Aya ya Da'wa
Aya ya Da'wa (Kiarabu: آیة الدعوة) (Surat al-Nahl: Aya ya 125) inafundisha njia za da'wa (kuwalingania watu) na kuwaita upande wa Mwenyezi Mungu na Mtume (s.a.w.w). Kwa msingi huo, Mwenyezi Mungu anamuamrisha Mtume wake atumie mbinu na njia tatu za hekima, mawaidha mema na kujadiliana kwa njia iliyo bora zaidi (mdahalo) kwa ajili ya kuitangaza dini ya Uislamu.
Wafasiri wa Qur'an wanasema, makusudio ya hekima katika Aya hii ni hoja na elimu ambayo inaondoa shaka katika nyoyo za watu na kuziamsha akili zilizolala. Kwa mujibu wao ni kuwa, mawaidha mazuri ambayo yamesisitizwa katika Aya hiyo ni njia na mbinu ya pili na ambayo inahusu hisia za wanadamu na kuwahimiza watu kuacha ubaya na kufanya mambo mema. Wanazingatia kujadiliana kwa namna iliyo bora kwamba, ni kwa ajili ya wale ambao akili zao zimejaa masuala ya uongo na akili zao zinapaswa kusafishwa kwa njia ya mjadala ili wawe tayari kuukubali ukweli. Katika njia hii, kwa kutumia misingi inayokubaliwa na mtu husika humshawishi na kumkinaisha kwa hoja.
Kwa mujibu wa wafasiri wa Aya ya Da'wa ni kwamba, wajibu wa Mtume (s.a.w.w) umewekewa mipaka kwenye ulianganiaji unaotokana na njia tatu zilizotajwa na ameuacha kwenye elimu ya Mwenyezi Mungu suala la ambaye atakubali na kuongoka na atakayekufuru na kupotea.
Nukta Jumla
Aya ya Da'wa, pamoja na aya chache za mwisho za Surat al-Nahl, ni mkusanyiko wa maagizo ya kimaadili ambayo yanahusu jinsi ya kukabiliana na wapinzani. [1] Makarim Shirazi ameyatambua maagizo haya kuwa ni msingi wa mbinu na mtindo wa mapambano ya Uislamu mkabala na wapinzani na anaamini kwamba, inaweza kutumika kila sehemu na katika kila zama. Anasema, katika majimui ya maagizo haya, kumeashiriwa mambo kama ya namna ya kulingania dini, adhabu, msamaha na kusimama kidete mkabala wa njama mbalimbali. [2]
Katika Aya ya 125 ya Surat al-Nahl, Mwenyezi Mungu anamfundisha Mtume wake njia za mazungumzo ya kimantiki na yenye kutengeneza [3] na anamtaka atumie hekima, mawaidha mema na kujadiliana kwa namna iliyo bora kuwaita watu katika njia ya Mwenyezi Mungu. [4] Allama Tabatabai’ anazichukulia njia hizi tatu kuwa ni maalumu kwa ajili ya kuzungumza na anamchukulia Mtume (s.a.w.w) kuwa ndiye mwenye jukumu la kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kupitia njia hizi tatu. [5] Sadeghi Tehrani pia anaamini kwamba, njia hizi tatu ndizo nguzo za mazungumzo na watu ambapo hutimika kujadiliana na watu wenye kiburi, ukaidi na wasioambilika, na kwa watu wenye asili salama na safi, hekima na mawaidha ndivyo vinavyohitajika. [6]
Kwa mujibu wa Muhammad Jawad Mughniyeh, sababu ya kwa nini njia hizi tatu za kulingania ukweli zimetajwa katika Aya hii ni kwamba kuhubiri dini na kumlingania mtu kuelekea kwa Mwenyezi Mungu kunapaswa kuwa mbali na shaka yoyote, na mlinganiaji hapaswi kulingania kwa Mungu kwa ajili ya kuimarisha cheo chake miongoni mwa watu. [7]
Wafasiri wameichukulia sehemu iliyo mwisho wa Aya kuwa ni dalili ya kuwa wajibu wa Mtume (s.a.w.w) kufikisha ujumbe tu; lakini Mwenyezi Mungu pekee ndiye anayejua ni nani aliyeongoka au anayeshika njia ya ukafiri na kufuru. [8]
Andiko la Aya na Tarjumi Yake
«ادْعُ إِلَى سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ»
Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.
(Surat al-Nahl: Aya: 125)
Mbinu Tatu za Kulingania Kuelekea Mungu
Katika Aya ya 125 ya Surat al-Nahl kumetajwa mbinu tatu za kulingania kuelekea Mungu yaani hekima, mawaidha mema na kujadiliana kwa namna iliyo bora. [9] Murtadha Mutahhari mwanafikra na msomi wa Kishia anasema kuhusu sababu ya kutengwa kuwalingania watu kwenye njia tatu kwamba, baadhi ya watu ni wenye hekima, akili na fikra, na wanapaswa kufikiwa kwa njia ya hekima, akili na hoja zenye nguvu. Watu wengine ni wajinga na walioghafilika na wanahitaji kuhubiriwa. Baadhi ya watu huishi kwa ukaidi na kutokuambilika, ambao unapaswa kujadiliwa nao kwa mdahalo, lakini bila shaka ni majadiliano mazuri. [10] Allama Tabatabai anazingatia njia hizi tatu kuwa sawa na maneno matatu maarufu ya hoja, hotuba na majadiliano katika elimu ya mantiki. [11]
Hekima
Sheikh Tabarsi ameitambua hekima katika Aya ya Da'wa kuwa ni Qur'ani. [12] Kwa mujibu wa Allama Tabatabai, hekima hapo ndio ile hoja ya kimantiki, isiyoacha shaka au utata kwa hadhira. [13] Baadhi ya wafasiri pia wanaifasiri hekima kuwa ni sayansi na wanajua kwamba ujuzi utazuia ufisadi na upotovu, utaamsha akili zilizolala na kutenganisha mema na mabaya. [14]
Mawaidha
Mbinu ya pili ya kulingania kwa Mungu, kwa kuzingatia Aya ya da'wa, ni kutumia mawaidha ambayo yanahusu hisia za watu [15] na kutoa upole, ulaini na wema kwa nafsi na roho ya mwanadamu. [16] Mawaidha yanawashajiisha watu kuacha mambo mabaya na machafu na badala yake kufanya mambo ya kupendeza; kwa namna ambayo ubaya unachukiza machoni mwao na matendo mema yanawafurahisha. Kulingana na Tabarsi, muwaidhi mwenye kauli na maneno mazuri hulainisha mioyo ya watu na kupanda mbegu za unyenyekevu mioyoni mwao. [17] Muhammad Mughniye pia anasema kuhusu mawaidha mema kwamba, katika mbinu hii mtu anapaswa kuepuka kauli za lawama na badala yake azungumze na mkosaji kwa njia isiyo ya moja kwa moja, na mhusika bila kujua ajisikie mwenye dhambi. [18] Kulingana na Makarem Shirazi, mawaidha huwa ni yenye kufaa pale yanapokuwa hayana utumiaji mabavu, kujiona mbora mhusika na kumdunisha na kumdhalilisha yule anayempa mawaidha na kuchochea hisia yake ya ukaidi na kutoambilika na ikiwa masharti haya hayatatimizwa, uwezekano wa kuwa na matokeo tofauti ni mkubwa sana. [19]
Majadiliano Yaliyo Bora
Njia na mbinu ya tatu ya kuwalingania watu juu ya Mwenyezi Mungu kulingana na Aya ya da'wa, ni hoja au mjadala bora zaidi. Njia hii imechukuliwa kuwa maalumu kwa wale ambao akili zao zimejaa masuala yasiyofaa na akili zao zinapaswa kusafishwa kwa njia ya mjadala ili wawe tayari kukubali haki na ukweli. Pia wamesema kuhusu njia hii kuwa isiwe na matusi, kufedhehesha na migongano ili kuacha athari zake kwa hadhira. [20] Allama Tabatabai, akinukuu riwaya kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s.) amesema kwamba maana ya mjadala ulio bora ni majadiliano kwa mujibu wa Sunna ya Qur'ani, ambapo ndani yake adabu ya Mungu imewekwa kuwa kiigizo na dira. [21] Kwa mujibu wake, majadiliano ni hoja na uthibitisho ambao husadikisha upande mwingine kulingana na misingi ambayo yeye mwenyewe anaikubali. [22]