Al-Istisqaa

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Al-Istisqa’)

Al-Istisqa (Kiarabu: الاستسقاء) ni sunna na ada ya kidini ambayo ndani yake hufanyika ibada ya kumuomba Mwenyezi Mungu (swt) mvua. Katika hadithi imeelezwa na kubainisha kwamba, wakati wa ukame yafanyike maombi ya kuomba mvua ambapo ndani yake kumebainishwa Swala na dua ya kuomba mvua. Kadhalika historia na hadithi mbalimbali zinaonyesha kuwa, Mtume (s.a.w.w) na Maimamu watoharifu (a.s) walifanya jambo hilo.

Katika vitabu vya dini, kumebainisha hukumu na adabu za kuomba mvua. Miongoni mwazo ni pale ilipoelezwa kwamba, ni mustahabu kuswali Swala ya kuomba mvua wakati kunapotokea janga la ukame. Ni bora kabla ya kuswali Swala hii, watu wafunge Saumu kwa muda wa siku tatu, na katika siku ya tatu wakazi wa mji watoke na kuelekea jangwani na baada ya kuswali Swala ya kuomba mvua kwa jamaa wamuombe mvua Mwenyezi Mungu (swt) hali ya kuwa wananyenyekea na kulia.

Miongoni mwa Swala mashuhuri ya kuomba mvua ni ile iliyoswaliwa na Imam Ali bin Mussa al-Ridha (a.s) ambapo Sheikh Saduq ameelezea hilo katika kitabu chake cha Uyun Akhbar al-Ridha na amesema kwamba, baada ya Swala hiyo mvua kubwa ilinyesha. Swala nyingine ni ile ya Sayyid Muhammad Taqi Khansari mmoja wa Marajii Taqlidi wa Qom, Iran. Inasimuliwa kwamba, baada ya ukame uliotokea mwaka 1323 Hijiria Shamsia katika mji huo, Marjaa huyo aliswali Swala ya kuomba mvua baada ya kuombwa na wananchi wa Qom ambapo baada ya Swala hiyo kulitokea mvua kubwa.

Maana ya kifiq’h na historia yake

Istisqa’ kilugha ina maana ya kuomba maji. Ama katika istilahi ya fiq’h, neno hili lina maana ya kuomba mvua kwa Mwenyezi Mungu baada ya ukata wa maji na ukame. [1] Katika vitabu vya hadithi [2] na fiq’h [3] kuna mlango unaojulikana kwa jina la Swala ya Mvua (Swalat al-Istisqa’) ambapo ndani yake kumezungumziwa na kubainishwa masharti ya kuomba mvua.

Historia ya kuomba mvua

Kumuomba Mwenyezi Mungu mvua ni jambo ambalo lilikuweko hata kabla ya kuja Uislamu. Kwa mfano kwa mujibu wa mwanahistoria Ibn Shahrashub ni kwamba, kuna wakati kulijitokeza ukata wa maji ambapo Abu Twalib akiwa pamoja na vijana na mabarobaro wa familia ya Abd al-Muttalib alielekea katika msikiti wa Makka (Masjid al-Haram) kwa ajili ya kuomba mvua. Inaelezwa kuwa, baada ya mvua kunyesha kufuatia maombi yao, alisoma mashairi yaliyotungwa kumuunga mkono Mtume (s.a.w.w). [4]

Baadhi ya hadithi za kuomba mvua

Katika vyanzo na vitabu vya hadithi kuna hadithi zinazoelezea kuomba mvua Mtume (saww) na Maimamu (a.s) ambazo zimenukuliwa zikieleza maagizo yao ya kuomba mvua kutoka kwa Mwenyezi Mungu baada ya kuibuka uhaba wa maji, kuswali Swala ya kuomba mvua, dua za kuomba wakati wa kuomba mvua pamoja na masharti mengine. Kwa mfano inaelezwa kuwa, kundi la watu lilimuendea Bwana Mtume na kumshtakia kuhusiana na uhaba na ukata wa maji. [5] Mtume alipanda katika mimbari na kumuomba Mwenyezi Mungu mvua. [6] Aidha imekuja katika hadithi ya kwamba Mtume (s.a.w.w),[7] Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) [8] na Imam Ali bin Mussa al-Ridha (a.s) [9] walifanya maombi mvua.

Kuna dua pia ambazo zimenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume na Maimamu za kusoma wakati wa kuomba mvua. [10] Dua ya 19 katika kitabu cha al-Sahifat al-Sajjadiyya inahusiana na kuomba mvua. [11]

Swala ya Istisqa’ na namna ya kuomba mvua

Katika shughuli ya kuomba mvua, huswaliwa Swala ambayo inatambulika kwa jina la Swala ya kuomba mvua. Fat'wa ya mafakihi inasema kuwa, ni mustahabu kuswali Swala hii wakati kunapojitokeza na uhaba wa maji [12] na inaswaliwa kwa jamaa. [13] Swala ya Istisqa’ ina rakaa mbili, takbira na kunuti yake ni kama ya Swala za idi mbili (Eidul-Fitr na Eidul-al-Adh’ha). Tofauti yake ni kuwa, katika kunuti ya Swala hii badala ya kusoma kunuti ya Swala za idi mbili, husomwa dua ya kuomba rehema na mvua. [14]

Baada ya kumaliza Swala, Imam wa Swala hii hugeuza joho lake nyumba mbele na kuliweka mabegani na kupanda mimbari. Kisha huelekea kibla na kupiga takbira 100 kwa sauti kubwa. Halafu huwageukia watu walioko upande wake wa kulia na kutamka Subhanallah mara 100 na kisha kuwageukia walioko katika upande wake wa kushoto na kutamka mara 100 La Hawla wala Quwwata Illa Billah. Baada ya hapo huwatazama watu na kusema Alhamdulilahi mara 100. Kisha baada ya hapo hunyanyua mikono yake juu na kumuomba mvua Mwenyezi Mungu na watu humfuata katika dua hiyo. Kisha baada ya hapo husoma hotuba na kuonyesha unyenyekevu wa hali ya juu. [15]

Hukumu nyingine

Baadhi ya hukumu nyingine ambazo ni katika mambo ya mustahabu ya Swala hii na adabu nyingine za kuomba mvua ambazo ni mustahabu ni hizi zifuatazo:

  • Watu wanafunga Saumu siku tatu kabla, na siku ya tatu wanatoka katika majumba yao na kwenda jangwani. [16]
  • Ni bora iwe siku ya Jumatatu na kama haikuwezekana basi Ijumaa. [17]
  • Ni vyema Swala hii isifanyike katika misikiti. [18]
  • Katika Swala hii, husemwa “al-Swalah al-Swalah” badala ya adhana na iqama. [19]
  • Ni mustahabu kuwachukua wazee na watoto wadogo kwa ajili ya Swala hii [20] na kuwatenganisha watoto na mama zao. [21] Sahib al-Jawahir anasema, kufanya hivi ni kwa ajili ya kuleta mazingira ya kulia na kutaka rehma za Mwenyezi Mungu. [22]

Matukio mashuhuri ya kuomba mvua

Sheikh al-Saduq, amesimulia kwa mapana na marefu katika kitabu chake cha Uyun Akhar al-Ridha tukio la Imam Ridha (a.s) kuomba mvua. Kwa mujibu wa nukuu yake ni kwamba, tukio hili lilifanyika katika mwaka mmoja uliokuwa na ukame na ilikuwa ni baada ya Maamun khalifa wa utawala wa Bani Abbasi kutoa ombi la hilo na mvua ilinyesha kwa wingi baada ya Imam Ridha (a.s) kuomba mvua. [23]

Aidha imeripotiwa kuwa, katika ukame wa mwaka 1900 huko Zanzibar (sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania), Sayyid Abdul-Hussein Mar’ashi (aliaga 1905 Miladia) mmoja wa wanazuoni wa Kishia aliyekuwa akiishi katika visiwa hivyo, aliwataka Mashia wajitokeze baada ya Swala ya alfajiri kwa ajili ya Swala ya kuomba mvua. Baada ya kukamilika Swala hiyo, mvua ilianza kunyesha. [24]

Uombaji mvua uliofanywa na Sayyid Muhammad Taqi Khansari, mmoja wa Marajii wa mji wa Qom, Iran nao pia ni tukio mashuhuri na limenukuliwa katika vitabu. Inaelezwa kuwa, mwaka 1323 Hijria Shamsia mvua haikunyesha katika mji wa Qom na mji huo ukawa umekabiliwa na hatari kubwa ya kukumbwa na janga la ukame. Mwanazuoni huyo alitoka siku mbili mtawalia nje ya Qom na kuswali Swala ya kuomba mvua. Katika siku ya pili ilinyesha mvua kali. [25].

Rejea

Vyanzo

  • ʿAbd al-Raḥmān, Maḥmūd. Muʿjam al-muṣṭalaḥāt wa l-alfāz al-fiqhīyya. Cairo: Dār al-Faḍīla, [n.d].
  • Abū Jayb, Saʿdī. Al-Qāmūs al-fiqhī lughāt-an wa Iṣṭilāḥ-an. Second edition. Damascus: Dār al-Fikr, 1408 AH.
  • Ḥillī, al-Ḥasan b. Yūsuf al-. Taḥrīr al-aḥkām al-sharʿiyya ʿalā madhhab al-imāmiyya. Edited by Ibrāhīm Bahādurī. Qom: Muʾassisat Imām al-Ṣādiq, 1420 AH.
  • Ḥillī, Jaʿfar b. al-Ḥasan al-. Sharāʾiʿ al-Islām fī masāʾil al-ḥalāl wa l-ḥarām. Edited by Muḥammad ʿAlī Baqqāl. Second edition. Qom: Muʾassisa-yi Ismāʿīlīyān, 1408 AH.
  • Ḥurr al-ʿĀmilī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Wasāʾil al-Shīʿa. First edition. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1409 AH.
  • Ibn Shahrāshūb, Muḥammad b. ʿAlī. Manāqib Āl Abī Ṭālib. Edited by Ḥāshim Rasūlī. Qom: Nashr-i ʿAllāma, 1379 Sh.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Second edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Najafī, Muḥammad al-Ḥasan al-. Jawāhir al-kalām fī sharḥ sharāʾiʿ al-Islām. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1404 AH.
  • Rughanī, Zahrā. Shīʿayān-i Khuja dar Āʾīna-yi Tārīkh. First edition. Tehran: Pazhūhishgāh-i ʿUlūm wa Muṭāliʿāt-i Farhangī, 1387 sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Muqniʿ fī al-fiqh. Qom: Muʾassisa al-Imām al-Hādī, 1415 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. ʿUyūn akhbār al-Riḍā. Edited by Mahdī Lājiwardī. Tehran: Nashr-i Jahān, 1378 AH.
  • Sharīf Rāzī, Muḥammad. Ganjīna-yi dānishmandān. Tehran: 1352-1354 Sh.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Tahdhīb al-aḥkām. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.