakama. Mtawala atampatia mume yule muhula wa miezi minne ili amrejee mkewe. Endapo hatofanya hivyo atamlazimisha amtaliki mkewe huyo. Hoja ya mafakihi kuhusiana na hili ni Aya ya 226 na 227 ya Surat al-Baqarah. Kuwa ndoa ni ya daima (siyo ya mutaa) na kuapa kutokutana kimwili na mkewe kwa uchache miezi minne ni miongoni mwa masharti ya kutimia Ilai.

Maana na nafasi yake

Ilai ni kiapo cha mume ya kwamba, hatofanya tendo la ndoa na mkewe. [1] Ilai ni haramu katika Uislamu na mafakihi wa Kiislamu wamebainisha hukumu na masharti maalumu kwa ajili ya kutimia hilo na hukumu za baada ya hapo. [2] Hoja na nyaraka za baadhi ya hukumu hizo zimetambuliwa kuwa zimetokana na Aya za 226 na 227 za Surat al-Baqara. [3] Maudhui ya Ilai (aina ya kiapo) ina mlango wa kujitegemea katika vyanzo vya Fiqhi. [4]

Historia

Makala asili: Aya ya Ilai

Ilai inatajwa kama aina ya talaka katika utamaduni wa zama za Ujahilia. [5] Katika zama za ujahilia, ikitokea kwamba, mwanaume amemchukia mkewe, basi alikuwa akiapa kwamba, hatakutana naye kimwili wala kumpa talaka [6] kwa miaka kadhaa [7] au mpaka mwisho wa umri wake. [8] Lengo la hatua hii lilikuwa ni kumtesa na kumuudhi mke, [9] kumuacha anatangatanga [10] na kumzuia asiolewe. [11] Imekuja katika Tafsiri ya Nemooneh kwamba, katika Aya ya 226 ya Surat al-Baqarah ada hii mbaya imepigwa marukufu na njia za kufungua kiapo hiki zimebainishwa [12] na imetolewa hukumu kwa maslahi ya wanawake na haki zake zimehuishwa. [13]

Hukumu za fi’qh

Ilai kimehesabiwa kuwa ni kitendo cha haramu na sababu yake imetajwa kuwa, ni haramu mume kutokutana kimwili na mkewe kwa muda wa zaidi ya miezi minne. [14] Baadhi pia wanasema kuwa, hukumu hii imechukuliwa kutoka katika Aya ya 226 ya Surat al-Baqarah: ((فَإِنَّ اللّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ; Hakika ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu)) [15]


Nguzo na masharti ya kutimia Ilai

Kumetajwa nguzo tatu kwa ajili ya Ilai: Mwenye kutoa kiapo cha Ilai (mume), mwenye kufanyiwa kiapo cha Ilai (mke) tamko la kiapo cha Ilai kwa kila lafudhi na lugha ambayo inaweka wazi na kubainisha hilo huwa sahihi. [16] Kumebainishwa masharti pia ya kutimia Ilai ambapo kama moja kati ya hayo halitakuweko, ilai haiwezi kutimia. Masharti hayo ni:

  • Mla kiapo (Ilai) anapaswa kuwa na akili timamu, baleghe, mwenye kusudio na mwenye kufanya hilo kwa hiari yake.
  • Kuapa kunapaswa kuwa kwa kutumia moja ya majina ya Mwenyezi Mungu.

Muda wa kuacha kukutana kimwili na mke haupaswi kuwa chini ya miezi minne.

  • Kuapa kuacha kukutana kimwili na kumuingilia mke katika uke.
  • Kabla ya kula kiapo cha Ilai mke na mume wanapaswa kuwa wamekutana kimwili.
  • Msukumo na sababu ya mfanya Ilai inapaswa kuwa ni kwa ajili ya kumuudhi mke.
  • Mke awe ni wa ndoa ya daima. [17]

Hukumu za baada ya Ilai

Mafakihi wanaamini kuwa, kama mwanaume atafanya kiapo cha Ilai, mke anaweza kwenda kushtaki kwa Mtawala wa Sheria (al-Hakim Shar’i). Mtawala wa sheria atampa mume muda wa miezi minne kumrejea mke wake na baada ya kukutana naye kimwili atoe kafara ya kuvunja kiapo. [18] Kama mwanaume katika kipindi na muda huu aliopatiwa na mtawala wa Sheria hatafanya hivyo, mtawala wa sheria atampa hiari baina ya kumrejea mke na kutoa talaka na kama atakataa kufanya lolote kati ya mawili hayo, atamlazimisha kuchagua baina ya hukumu kufungwa na kubinywa katika kupewa chakula. [19] Baadhi ya mafakihi wanaamini kwamba, katika hali hii mtawala wa sheria anaweza kumpa talaka mwanamke huyo. [20]