Nenda kwa yaliyomo

Abu Jahl

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Baba wa wajinga)

Amr bin Hishām bin Mughīra al-Makhzūmi mashuhuri kwa jina la Abu Jahl (kiarabu: أبو جهل) (aliaga dunia mwaka wa 2 Hijiria) alikuwa mmoja wa wapinzani wa Mtume (s.a.w.w) na Uislamu katika mji wa Makka . Kupanga njama za kumuua Mtume (s.a.w.w), kuwatesa na kuwatisha watu waliokuwa wakisilimu na ambao ni wageni katika Uislamu, kuwazuia watu wasisikilize Aya za Qur'an, kumtusi na kumvunjia heshima Bwana Mtume (s.a.w.w), kufanya njama za kukatwa uhusiano wa Quraishi na Bani Hashim na kuandaa mazingira ya kutokea vita vya Badr ni miongoni mwa mambo yaliyofanywa na Abu Jahl dhidi ya Uislamu na Waislamu. Wafasiri wamemzungumzia Abu Jahl takriban katika Aya 30 wakati wakitoa maelezo na tafsiri ya Aya hizo. Kwa maana kwamba, kuna Aya zisizopungua 30 ambazo zimemzungumzia adui huyu wa Mtume (s.a.w.w) na Uislamu.

Abu Jahl alikuwa na nafasi na mchango mkubwa na wa asili wa kutokea vita vya Badr na aliuawa katika vita hivyo hivyo akiwa katika jeshi la washirikina.

Nasaba, Kuniya na Lakabu

Amr bin Hisham bin Mughira au Abu Jahl kama anavyojulikana zaidi alikuwa miongoni mwa wapinzani wa Mtume na daima alikuwa akimfanyia uadui Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu. [1] Baba yake ni Hisham bin Mughira anayetokana na kabila la Bani Makhzum na maqureshi walifanya kifo chake kuwa mwanzo wa kalenda yao. [2] Mama yake ni Asma' binti Mukhriba bin al-Jandal al-Handhali kutoka kabila la Bani Tamim. [3] Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana alikuwa akifahamika pia kama Handhaliya. [4]

Kuniya ya Abu Jahl ilikuwa Abul-Hakam lakini alimuita kwa kuniya ya Abu Jahl. [5] Sababu ya kupewa jina hili imetajwa kuwa ni ujahili na ujinga aliokuwa nao pamoja na uadui wake dhidi ya Uislamu. [6] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (saww) ni kwamba, Firauni wa umma wa Kiislamu ni Abu Jahl. [7] Kwa mujibu wa ripoti ya Waqidi katika kitabu cha Maghazi ni kuwa, kabla ya kuanza vita vya Badr, baada ya kuswali Swala ya Suna aliwalaani namna hii makafiri akiwemo Abu Jahl: (أَللّهُمَّ لَايُفْلِتَنَّ فِرْعَوْنُ هذِهِ الاُمَّةِ أَبُوجَهْلُ بْنُ هِشَامٍ ; Ewe Mola! Nakuomba Firauni wa umma huu, Abu Jahl bin Hisham asifanikiwe kukimbia). Haukupita muda, Abuu Jahl akauawa na jeshi la Waislamu. [8]

Ikrima bin Abi Jahl, mtoto wa Abu Jahl ambaye alikuwa akimfanyia uadui Mtume (saww), baada ya kukombolewa Makka aliachana na ukafiri na kusilimu. [9]

Upinzani Dhidi ya Uislamu

Abu Jahl alikuwa akimfanyia uadui Mtume Muhammad (saww) na alikuwa akimtusi Mtume kwa mbinu na njia mbalimbali [10] na akimvunjia heshima. [11] Kadhalika sababu ya kushuka baadhi ya Aya zimetambuliwa kuwa ni kutokana na mwenendo wa Abu Jahl pamoja na upinzani wake dhidi ya Uislamu na Mtume wa Allah. [12] Katika Dairat al-Maarif (tabu kubwa la maarifa yaani insaiklopidia kumetajwa Aya 32 ambazo wafasiri wamezitambua kuwa, zinamhusu Abu Jahl. [13] Abu Jahl alichukua hatua na kufanya mambo mbalimbali ili kuzuia kuenea na kupata nguvu Uislamu ambapo baadhi ya hatua hizo ni:

Kuzuia Watu Wasisikilize Aya za Qur'an

Muhammad ibn Ahmad Qurtubi anasema katika tafsiri ya Aya ya: (وَ قَالَ الَّذِینَ کَفَرُواْ لَا تَسْمَعُواْ لهَذَا الْقُرْءَانِ وَ الْغَوْاْ فِیهِ لَعَلَّکمُ‌ْ تَغْلِبُون‌ ; Na walio kufuru walisema: Msiisikilize Qur'an hii, na timueni zogo, huenda mkashinda)[14] ya kwamba imenukuliwa kutoka kwa Ibn Abbas akisema kuwa, kila mara Mtume alipokuwa akisoma Qur'an, Abu Jahl alikuwa akisema, timueni zogo ili watu wasifahamu na kuelewa anachokisema. [15]

Mpangaji wa Mkakati wa Kuuawa Mtume

Kwa mujibu wa nukuu ya Abdul Malik ibn Hisham ni kwamba, washirikina wa Makka walikusanyika Dar al-Nadwa kwa ajili ya kuchukua uamuzi kuhusiana na namna ya kukabiliana na Mtume (s.a.w.w) ambapo kila mmoja alitoa pendekezo lake. Abu Jahl alitoa pendekezo lake kwa kusema: Tumuue Mtume, lakini mauaji yake yanapaswa kuyashirikisha makabila yote, ili Bani Hashim wasiweze kupigana vita na makabila yote kwa ajili ya kulipiza kisasi na hivyo kulazimika kukubali dia. Hatimaye pendekezo lake hilo lilikubaliwa na kwa msingi huo wakakubaliana kutekeleza mpango wao usiku na kila kabila litoe mtu mmoja. Abu Jahl alikuwa miongoni mwa hadhirina na alikuwa akiwashajiisha walioteuliwa kutekeleza mpango huo. Hata hivyo kuondoka Mtume na Imam Ali kulala sehemu yake, ni hatua ambayo ilipelekea kufeli mpango wao huo.[16] Abu Jahl alikuwa amefanikiwa kuwa mjumbe katika Dar al-Nadwa akiwa na umri wa miaka 30. Hii ni katika hali ambayo, katika zama hizo, wajumbe wa Dar al-Nadwa ukiacha kabila la Bani Qusay walipaswa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 40. [17]

Kuwatesa na Kuwatisha Watu Waliokuwa Wakisilimu

Abu Jahl alikuwa akiwazuia watuu kuingia katika Uislamu. [18] Ikitokea mtu amesilimu alikuwa akimtisha na kumtesa ili aachane na Uislamu. [19] Miongoni mwa watu waliokuwa wakiteswa na Abu Jahl kutokana na kusilimu kwao na kumuunga mkono Mtume (s.a.w.w) ni Bilal Habashi,[20] Yasir bin Ammar na Sumayyah bint Khabbat. Sumayyah bint Khabbat aliyekuwa mama wa Ammar bin Yasir alikufa shahidi kutokana na mateso ya Abu Jahl.[21] Kadhalika Iyash bin Abi Rabia, kaka wa mama yake Abu Jahl (mjombake) aliyekuwa amefunga safari kuelekea Madina kwa ajili ya kuungana na muhajirina alichukua hatua ya kumrejesha Makka akiwa amefika Quba na kisha akamtia jela.[22] Kwa mujibu wa nyaraka za historia, Abu Jahl alikuwa na mipango na mikakati mbalimbali dhidi ya Waislamu wapya; kama mtu akisilimu na kuingia katika Uislamu na akawa ana nafasi na cheo katika jamii alikuwa akifanya kila awezalo kumdhalilisha na kumfanya akose hadhi na itibari katika jamii. Kama mtu huyo alikuwa mfanyabiashara alikuwa akitishia kumuwekea vikwazo na kumkwamishia biashara yake na hivyo kusambaratisha mali na mtaji wake, na kama alikuwa mtu dhaifu basi Abu Jahl alikuwa akimpiga na kumuweka chini ya mashinikizo na mbinyo.[23]

Kuandaa Mazingira ya Vita vya Badr

Makala asili: Vita vya Badr

Vyanzo mbalimbali vya historia vinaonyesha kuwa, Abu Jahl alikuwa na mchango mkubwa katika kutokea vita vya Badr. Kabla ya kutokea vita hivyo, Mtume (s.a.w.w) alimlaani Abu Jahl pamoja na Zam'a ibn al-Aswad kutokaana na kung'ng’ania vita. [24] Katika mwaka wa pili Hijria, msafara wa makureshi uliokuwa ukiongozwa na Abu Sufiyan ulikabiliwa na vitisho kutoka kwa Waislamu. Abu Sufiyan akaomba msaada kutoka kwa makureshi. Abu Jahl alifunga safari akiwa na jeshi na kutoka Makka kwa ajili ya kwenda kutoa msaada. Pamoja na kuwa, msafara ule ulipita salama salmini, lakini Abu Jahl aling'ang'ani kulipeleka jeshi la Makka katika visima vya Badr [25] na hapo vikatokea vita baina yao na jeshi la Waislamu. Jeshi la Makka likashindwa na Waislamu na Abu Jahl pamoja na idadi kadhaa ya viongozi wa Kureshi waliuawa. [26] Abu Jahl aliuawa na Muadh bin Amr na watoto wa Afraa na Abdallah bin Mas'ud akatenganisha akatenganisha na mwili kichwa cha Abu Jahl.[27]

Rejea

  1. Tazama Ibn Ishaq, Sira Ibn Ishaq, Shule ya Masomo ya Al-Tarikh na Al-Maarif al-Islamiyya, uk 145.
  2. Ibn Habib al-Baghdadi, al-Muhabbar, Dar al-Faq al-Jadidah, uk 139.
  3. Ibn Hisham, Al-Sirah Al-Nabiwiyah, Dar al-Marifah, Juz.1, uk. 623.
  4. Angalia katika Balazri, Ansab al-Ashraf, 1959, juzuu ya 1, uk. 291.
  5. Balazri, Ansab al-Ashraf, 1959, juzuu ya 1, uk. 125.
  6. Ibn Darid, Al-Ishtaqaq, 1411 AH, uk.148.
  7. Ibn Ishaq, Sira Ibn Ishaq, Shule ya Masomo ya Al-Tarikh na Al-Maarif al-Islamiyya, uk 210.
  8. Waghadi, Maghazi, Juz. 1, uk. 46.
  9. Ibn Jozi, al-Muntazem, 1412 AH, juzuu ya 4, uk. 155-156.
  10. Ibn Hisham, Al-Sirah al-Nabawiyah, juzuu ya 1, uk. 291.
  11. Ibn Hisham, Al-Sirah al-Nabawiyyah, juzuu ya 1, uk. 298-98.
  12. Kwa mfano, angalia Vahidi, Asab Nazul Al-Qur'an, 1411 AH, uk.487 Tabari, Jame al-Bayan, juzuu ya 22, uk. 99.
  13. Kutangaza Kurani kutoka kwenye Encyclopedia of the Holy Quran, 1385, Juz. 1, uk. 381-391.
  14. Surah Fusilat, aya ya 26.
  15. Qurtubi, Tafsir al-Qurtubi, 1405 AH, juzuu ya 15, uk. 356.
  16. Ibn Hisham, Al-Sirah al-Nabawiyyah, Dar al-Marifah, juzuu ya 1, uk. 482-483.
  17. Ibn Darid, Al-Ishtaqaq, 1411 AH, uk. 155.
  18. Ibn Hisham, Al-Sirah al-Nabawiyyah, Dar al-Marifah, juzuu ya 1, uk. 320.
  19. Ibn Hisham, Al-Sirah al-Nabawiyyah, Dar al-Marifah, juzuu ya 1, uk. 320.
  20. Ibn Athir, Asdal Ghabah, 1409 AH, Juz. 1, uk. 243.
  21. Ibn Abd al-Barr, al-Estiyab, 1412 AH, juz.4, 1865.
  22. Ibn Saad, Tabaqat al-Kubari, 1410 AH, juzuu ya 4, uk. 96.
  23. Wasifu wa Ibn Hisham, juz. 1, uk. 279
  24. Waqadi, Al-Maghazi, 1409 AH, juzuu ya 1, uk.46.
  25. Waqidi, al-Maghazi, 1409 AH, juz. 1, uk. 37.
  26. Waqidi, Al-Maghazi, 1409 AH, Juz. 1, uk. 91-89.
  27. Waqadi, Al-Maghazi, 1409 AH, juz. 1, uk. 91.

Vyanzo

  • Ibn Athir, Ali bin Muhammad, Asad al-Ghaba fi Marafah al-Sahaba, Beirut, Dar al-Fikr, 1409 AH/1989 AD.
  • Ibn Ishaq, Muhammad bin Ishaq, wasifu wa Ibn Ishaq, Shule ya Al-Tarikh na Al-Ma'arif al-Islamiyya, Bita.
  • Ibn Jozi, Abd al-Rahman bin Ali, al-Muntazem, mtafiti: Atta, Muhammad Abd al-Qader, Atta, Mostafa Abd al-Qader, Beirut, Dar al-Kitab al-Alamiya, chapa ya kwanza, 1412 AH.
  • Ibn Habib al-Baghdadi, Muhammad bin Habib, Al-Mohbar, Al-Za Lichten Shattir utafiti, Beirut, Dar al-Afaq al-Jadidah, Beta.
  • Ibn Habib, Muhammad, Al-Mohbar, kwa juhudi za Ilze Lishten Shtner, Hyderabad Deccan, 1361 AH/1942 AD.
  • Ibn Darid, Muhammad bin Hasan, Al-Ishtaqaq, utafiti na maelezo: Abdus Salam Muhammad Haroun, Beirut, Dar Al-Jail, 1411 AH/1991 AD.
  • Ibn Saad, Muhammad Ibn Saad, Tabaqat al-Kabri, Utafiti wa Muhammad Abdul Qadir Atta, Beirut, Dar al-Kutb al-Alamiya, 1410 AH/1990 AD.
  • Ibn Abd al-Barr, Yusuf bin Abdallah, Al-Istiyab fi Marafah al-Ashab, Utafiti wa Ali Muhammad Al-Bajawi, Beirut, Dar al-Marafah, 1412 AH/1992 AD.
  • Ibn Hisham, Abd al-Malik bin Hisham, Al-Sirah al-Nabawiyah, cha Mustafa Saqqah na wengineo, Cairo, 1375 AH/1955 AD.
  • Balazari, Ahmed bin Yahya, Ansab al-Ashraf, cha Muhammad Hamidullah, Cairo, 1959.
  • Tabari, Muhammad bin Jarir, Jame al-Bayan fi Tafsir al-Qur'an, Daral al-Marafe, Beirut, 1412 AH.
  • Qurtubi, Muhammad bin Ahmad, Tafsir al-Qurtubi, Utafiti wa Muhammad Mohammad Hassanin, Beirut, Dar Ihya Al-Trath al-Arabi, 1405/1985.
  • Kituo cha Utamaduni na Elimu cha Qur'ani, Tangazo la Kurani kutoka kwa Ensaiklopidia ya Qur'ani Tukufu, Qom, Bostan Kitab, 1385.
  • Vahedi, Ali Ibn Ahmad, Kitabu cha Wahyi wa Qur'ani, kilichotafitiwa na Kamal Basiuni Zaalul, Beirut, Dar al-Kitab al-Alamiya, 1411 AH.
  • Waqidi, Muhammad bin Omar, Al-Maghazi, utafiti wa Marsden Jones, Beirut, chapa ya tatu, 1409 AH/1989 AD.