Al-Bakka’un

Kutoka wikishia

Bakka’un / bakka’in (Kiarabu: البكّاؤون) au wenye kulia sana ni watu saba miongoni mwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w) ambao waliondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu hii kwa sababu ya kulia sana kutokana na kushindwa kwao kushiriki katika vita vya Tabuk. Kwa mujibu wa nukuu ya wafasiri wa Qur’an ni kwamba, sababu ya kushuka Aya ya 92 ya Surat Tawba ni kwa sababu ya kulia sana watu hawa. Kadhalika kwa mujibu wa hadithi zingine, Nabii Adam (a.s), Nabii Ya’qub (a.s), Nabii Yusuf (a.s), Bibi Fatma Zahra (a.s) na Imam Zainul-Abidin (a.s) wametambuliwa kuwa miongoni mwa Bakka’un (waliaji sana).

Masahaba saba

Wenye kulia sana au waliaji sana walikuwa ni watu saba kutoka katika masahaba wa Mtume (s.a.w.w) ambao walikuja kwa Mtume kutokana na uhaba wa fedha na kuomba msaada wa kipando ili waweze kushiriki katika vita vya Tabuk. Mtume akawaambia kwamba hakuwa na msaada wa kipando cha kuwapeleka vitani. Hawakuweza kushiriki katika vita hivyo walilia sana na kutaka kurejea, basi baadhi ya maswahaba wakawapa kipando na kuwapeleka vitani. [1] Katika vyanzo, watu hawa saba ambao majina yao yametajwa kwa sura tofauti, wameelezwa kuwa ni Bukka’un (waliaji sana). [2] Vita vya Tabuk vilitokea mwaka wa 9 Hijiria, [3] na katika hali ya hewa ya joto kali mno, [4] na kutoka na umasikini wa masahaba jeshi lao likafahamika kwa jina la "Jaish al-Usra" [5] Katika vita hivi, vipando na suhula za kivita ni jambo lililokuwa mikononi mwa wapiganaji. [6] Bukka’in maana yake ni waliaji sana.

((وَلاَ عَلَى الَّذِينَ إِذَا مَا أَتَوْكَ لِتَحْمِلَهُمْ قُلْتَ لاَ أَجِدُ مَا أَحْمِلُكُمْ عَلَيْهِ تَوَلَّوْا وَّأَعْيُنُهُمْ تَفِيضُ مِنَ الدَّمْعِ حَزَنًا أَلاَّ يَجِدُواْ مَا يُنفِقُونَ ; Wala wale waliokujia ili uwachukue ukasema: Sina kipando cha kukuchukueni. Tena wakarudi na macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kukosa cha kutoa)). [7] Kwa mujibu wa nukuu ya baadhi ya wafasiri Aya hiyo ilishuka kwa watu hao, [8] licha ya kuwa kuna uwezekano mwingine uliozungumziwa na kutajwa pia kuhusiana na sababu ya kushuka Aya hii. [9]

Watu wengine watano

Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) ni kuwa, waliaji sana ni watu watano: Nabii Adam (a.s) kutoka na kuondolewa peponi, Nabii Ya’qub kutokana na kutengana na Yusuf, Nabii Yusuf kutokana na kutengana na baba yake Ya’qub, Fatma Zahra (a.s) katika msiba wa baba yake Muhammad (s.a.w.w) na Imamu Zainul-Abidina (a.s) katika masaibu na misiba ya tukio la Karbala ambao inaelezwa walikuwa wakilia sana. [10]