Nenda kwa yaliyomo

Funga ya Kukaa Kimya

Kutoka wikishia

Funga ya ukimya (Kiarabu: صوم الصَمت) ni kitendo chenye rangi ya kidini, ambacho mtu huamua kwa makusudi kutenda amali hiyo kwa nia ya kumkaribia Mwenye Ezi Mungu na kwa nia ya kufunga, ambapo mtu huyo hukaa kimya kwa kipindi cha masaa fulani au siku nzima bila kunena neno lolote kutoka mdomoni mwake. Kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wa fiqhi wa Kishia na Kisunni, ni haramu mtu kufunga funga ya ukimya. Wanazuoni hawa wanaeleza kwamba; funga ya aina hii haijaruhusiwa ndani ya maandiko na mafundisho ya Kiislamu, kwani inapingana na misingi ya dini ya Allah. Ingawa, iwapo mtu fulani atakaa kimya bila kuwa na nia ya kufunga, kisha kimya hicho kikapatikana ndani ya funga hiyo na kuendelea kwa siku nzima, kitendo hicho hakitahesabiwi kuwa ni haramu. Kwa maneno mengine, haukatazwi mtu kuwa na ukimya wa muda mrefu bila nia ya kufunga. Inasemekana kwamba funga ya ukimya ilikuwa ni desturi iliyokuwepo na kufuatwa na jamii ya Bani Israil, ambao ni watu wa kizazi kilichopita kabla ya kuja kwa Uislamu. Hata hivyo, desturi hii ya funga ya ukimya ilifutwa na Sheria za Kiislamu, na hivyo haikupaswa kuendelezwa katika dini ya Uislamu. Uislamu ulifuta amri hii na kuweka wazi kwamba ibada za kufunga zinapaswa kufuatwa kulingana na mafundisho yaliyowekwa na bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w). Kwa kifupi, ingawa funga ya ukimya ilikuwa na nafasi yake katika desturi za dini za zamani, Uislamu umetoa mwongozo tofauti unaoendana na mafundisho yake maalum, na hivyo kuondoa hitaji la funga ya aina hii katika utekelezaji wa ibada za Kiislamu.

Dhana, Maana na Historia ya Funga ya Ukimya

Funga ya ukimya ni kitendo cha mtu kukaa kimya bila kusema kitu kuanzia asubuhi hadi jioni au kwa muda ya masaa fulani ya siku hiyo, kwa nia ya kujikurubisha kwa Mwenye Ezi Mungu na kwa nia ya kufunga saumu hiyo. Lengo hasa la funga hii ya kujiepusha na mazungumzo ni kufikia utulivu wa kiroho na kuimarisha ukaribu wake na Mola wake. [1] Wanazuoni wa fiqhi wa madhehebu ya Kishia wamejadili kwa kina hukumu ya funga ya ukimya pamoja na hali ya mtu kukaa kimya bila kuwa na nia ya kufunga kwa muda wote wa siku nzima. [2]

Allama Majlisi, mmoja wa wanazuoni wa Hadithi wa Kishia (aliyefariki mwaka 1110 Hijria), anaamini kwamba; funga ya ukimya ilikuwa ni inajuzu (halali) kwa Bani Israil na ilikuwa moja ya masharti ya khalwa (kuwasaika na Mwenye Ezi Mungu) miongoni mwa wacha-Mungu wa Bani Israil; ila ibada hii ilibaitlishwa na sheria za Kiislamu. [3] Kwa hiyo kwa mtazamo wa Allama Majlisi ni kwamba; kitendo hichi kilikuwa na nafasi maalum katika maisha ya kidini ya Bani Israil na kilizingatiwa kama ni njia mojawapo ya kujitakasa na kumkaribia Mwenye Ezi Mungu. Hata hivyo, amri hii ya funga ya ukimya ilifutwa na Uislamu ulileta mafundisho mapya na kuweka njia maalum za kufunga, ambazo hazijumuishi ukimya kama sehemu ya funga. Hii inamaanisha kwamba, ingawa funga ya ukimya ilikuwa na umuhimu wake katika dini za zamani, ila haijumuishwi tena katika utekelezaji wa ibada za Kiislamu. Baadhi ya wanazuoni na watafiti wa kidini wamesema kwamba; Aya ya 26 ya Surat ya Maryam inathibitisha kuwa funga ya ukimya ilikuwa ni ibada halali kwa jamii ya Bani Israil. Aya hii, inasimulia jinsi bibi Mariamu (Maryam) alivyo mbiwa akae kimya na asizungumze na watu yeyote yule hali akiwa katika amali hii, nayo ni ishara ya kwamba aina hii ya funga ilikuwa ni sehemu ya ibada zao. Ila ibada hii ilikuja futwa na sheria za Kiislamu. [4]

Katika baadhi ya Hadithi na simulizi za kidini, funga ya ukimya imeelezewa kwa neno «زَمٌّ» (zammu). [5] «Zammu» ni neno linalomaanisha hatamu, ambayo ni kifaa kilichotumika kuongoza ngamia kwa kuwawadhibiti na kuwaongoza njia maalumu. Wacha-Mungu wa Bani Israil walikuwa wakitumia kifaa kinachofanana na hatamu hii na kuweka mdomoni mwao, ili kuwazuia wasizungumze kwa muda wote wa siku nzima. [6]

Uharamu wa Funga ya Ukimya

Wanazuoni wa pande zote mbili; Kishia na Kisunni, [7] wameharamisha ibada ya saumu ya ukimya yenye nia ya kukaa kimya kwa makusudio ya kujikaribisha na Mwenye Ezi Mungu. [8]

Mtazamo wa Shia

Funga ya ukimya Katika vyanzo vya fiqhi ya Kishia, inachukuliwa kuwa ni haramu na imeorodhesha kwenye fungu la funga zisizo kubalika katika sheria za Kiislamu. [9] Wanazuoni wa Kishia wakitoa hoja juu ya uharamu wa funga hii wamesema kwamba; Hadithi nyingi zinazopokewa kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na maimamu watakatifu, zinaoenekana kuponda na kupinga funga ya ukimya na zimekataa funga ya aina kama hiyo. Hadithi hizi zinaonyesha wazi kwamba funga ya ukimya haikubaliki na inachukuliwa kama kitendo kiendacho kinyume na sheria za Kiislamu. [10] Fadhili Lankarani, mmoja wa wanazuoni maarufu wa Kishia, anasisitiza kwamba Sheria za Kiislamu zimeweka wazi vitendo vyote vinavyohitajika kwa mtekelezaji wa amali ya saumu, iwe ya wajibu au ya haramu, yote yamefafanuliwa ndani ya sheria za Kiislamu. Kulingana na mtazamo wake, funga ya ukimya haina mahali katika orodha hii ya vitendo vilivyoamriwa na katika masharti ya ibada hii, hivyo basi kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kuzua jambo ambalo halikuwepo ndani ya dini (Bid’a). [11]

Wanazuoni wa fiqhi wanatofautisha kati ya ukimya wa kawaida na ukimya unaokusudiwa kama ni sehemu ya funga. Wakifafanu suala hili wamesema kwamba; ukimya bila kuwa na nia maalum ya kufunga, hata kama utachukua muda wote wa siku nzima, hauwezi kupingana na sheria za kidini na hauhesabiwi kama ni kitendo kisichokubalika. [12] Hii ina maana kwamba; mtu anaweza kukaa kimya kwa muda wote wa siku nzima kwa sababu nyingine yoyote, kama vile kwa makusudi ya kujizuia na mazungumzo, au kwa sababu nyingine binafsi, bila yeye kuliingiza tendo hilo katika muktadha wa funga. Katika hali hii, ukimya huo hautachukuliwa kuwa ni haramu na wala hakuna ubaya wowote au adhabu fulani kwa mfanyaji wa tendo hilo.

Mtazamo wa Kisunni

Wanazuoni wa Kisunni, baada ya kunukuu Hadithi kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), wameiorodhesha amali ya funga ya ukimya katika orodha ya amali ziendazo kinyume na mafunzo ya Kiislamu, kwa hiyo funga hii ni haramu kwa mtazamo wa wanazuoni wa upande wa madhehebu ya Kisunni. [13] Kwa mfano, Abu Hanifa, ambaye ni imamu wa madhehebu ya Hanafiyya, alimetoa msimamo wa wazi juu ya hukumu ya amali hii. Yeye anasema kwamba funga hii ni haramu, na katu haikubaliki ndani ya sheria ya Kiislamu. [14] Zamakhshari, mfasiri maarufu wa Kisunni, pia alithibitisha uharamu wa funga hii. [15] Aidha, Ibn Qudama, miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa upande wa Kisunni, alikubaliana na maoni haya na kuonyesha kwamba funga ya ukimya ni kinyume na mafundisho ya Kiislamu. [16]

Mada Zinazo Husiana