Husseini Minni Wa Anna Min Hussein
Hussein anatokana na mimi na mimi ninatokana na Hussein (Kiarabu: حسين مني وأنا من حسين) ni hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ambayo inaonyesha fadhila za Imamu Hussein (a.s). Hadithi hii imenukuliwa katika vitabu na vyanzo mbalimbali vya hadithi vya Kisunni na Kishia. Chanzo na kitabu kikongwe kabisa kilichonukuu hadithi hii ni “al-Musannaf” kilichoandikwa na Ibn Abi Shaybah (aliaga dunia:235 Hijiria), mmoja wa Maulamaa wa Kisunni.
Na katika vyanzo vya hadithi vya Kishia, hadithi hii ilinukuliwa kwa mara ya kwanza katika kitabu cha Kamil al-Ziyaraat kilichoandikwa na Ibn Qulaweyh (aliaga dunia 368 Hijiria).
Kwa itikadi ya baadhi, hadithi inabainisha umoja wa kiroho uliopo baina ya Mtume (s.a.w.w) na Imamu Hussein (a.s) na kwamba, kumpenda Hussein ni sababu ya kupendwa na Mwenyezi Mungu na inaashiria pia kuendelea kizazi cha Maimamu wa Kishia kupitia kwa Imamu Hussein (a.s) Kadhalika watafiti wa masuala ya kihistoria wanaamini kwamba, ibara ya “ana min Hussein” (mimi natokana na Hussein) inaashiria juu ya kubakia dini ya Uislamu kupitia mapinduzi na harakati ya Imamu Hussein (a.s).
Hadithi hii imeandikwa juu ya mlango wa kuingia katika Haram ya Imamu Hussein (a.s).
Utambulisho na nafasi
Hadithi ya Hussein Minni (Hussein anatokana na mimi) ni katika hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) inayobainisha fadhila za Imamu Hussein (a.s). Kwa mujibu wa Sayyid Hashim Bahrani, hadithi hii inaonyesha mapenzi ya Mtume (s.a.w.w) kwa Imamu Hussein (a.s) na imerudiwa na kukaririwa mara nyingi katika vyanzo vya (hadithi) Shia na Sunni. [1] Hadithi ya “Hussein Minni” imeandikwa juu ya mlango wa kuingia katika Haram ya Imamu Hussein (a.s). [2] Kadhalika hadithi hii imeandikwa kwa kuchongwa juu ya pembe sita za nguzo za Kaburi la Imamu Hussein (a.s). [3]
Kwa mujibu wa vyanzo vya hadithi, [4] Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimuona Hussein (a.s) akicheza na watoto wakati akiwa njiani kuelekea sehemu aliyokuwa amealikwa. Mtume (s.a.w.w) alikwenda kumpokea Hussein (a.s) na akafungua mikono yake na kumkumbatia kisha akasema: «حُسَیْنٌ مِنِّی وَ أَنَا مِنْ حُسَیْنٍ، أَحَبَّ اَللَّهُ مَنْ أَحَبَّ حُسَیْناً، حُسَیْنٌ سِبْطٌ مِنَ اَلْأَسْبَاطِ؛ ; “Hussein anatokana na mimi na mimi natokana na Hussein, Mwenyezi Mungu ampende ampendaye Hussein”, Hussein ni mjukuu katika wajukuu. [5]
Maudhui ya hadithi
Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti, maudhui ya hadithi hii inajumuisha madhumuni zifuatazo:
- Umoja wa kiroho wa Mtume (s.a.w.w) na Imamu Hussein (a.s).
- Kumpenda Hussein (a.s) ni sababu ya kupendwa na Mwenyezi Mungu.
- Kuendelea kizazi cha Maimamu wa Waislamu wa Kishia kupitia kwa Hussein (a.s). [6]
Manawi (aliaga dunia: 1031) mmoja wa Maulamaa wa Kishafi katika kutoa ufafanuzi wa hadithi hii amenukuu kutoka kwa Kadhi Waki’i kwamba; Mtume (s.a.w.w) alikuwa akifahamu nini kitatokea baina yake na umma wake na kwa msingi huo katika hadithi hii amemtaka Hussein tu na hili ni jambo ambalo linakumbusha kwamba, katika suala la huba, kuvunjiwa heshima na vita, Imamu Hussein yuko sawa na Mtume, na hili jambo limetiliwa mkazo na ibara ya: ((احب الله من احب حسینا، ; “Mwenyezi Mungu ampende ampendae Hussein”)); kwani kupenda Hussein (a.s), ni kumpenda Mtume (s.a.w.w) na kumpenda Mtume (s.a.w.w) ni kumpenda Mwenyezi Mungu. [7]
Baqir Sharif Qarashi (aliaga dunia: 1433) mtafiti wa historia ya Ahlul-Bayt (a.s) anasema: Ibara ya: Mimi ninatokana na Hussein” inaashiria nukta hii kwamba, mapinduzi na harakati ya Imamu Hussein (a.s) na kuuawa kwake shahidi, imekuwa sababu ya kubakia dini ya Uislamu na kwa msingi huo kubakia dini iliyoletwa na Mtume kutatimia kupitia kwa Imamu Hussein (a.s). [8]
Vyanzo na itibari ya hadithi
Chanzo na kitabu kikongwe kabisa kilichonukuu hadithi hii ni “al-Musannaf” kilichoandikwa na Ibn Abi Shaybah (aliaga dunia:235 Hijiria), [9] mmoja wa Maulamaa wa Kisunni, [10] ambaye anatambulika kama mtaalamu wa kuaminika katika taaluma ya utambuzi wa wapokezi wa hadithi. [11] Na katika vyanzo vya hadithi vya Kishia, hadithi hii ilinukuliwa kwa mara ya kwanza katika kitabu cha Kamil al-Ziyaraat kilichoandikwa na Ibn Qulaweyh (aliaga dunia 368 Hijiria). [12] Kisha ikanukuliwa katika vitabu vya Sherh al-Akhbar, kilichoandikwa na Kadhi Nu’man Maghribi (aliaga dunia: 363 Hijiria) [13], al-Irshad cha Sheikh Mufid (aliaga dunia: 413 Hijiria) [14] na baada ya hapo vikafuata vyanzo vingine kunukuu hadithi hii. [15] Allama Majlisi (aliaga dunia: 1110 Hijiria), amekitambua kitabu cha Kamil al-Ziyaraat kuwa ni katika misingi ya ya kuaminika na mashuhuri miongoni mwa mafakihi (wanazuoni wa fikihi) wa Kishia. [16]
Wapokezi wa mlolongo wa sanadi (mapokezi) wa hadithi hii, kwa mujibu wa nukuu ya Kamil al-Ziyaraat ni: Muhammad bin Abdallah Ja’afar Himyari, Abi Said Hassan bin Ali bin Zakariya Adawi Basri, Abd al’Alam bin Hammad Basri, Wahb, Abdallah bin Othman, Said bin Abi Rashid na Ya’la Amiri. [17]
Miongoni mwa vyanzo vya Kisunni vilivyonukuu hadithi hii ni: Musnad Ahmad bin Hambal, [18] Sunan ibn Majah, [19] Sunan Tirmidhi, [20] na al-Mustadrak Alaa Sahihein [21] cha Hakim Neyshabouri. Hakim Neyshabouri ameitambua hadithi hii kwamba ni sahihi, [22] huku Haythami [23] na Tirmidhi [24] wakiitambua kuwa ni hadith Hasan.
Bibliografia
Kwa mujibu wa nukuu ya Agha Bozorg Tehrani ni kuwa, kumeandikwa vitabu viwili kwa anuani ya "Sherh Hadith Hussein Minni wa Anna Min Hussein". Waandishi wa vitabu hivi ni: Sayyid Muhammad, mtoto wa Sayyid Deldar Ali Naqvi na Mirza Muhammad bin Kazim Hindi (aliyefariki: 1289 Hijria), miongoni mwa wanafunzi wa Sayyid Hussain bin Sayyid Deldar Ali Naqvi 25] Pia, kwa mujibu wa baadhi ya waandishi wa orodha, Muhammad Khalizadeh (aliyefariki: 1342 Hijiria Shamsia) aliandika kitabu kiitwacho "Hadith Hussein Min wa Ana Min Hussein" ambacho kilichapishwa huko Najaf. [26]
Rejea
Vyanzo