Nenda kwa yaliyomo

Bilal Muslim Mission

Kutoka wikishia

Bilal Muslim Mission (Kiarabu: بلال مسلم ميشن) ni taasisi ya kitablighi, kielimu na mambo ya kheri. Bilal Muslim Mission ni katika asasi zenye mfungamano na Jumuiya ya Khoja Shia Ith’naasharia. Taasisi hii iliasisiwa 1968 na Allama Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, mmoja wa viongozi wa Kishia nchini Tanzania na inaendesha shughuli zake pia katika mataifa mengine kama Kenya, Madagascar, Burundi, Marekani na Canada.

Miongoni mwa shughuli muhimu za Taasisi ya Bilal Muslim Mission ni: Kuwatuma mubalighina katika miji na vijiji, kutoa huduma za umma kama vile misaada kwa masikini Waislamu na Wakristo, kuchapisha na kusambaza vitabu na majarida kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza na vilevile kutoa mafunzo ya Kiislamu na Kishia kwa wanafunzi wa Kishia. Sayyid Muhsin Hakim, Sayyid Abul-Qassim Khui na Sayyid Ali Sistani ni miongoni mwa Marajii wa Kishia ambao wameafiki kutolewa fungu (hisa) la Khumsi la Imamu kwa taasisi hii.

Kuasisiwa na kupanua shughuli zake

Sayyid Saeed Akhtar Rizvi

Taasisi ya Bilal Muslim Mission ikiwa asasi ya masuala ya misaada na kheri, ilisajiliwa mwaka 1968 nchini Tanzania. [1] Sayyid Saeed Akhtar Rizvi mwaka 1964 aliwasilisha mpango wa kitablighi katika Baraza Kuu la Shirikisho la Khoja Ith’naasharia Afrika. Hata kama mpango huu haukukubaliwa na shirikisho hilo, lakini Jumuiya ya Khoja Ith’naasharia Dar es Salaam ililifanya hilo kuwa katika ajenda ya sera zake za kitablighi na kuanzisha Taasisi ya Bilal Muslim Mission. [2]

Makao makuu ya Bilal Muslim Mission yapo jijini Dar es Salaam Tanzania [3] na asasi hii inaendesha shughuli zake katika aghalabu ya miji ya Tanzania. Mbali na Tanzania, Bilal Muslim Mission inaendesha shuhuli zake pia katika nchi za Kenya, Madagascar, Burundi, Trinidad na Tobago, Guyana na Marekani. [4] Inaelezwa kuwa, tawi muhimu zaidi la Bilal Muslim Mission baada ya Dar es Salaam Tanzania linapatikana nchini Kenya. [5] Kuanzia 1992, tawi la Bilal Muslim Mission lilianza shughuli zake nchini Marekani na harakati za kitablighi na ufikishaji ujumbe wa Uislamu zikashika kasi nchini Marekani na Canada. [6] Nchi za Guyana na Trinidad na Tobago zilikuwa chini ya harakati za Bilal Muslim ya Tanzania kabla ya taasisi hiyo kuanzisha tawi lake nchini Marekani. Baada ya Bilal Muslim Mission kuasisiwa nchini Marekani, nchi hizo zikawa chini ya asasi hiyo nchini Marekani. [7]

Shughuli

Taasisi ya Bilal Muslim Mission, inaendesha shughuli na harakati mbalimbali kama vile kuchapisha na kusambaza vitabu na majarida ya Kiislamu na Kishia, kutoa mafunzo ya Kiislamu na Kishia, kuwatuma mubalighina katika maeneo mbalimbali ya miji na vijiji na vilevile kutoa huduma za umma:

  • Kutumwa mubalighina katika miji na vijiji mbalimbali katika nchi kama Tanzania, Kenya, Madagascar, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Inaelezwa kuwa, kazi ya mubalighina hao ni moja ya sababu za kuenea madhehebu ya Shia katika maeneo ya miji na vijiji katika mataifa tajwa. Mubalighina hao walikuwa na mawasiliano na wafungwa Waislamu na Wakristo katika magereza mbalimbali ya nchi tofauti na walikuwa wakiwapatia vitabu na makala mbalimbali zinazochapishwa na Bilal Muslim Mission. [8]
  • Huduma za umma: Tasisi hiyo imetoa huduma kubwa za umma kwa masikini Waislamu na Wakristo. Huduma hizo ni kama kuanzisha kambi za muda za utoaji huduma za tiba ya macho na kadhalika katika miji na vijiji, kuanzisha vituo vya afya (zahanati) mashariki na kusini mwa Afrika, kupambana na maradhi ya malaria na ukimwi (AIDS), kujenga shule, misikiti na kugawa vyakula na nguo kwa wahitaji. [9]
  • Kuchapisha na kusambaza majarida kama Sauti ya Bilal kwa lugha ya Kiswahili na Light kwa lugha ya Kiingereza: Toleo la kwanza la jarida la Light lilichapishwa 1963 likiwa na idadi ya nakala 75. Jarida la Sauti ya Bilal ambalo kwa mara ya kwanza lilichapishwa na kusambazwa na Ali Dina mmoja wa Mashia wa Kikhoja, mwaka 1967 lilikabidhiwa kwa Bilal Muslim Mission Tanzania. [10]
  • Kuchapisha na kusambaza vitabu vya Kiislamu kwa lugha za Kiingereza na Kiswahili: [11] Vitabu hivi pamoja na majarida ya Bilal Muslim Mission hutolewa bure katika shule, madrasa na vyuo vya Kiislamu na misikiti katika nchi za Marekani, Canada, Guyana, India, Pakistan, Sri Lanka, Thailand, Indonesia n.k. [12]
  • Kutoa mafunzo ya elimu za Kiislamu na Kishia kwa wanafunzi wa Kishia: Hili lilianza kufanyika kwa kutuma kundi la wanafunzi wa masomo ya dini (matalaba) kwenda kusoma masomo ya dini. Kundi hili awali lilipelekwa Najaf-Iraq na kujishughulisha na kusoma huko. Kisha baadaye kutokana na baadhi ya mibinyo iliyokuwa ikitawala katika zama za utawala wa Chama cha Baath cha Iraq, kundi hilo likapelekwa Lebanon na baadaye likajiunga na Chuo cha Kidini cha Qom (Hawza). Baadaye kundi la wanafunzi hawa lilirejea nyumbani na kuwa walimu wa kwanza wenyeji katika shule za Bilal Muslim Mission nchini Tanzania na Kenya na hivyo likajishughulisha na kufundisha masomo na taaluma mbalimbali za Kiislamu. [13] Taasisi ya Bilal mbali na kuanzisha shule za bweni katika nchi za Tanzania na Kenya, ilianzisha pia masomo ya Kiislamu kwa njia ya posta kwa ajili ya Waislamu wenye shauku na mapenzi ya kujua dini yao ambapo masomo hayo yanajumuisha historia ya Uislamu, maisha ya Maasumina, akhlaq ya Kiislamu na mafundisho mbalimbali ya madhehebu ya Shia. [14] Kozi hizi zimechukua mkondo mpana zaidi katika zama hizi za mawasiliano ya intaneti. [15]

Kujikimu kigharama

Rasul Ja’afarian anasema katika kitabu cha Atlas of Shia kwamba: Bilal Muslim Mission inajikimu kigharama kupitia katika mambo mbalimbali kama vile kuwekeza katika sekta mbalimbali. [16] Aidha kundi fulani la Marajii Taqlidi wa Kishia limeafiki kutolewa hisa ya Imam kwa ajili ya Taasisi ya Bilal Muslim Mission; miongoni mwao ni: Sayyid Muhsin Hakim, Sayyid Abul-Qassim Khui na Sayyid Ali Sistani. [17]

Rejea

Vyanzo