Dhi Qar (Kifarsi: ذی‌قار) ni eneo ambalo kijiografia linapatikana kusini mwa Iraq ambapo katika eneo hilo kulitokea vita vya Dhi Qar baina ya utawala wa ukoo wa Sasanian na Waarabu baada ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (s.a.w.w). Vita hivyo vilimalizika kwa Waarabu kuibuka na ushindi. Kadhalika Imam Ali ibn Abi Twalib (a.s) mwaka 36 Hijiria akiwa na lengo la kwenda kupambana katika vita vya Jamal (ngamia alisimama katika eneo la Dhi Qar na akawahutubia masahaba zake akiwa katika eneo hilo. Hotuba hiyo imenukuliwa katika kitabu cha Nahaj al-Balgha.

Ramani ya Dhi Qar kusini mwa Iraq

Hii leo Dhi Qar ni jina la mkoa ulioko kusini mwa Iraq ambao makao yake makuu ni Nasiriyah. Mkoa wa Dhi Qar una wakazi zaidi ya milioni mbili ambao wengi wao ni wafuasi wa madhehebu ya Ahlul-Beiti (a.s). Mji wa Ur ni katika turathi za kiutamaduni za mkoa huu na ndilo eneo ambalo alizaliwa hapo Nabii Ibrahim (a.s). Katika eneo hilo kunapatikana pia hekalu la Ziggurat.

Kiografia na sababu ya kuitwa kwa jina hilo

Dhi Qar ni eneo lililopo baina ya mji wa Basra na Kufa kusini mwa Iraq. [1] Yaqut Hamawi anasema: Katika eneo hilo kulikuweko na kisima cha maji kilichokuwa mali ya kabila la Bakr ibn Wail kilichokuwa kikifahamika kwa jina la Dhu Qar. [2] Abul Hassan Bayhaqi msomi na mwanazuoni wa karne ya 6 Hijria anasema pia kuwa, eneo hilo lilitwa kwa jina la Dhi Qar kutokana na uwepo wa kisima ambacho maji yake yalikuwa meusi kama lami.[3]

Matukio

Miongoni mwa matukio ya kihistoria yaliyonukuliwa kuhusiana na eneo la Dhi Qar, ni vita baina ya Waarabu na utawala wa ufalme wa Sasanian na jingine ni kusimama hapo Imam Ali (a.s) wakati alipokuwa njiani kuelekea katika Vita vya Jamal.

Vita vya Dhi Qar

Vita vya Dhi Qar vilitokea katika eneo hilo baina ya kabila la Bakr ibn Wail na wapiganaji wa Khosro Parviz mfalme wa wakati huo wa ukoo wa Sasanian wa Iran. [4] Vita hivyo ambavyo vinaelezwa kuwa sababu yake ya kutokea ni kuuawa Nu’man ibn Mundhir al-Lakhmi mmoja wa viongozi wa makabila ya Kiarabu. Kiongozi huyo aliuawa na Khosro Parviz, [5]. Vita hivyo vilitokea wakati Bwana Mtume (s.a.w.w) alipokuwa na umri wa miaka 40; lakini baadhi wanasema, vita hivyo vilitokea baada ya Vita vya Badr na katika kipindi cha Mtume (s.a.w.w) kuweko mjini Madina. [6] Katika vita hivyo, Waarabu walimshinda mjumbe wa Khosro Parviz. Mtume (s.a.w.w) amenukuliwa akisema kuhusiana na hilo: “Hii ni mara ya kwanza Waarabu wanapata ushindi kwa wasiokuwa Waarabu na kufanikiwa kuchukua haki yao kwa baraka zangu”.[7]

Njia ya Vita vya Jamal

Kwa mujibu wa vyanzo vya historia, Imam Ali ibn Abi Twalib (a.s) alifunga safari kutoka Madina akiwa na jeshi lake kwa ajili ya kuelekea upande wa Iraq ili kupigana na Aisha, Talha na Zubeir na mwanzoni mwa kuingia Iraq alisimama na kubakia na jeshi lake katika eneo la Dhi Qar. [8] Imenukuliwa kutoka kwa Abdallah ibn Abbas kwamba: Wakati walipofika katika eneo la Dhi Qar alimuuliza Imam Ali (a.s): “Kutoka katika mji wa Kufa kumejitokeza watu wachache kwa ajili ya kukusaidia.” Imam Ali (a.s) akasema: “Watajitokeza watu 6,560 bila kupungua wala kuongezeka kwa ajili ya kuja kunisaidia.” [9] Baada ya hapo tulibakia Dhi Qar kwa muda wa siku 15 mpaka tukasikia milio ya farasi na nyumbu na jeshi la Kufa likaungana na sisi. Nikawahesabu, na kuona idadi yao ni ileile ambayo Imam Ali (a.s) aliitaja hapo kabla. [10]

Kadhalika imenukuliwa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba, siku moja tulipokuwa katika eneo la Dhi Qar nilimuendea Imam Ali (a.s) na kumkuta akiwa anashona viatu vyake. Akaniuliza hivi viatu vina thamani gani? Nikasema, havina thamani. Akasema, naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba, viatu hivi vilivyoraruka ni vya thamani zaidi kwangu kuliko kukutawaleni (kuwa na utawala juu yenu), isipokuwa kama nitaweza kusimamisha haki na kuondoa batili.” Kisha akatoka nje na kuwahutubia watu. [11] Hotuba hii imenukuliwa katika Nahaj al-Balagha na katika hotuba hiyo Imam Ali ibn Abi Twalib (a.s) alizungumzia hekima ya kubaathiwa Mitume na ubora wake na kulaumu wapinzani. [12]

Mkoa wa Dhi Qar

 
Ramani ya Mkoa wa Dhi Qar

Nchini Iraq kuna mkoa unaojulikana kwa jina la Dhi Qar ambao makao yake makuu ni mji wa Nasiriyah. Mkoa wa Dhi Qar upo umbali wa kilomita 180 kutoka Basra na kilomita 360 kutoka mji mkuu Baghdad. [13] Mwanzoni mwa kuasisiwa kwake mkoa huo ulijulikana kwa jina la al-Muntafak na katika zama za Jamhuri ulibaduilishwa jina la kufahamika kwa jina la Nasiriyah. Mnamo mwaka 1969 serikali ya chama cha Baath ilibadilisha jina la mkoa huo na kuwa Dhi Qar. [14]

 
Sehemu ya ibada katika mji wa Ur

Mkoa wa Dhi Qar una wakazi wapatao milioni mbili ambapo akthari ya wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia. Wakazi wengine wa mkoa huo ni wafuasi wa madhehebu ya Sunni, Mandaens (Wamandai) na Wakristo. Mji wa Ur ni katika turathi za kiutamaduni za mkoa huu ambapo ni mahali wanapoishi Wasumero na Wakkadia. [15] Hili ndilo eneo ambalo alizaliwa hapo Nabii Ibrahim (a.s). [16] Katika eneo hilo kunapatikana pia hekalu la Ziggurat. [17]

Rejea

Vyanzo

  • Bayhaqī, ʿAlī b. Zayd. Maʿārij nahj al-balāgha. Qom: Kitābkhāna-yi Āyat Allāh al-Marʿashī, 1409 AH.
  • Ibn Abī l-Ḥātam, ʿAbd al-Raḥmān b. Muḥammad. Tafsīr al-Qurʾān al-ʿaẓīm. Edited by Asʿad Muḥammad al-Ṭayyib. 3rd edition. Riyadh: Maktabat Nazār Muṣṭafā al-Bāz, 1419 AH.
  • Ibn Abī l-Ḥadīd, ʿAbd al-Ḥamīd b. Hibat Allāh. Sharḥ Nahj al-balāgha. Qom: Maktabat Āyat Allāh al-Marʿashī, 1404 AH.
  • Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Abī l-Karam. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār Ṣādir, 1385 AH-1965.
  • Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Murūj al-dhahab wa maʿadin al-jawhar. Edited by Asʿad Dāghir. Qom: Dār al-Hijra, 1409 AH.
  • Sayyid Raḍī, Muḥammad Ḥusayn. Nahj al-balāgha. Edited by Ṣubḥī Ṣaliḥ. Qom: Nashr-i Hijrat, 1414 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-umam wa l-mulūk. 2nd edition. Beirut: Dār al-Turāth, 1967.
  • Ṭurayḥī, Fakhr al-Dīn b. Muḥammad al-. Majmaʿ al-baḥrayn. Edited by Sayyid Aḥmad Ḥusaynī. Tehran: al-Maktaba al-Murtaḍawīyya, 1375 SH.
  • Yāqūt al-Ḥamawī. Muʿjam al-buldān. 2nd edition. Beirut: Dār Ṣādir, 1995.