Al-Asma’ al-Husna
- Kuna tofauti baina ya asma’ na sifat (majina na sifa)
Al-Asma’ al-Husna (Kiarabu: الأسماء الحسنى)ni istilahi ya Kiqur’ani ambayo ina maana ya majina mazuri na bora ya Mwenyezi Mungu. Neno na istilahi hii imekuja ndani ya sura nne za Qur’ani. Katika moja ya Aya zenye neno hili inaelezwa kuwa, muiteni (muombeni) Mwenyezi Mungu kwa majina haya. Maulamaa wa Kiislamu wanaamiini kwamba, makusudio ya majina mazuri ya Mwenyezi Mungu ni sifa zake ambazo zote ni nzuri.
Aidha wanasema kuwa, kwa mujibu wa Aya hii Asma’ al-Husna (majina mazuri) ni makhsusi kwa Mwenyezi Mungu. Katika baadhi ya hadithi, Ahlul-Bayt (a.s) wametambulishwa kuwa ni misdaq na mfano wa Asma’ al-Husna ambapo ili kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu ni lazima kupitia kwao.
Al-Asma’ al-Husna; Majina Mazuri ya Mwenyezi Mungu
Al-Asma’ al-Husna ni neno lililochukuliwa kutoka katika Qur'ani ambalo lina maana ya majina mazuri na bora ya Mwenyezi Mungu. [1] Neno na istilahi hii imekuja ndani ya sura nne za Qur’ani: Surat Taha Aya ya 8, Surat Hashr Aya ya 24, Surat A’raf Aya ya 180 na Surat Israa Aya ya 110. Katika Aya hizi imekuja kwamba: ‘Mwenyezi Mungu ana majuina mazuri kabisa”. [2] katika Surat al-A’raf baada ya «Mwenyezi Mungu ana amajina mazuri kabisa» Waislamu wametakiwa kumuita na kuomba Mwenyezi Muhngu kwa majina hayo. Sehemu ya Aya hiyo inasema: Basi muombeni kwa hayo. [3]
Makusudio ya Asma’ al-Husna
Wafasiri wa Qur’ani wana mitazamo tofauti kuhusiana na makusudio ya al-Asma’ al-Husna. Fadhl bin al-Hassan al-Tabarsi amesema katika tafsiri yake ya Maj’ma’ al-Bayan kwamba: Majina ya Mwenyezi Mungu yametambuliwa kuwa mazuri kutokana na kuwa, Mwenyezi Mungu ana majina ambayo yana maana nzuri; kama vile Jawad, Rahim, Razzaq, na Karim. [4] Sheikh Tusi anasema katika kitabu chake cha tafsiri ya Qur’ani cha al-Tibyan fi Tafsir al-Qur’ani: Makusudio ya majina ya Mwenyezi Mungu ni sifa zake ambazo zote ni nzuri. [5] Waandishi wa tafsiri ya Qur’ani ya Tafsir Nemooneh wao pia wameichagua na kuiafiki rai na mtazamo huu.[6]
Hata hivyo kwa mtazamo wa Allama Tabatabai, makusudio ya Asma’ al-Husna (majina mazuri kabisa) ni yale majina ambayo yana maana ya wasifu; yaani ambayo yanatoa ishara na dalili za sifa zake maalumu; kama vile Jawad, Adil na Rahim; na sio kundi la yale majina ambayo yanatoa ishara tu kuhusiana na dhati ya Mwenyezi Mungu (tujaalie hivyo kama kutakuwa na majina kama hayo); kama vile majina ya Zayd na Amru ambayo kimsingi hayaashiria sifa maalumu ya mtu. [7]
Majina Mazuri ni Makhsusi kwa Mwenyezi Mungu
Baadhi ya wafasiri wa Qur’ani wa Kishia na Kisuni wanaamini kwamba, Aya inayosema: “Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa”[8], inaashiria kwamba, majina mazuri ni makhsusi kwa Mwenyezi Mungu tu; kwani neno Mwenyezi Mungu limekuja mwanzo wa sentensi, na hii katika lugha ya Kiarabu, ni ishara ya msisitizo na maana na mafuhumu hiyo kuwa na hali ya kuhodhi na kuhusika nayo tu. Fauka ya hayo, asma’ imekuja kwa alif na laam ambapo hii ina ishara kwamba, asma’ ni jumuishi. [9] Kwa mujibu wa Allama Tabatabai maana ya Aya ni hii kwamba, kila jina zuri kabisa katika ulimwengu wa uwepo ni la Mwenyezi Mungu na hakuna mtu ambaye ni mshirika na Mwenyezi Mungu katika hilo. Hata hivyo, maneno haya hayana hayapingani na kauli kwamba, baadhi ya sifa kama elimu na rehma zinaweza kunasibishwa na asiyekuwa yeye; kwani makusudio ni kwamba, ukweli hasa wa mambo majina haya ni maalumu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.[10]
Ahlul-Bayt; Mfano wa Majina Mazuri
Katika baadhi ya hadithi, Ahlul-Bayt (a.s) wametambulishwa kuwa misdaqi na mifano ya wazi ya majina mauzri. Kwa mfano Sheikh Kulayni (Thiqat al-Islam) anasema kuhusiana na Aya ya: «Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa hayo», ananukuu hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) ya kwamba: Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, sisi ndio majina mazuri, ambapo Mwenyezi Mungu hakubali amali yoyote ile ya waja bila ya wao kuwa na utambuzi na sisi. Muhammad ibn Masoud Ayyashi (aliaga dunia 320 Hijria) mmoja wa wafasiri wa Qur’ani wa Kishia ameandika chini ya Aya hii hadithi aliyonukuu kutoka kwa Imamu Ridha (a.s) kwamba: Wakati wa kukabiliwa na shida na mambo Mungu, tuombeeni msaada na hii ndio ile:[11](وَ لِلَّهِ الْأَسْماءُ الْحُسْنى فَادْعُوهُ بِها ; Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa hayo),[12]
Kwa kuzingatia hadithi hizi, baadhi ya wahakiki wamesema kuwa, makusudio ya «basi muombeni kwa hayo», ni kufanya tawassuli «kuomba kupitia» kwa Ahlul-Bayt (a.s). [13]
Rejea
- ↑ Makarem Shirazi, Payam Qur'an, 1369, juzuu ya 4, uk. 40.
- ↑ Fakhr Razi, al-Tafsir al-Kabir, 1420 AH, juzuu ya 15, uk.412.
- ↑ Surah A'raf, aya ya 180.
- ↑ Tabarsi, Majmaal Bayan, 1372, juzuu ya 4, uk.773.
- ↑ Sheikh Tusi, al-Tabayan, Dar Ihya al-Trath al-Arabi, juzuu ya 5, uk.39-40.
- ↑ Makarem Shirazi, Tafsir al-Nashon, 1374, juzuu ya 7, uk. 23.
- ↑ Tabatabaei, Al-Mizan, 1417 AH, Juzuu ya 8, uk. 342-343.
- ↑ Surah A'raf, aya ya 180.
- ↑ Angalia katika Fakhr Razi, al-Tafsir al-Kabir, 1420 AH, juzuu ya 15, uk. 414; Tabatabaei, Al-Mizan, 1417 AH, Juz. Zaheili, al-Tafsir al-Munir, 1418 AH, juzuu ya 9, uk. 175.
- ↑ Tabatabaei, Al-Mizan, 1417 AH, Juzuu ya 8, uk. 449.
- ↑ Kelini, Kafi, 1407 AH, juzuu ya 1, uk. 143-144.
- ↑ Eyashi, Kitab al-Tafseer, 1380 AH, juzuu ya 2, uk.42.
- ↑ Angalia Dehkordi Esfahani, Lamaat katika maelezo ya sala ya Samat, 1385, uk. 28-35.
Vyanzo
- Dehkordi Esfahani, Seyyed Abulqasem, na Majid Jalali Dehkordi, Lamaat katika maelezo ya sala ya Samat, Qom, Bostan Kitab, 1385.
- Zaheili, Wahba, al-Tafsir al-Munir fi al-Aqeedah wa al-Shari'a wa al-Manhaj, Beirut, Dar al-Fakr al-Mawdani, 1418 AH.
- Sheikh Tusi, Muhammad bin Hassan, al-Tabyan fi Tafsir al-Qur'an, utafiti na Ahmed Qusayr Amili, Beirut, Dar Ihya al-Trath al-Arabi, Bita.
- Ayashi, Mohammad Bin Masoud, Kitab al-Tafsir, iliyofanyiwa utafiti na Seyyed Hashem Rasouli Mahalati, Tehran, Ilmia Printing House, 1380 AH.
- Tabatabai, Seyyed Mohammad Hossein, Al-Mizan fi Tafsir al-Qur'an, Qom, Ofisi ya Machapisho ya Kiislamu, chapa ya tano, 1417 AH.
- Tabarsi, Fazl bin Hassan, Majma al-Bayan fi Tafsir al-Qur'an, Tehran, Nasser Khosro, chapa ya tatu, 1372.
- Fakhr Razi, Muhammad bin Omar, al-Tafsir al-Kabir, Beirut, Dar Ihya Al-Tarath Al-Arabi, 1420 AH.
- Kilini, Muhammad bin Yaqub, al-Kafi, kilichohaririwa na Ali Akbar Ghafari na Muhammad Akhundi, Tehran, Darul Kitab al-Islamiya, 1407 AH.
- Makarem Shirazi, Nasser, Payam Qur'an, Qom, Shule ya Amir al-Momenin, 1369.
- Makarem Shirazi, Nasser, Tafsir al-Nashon, Tehran, Dar al-Katb al-Islamiya, 1374.
- https://lms.motahari.ir/book-page/23/آشنایی%20با%20قرآن،%20ج%206?page=207