Utawala wa Idrisiyyah
Utawala wa Idrisiyyah (utawala wa ukoo wa Idris) ilikuwa serikali ya kwanza ya Kiislamu nchini Morocco, ambayo wengine wanaiona kuwa serikali ya kwanza ya Kishia duniani. Serikali hii ilianzishwa mwishoni mwa karne ya Pili Hijria na mmoja wa wajukuu Imam Hassan Mujtaba (a.s.) aliyeitwa Idris bin Abdullah. Utawala wa Idrisiyyah ulikuwa na mamlaka juu ya Morocco na sehemu za Algeria ya sasa na uliendelea kuwepo kwa karibu karne mbili, na hatimaye, mwaka 375 H, ulifikia tamati baada ya kuuawa mtawala wa Idrisiyyah (kutoka ukoo wa Idris). Mtawala huyo aliuawa na Bani Umayya wa Andalusi. Nafasi ya Idrisiyyah katika kueneza Uislamu, kushamiri kwa ustaarabu wa Morocco, kueneza uadilifu na kuleta ustawi wa kiuchumi imezingatiwa kuwa muhimu. Katika kipindi cha Idrisiyyah Chuo Kikuu cha Qarawiyyin kilijengwa; Chuo Kikuu ambacho kinajulikana kama taasisi ya kwanza ya elimu ya juu ulimwenguni ambayo bado iko hai hadi leo. Inasemekana kuwa kutokana na kukosekana mazingira mazuri, watawala hao hawakuchukua hatua yoyote kwa ajili ya kueneza Ushia miongoni mwa watu wa Morocco. Mbinu yao ya utawala ilikuwa ya muundo wa baraza, na wakuu na wazee walikuwa na mchango na nafasi katika maamuzi ya serikali. Kwa ajili hiyo, siasa za Idrisiyyah zimechukuliwa kuwa mfumo ulio karibu zaidi na mfumo wa kisiasa wa Kiislamu. Ustahiki wao katika kusimamia mambo na kuhusishwa kwao na Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) kumewafanya wakubalike sana. Hawakutumia nguvu kupata au kuimarish madaraka. Hii leo Idrisiyyah wanajulikana kama shakhsia wakubwa na bado wanaheshimiwa na watu wa Morocco. Jouti, Meshishi, Alami na Wazani ni miongoni mwa familia zinazojulikana za Idrisiyyah.
Utawala wa Idrisiyyah
Taarifa za utawala
Majina mengine: Idrisiyyah
Muasisi: Idris bin Abdallah bin Hassan bin Hassan bin Ali (as).
Mwaka wa kuasisiwa: 172 H.
Ukubwa wa kijiografia: Moroco na sehemu ya Algeria.
Madhehebu: Shia Zaydiya.
Sifa Maalumu: Serikali ya kwanza ya madhehebu ya Shia kutoka katika familia na wajukuu wa Imamu Ali (a.s).
Aina ya utawala: Kienyeji/kieneo.
Hatua muhimu: Kuanzisha miji kadhaa mipya, kuchanua uchumi na utamaduni wa eneo.
Sababu ya kusambaratika: Uasi wa muda mrefu wa madola makubwa ya kandokando (Bani Umayyah Andalusia na Fatimiyah)
Watu
Idris mkubwa, Idris bin Idris bin Abdallah, Yahya bin Idris bin Omar.
Umuhimu wa utawala wa Idrisiyyah
Utawala wa Idrisiyyah unachukuliwa kuwa serikali ya kwanza ya Kishia katika ulimwengu wa Kiislamu, na serikali ya kwanza ya Kiislamu ya Morocco, [1] na inaelezwa kwamba ilikuwa na nafasi muhimu katika kuenea kwa Uislamu katika eneo hilo. [2] Pia, serikali hii imechukuliwa kuwa mojawapo ya serikali zenye ushawishi mkubwa katika tawala za magharibi mwa ulimwengu wa Kiislamu [3], ambayo ilifanikiwa kuunda enzi nzuri sana na zinazong’ara. [4]
Hatua za kielimu na kiutamaduni
Ushawishi na taathira ya utawala wa ukoo wa Idris (Idrisiyyah) katika uwanja wa utamaduni na ustaarabu madhubuti imetathminiwa na kuelezwa kwamba, ustaarabu wa Morocco katika zama hizi ulikuwa na ustawi mkubwa. [5] Msikiti wa Chuo Kikuu cha Qarawiyyin, ambacho kimesajiliwa katika kitabu cha rekodi cha Guinness (kitabu cha rekodi za dunia) kuwa chuo kikuu kongwe zaidi duniani, [6] kiliasisiwa katika enzi ya Idrisiyyah. [7] Mji wa Fes, ambapo msikiti huu na chuo kikuu vinapatika huko, pia ulijengwa mwanzoni mwa serikali ya Idrisiyyah, na kugeuka na kuwa kituo cha kielimu na katika duru zilizofuata ambapo wasomi kutoka nchi zingine walikuwa wakiingia na kutoka katika eneo hilo likitambulika kama kituo cha elimu. [8] Pia inasemekana kuwa kipindi hiki kilishuhudia kupigwa hatua kubwa mno katika uga wa fasihi. [9]
Hatua za kijamii
Mafanikio katika uwanja wa uadilifu na uchumi chini ya kivuli cha kufanyia kazi hukumu za kisheria na kuheshimu usawa kati ya Waarabu na mabedui wa Kiafrika inahesabiwa kuwa sifa mojawapo ya serikali hii. [10] Kutokuwa na chuki na taasubi ya mbari ya Kiarabu utawala wa Idrisiyyah kulipelekea furaha na kuwavutia mabedui waliokuwa wakilalamikia ukiritimba wa madaraka wa Waarabu [11] na kuanzishwa mafungamano ya kifamilia pamoja nao kuliimarisha misingi ya utawala wa Idrisiyyah. [12]
Nafasi ya wanawake katika enzi ya Idrisiyyah pia inachukuliwa kuwa mojawapo ya mambo chanya ya ukoo huu. [13] Katika muktadha huu, nafasi ya Kenza, mke wa Idris I, na Husna, mke wa Idris II, katika utawala wa serikali imetajwa katika kuongoza na kusimamia masuala ya utawala. [14] Muanzilishi pia wa msikiti na Chuo Kikuu cha Qarawiyyin (Al-Karaouine) ni mwanamke aliyejulikana kwa jina la Fatima al-Fihri. [15]
Sifa maalumu za kisiasa
Kwa mujibu wa mwandishi wa Historia na Ustaarabu wa Morocco, njia na mbinu ya utawala wa Idrisiyyah ilikuwa aina ya utawala wa karibu zaidi kwa Uimamu kwa mtazamo wa Uislamu. [16] Kwa kuzingatia ripoti hii, hawakujilazimisha kwa watu kwa kutumia nguvu za kijeshi, ukandamizaji au hila na ujanja; bali, watu waliwafadhilisha na kuwapokea kwa sababu ya ustahiki wao na vilevile nasaba yao inayoishia kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Katika muundo wa kisiasa wa watu wa ukoo wa Idris, madaraka hayakuwa mahususi kwa Imamu pekee; badala yake, mfumo wa kisiasa ulikuwa wa mfumo wa baraza (mjumuiko wa watu kadhaa) ambamo ndani yake wazee na shakhsia wakubwa wa kikabila walikuwa na mchango na nafasi katika maamuzi ya serikali, na hilo lilifanya watu watambue kuwa serikali inatokana na wao. Uhusiano wao na watu ulipelekea kudhoofika kwa vikundi vya kizandiki. [17]
Wahakiki wa historia wameandika kwamba, Idrisiyyah huwachukulia wapinzani wao kuwa na uhuru wa kufanya mambo yao. Kwa mfano, waliwapa hifadhi kundi lililokuwa likiwapinga kisiasa na kidini [18] na hata wakamtoa mtu miongoni mwao na kumpatia wadhifa wa uwaziri. [19] Hawakuchukua ushuru mkubwa kutoka kwa watu, hawakuwa na majumba makubwa, na hawakupenda kujifurahisha na kuishi maisha ya anasa, na mmoja wao pekee ambaye alikengeuka hilo aliuzuliwa na watu. [20] Ingawa serikali ya Idrisi ilikuwa na nguvu kubwa ya kiroho na kimaanawi na iliheshimiwa miongoni mwa watu, lakini haikuwa na nguvu zisizo za kawaida za kisiasa na kijeshi [21] na ilikuwa ikitaabika kwa udhaifu wa kiutawala. Udhaifu huu ukawa sababu ya kushindwa kwao na maadui. [22]
Hitilafu kuhusiana na madhehebu ya Idrisiyyah
Kuhusu madhehebu ya Idrisiyyah, kuna nyaraka chache za kihistoria, na kwa sababu hii, wanahistoria wanatofautiana katika suala hili. [23] Wengine wamemwita Idris bin Abdullah, mwanzilishi wa silsila ya Idrisi kuwa ni Mshia [24] na kuiona serikali ya Idrisiyyah kama serikali ya Kishia. [25] Kwa upande mwingine, wengine wamepinga uwezekano huo na kulitolea hoja jambo hilo. [26] Inawezekana pia kuwa Idrisiyyah awali walikuwa wafuasi wa madhehebu ya Shia na baada ya kuenea kwa madhehebu ya Maliki huko Morocco wakawa Masunni. Wale wataalamu waliomchukulia Idriss kama Shia wanatofautiana kama wao walikuwa ni Zaydi [28], Ismaili [29] au Shia wa Maimamu Kumi na Mbili. [30]. Pia, Ushia wa Al-Idris umechukuliwa kuwa Ushia dhaifu, ambao ulikuwa wa kisiasa badala ya kuwa wa kiitikadi. [31]
Hoja za Idrisiyyah kuwa ni Mashia
Baadhi ya hoja zinazotajwa kuwamtambua Idrisiyyah kuwa ni Shia ni hizi zifuatazo: Khutba za Idris, ambazo zinasemekana kuwa na ubainifu wa haki ya Ahlul-Bayt (a.s) kwa ukhalifa; sarafu zilizosalia kutoka zama za Idris, ambapo jina la Imam Ali (a.s.) ambazo zimeandikwa ibara isemayo: «علیٌ خیرُ النّاس بعدَ النَّبی " Ali ni mbora wa watu baada ya Mtume"; kauli za watu kama vile Ash'ari na Ibn Khaldun juu ya Ushia wa ukoo wa Idris, pamoja na kukiri kwa Ushi'a kwa watawala wa baadaye wa Idris. [32] Inasemekana kwamba katika zama za Idrisiyyah, Morocco haikuwa tayari kwa ajili ya kuenezwa Ushia na wao pia hawakufanya juhudi za kuwaingiza watu kwenye Ushia. Na kama kulichukuliwa hatua zozote basi athari zake ziliondoka na kupotea katika duru zilizofuata. [33] Badala yake, walipigana dhidi ya Makhawariji na kueneza upendo wa Ahlu al-Bayt (a.s.) na pia wakaeneza Uislamu miongoni mwa Wakristo. [33]
Kupanda na kushuka kwa utawala wa Idrisiyyah
Mahali pa kuanzia utawala wa Idrisiyyah ilikuwa ni kuhama kwa Idris bin Abdullah kwenda Morocco. Inasemekana kwamba yeye, ambaye alikuwa mmoja wa manusura wa Harakati ya Fakhkh, [34] kwa siri na kama mtumwa wa mtu aitwaye Rashid, ambaye kwa hakika alikuwa mtumwa wake mwenyewe, [35] pamoja na msafara wa kibiashara, walihama kutoka Madina na kwenda Misri na kutoka huko hadi Morocco. [36] Rashid alikuwa na nafasi muhimu katika kuanzishwa na kuimarishwa serikali ya Alawi ya ukoo wa Idris. [37]
Wengine wanaamini kwamba Idris aliamua kusafiri bila mpango wa hapo kabla na ili tu kuondokana na msako na ufuatiliaji utawala wa Bani Abbas, na aliichagua Morocco kwa sababu mtumwa wake alikuwa bedui (barbarian) kutoka Afrika; lakini wengine wanaamini kuwa safari ya Idris ilitokea kwa mpango wa kabla na ilitokea kama kiungo katika mnyororo. [38] Vile vile imeelezwa kwamba, uwepo wa kaka za Idris huko Afrika hususan huko Tlemcen ndiko kulikoandaa mazingira ya safari yake na hata inasemekana kwamba, hii haikuwa safari ya kwanza ya Idris kwenda Morocco. Kadhalika imeelezwa kuwa, alikwenda huko katika fremu ya misheni za kitablighi za Halwani na Sufiyani ambao walitumwa Morocco na Imam Sadiq (a.s.). [39]
Baada ya kuishi Tangier kwa karibu miaka miwili ambayo haikuambatana na mafanikio katika suala mahubiri na ufikishaji ujumbe wa Uislamu, [40] Idris alikwenda katika mji wa Volubilis, ambako alikaribishwa na Is’haq bin Muhammad, mkuu wa kabila la Aruba. Is’haq alimwoza binti yake kwa Idris, akajitoa kwa ajili yake na akawaalika watu wake watoa kiapo cha utii kwa Idris. Baada ya kabila la Aruba, idadi ya makabila mengine pia yaliahidi utii kwa Idris [41] na hivyo katika mwaka 172 H, serikali ya Idrisi iliundwa baada ya kupata kiapo cha utii wa makabila ya Berber. [42] Serikali hii iliendelea kwa miaka 375 kwa kupanda na kushuka chini na mwishowe, ilifikia tamati katika mzozo kati ya Bani Umayya wa Andalusia na Fatimiyah. [43]
Duru za kihistoria za utawala wa Ki-Idris
Historia ya utawala wa Idrisi imegawanywa katika vipindi viwili: Kipindi cha kwanza kilikuwa enzi ya nguvu, mamlaka na utawala, na kipindi cha pili kilikuwa wakati wa mtawanyiko na juhudi zisizo na matunda za kurejesha mamlaka na hatimaye kusambaratika. [44] Yahya IV, Sultani mwenye nguvu zaidi wa ukoo wa Idris, ambaye ukubwa wa utawala wake uliwashindwa watawala wengine, alikabiliwa na ujio wa Fatimiyyah na shambulio lao huko Fes. Alishindwa katika vita hivi na akawa chini ya Fatimiyyah. Ilikubaliwa kwamba abakie kuwa mtawala wa Fes, lakini angesoma khutba kwa jina la Khalifa wa Fatimiyyah. Sehemu iliyosalia ya eneo la Idris pia ilikabidhiwa kwa Musa bin Abi al-Aafia, mtawala aliyeteuliwa wa Fatimiyyah. Musa, ambaye pia alikuwa na tamaa na eneo la Fes, alimfunga na kumtesa Yahya baada ya muda fulani na kisha kuchukua mali yake [45] na kumfukuza pamoja na familia yake. Kwa njia hii, aliteka eneo lote la Idrisiyyah. [46]
Muda fulani baadaye, mmoja wa watu wa familia ya Idris, aitwaye Hassan bin Muhammad Hajjam, alianzisha harakati huko Fes na kuchukua utawala wake na miji kadhaa ya jirani. Lakini utawala wake haukudumu na karibu miaka miwili baadaye, Musa alitawala tena Fes, na wakati huu alihamisha familia ya Idrisi hadi kwenye ngome ya Hajar al-Nasr na kuwafunga. [47] Baada ya kuishi Hajar al-Nasr kwa miaka michache, Idrisiyyah walimuua kamanda wa ngome hiyo kwa wakati mwafaka na baada ya kuondoka hapo, walichukua uongozi wa makabila yaliyoizunguka, [48] lakini mara hii pia walishindwa kuunda serikali huru na walilazimika kukubali amri ya Khalifa wa Bani Umayya wa Andalusia na hivyo kusalia madarakani. [49] Kwa kutokea mabadiliko ya milinganyo ya kisiasa, utawala wa Idrisiyyah ulibadilishwa mara kadhaa zaidi kati ya Bani Umayya na Fatimiyya, na hatimaye mwaka 375 H, wakati mtawala wa wakati huo Idris alipouawa, uliangamizwa na Bani Umayya wa Andalusia. Inapaswa kutajwa kwamba karibu miaka thelathini baadaye, mmoja wa manusura wa Aal-Idris aitwaye Ali bin Hammoud alifanikiwa kupindua serikali ya Umayya ya Andalusia na kuanzisha serikali mpya iliyoitwa serikali ya Bani Hammoud huko Andalusia. [50] Pia, katika nusu ya kwanza ya karne ya 14, mmoja wa Waidrisi aliunda serikali katika maeneo machache Peninsula ya Kiarabu na kufufua jina la serikali ya Idrisiyyah kwa mara nyingine tena. [51]
Watawala wa Ki-Idris
Idris bin Abdallah bin Hassan Muthanna, mmoja wa wajukuu wa Imam Hassan al-Mujtaba (a.s) ni muasisi na mtawala wa kwanza kutoka ukoo wa Idris. Ameelezwa kuwa mtu mwema, mwenye tabia njema, muadilifu, jasiri, mwenye kusamehe na mshairi. [52] Baada ya kuanzishwa serikali ya Idris na ushindi wa awali, Harun al-Rashid alihisi vitisho na akamtuma mtu aitwaye Suleiman bin Jarir, anayejulikana kama Shammakh, ambaye anasemekana kuwa mwanateolojia wa Kizaydiyyah, ili kumuondoa Idris. Shammakh alijikurubisha kwake na kufanikiwa kupata nafasi ya juu kwake. Alikuwa akinukuu fadhila za Ahlul-Bayt (a.s.) katika mikutano na akitoa hoja za kuthibitisha Uimamu wa Idris, siku moja, wakati Rashid hayupo, alimpa sumu Idris na akakimbia. [54]
Baada ya kifo cha Idris, busara na hekima ya Rashid ambaye mfanyakazi wake iliokoa serikali changa ya Idris kutokana na maangamizi. Rashid aliwakusanya wazee na wanaume na kuwashauri wasubiri hadi mke wa Idris ajifungue na ikiwa ni mvulana watoe kiapo cha utii kwake na ikiwa ni msichana wachague mtu miongoni mwao. Baada ya kubainika kuwa mtoto wa Idris ni mvulana, walimpa jina la baba yake na Rashid akachukua madaraka ya malezi yake, akamfundisha fiqhi, hadithi na vita, na akala kiapo cha utii kwa ajili yake akiwa na umri wa miaka kumi na moja.[55] Idris II alishika hatamu za uongozi kwa kujitegemea akiwa na umri wa miaka kumi na saba [56]. Kwa jumla, watawala 13 na Imamu wa Idris walitawala, ambapo tisa walikuwa wa kipindi cha kwanza na wanne walikuwa wa kipindi cha pili. [57]
- Idris I.
- Idris II.
- Muhammad bin Idris (Al-Muntasir).
- Ali bin Muhammad bin Idris.
- Yahya (wa kwanza) bin Muhammad.
- Yahya (wa pili) bin Yahya.
- Ali bin Omar bin Idris.
- Yahya (wa tatu) Al-Muqaddam.
- Yahya (wa nne).
- Hassan al-Hajjam.
- Qassim bin Muhammad.
- Abu al-Ishi Ahmad bin Qassim
- Hasan bin Qasim Ganun
Mahusiano ya kisiasa ya Idrissiyah
Makhawariji walikuwa ni moja ya serikali zilizokuwa jirani na Idrisiyyah, ambao walikuwa na mahusiano ya mvutano kutokana na sababu za kiitikadi na kisiasa. Idris II aliamiliana kwa ukali na Makhawariji na mwanawe pia alikuwa na uhusiano mbaya nao. [58] Mgogoro kati ya Makhawariji na Idrisiyyah uliendelea hadi mwisho wa kipindi cha kwanza cha utawala wa Idrisiyyah, na mara moja, katika kipindi cha Ali bin Omar bin Idris, kulipelekea kutekwa kwa sehemu za mji mkuu wa Idrisiyyah. [59] Mahusiano ya Aal-Idris na majirani zake Bani Umayya yalikuwa yamejikita katika uadui. Hata hivyo, wakati wa utawala wa Abu al-Ish Ahmad bin Qasim, mmoja wa watawala wa Idris katika kipindi cha pili, walikuja kuwa marafiki wa Bani Umayya [60].
Akthari ya majirani wengine wa serikali ya Idrisiyyah, ingawa wakati mwingine waliwaunga mkono dhidi ya Bani Umayya, lakini walikuwa ndio sababu ya mashinikizo ya vyombo vya utawala vya ukhalifa wa Kiabbas. [61] Fatimiyyah nao pia walikuwa na siasa za undumakuwili kwa Idrisiyyah na hatimaye wakadhibiti eneo la utawala la Aal Idris. [62] Imenukuliwa kwamba, utawala wa Ki-Idris ulituma balozi katika baraza la utawala la Charlemagne. [63]
Eneo la utawala la Idrisiyyah
Waidrissia walikuwa wakitawala Maghrib al-Aqswa, ambayo inaweza kutambuliwa leo kuwa ni ardhi ya nchi mbili za Morocco na Algeria. [64] Katika kipindi cha kwanza, serikali ya Idrisi, iliyokuwa na mamlaka na uhuru, iliweza kupanua eneo lake la utawala kaskazini hadi Wahran na Tlemcen [65] na vilevile katika mwelekeo wa kusini, pia walisonga mbele hadi Sus Aqsa na hata maeneo yake ya kusini zaidi. [66] Mto Moulouya pia umetambulishwa kama mpaka wa mashariki wa serikali yao. [67]
Katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Idrisi, mji wa Fes, ambao ulijengwa kwa amri ya Idris II, ulikuwa mji mkuu wa Idrisiyyah. [68] Katika kipindi cha pili, Waidrisi walitawala miji kadhaa, ikiwa ni pamoja na Basra (mji katika Maghrib al-Aqswa, kati ya Tangier na Fes) [69], Asil na Hajar al-Nasr hawakwenda mbali zaidi hapo. [70]
Shakhsia wa Idrisiyyah katika kipindi cha historia
Waidris, ambao wanajulikana kama shakhsia wakubwa na bado wanaheshimiwa na watu wa Morocco. [71] Jouti, Meshishi, Alami na Wazani ni miongoni mwa familia zinazojulikana za Idrisiyyah ambazo zingalipo hadi leo. [72]
Katika chote cha historia, miongoni mwa familia ya Idrisi, kumekuwa na watu mashuhuri na wenye taathira ambao wamekuwa na ushawishi katika nyanja mbalimbali za kielimu, kitamaduni, kisiasa n.k. Sharif Idrisi, Abdul Qadir Jazayeri, Muhammad bin Ali Alawi na ndugu wa Ghimari walikuwa miongoni mwa watu mashuhuri wa Idrisi.
- Sharif Idrisi
Muhammad bin Muhammad Idrisi, anayejulikana kama Sharif Idrisi, mwanajiografia wa karne ya 5 na 6 Hijria, ni katika wajukuu wa Hamudiyan wa Andalusia na kwa njia hiyo anatokana na kizazi cha Waidrisia. [73] Nasa eneo lililopo kwenye sayari ya Pluto limetajwa kwa jina lake. [74] Pia anatajwa kuwa daktari mwenye nguvu, mfamasia na mshairi, na kitabu chake Nuzhatul-Mushtaq fi Ikhtaraq-e-Afaq ni kazi muhimu iliyotambulishwa katika uga wa jiografia. [75] Alitengeneza mfano mdogo wa sayari ya dunia kwa sura ya tufe na iliyotengenezwa kwa fedha, ambayo haipatikani sasa; lakini ramani zilizochorwa naye bado zinapatikana na mtafiti Mjerumani aitwaye Konrad Miller alizichapisha mwaka wa 1997. [76]
- Ndugu wa Ghimari
Ahmad, Abd al-Aziz na Abdullah Ghimari walikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kisunni katika elimu ya hadithi katika karne za hivi karibuni [77] na ni katika wapinzani wa Ibn Taymiyyah na Muhammad bin Abd al-Wahhab, [78] kutoka kizazi cha Idrisa.[79]
- Muhammad bin Alawi al-Aalawi: Ni katika mafakihi wa madhehebu ya Maliki katika karne ya 15 Hijria na ni katika wakosoaji wa Uwahabi. [80]
- Muhammad bin Ali Idrisi: Huyu alikuwa mmoja wa watu wa familia ya Idrisi ambaye katika karne ya 14 alifanikiwa kuunda serikali katika sehemu ya Peninsula ya Kiarabu ambayo ilikuwa maarufu kwa jina la dola la Idrisi. [81] Serikali hii kuanzia mwaka 1327 H ilikuwa ikiongoza maeneo ya Sabia, Tihamah, Asir na Jazan na mwaka 1351 ilisambaratika kufuatia mashambulio ya ukoo wa Aaal Saud. [82]