Dua ya thelathini na sita ya Sahifa Sajjadiyya
Dua ya thelathini na sita ya Sahifa Sajjadiyya: ni miongoni mwa dua zilizorithiwa na kunukuliwa kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s). Imeripotiwa kuwa Imamu (a.s), aliitumia dua hii katika maombi yake yaliyofuatia baada ya kushuhudia kwake matukio ya hali ya hewa kama vile mawingu, umwesa (mmweko wa radi), na ngurumo ya radi. Katika dua hii, Imamu Sajjad (a.s) anachukulia matukio ya radi na umwesa (mmweko), kama ni dhihirisho au akisiko la alama maalu za Mwenye Ezi Mungu. Hivyo Imamu (a.s) hakuacha kumuomba Mola wake mvua yenye baraka baada kuona alama hiyo kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu. Kadhalika, dua hii inahimiza dhana ya unyenyekevu na maombi ya dhati kama ni moja ya njia msingi za kujiepusha na maafa. Hii ni kwa kuwa maombi na unyenyekevu, humweka mwanadamu katika hali ya unyonge mbele ya mamlaka makuu ya Kiungu, ikionesha kuwa yeye hana uwezo wa kujilinda dhidi ya nguvu na ghadhabu za Mola wake. Ufafanuzi na uchambuzi wa dua ya thelathini na sita ya Sahifa Sajjadiya, unapatikana katika vitabu vilivyotoa tafsiri chambuzi za Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya kifasri vikichambua dua hii pamoja na dua nyengine za Sahifa Sajjadiyya, ni pamoja na; kitabu kiitwacho 'Shuhud wa Shinakht', kazi ya kitaaluma ya Hassan Mamduhi Kermanshahi, na kitabu 'Riyad as-Salikin', kazi andishi ya Sayyid Ali Khan Madani, iliyoandikwa kwa lugha ya Kiarabu.
Mafundisho Yaliyomo Ndani ya Dua ya Thalathini na Sita Dua ya thelathini na sita ni miongoni mwa dua tukufu za Sahifa Sajjadiya, zitokazo kwa Bwana wetu Imamu Ali Zainul Abidin (a.s). Kwa mujibu wa nukuu zilizripotiwa kuhusiana na dua hii, ni kwamba; Yeye (a.s), alikuwa akiisoma dua hii pindi anapoona mawingu na kushuhudia radi na mweko (umwesa) wenye alama ya rehema (mvua) za Mwenye Ezi Mungu. Kama anavyoeleza Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah katika kitabu cha Afaq al-Ruh; dua hii inatufunza jinsi ya wanadamu wanavyotakiwa kuyatazama matukiombali mbali ya kimaumbile. Kwa mtazamo wa Sayyid Muhammad Fadhlullah, ni kwamba; dua hii ni alama inayoakisi hali ya sifa za kiroho alizonazo Imamu Zainul abidina (a.s.), ambaye alikiona kila kitu katika ulimwengu huu kama ni ishara wazi ya kuwepo kwa Allah (s.w.t), na kuwa ni njia (nyenzo) ya kumshukuru na kumuomba Mwenye Ezi Mungu, ili atuzidishie neema Zake na atuepushie shari mbali mbali. [1] Aidha, bwana Mamduhi Kermanshahi katika uchambuzi wake ya dua hii, anabainisha akisema kwamba; Muumini wa kweli huona mfumo wote wa kimaumbeli, kuwa umo chini ya udhibiti wa Mamlaka ya Mwenye Ezi Mungu. Hivyo, hujitahidi kutumia kila tukio kama ni fursa ya kukurubia kwa Mola wake. [2] Mafundisho yaliyomo katika dua hii ni yamekuja kama ifuatayo: • Radi, umwesa (mmweko), mawingu na mvua ni miongoni mwa alama za qudra (uweza) ya Mwenye Ezi Mungu. • Ufalme na mamlaka ya Mwenyezi Mungu juu ya nidhamu na mfumo wa maumbile, pamoja na mtirirko wa maumbile uliodhibitiwa na mkondo wa sheria za uumbaji. • Mwingiliano na mafungamano thabiti baina ya maisha ya binadamu na utaratibu wa kimazingira duniani (mfumo wa ulimwengu). • Kuomba mvua ya baraka (neema) na kujikinga na adha (hasara) za mvua. • Unyenyekevu na kilio mbele ya Mwenye Ezi Mungu, kwa ajili ya kuepushwa na shari. • Kuwasilisha ombi la kumtaka Mwenye Ezi Mungu asituwekechini ya mamlaka ya mwengine yoyote yule asiyekuwa Yeye. • Majanga ya ukame na ufukara ni matunda yatokanayo na ukorofi na kushikamana na tabia mibaya. • Utajiri na uzima wa afya kwa mwanadamu, vipo chini ya kivuli cha rehma za Mwenye Ezi Mungu. • Udhaifu wa kiumbe katika kujikinga na hasira (adhabu) za Mwenye Ezi Mungu. • Ukunjufu wa uweza mkuu wa Mwenye Ezi Mungu usio na mipaka. • Kumshukuru na kumtakasa Mwenye Ezi Mungu kwa ajili ya neema zake zisizo na mipaka. • Dhana ya Mungu kukubali kiwango kidogo cha shukurani kutoka kwa viumbe wake. • Hakika marejeo na hatima ya yetu ni kwa Allah. (Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un). [3] Tafsiri Chambuzi za Dua ya Thalathini na Sita Kuna kazi kadhaa andishi zilzizoandikwa kwa lugha mbali mbali, katika jitihada za kufasiri na kuchambua za Sahifa Sajjadiyaa ikiwemo Dua ya thalathini na sita ya kitabu hicho. Miongoni mwa kazi chambuzi zilizoandikwa kwa lugha ya Kifarsi ni pamoja na; kitabu cha Shuhud wa Shinakht, kazi ya Muhammad-Hassan Mamduhi Kermanshahi, [4] na Sharh wa Tarjomeh Sahife Sajjadiyye, kazi ya Sayyid Ahmad Fahri. [5] Aidha, waandishi wengine kadhaa walioandika na kuwasilisha ufafanuzi wa Dua ya thelathini na sita sambamba na dua nyengine zilizomo katika kitabu cha Sahifa Sajjadiyya kwa lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa kazi za Kiarabu kuhusiana na dua hizo, ni pamoja na; Riadhu as-Salikin, kazi ya Sayyid Ali Khan Madani, [6] Fi Dhilali as-Sahifa as-Sajjadiyya, kazi ya Muhammad Jawad Mughniyyah, [7] Riadhu al-Arifina, kazi iliyofanywa na Muhammad bin Muhammad Darabi [8] na Afaq ar-Ruh, kazi ya Sayyid Muhammad Hussein Fadlallah. [9] Zaidi ya hayo, pia kuna wanazuoni waliotenga wakati wa kwa ajili ya kazi ya uchambuzi wa istilahi na msamiati wa dua hii, sambamba na dua nyengine za kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa jitihada maarufu maaru zaidi kuhusiana na kazi hiyo, ni pamoja na; Ta'liqat Alaa as-Sahifa as-Sajjadiyya, kazi ya Faidhu Kashani [10] na Sharhu as-Sahifa as-Sajjadiyya, kazi ya Izzu al-Din al-Jazairi. [11]
Matini ya Kiarabu Pamoja na Maelezo kwa Kiswahili وَ كَانَ مِنْ دُعَائِهِ عَلَيْهِ السَّلَامُ إِذَا نَظَرَ إِلَى السَّحَابِ وَ الْبَرْقِ وَ سَمِعَ صَوْتَ الرَّعْدِ Ni ifuatayo ilikuwa ni miongoni mwa dua yake (rehema na amani ziwe juu yake), aliyokuwa akiomba pindi alipokuwa akishuhudia tukio la kutokea kwa mawingu na umwesa (mmweko), pamoja na mngurumo wa radi. اللَّهُمَّ إِنَّ هَذَيْنِ آيَتَانِ مِنْ آيَاتِكَ، وَ هَذَيْنِ عَوْنَانِ مِنْ أَعْوَانِكَ، يَبْتَدِرَانِ طَاعَتَكَ بِرَحْمَةٍ نَافِعَةٍ أَوْ نَقِمَةٍ ضَارَّةٍ، فَلَا تُمْطِرْنَا بِهِمَا مَطَرَ السَّوْءِ، وَ لَا تُلْبِسْنَا بِهِمَا لِبَاسَ الْبَلَاءِ. Ewe Mwenye Ezi Mungu, hakika hivi viwili ni alama mbili miongoni mwa alama Zako, na ni wasaidizi wawili miongoni mwa wasaidizi wako. Vinaharakisha kutii amri yako, ambavyo ima huwa ni vyenye rehema yenye manufaa, au ni vyenye kubeba adhabu yenye kuumiza. Hivyo, usitunyeshezee mvua yenye madhara kupitia viwili hivi, na wala usije ukatuvike vazi la maafa.
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ أَنْزِلْ عَلَيْنَا نَفْعَ هَذِهِ السَّحَائِبِ وَ بَرَكَتَهَا، وَ اصْرِفْ عَنَّا أَذَاهَا وَ مَضَرَّتَهَا، وَ لَا تُصِبْنَا فِيهَا بِآفَةٍ، وَ لَا تُرْسِلْ عَلَى مَعَايِشِنَا عَاهَةً.
Ewe Mwenye Ezi Mungu, mbariki Muhammad na Aali zake, na uteremshe manufaa na baraka za mawingu haya. Na utuepushe na madhara na uharibifu wake. Na wala usitupatilize usituvike janga lolote lile kupitia mawingu hayo, wala usilete uharibifu katika njia za maisha yetu (njia za rizki zetu). اللَّهُمَّ وَ إِنْ كُنْتَ بَعَثْتَهَا نَقِمَةً وَ أَرْسَلْتَهَا سَخْطَةً فَإِنَّا نَسْتَجِيرُكَ مِنْ غَضَبِكَ، وَ نَبْتَهِلُ إِلَيْكَ فِي سُؤَالِ عَفْوِكَ، فَمِلْ بِالْغَضَبِ إِلَى الْمُشْرِكِينَ، وَ أَدِرْ رَحَى نَقِمَتِكَ عَلَى الْمُلْحِدِينَ. Ewe Allah, na ikiwa umeiteremsha (mvua/dhoruba hii) kuwa ni adhabu, na umeileta kwa hasira (kutokana na ghadhabu Zazko), basi hakika sisi tunajilinda Kwako kutokana na ghadhabu Zako, na tunakusihi (tunakulilia) na kukuomba msamaha Wako. Basi igeuze ghadhabu hiyo iwaendee washirikina, na lizungushe gurudumu la mateso Yako juu ya wapinzani wa dini (wakanushaji).
اللَّهُمَّ أَذْهِبْ مَحْلَ بِلَادِنَا بِسُقْيَاكَ، وَ أَخْرِجْ وَحَرَ صُدُورِنَا بِرِزْقِكَ، وَ لَا تَشْغَلْنَا عَنْكَ بِغَيْرِكَ، وَ لَا تَقْطَعْ عَنْ كَافَّتِنَا مَادَّةَ بِرِّكَ، فَإِنَّ الْغَنِيَّ مَنْ أَغْنَيْتَ، وَ إِنَّ السَّالِمَ مَنْ وَقَيْتَ
Ewe Mwenye Ezi Mungu, uondosha ukame unaoikabili ardhi yetu kwa unyeshezaji Wako, na uondoe ghadhabu na vinyongo vilivyomo vifuani mwetu kwa neema ya riziki Zako. Usitushughulishe na chochote kile kisichokuwa Wewe, na usitustishie (usikikate) chanzo cha fadhila Zako kwetu, sote kwa pamoja. Hakika, mwenye utajiri (wa kweli) ni yule uliyemtajirisha, na hakika mwenye amani (ya kweli) ni yule uliyemlinda (uliyepa himaya Yako).
مَا عِنْدَ أَحَدٍ دُونَكَ دِفَاعٌ، وَ لَا بِأَحَدٍ عَنْ سَطْوَتِكَ امْتِنَاعٌ، تَحْكُمُ بِمَا شِئْتَ عَلَى مَنْ شِئْتَ، وَ تَقْضِي بِمَا أَرَدْتَ فِيمَنْ أَرَدْتَ
Hakuna yoyote yule mwenye uwezo kutoa kinga isipokuwa Wewe peke Yako, na wala hakuna epuko lolote (linaloweza kukimbiliwa) kwa ajili ya kujilinda dhidi ya mamlaka Yako makuu. Unatoa hukumu Yako kwa umtakaye kulingana na matakwa, na unapitisha amri (Yako) kwa umtakaye kulingana na irada Yako (kulingana na matakwa Yako). فَلَكَ الْحَمْدُ عَلَى مَا وَقَيْتَنَا مِنَ الْبَلَاءِ، وَ لَكَ الشُّكْرُ عَلَى مَا خَوَّلْتَنَا مِنَ النَّعْمَاءِ، حَمْداً يُخَلِّفُ حَمْدَ الْحَامِدِينَ وَرَاءَهُ، حَمْداً يَمْلَأُ أَرْضَهُ وَ سَمَاءَهُ Hivyo, sifa njema zote zinakustahikia Wewe kutokana na ulinzi uliotupa dhidi ya majanga (mbali mbali), na shukrani zote ni Zako Wewe kwa fadhila ulizotukirimu nazo. Ni sifa ambazo kiwango chake kinazidi sifa za wahimidi wote. (Tunamsifu na kumhimidi Mwenye Ezi Mungu) kwa sifa zenye kiwango cha kuenea na kujaza ardhi pamoja na mbingu Zake. إِنَّكَ الْمَنَّانُ بِجَسِيمِ الْمِنَنِ، الْوَهَّابُ لِعَظِيمِ النِّعَمِ، الْقَابِلُ يَسِيرَ الْحَمْدِ، الشَّاكِرُ قَلِيلَ الشُّكْرِ، الْمُحْسِنُ الْمُجْمِلُ ذُو الطَّوْلِ، لَا إِلَهَ إِلَّا أَنْتَ، إِلَيْكَ الْمَصِيرُ.
Hakika Wewe ndiye “Al-Mannan” (Mpaji/mtoaji) kwa upaji mkubwa mno, Al-Wahhab (Mtoaji) wa neema adhimu, Mpokeaji wa himidi zilizo chache, na “Ash-Shakur” (Mwenye shukrani) kwa shukrani zilizo chache. Wewe ni “Al-Muhsin” (Mwenye Hisani), “Al-Mujmil” (Mwenye kupamba), Dhul-Tawl (Mwenye Nguvu na Fadhila). “La ilaha illa Anta” (Hapana mola ila Wewe tu), na Kwako ndiyo marejeo (ya kila kitu).