Dua ya Kumi na Tatu ya Sahifa Sajjadiyya: ni dua iliyopokewa kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s), nayo ni dua iliyobeba na kuakisi dhana ya utegemezi wa mwanadamu kwa Mola wake, pamoja na ukwasi kamili wa Mwenye Ezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala. Pia Imamu Sajjad (a.s) katika dua hii, anatoa mwanga juu ya neema za Mwenye Ezi Mungu zisizo na kikomo na hali ya kutobadilika kwa hekima Mwenye Ezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala. Aidha, dua hii inatufumbua macho ya kuwa; kunyimwa na kukata tamaa ndiyo hatima ya kuelekeza maombi kwa asiyekuwa Mungu, na kwamba dhambi ni sababu hasa ya kujitenga na hadhara ya Mwenye Ezi Mungu. Vilevile, Imamu Sajjad (a.s) anabainisha kuwa; kuomba katika sijda na kumswalia Mtume (s.a.w.w) pamoja na Aali zake ni miongoni mwa nyenzo asili za kukubaliwa kwa dua zetu.

Dua hii ya Kumi na Tatu imeshereheshwa na kuchambulia kwa kina kabisa katika vitabu vya tafsiri za Sahifa Sajjadiyya, kama vile kitabu Diyare Asheghan cha Hossein Ansarian na Shuhud wa Shenakht, kazi ya Hassan Mamduhi Kermanshahi. Vitabu viliwili hivi ni vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiajemi. Na kitabu cha Riyadhu al-Salikin cha Sayyid Ali Khan Madani, ni kitabu chenye kufasiri na kufafanua dua za kitabu cha Sahifa Sajjadiyya kwa lugha ya Kiarabu.


Misingi ya Mafunzo Yaliomo Ndani Yake

Dhamira kuu ya dua ya kumi na tatu ilioko katika maandiko ya Sahifa Sajjadiyya, ni kubainisha hali ya uhitaji wa mwanadamu kwa Muumba wake na kutokuwa na hiari katika kurejea kwenye mamlaka ya Mola wake. Aidha, dua hii inachambua mapungufu ya viumbe katika kukidhi mahitaji yao binafsi. Akitumia uchambuzi huo kama ni nyezo ya kukaribiana na Mola wake, Imamu Sajjad ameonekana akiwasilisha maombi yake kwa Mola wake akitariji fadhila Zake Subhanahu Wataala. [1] Misingi ya mafunzo ya dua ya kumi na tatu, [2] ipokewa kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s.) ikiwa imebeba ndani yake maudhui zifuatazo:


·        Mungu ndiye upeo na hitimisho la kiu za maombi ya waombaji.

·        Viumbe wote kimaumbile (kiontolojia), wako chini ya hali ya kusalimu amri mbele ya uwezo wa Mwenye Ezi Mungu.

·        Neema za Allah kwa waja wake hazihesabiki na wala hazina  masimango ndani yake.

·        Neema na utoaji wa Kiungu hauna masharti ya kibiashara, wala utoaji Wake hautaraji malipo.

·        Utegemezi wa viumbe kwa Mola wao na ukwasi kamili wa Mungu dhidi ya viumbe wake.

·        Kuepukana na ufukara kupitia utajiri wa Mwenye Ezi Mungu.

·        Hazina za Mungu ni hazina zisizo na mwisho (mipaka).

·        Mwenyezi Mungu ndiye shabaha na kilele cha harakati zote, na kila kitu kinamrejea Allah Ambaye ndiye lengo na marejeo ya kila kitu.

·        Kamwe Hekima za Mwenye Ezi Mungu si zenye kubadiliki.

·        Mwenye Ezi Mungu ni mwenye ukamilifu usio na kifani.

·        Mwenye Ezi Mungu ndiye chanzo pekee cha ufumbuzi wa kila changamoto.

·        Malipo na hatima ya kumwomba asiyekuwa Allah, ni kukata tamaa na kunyimwa.

·        Inatupasa kumuomba Mungu peke yake, kumtaka msaada, na kuwa na dhana njema juu ya Mwenye Ezi Mungu katika kuamiliana nasi.

·        Taufiki na fadhila za Mwenye Ezi Mungu ndiyo sababu ya kuepukana na mitelezo na upotofu.

·        Kuwa na matumaini kama zao msingi la kuwa na imani thabiti juu ya uwepo wa Mungu.

·        Maasi ndiyo pazia zito zaidi linalomtenganisha mja na kumweka mbali na hadhara takatifu ya Mola wake.

·        La msingi na lenye matumaini zaidi, ni kuomba fadhila za Mungu badala ya uadilifu wake.

·        Kumlilia na kumnyenyekea Allah kwa dhati katika maombi yetu.

·        Kumuomba Alla atuepushe na kunyimwa kwa fadhila Zake.

·        Utegemezi kamili wa kimatendo wa kumtegemea Mwenye Ezi Mungu katika kila kitu.

·        Kumsalia Mtume (s.a.w.w) na Aali zake ndiyo nyezo msingi kukubaliwa kwa mahitaji mja.

·        Utulivu wa mwanadamu unatokana na neema za Mwenye Ezi Mungu.

·        Kuwaomba viumbe ni tunda linalozaliwa na wasiwasi na udanganyifu wa nafsi.

·        Kutochoka kwa Mwenye Ezi Mungu kutokanai na maombi ya waja Wake.

·        Taufiki ya kuomba ipo chini ya kivuli cha majaaliwa ya Mwenye Ezi Mungu.

·        Ufanisi wa kuwasilisha maombi katika hali ya kusujudu. [3]


Tafsiri Fafanuzi za Dua ya Kumi na Tatu

Dua ya kumi na tatu imetafsiriwa na kufafanuliwa kwa lugha ya Kiajemi katika vitabu vilikuja kutoa sherhe (ufafanuzi) wa Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Diyare Asheqan kilichoandikwa na Hussein Ansarian, [4] Shohud wa Shenakht kilichoandikwa na Muhammad-Hassan Mamdouhi Kermanshahi, [5] na Sharhe wa Tafsir Sahife Sajjadiyya, kilichoandikwa na Sayyid Ahmad Fahri. [6]

Halikadhalika, dua hii tukufu ya kumi na tatu imepata kushereheshwa (kuchambuliwa) kwa lugha ya Kiarabu na wanazuoni mbali mbali walikuja kufasiri na kutoa uchambuzi wa kitabu cha Sahifa Sajjadiyya kwa lugha ya Kiarabu. Baadhi ya vitabu chambuzi vilivyochambua dua hii ni pamoja na; Riyadhu as-Salikin cha Sayyid Ali-Khan Madani, [7] Fi Dhilali as-Sahifa as-Sajjadiyya, cha Allamah Muhammad Jawad Mughniyya, [8] Riyadh al-'Arifina cha Sheikh Muhammad bin Muhammad Darabi [9] na Afaq ar-Ruh cha Sayyid Muhammad Hussein Fadhluallah. [10] Pia msamiati wa maneno yake matukufu yamepata ufafanuzi katika sherhe ya kilugha (kamusi) iitwayo Ta'liqat 'ala as-Sahifa as-Sajjadiyya, kitabu kilichoandikwa na mwanachuoni maarufu aitwaye Faidhu Kashani. [11]


Matini ya Dua na Tafsiri Yake

وَ كَانَ مِنْ دُعَائِهِ عَلَيْهِ السَّلَامُ فِي طَلَبِ الْحَوَائِجِ إِلَي اللَّهِ تَعَالَي

Na miongoni mwa dua zake (rehema na amani ziwe juu yake), ilikuwa ni ile dua ya kuwasilisha haja zake kwa Mwenye Ezi Mungu Mtukufu.

اللَّهُمَّ يَا مُنْتَهَى مَطْلَبِ الْحَاجَاتِ

Ewe Mola wangu Mlezi! Ewe ambaye Yeye ndiye hitimisho la matakwa (haja za waja).

وَ يَا مَنْ عِنْدَهُ نَيْلُ الطَّلِبَاتِ

Na Ewe ambaye kwake Yeye ndiko kunakopatikana (utimilifu wa) maombi yote.

وَ يَا مَنْ لَا يَبِيعُ نِعَمَهُ بِالْأَثْمَانِ

Na Ewe Yule asiyeuza fadhila Zake kwa thamani fulani.

وَ يَا مَنْ لَا يُكَدِّرُ عَطَايَاهُ بِالِامْتِنَانِ

Na Ewe (Mkarimu) asiyechafua fadhila zake kwa masimbulizi.

وَ يَا مَنْ يُسْتَغْنَى بِهِ وَ لَا يُسْتَغْنَى عَنْهُ

Na Ewe chanzo cha utoshelezaji (cha wenye kujitosheleza), ambaye ni tegemeo lisiloweza kuepukika.

وَ يَا مَنْ يُرْغَبُ إِلَيْهِ وَ لَا يُرْغَبُ عَنْهُ

Na Ewe mtakwa (wa wenye shauku ya kupenda vizuri) ambaye ni kipeo cha shauku, na kamwe si mchukiwa.

وَ يَا مَنْ لَا تُفْنِي خَزَائِنَهُ الْمَسَائِلُ

Na Ewe Yule ambaye wingi wa haja (za waja) haukaushi hazina Zake.

وَ يَا مَنْ لَا تُبَدِّلُ حِكْمَتَهُ الْوَسَائِلُ

Na Ewe Yeye ambaye hekima zake haiwezi kubadilishwa na mbinu wala nyezo zozote zile.

وَ يَا مَنْ لَا تَنْقَطِعُ عَنْهُ حَوَائِجُ الْمُحْتَاجيِنَ

Na Ewe ambaye mkururo wa mahitaji ya wahitaji hayakomi kuja kwako Wewe.

وَ يَا مَنْ لَا يُعَنِّيهِ دُعَاءُ الدَّاعِينَ .

Na Ewe Ambaye haelemewi (hachoshwi) na (wingi wa) maombi ya waombaji.


تَمَدَّحْتَ بِالْغَنَاءِ عَنْ خَلْقِكَ وَ أَنْتَ أَهْلُ الْغِنَى عَنْهُمْ


Umesifika kwa sifa ya kutowahitaji viumbe Wako, na hakika Nawe ndiye unayestahili kutokuwa na haja nao.

وَ نَسَبْتَهُمْ إِلَى الْفَقْرِ وَ هُمْ أَهْلُ الْفَقْرِ إِلَيْكَ .

Na uliwavisha (viumbe Wako) vazi (umbile) la utegemezi, na huo ndio uhalisia wao mbele yako.

فَمَنْ حَاوَلَ سَدَّ خَلَّتِهِ مِنْ عِنْدِكَ ، وَ رَامَ صَرْفَ الْفَقْرِ عَنْ نَفْسِهِ بِكَ فَقَدْ طَلَبَ حَاجَتَهُ فِي مَظَانِّهَا ، وَ أَتَى طَلِبَتَهُ مِنْ وَجْهِهَا .

                                                                                                                                              

Basi yeyote yule anayejaribu kutatua mapungufu yake kupitia Kwako, na akataka kuondoa ufukara wake kwa msaada Wako, kwa hakika huyo ameomba haja yake mahali panapostahili, na ameshughulikia ombi lake kwa njia sahihi kabisa.


وَ مَنْ تَوَجَّهَ بِحَاجَتِهِ إِلَى أَحَدٍ مِنْ خَلْقِكَ أَوْ جَعَلَهُ سَبَبَ نُجْحِهَا دُونَكَ فَقَدْ تَعَرَّضَ لِلْحِرْمَانِ ، وَ اسْتَحَقَّ مِنْ عِنْدِكَ فَوْتَ الْاِحْسَانِ.

Na yeyote yule anaye elekeza hitaji lake kwa yeyote miongoni mwa viumbe vyako, au akamchukulia kiumbe huyo kuwa ndiye chanzo cha mafanikio yake badala Yako, basi bila shaka yeye atakuwa amejiweka katika hatari ya kunyimwa, na anastahili kupoteza fursa ya kupata ukarimu wako.

اللَّهُمَّ وَ لِي إِلَيْكَ حَاجَةٌ قَدْ قَصَّرَ عَنْهَا جُهْدِي ، وَ تَقَطَّعَتْ دُونَهَا حِيَلِي ، وَ سَوَّلَتْ لِي نَفْسِي رَفْعَهَا إِلَى مَنْ يَرْفَعُ حَوَائِجَهُ إِلَيْكَ ، وَ لَا يَسْتَغْنِي فِي طَلِبَاتِهِ عَنْكَ ، وَ هِيَ زَلَّةٌ مِنْ زَلَلِ الْخَاطِئِينَ ، وَ عَثْرَةٌ مِنْ عَثَرَاتِ الْمُذْنِبِينَ

Ewe Mola wangu, nami nina shida (hitaji) Fulani Kwako, ambayo jitihada zangu zimepwaya katika kuifikia (shida hiyo), na hila zangu zote zimekatika pasi na kuipata. Kisha, nafsi yangu ikanipambia wazo la kuiwasilisha kwa kiumbe ambaye naye huinua haja zake Kwako (ambaye hata haja zake pia zinamshinda), wala hawezi kujitoshelezea haja zake pasi Nawe. Bila shaka hili ni telezo katika matelezo ya wenye hatia, na ni anguko katika maanguko ya wenye makosa.


ثُمَّ انْتَبَهْتُ بِتَذْكِيرِكَ لِي مِنْ غَفْلَتِي ، وَ نَهَضْتُ بِتَوْفِيقِكَ مِنْ زَلَّتِي ، وَ رَجَعْتُ وَ نَكَصْتُ بِتَسْدِيدِكَ عَنْ عَثْرَتِي .

Kisha, nilizindka kutoka katika uzembe wangu kupitia ukumbusho Wako ulionikumbusha nao, nikasimama sawa na kuachana na mtelezo wangu kupitia taufiki Yako, na nikarejea na kujiepusha na maanguko yangu kupitia uelekezi (udhibiti) Wako.

وَ قُلْتُ سُبْحَانَ رَبِّي كَيْفَ يَسْأَلُ مُحْتَاجٌ مُحْتَاجاً وَ أَنَّى يَرْغَبُ مُعْدِمٍ اِلَي مُعْدِمٍ

Kisha nikasema: Ametakasika Bwana wangu! Inawezekanaje mhitaji kumuomba msaada mhitaji mwenzake, na iweje maskini amtegemee maskini mwingine?

فَقَصَدْتُكَ ، يَا إِلَهِي ، بِالرَّغْبَةِ ، وَ أَوْفَدْتُ عَلَيْكَ رَجَائِي بِالثِّقَةِ بِكَ

Kwa hivyo, nilikuelekea Wewe, Ee Mungu wangu, nikiwa na shauku kubwa (Kwako), na nikaliwasilisha tumaini langu Kwako, huku nikiwa na imani kamili Kwako.

وَ عَلِمْتُ أَنَّ كَثِيرَ مَا أَسْأَلُكَ يَسِيرٌ فِي وُجْدِكَ ، وَ أَنَّ خَطِيرَ مَا أَسْتَوْهِبُكَ حَقِيرٌ فِي وُسْعِكَ ، وَ أَنَّ كَرَمَكَ لَا يَضِيقُ عَنْ سُؤَالِ أَحَدٍ ، وَ أَنَّ يَدَكَ بِالْعَطَايَا أَعْلَى مِنْ كُلِّ يَدٍ .

Na nikatambua (nikabaini) kwamba maombi yangu mengi ni jambo dogo sana mbele ya utajiri Wako, na kwamba jambo kubwa ninaloomba Kwako, ni dogo sana mbele ya uwezo Wako mkuu. Pia, nikatambua kwamba ukarimu Wako haupunguzwi na ombi la yeyote, na kwamba Mkono Wako katika kutoa ni mkuu kuliko mikono yote.

اللَّهُمَّ فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ احْمِلْنِي بِكَرَمِكَ عَلَى التَّفَضُّلِ ، وَ لَا تَحْمِلْنِي بِعَدْلِكَ عَلَى الِاسْتِحْقَاقِ ، فَمَا أَنَا بِأَوَّلِ رَاغِبٍ رَغِبَ إِلَيْكَ فَأَعْطَيْتَهُ وَ هُوَ يَسْتَحِقُّ الْمَنْعَ ، وَ لَا بِأَوَّلِ سَائِلٍ سَأَلَكَ فَأَفْضَلْتَ عَلَيْهِ وَ هُوَ يَسْتَوْجِبُ الْحِرْمَانَ .

Ewe Mola, mshushie rehema na baraka Muhammad na Aali zake. Na Unihukumu kwa msingi wa fadhila za ukarimu Wako, na wala si kwa msingi wa uadilifu Wako kama ninavyostahili. Kwa hakika, mimi si mtamaniji (mtaraji) wa kwanza aliyeelekea Kwako nawe Ukamkirimu, hali akistahili kunyimwa; wala mimi si mwombaji wa kwanza aliyeomba ombi lake nawe ukamneemesha kupita kiasi, ingawa hali yake ilihistahili kunyimwa (umarufuku).

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ كُنْ لِدُعَائِي مُجِيباً ، وَ مِنْ نِدَائِي قَرِيباً ، وَ لِتَضَرُّعِي رَاحِماً ، وَ لِصَوْتِي سَامِعاً .

Ewe Mola, mshushie rehma Zako Muhammad na Aali zake; na Uwe ni mwenye kuitikia dua yangu, na uwe karibu na wito wangu, na uwe mwenye huruma kwa unyenyekevu wangu, na uwe msikivu kwa sauti yangu.

وَ لَا تَقْطَعْ رَجَائِي عَنْكَ ، وَ لَا تَبُتَّ سَبَبِي مِنْكَ ، وَ لَا تُوَجِّهْنِي فِي حَاجَتِي هَذِهِ وَ غَيْرِهَا إِلَى سِوَاكَ

Na usikatize matumaini yangu kwako, wala usilikate unganisho langu (linaloniunganisha) Nawe, na usinielekeze kwa yeyote yule, si katika hitaji langu hili wala mengineyo, isipokuwa kwako Wewe tu.

وَ تَوَلَّنِي بِنُجْحِ طَلِبَتِي وَ قَضَاءِ حَاجَتِي وَ نَيْلِ سُؤْلِي قَبْلَ زَوَالِي عَنْ مَوْقِفِي هَذَا بِتَيْسِيرِكَ لِيَ الْعَسِيرَ وَ حُسْنِ تَقْدِيرِكَ لِي فِي جَمِيعِ الْأُمُورِ

Na Nisimamie, Ee Mola, katika kufikia ufanisi wa matakwa yangu, utimilifu wa haja (shida) yangu, na upatikanaji wa hitaji langu, kabla ya mimi kuondoka katika kikao changa hichi (nilichokaa). Niwafikishe kupitia uwepesishaji Wako wa kurahisisha yaliyo mazito, na kwa uzuri wa makadirio Yako kwangu katika  mahijati yangu yote.


وَ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ صَلَاةً دَائِمَةً نَامِيَةً لَا انْقِطَاعَ لِأَبَدِهَا وَ لَا مُنْتَهَى لِأَمَدِهَا ، وَ اجْعَلْ ذَلِكَ عَوْناً لِي وَ سَبَباً لِنَجَاحِ طَلِبَتِي ، اِنَّكَ وَاسِعٌ كَرِيمٌ .

Na mshushie rehem ana baraka Muhammad na Aali zake, baraka zenye ustawi wa daima, zisizo na kikomo katika umilele wake wala zisizo na mwisho katika muda wake. Na uzifanye kuwa ni kisaidizi kwangu na njia ya kufanikishia mahitaji yangu. Hakika, Wewe ni Mwenye Mkarimu usiye na mipaka (katika ukarimu Wako).

وَ مِنْ حَاجَتِي يَا رَبِّ كَذَا وَ كَذَا . (تَذْكُرُ حَاجَتَكَ ثُمَّ تَسْجُدُ وَ تَقُولُ فِي سُجُودِكَ) فَضْلُكَ آنَسَنِي ، وَ إِحْسَانُكَ دَلَّنِي ، فَأَسْأَلُكَ بِكَ وَ بِمُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، صَلَوَاتُكَ وَ عَلَيْهِمْ أَن لَا تَرُدَّنُِي خَائِباً .

Na miongoni mwa haja zangu, Ee Mola wangu Mlezi, ni (haja fulani na fulani) ... (Hapa mwombaji hutakiwa ataje ombi lake). (Ee Mola wangu Mlezi kwa hakika) Fadhila zako zimenipa faraja, na wema wako umeniongoza. Hivyo nakuomba Wewe kukupitia Wewe  Mwenyewe, na kupitia kwa mpitia Muhammad na Aali zake—rehma zako ziwe juu yao—hivyo basi usinikatishe tamaa (katika maombi yangu haya).