Chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia)

Kutoka wikishia

Chuki dhidi ya Uislamu (Kiarabu: الإسلاموفوبيا أو رُهاب الإسلام) ni kuleta hofu na chuki zilizoratibiwa kuhusiana na Uislamu na madhihirisho ya Waislamu na kuwaonyesha watu wengine kwamba, dini hii ni tishio na hatari. Chuki dhidi ya Uislamu ni kuonyesha kuwa jambo la kawaida na kujuzisha aina mbalimbali za ubaguzi, utumiaji mabavu, ukatili na kutekeleza vitendo vya kuwatenga na kuwanyima haki Waislamu na taasisi na mashirika ya Kiislamu. Chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) inachukuliwa kuwa jambo la kidini, kisiasa, kitamaduni na kijamii, ambalo licha ya kuwa na muktadha wa kihistoria, lilipata umaarufu zaidi mwishoni mwa karne ya 20, hususan baada ya mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 huko nchini Marekani.

Kwa mujibu wa watafiti, baadhi ya sababu na mazingira ya kuenea kwa chuki dhidi ya Uislamu ni pamoja na: Kutopatana (kutoafikiana) kwa kihistoria kati ya serikali za Kiislamu na Magharibi, migongano iliyopo ya maadili ya Ulaya na Kiislamu, watu wa Magharibi kutokuwa na ufahamu Wamagharibi kuhusiana na utambulisho wa Uislamu, kuongezeka kwa misingi ya Kiislamu na vitendo vya ukatili vinavyofanywa na watu wenye mielekeo ya Uislamu, kujengwa mazingira hasi na kuunda maoni yanayotangazwa na vyombo vya habari vya Magharibi ambavyo kimsingi huwa ni propaganda chafu dhidi ya Uislamu.

Ili kukabiliana na mwenendo wa uenezaji chuki dhidi ya Uislamu, kuna mikakati iliyoependekezwa ambayo ni: Kupanuliwa vyombo vya pamoja vya habari vya Kiislamu ili kuonyesha sura chanya ya ulimwengu wa Kiislamu, kuanzishwa kwa mawasiliano yenye nidhamu na mpangilio na kupanua vituo vya kidini vya Magharibi, uimarishaji ubadilishanaji wa ndani wa kiustaarabu kwa ajili ya kudhoofisha harakati na mikondo ya itikadi kali na ya kimsingi na kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu.

Katika uwanja huu, kumetolewa radiamali mbalimbali ambapo miongoni mwazo ni barua na ujumbe wa Ayatullah Khamenei kwa vijana wa Ulaya na Amerika ya Kaskazini unaowataka warejee katika vyanzo na maandiko ya Kiislamu kwa ajili ya kuijua dini ya Uislamu.

Nafasi

Hii leo suala la chuki dhidi ya Uislamu linatambuliwa kuwa mkakati muhimu kabisa wa ulimwengu wa Magharibi na Ukristo kwa minajili ya kukabiliana na ulimwengu wa Kiislamu. [1] Inasemekana kudhihiri jambo hili katika ulimwengu wa sasa kulitokana na hitilafu na migongano baina ya ulimwengu wa Kiislamu na ulimwengu wa Magharibi katika siku za hivi karibuni na za mbali. [2] Baadhi ya sababu za umuhimu wa kuchunguza jambo hili ni kama zifuatazo: Mafanikio ya kiwango fulani ya ulimwengu wa Magharibi katika kueneza mradi wa chuki dhidi ya Uislamu na, matokeo yake, kuongezeka kwa mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu na kushadidi anga na mazingira ya hali ya kutoaminiana baina ya Waislamu na Wamagharibi. [3]

Neno «Chuki dhidi ya Uislamu» (Islamophobia) licha ya kuweko mifano na vielelezo vyake katika historia ndefu ya matukio ya kisiasa na kijamii ya ulimwengu, [4] lakini ni katika islahi mpya ambayo iliibuka katika muongo wa 1980 na kuenea zaidi baada ya mashambulio ya Septemba Mosi nchini Marekani. [5] Katika duru hii wameutaja Uislamu kama ufalme wa kishetani badala ya Ukomonisti na kuuhesabu kuwa ni hatari kwa amani na usalama wa dunia. [6]

Maana

Chuki dhidi ya Uislamu (kwa Kiingereza: Islamophobia) kunaelezwa kuwa maana yake ni kueneza woga, hofu na chuki isiyo ya kimantiki kuhusu Uislamu na Waislamu. [7] Imekuja katika ripoti yenye anuani: “Chuki dhidi ya Uislamu: Changamoto Dhidi Yetu Sote”: Chuki dhidi ya Uislamu ni hofu, woga na chuki dhidi ya Uislamu ambayo hupelekea wafukuzwe katika maisha ya kiuchumi, kijamii na ya jumla katika nchi zisizo za Kiislamu na kutekelezwa ubaguzi dhidi yao. [8]

Watafiti wa masuala ya kisiasa wametambua madhumuni na lengo la chuki dhidi ya Uislamu kwamba, ulimwengu wa Uislamu na hasa Waislamu wanaoishi katika nchi za Magharibi wachukuliwe na kuonekana kuwa ni chanzo cha tishio na hatari kwa watu wengine, utamaduni na ustaarabu wa Magharibi. [9] Miongoni mwa viashiria vingine vilivyowasilishwa katika uelewa wa chuki dhidi ya Uislamu ni mambo kama vile mtazamo wa kubakia nyuma (kimaendeleo), utumiaji mabavu na ugaidi kuwa eti ni sifa ya Waislamu. [10]

Baadhi ya watafiti wamechukulia chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) kama ni mjumuiko wa mawazo na taswira ambazo zina mahusiano na watu maalumu kama vile magazeti na kanali za satelaiti ambazo zimeibua fikra hii na kuipa nguvu. [11] Kulingana na Asghar Eftekhari, mtafiti wa kisiasa ni kuwa, chuki dhidi ya Uislamu ni uundaji wa taswira mbaya na hasi ya kiakili ya Uislamu jambo linalotekelezwa na vyombo vya habari vya ulimwengu wa Magharibi ambapo kupitia hilo, mlengwa anaonyesha hisia hasi (kinadharia au kivitendo) kwa kuanzishwa na kuendelezwa mfumo wa Kiislamu. [12] Kwa maana kwamba, anakuwa na mtazamo mbaya na Uislamu kutokana na kuathirika na propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Mbinu za Kisasa cha Chuki Dhidi ya Uislamu

Katuni inayo jaribu kuonesha sura hasi ya Uislamu

Kwa mujibu wa kile kilichokuja kuhusu utafiti wa chuki dhidi ya Uislamu ni kwamba, jambo hili hudhirika katika mambo manne ya anga jumla ya jamii, makundi, vyama, vyombo vya habari na serikali kwa kutumika mbinu na mikakati mbalimbali kama utumiaji mabavu, ubaguzi, kutolewa hukumu ya kabla ya kitendo (kuunda taswira isiyo sahihi) na kufukuzwa Waislamu. [13]

  • Utumiaji mabavu: Hujuma na kushambuliwa kimwili, kubomolewa na kuharibiwa mali na vilevile mashambulio ya matusi.
  • Ubaguzi: Kubaguliwa katika haki za kiraia; kwa mfano katika maeneo ya kazi na katika utoaji wa huduma za kiafya na kielimu.
  • Kutolewa hukumu ya kabla ya kitendo: Kuhukumu kabla kunatekelezwa katika nyuga mbili za vyombo vya habari na maamiliano ya kila siku na Waislamu kama vile kuchora vibonzo na vikatuni dhidi ya Uislamu na kuvunjia heshima matukufu ya Uislamu kama Qur’an.
  • Kufukuzwa: Kuwafukuza Waislamu katika uga wa siasa, masuala ya uongozi, ajira, usimamizi na nyadhifa. [14]

Historia Fupi ya Kuenea Chuki Dhidi ya Uislamu Katika Ulimwengu wa Magharibi

Kwa mujibu wa watafiti wa masuala ya kisiasa, kuundwa kwa harakati za Kiislamu katika miaka ya 50 hadi 70 ya karne ya 20 zenye malengo ya kupinga ukoloni na wazo la kuwa na kuja na fikra ya kutaka serikali ya ulimwengu Uislamu utawale dunia) [15], pamoja na kutambulishwa Uislamu kama pingamizi muhimu zaidi dhidi ya harakati za Magharibi baada ya kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti, [16] ni mambo ambayo yalipelekea mataifa makubwa duniani kuchukua hatua za kudhoofika na kuuondoa Uislamu kwenye milingano ya madaraka, na kutumia mikakati kama vile mradi wa chuki dhidi ya Uislamu dhidi ya mkakati wa Mwito wa Kiislamu. [17]

Kadhalika imeelezwa kwamba wananadharia wa kisiasa wa Magharibi kama vile Samuel Huntington na Bernard Lewis wamejaribu kuingiza chuki dhidi ya Uislamu kwa kutumia dhana kama vile muelekeo wa Kiislamu, muelekeo wa kimsingi na muelekeo wa Kisunna. Juhudi hizi zimefaulu kutokana na kuweko ya baadhi ya masuala katika nchi za Kiislamu, kama vile shughuli za vurugu za makundi yenye itikadi na misimamo kali na ya kufurutu ada. [18]

Mazingira na Sababu

Kuenea kwa chuki dhidi ya Uislamu hususan katika nchi za Magharibi kunahesabiwa kuwa ni matokeo ya muktadha wa kihistoria na uhusiano kati ya Waislamu na nchi za Magharibi na kunaathiriwa na mambo mengi ya kiutamaduni, kijamii na kisiasa. [20]

Sababu kadhaa zimezingatiwa kuwa za ufanisi katika kuenea kwa chuki dhidi ya Uislamu; miongoni mwazo ni: Mgongano wa masilahi na thamani tofauti za ulimwengu wa Kiislamu na Magharibi, vitendo vya ukatili na utumiaji mabavu vya maikundi vya Kiislamu yenye misimamo mikali, migogoro ya kihistoria ya Israel-Waarabu, ujinga na ukosefu wa utambuzi wa Uislamu na Waislamu, hofu ya Wamagharibi juu ya tishio la kiidadi na kiutamaduni la Waislamu na kuunda na kuyapa muelekeo maoni ya umma kunakofanywa vyombo vya habari. [21]

Mazingira ya Kihistoria

Wanafikra wengi wanazirejesha sababu za woga na chuki ya Wamagharibi dhidi ya Uislamu kuwa sio kwenye matukio ya zama za zama hizi, bali kwenye hitilafu za kihistoria kati ya serikali za Kiislamu na Magharibi na migongano ya thamani za Ulaya na Kiislamu. [22] Kundi hili linaashiria mkondo wa wazi na unaoendelea wa kutopatana kama vile kudhihiri Uislamu na kukabiliana na utawala wa Roma na Ukristo, [23] kukombolewa Andalusia, vita vya msalaba katika Zama za Kati, [24] migogoro ya Dola ya ufalme wa Othmania na Wazungu na ukoloni wa mataifa ya Ulaya katika karne ya 18 na 19 katika ulimwengu wa Kiislamu. [25]

Madhaifu Ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu

Kuweko kwa nukta nyingi dhaifu katika ulimwengu wa Kiislamu ni miongoni mwa nyuga na mazingira muhimu kabisa yanayohesabiwa kuwa yamechangia kuimarishwa na kuendelezwa mradi wa chuki dhidi ya Uislamu. Mambo hayo ni kama mgawanyiko wa kimadhehebu, udhaifu wa mfungamano baina ya nchi za Kiislamu, kubaki nyuma kimaendeleo, umaskini, udshaifu wa wananchi kuwa na nafasi katika masuala ya uongozi na kutokuwa na uhalili tawala nyingi za nchi za Kiislamu, kuweko vitendo vya utumiaji mabavu wa kikabili, kikaumu, udhaifu wa haki za binadamu na kukanyagwa haki za wanawakae na vilevile udhaifu wa teknolojia ya habari katika ulimwengu wa Kiislamu ikilinganishwa na ulimwengu wa Magharibi. [26]

Kutokuwa na Ufahamu Wamagharibi Kuhusu Utambulisho wa Uislamu

Kutokuwa na ufahamu juu ya asili na utambulisho wa Uislamu na Waislamu kumetambuliwa kuwa mojawapo ya sababu muhimu zaidi za chuki dhidi ya Uislamu. [28] Kulingana na watafiti, hali hii ya kutokuwa na ufahamu ni kuwa kiasi kwamba Wamagharibi wengi wanafikiri kwamba Waislamu wote ni Waarabu. Pia, imesemwa kwamba katika imani ya watu wa Magharibi, hakuna neno linalofungamana na jina la Uislamu zaidi ya neno jihadi; Neno ambalo wanaamini ni ishara na nembo ya utumiaji mabavu na mauaji. [29]

Woga

Miongoni mwa sababu nyinginezo, za kuweko hisia hasi dhidi ya Waislamu zimerejeshwa kwenye mzizi wa hofu ya Uislamu katika nchi za Magharibi. Hofu hii imeainishwa katika makundi mawili: "woga wa kihistoria" na "woga wa kisasa". Hofu ya kihistoria au mtazamo wa kuonyesha Uislamu kuwa hatari ya kidini ni jambo ambalo lilikuwa likizungumziwa na wamishionari (mubalighina wa Kikristo) kuhusiana na zama za ushindani baina ya dini mbili za Uislamu na Ukristo katika kukomboa ardhi mbalimbali. Woga wa kisiasa au mtazamo wa kuuonyesha Uislamu kuwa ni hatari ya kisiasa na uwezekano wa kubadilika Uislamu na kuwa nguvu imara na madhubuti ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Utendaji huu kwa Uislamu ulienezwa na wanasiasa wa Magharibi. [30]

Uhajiri na Kuongezeka Idadi ya Waislamu Barani Ulaya

Kuhama na kuhajiri makundi mengi ya Waislamu kuelekea Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia kwa ajili ya kazi na ongezeko la idadi ya Waislamu katika nchi za Ulaya kumezingatiwa kuwa sababu nyingine ya kuenea chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya. [31] Imeelezwa kuwa, kuchukua muda mrefu uhajiri huu kulipelekea kuundika jamii, jamii za walio wachache za Kiislamu na kudhihirika vizazi vya pili na vya tatu vya wahajiri katika nchi za Magharibi na hatua kwa hatua Uislamu ukageuka na kuwa moja ya dini kuu barani Ulaya na katika baadhi ya nchi dini hii imekuwa dini ya pili kwa ukubwa. [32] Kwa mujibu wa watafiti hao, wahamiaji Waislamu waliohamia Ulaya baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia walikuwa na uwezo mdogo wa kuzoea utamaduni wa Ulaya na kutokana na hii hali ya kutonasibiana ikapelekea kujitokeza aina fulani ya kuhukumu kabla na kwa njia ya hasi baina ya watu wa Ulaya kuhusiana na Waislamu wote. [33] Ni kwa sababu hii, ndio maana Wamagharibi na haswa vyombo vyao vya habari vina wasiwasi kuhusu mabadiliko ya muundo wa kijamii na idadi ya watu na malengo ya kiutamaduni na hili limekuwa chimbuko la kuendesha propaganda chafu na chuki dhidi ya Uislamu. [34]

Kudhihiri Muelekeo wa Kimsingi wa Kiislamu

Kuenea kwa itikadi zinazohusiana na Uislamu wa kisiasa hususan katika sura ya kuibuka makundi yenye misimamo mikali na vitendo vyao, kumezingatiwa kuwa miongoni mwa sababu muhimu za kuenea chuki dhidi ya Uislamu ndani ulimwengu wa Kiislamu. Watafiti wanasema kuwa, kuibuka makundi ya kisalafi kama Ikhwanul-Muslimin, Jamaat al-Muslimin, makundi ya kitakfiri na ya kijihadi, Al-Qaeda, Taliban na Daesh (ISIS) [36] na kutekeleza vitendo vya kigaidi kama vile tukio la Septemba 11, [37] mauaji ya kiholela nchini Iraq na Syria na kutekelezwa operesheni za kujitoa mhanga na makundi hayo [38] kote ulimwenguni, vilisababisha kupatikana nguvu ya vyama vya mrengo wa kulia vilivyokithiri barani Ulaya. Kwa kuunganisha ukosefu wa usalama wa Ulaya na wahamiaji Waislamu, vyama hivi katika Ulaya viliweza kueneza mjadala wa chuki dhidi ya Uislamu na kupitisha sheria za kibaguzi dhidi ya Waislamu. [39]

Shughuli za Vyombo vya Habari

Kustafidi na fursa ya uwezo mbalimbali wa vyombo vya habari na ushawishi na taathira zao kubwa katika kuunda anga na kuunda maoni ya umma kumezingatiwa kuwa mojawapo ya mambo muhimu katika kuenea kwa hali ya chuki ya Uislamu; [40] kiasi kwamba, baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi vinatambua kama chanzo kikuu cha Uislamu. [41] Kwa kuzingatia msingi huu, chuki ya Uislamu inaundwa na picha na ukweli hupata maana katika muktadha wa picha hizi. [42] Kulingana na watafiti, ufahamu wa raia wa Magharibi kuhusu Uislamu unategemea na kufungamana sana vyombo vya habari na mara chache hurejelea vyanzo vya utafiti; ni kwa ajili hiyo ndio maana vyombo vya habari vina uwezo usiopingika katika kuunda fikra hasi za watu wa Magharibi na kubainisha mienendo yao kwa Uislamu na Waislamu. [43]

Mikakati ya Kukabiliana na Mpango wa Chuki Dhidi ya Uislamu

Katika kukabiliana na mradi na propaganda za chuki dhidi ya Uislamu, mazingira na sababu za kuenea kwake, watafiti na wanasiasa wa ulimwengu wa Kiislamu wametoa mapendekezo kadhaa; miongoni mwayo ni:

  • Kupanua vyombo vya pamoja vya Uislamu kwa ajili ya kuonyesha tena sura chanya ya ulimwengu wa Kiislamu.
  • Kuanzisha mawasiliano ya moja kwa moja baina ya Waislamu wanaoishi katika ulimwengu wa Magharibi kupitia taasisi na jumuiya za kiraia.
  • Kuanzisha mawasiliano yenye nidhamu na wigo mpana na vituo vya kidini vya Magharibi.
  • Kuimarisha mabadilishano ya ndani ya kiustaraabu kwa ajili ya kudhoofisha harakati zenye misimamo ya kufurutu ada.
  • Kuanzisha suhula za lazima (kiutafiti na kiutalii) kwa ajili ya kutambulisha Uislamu wa kweli. [44]
  • Kuzingatia misingi ya Uislamu katika kujiepusha na hitilafu za ndani za ulimwengu wa Kiislamu (kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu).
  • Udharura wa wananchi kuwa na nasi muhimu katika uongozi wa mataifa ya Kiislamu kwa kuimarisha utawala wenye ridhaa ya wananchi. [45]
  • Kupambana na nembo za kufurutu ada za kidini.
  • Kuanzisha mipaka baina ya watu wenye misimamo ya kufurutu ada na Waislamu wengine. [46]

Radiamali ya Kuenea Chuki Dhidi ya Uislamu

Katika kujibu na kutoa radiamali ya kuenea na kuchukua wigo mpana chuki dhidi ya Uislamu katika ulimwengu wa Magharibi kuna hatua zilizochukuliwa na viongozi na wanafikra wa ulimwengu wa Kiislamu ambapo miongoni mwa hatua hizo ni bartua ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka 2014 akiwahutubu vijana wa Ulaya na Amerika ya Kaskazini. Baada ya kutokea tukio la kigaidi nchini Ufaransa lililofanywa na makundi ya Kiislamu yenye kufurutu ada, Ayatullah Khamenei aliandika barua akiwahutubu vijana wa Ulaya na Amerika ya Kaskazini ambapo ndani ya barua yake hiyo aliwataka vijana hao kuutambua na kuufahamu Uislamu kupitia maandiko na vyanzo vyake vikuu na vya asili yaani Qur’an na maisha ya Bwana Mtume (s.a.w.w) badala ya kutegemea vyombo vya habari. [47]