Sherehe ya maulidi ya Mtume (s.a.w.w)

Kutoka wikishia
Sherehe ya kuzaliwa Mtume(s.a.w.w) Indonesia

Sherehe ya maulidi ya Mtume(s.a.w.w) inaashiria na kurejea katika kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Bwana Mtume(s.a.w.w). Waislamu wa kishia na kisuni huadhimisha na kufanya sherehe ya Maulidi wakikumbuka kuzaliwa mbora huyo wa viumbe na Mtume wa mwisho wa Allah. Lakini kundi la mawahabi lenyewe linaaamini kwamba, sherehe ya maulidi ya Mtume ni bidaa na uzushi, kwani katika zama za Mtume na masahaba hakukufanyika sherehe kama hii.

Wanazuoni wa kiislamu katika kuwajibu mahawabi wamesema: Licha ya kuwa katika zama za Bwana Mtume(s.a.w.w) hakukufanyika sherehe ya maulidi ya Mtume, lakini hilo halijakatazwa katika sheria na mafundisho ya uislamu, na kwa msingi huo kuadhimisha maulidi kwa ajili ya Mtume sio bidaa wala uzushi bali kufanya hivyo ni jambo zuri na linalofaa.

Aidha ili kuhalalisha sherehe ya maulidi ya Mtume kumetumiwa Aya za Qur’an kama hoja ya kwamba, kumeusiwa kumtukuza, kuonyesha huba na mapenzi na kumthamini Bwana Mtume(s.a.w.w). Ripoti za historia kuanzia karne ya 4 Hijiria na baada ya hapo zinaonyesha kuwa, waislamu walikuwa wakifanya sherehe ya maulidi ya Mtume. Kadhalika wakazi wa Makka walikuwa wakikusanyika katika kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume(s.a.w.w) mahali alipozaliwa Mtume na kujishughulisha na dua, kumdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu sambamba na kufanya tabaruku kwake mpaka katika zama za utawala wa Aal-Saud wakati eneo hilo lilipoharibiwa na kubomolewa.

Waislamu wa madhehebu ya shia wanaamini kuwa, Mtume alizaliwa 17 Rabiul-Awwal(mfunguo sita) huku waislamu wa madhehebu ya suni wakiamini kwamba, mbora huyo wa viumbe alizaliwa 12 Rabiul-Awwal. Maulamaa wa kishia wanaamini kuwa, ni mustahabu kutoa sadaka na kufanya mambo ya kheri katika siku hii, kuwafurahisha waumini na kadhalika. Kwa upande wao Waislamu wa Ahlu Sunna wameusia kutoa zawadi na kuwalisha masikini katika siku ya kukumbuka kuzaliwa Bwana Mtume (s.a.w.w). Kwa msinghi Waislamu wa mataifa mbalimbali hufanya sherehe na maadhimisho ya kuzaliwa Bwana Mtume(s.a.w.w) ambayo ni mashuhudi kama sherehe ya Maulidi ya Mtume. Siku ya kuadhimisha Maulidi ya Mtume ni mapumziko rasmi katika baadhi ya nchi kama Iran, Afghanistan, Iraq, India, Pakistan, Indonesia, Misri na Tanzania.

Umuhimu na historia

Sherehe ya kuzaliwa Mtume(s.a.w.w) Yemen

Sherehe ya maulidi ya Mtume(s.a.w.w) inaashiria na kurejea katika kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Bwana Mtume (saww). Kujuzu au kutojuzu kufanya sherehe ya maulidi ya Mtume ni miongoni mwa mambo ambayo Waislamu wanatofautiani na kundi la mawahabi. Kwa mujibu wa waislamu inajuzu kufanya sherehe ya maulidi ya Mtume. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Waislamu katika nchi mbalimbali huadhimisha na kufanya sherehe ya maulidi katika siku ya kukumbuka kuzaliwa mbora wa viumbe na rehma kwa walimwengu wote yaani Muhammad ibn Abdullah. [1] Kadhalika siku ya kuadhimisha Maulidi ya Mtume ni mapumziko rasmi katika baadhi ya nchi kama Iran, Indonesia, [2] India, [3] Pakistan, [4] Misri, [5] Tanzania na kadhalika. [6]. Hata hivyo mawahabi wao wanaamini kuwa, kusherehea maulidi ya Mtume ni bidaa na haramu.[1]

Historia ya kufanyika sherehe ya maulidi ya Mtume inarejea nyuma katika karne za nne na tano Hijiria. Ahmad ibn Ali Maqrizi mwandishi wa historia wa karne ya 9 Hijiria amesema kuwa: Sherehe ya maulidi ya Mtume ilienea katika zama za utawala wa Fatimiyah (297-567 H) nchini Misri.[2] Kadhalika kwa mujibu wa ripoti zilizoko katika vyanzo vya historia ni kuwa, Muzaffereddin Gokbori (aliaga dunia 630 H), kamanada wa Salahuddin Ayyubi na mtawala wa Erbil alikuwa akifanya sherehe ya kuzaliwa Mtume katika mwezi wa Rabiul-awwal.[3]

Sherehe ya maulidi ni bidaa?

Sherehe ya kuzaliwa Mtume(s.a.w.w) Iraq

Kundi la mawahabi linasema kuwa, kufanya sherehe ya kuzaliwa Mtume wa uislamu ni bidaa.[4] Abdul-Aziz ibn Baz ni mmoja wa maulamaa wa kiwahabi ambaye anaamini kuwa, maulidi ni bidaa. [11] Wanazuoni wa Kisalafi, wanaamini kuwa, kushiriki katika sherehe ya maulidi ya Mtume, kukaa katika shehemu inapofanyika sherehe hii au kula chakula kinachogawiwa katika hafla hiyo ni haramu.[5] Vile vile baadhi ya waandishi wao wanawanasabisha wanaofanya sherehe ya maulidi ya Mtume na ufasiki, kutokuwa na dini na kadhalika.[6] Sababu na hoja ya mawahabi ya kutambua kuwa, maulidi ni bidaa ni kwamba, sherehe kama hii haikufanyika katika zama za Mtume na masahaba. [14]





Majibu ya maulamaa wa kishia na kisuni

Sherehe ya kuzaliwa Mtume(s.a.w.w) Iran

Kwa mujibu wa wanaopinga hoja ya mawahabi ni kuwa, pamoja na kuwa, hakujanukuliwa kauli ya moja kwa moja katika sharia ya Kiislamu kuhusiana na maulidi ya Mtume, lakini Aya za Qur’an Tukufu zinaunga mkono sherehe hii. [15] Mafuhumu na maana jumla ya Qur’an kama vile kuonyesha huba na mapenzi kwa Mtume (s.a.w.w), [16] na udharura wa kumthamini, kumtukuza na kumheshimu [17] zimetumiwa kama zinazohalalisha kufanya sherehe ya maulidi ya Mtume. [18] Ayatullah Ja’afar Sobhani, mjuzi na mmoja wa wanazuoni wa kishia anasema: Kufanya sherehe ya maulidi ni kuonyesha huba na mapenzi kwa Mtume; mapenzi ambayo Qur’an imetoa agizo kwayo. [19] Vilevile kwa kutumia Aya za mwisho za Surat al-Maidah ambazo kwa mujibu wake Nabii Issa(a.s) alimuomba Mwenyezi Mungu kwa kusema: Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshia chakula kutoka mbinguni ili kiwe sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanaoruzuku. Historia inaonyesha kuwa, Nabii Issa akiwa pamoja na Hawariyyun (Mitume na wajumbe 12 wa Nabii Issa) alisherehekea pamoja nao baada ya kushushwa chakula hicho kutoka mbinguni na wakristo wanafanya sherehe katika siku hiyo.

Sheikh Ja’afar Sobhani anaamini kuwa, kuna ulazima wa kufanya sherehe kwa sababu Mtume ameiokoa dunia na kuabudu masanamu na ujahili, na neema hii ni kubwa kuliko chakula kutoka mbinguni kilichoshushwa kwa Hawariyyun. [20]

Shakhsia wakubwa wa Ahlu Sunna kama: Sari Saqati (253 Miladia), Junayd Baghdad (aliaga 297 H), Imam Yafi’i (aliaga dunia 768 H) na Hassan bin Omar bin Habib (aliaga dunia 779 H) kila mmoja kati yao ametumia ibara mbalimbali na kuonyesha kuwa, kudhihirisha furaha na kufanya sherehe ya maulidi ya Mtume ni jambo zuri, ni njia ya kufikia imani, kunufaika na neema za peponi na kadhalika. [21]

Yusuph Qardhawi (aliyefariki mwaka 2020 Miladia) mmoja wa wanazuoni na maulamaa wa zama hizi wa kisuni akitumia baadhi ya Aya za Quran amelitambua suala la kufanya sherehe ya maulidi ya Mtume kwamba, linajuzu. [23]. Anaamini kuwa, kufanya sherehe kwa ajili ya maulidi ya Mtume na matukio mengine ya kiislamu, kimsingi ni kukumbuka neema za Mwenyezi Mungu ambazo amewaruzuku na kuwapatia Waislamu na hii hali ya kukumbuka si tu kwamba, sio bidaa na haramu, bali ni jambo zuri na linalofaa. [22]Tahir Qadiri, mmoja wa wanazuoni wa kisuni anasema: Kufanya jambo lilolote la mubaha (lililoruhusiwa) na ambalo halijakatazwa katika sheria ya kiislamu na kulibadilisha kuwa utamaduni wa jamii na lengo likawa ni kuonyesha furaha kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume(s.a.w.w) hakuna tatizo. [24]

Kwa mujibu wa hadithi zilizonukuliwa katika kitabu cha Iqbal al-A’amal ni kuwa: Kufunga swaumu katika siku ya kukumbuka kuzaliwa Bwana Mtume (s.a.w.w) thawabu zake ni sawa na kufunga mwaka mzima. [25] Vilevile maulamaa wa kishia wanasema: Ni mustahabu kutoa sadaka, kutembelea na kufanya ziara katika maeneo walipozikwa shakhsia muhimu, [26], kufanya mambo ya kheri, kuwafurahisha waumini na kadhalika katika kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume (s.a.w.w). [27] Katika hadithi zilizopokewa upande wa waislamu wa madhehebu ya shia kuna hadithi zinaoonyesha kuwa, kuna swala maalumu inayoswaliwa katika siku hii. [28] Kwa upande wake masuni wao wametilia mkazo kufanya mambo yafuatayo katika siku hii: Kutoa hotuba kuhusiana na Mtume, kusoma Qur’an, kuunga udugu, kutoa zawadi na kuwalisha masikini. [29]

Sehemu na mahali alipozaliwa

Sherehe ya kuzaliwa Mtume(s.a.w.w) Malasyia


Kuhusiana na tarehe ya kuzaliwa Bwana Mtume (s.a.w.w) kuna hitilafu baina ya waislamu. [30]. Ni mashuhuri kwamba, Waislamu wa madhehebu ya suni wanasema, Mtume Muhammad alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita (Rabiul-Awwal) mwaka wa Tembo (570 Miladia) na waislamu wa madhehebu ya shia wanasema, alizaliwa tarehe 17 mfunguo sita (Rabiul-Awwal) mwaka huo huo. [31) Kwa msingi huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezitangaza siku za baina ya tarehe 12 hadi 17 mfunguo sita kuwa ni wiki ya umoja baina ya waislamu. [32] Lengo la Iran kutangaza wiki ya umoja ni kuandaa makongamano na mikutano mbalimbali na kujadili changamoto zinazoukabili umma wa kiislamu pamoja na njama za maadui za kila leo.

Sherehe ya kuzaliwa Mtume Morocco

Mtume Muhammad(s.a.w.w) alizaliwa katika nyumba moja katika eneo la Shia’b Abi Twalib. [33] Kwa mujibu wa Muhammad ibn Omar Bahraq, mwanazuoni wa kishafii (aliyefariki mwaka 930 H) ni kuwa, wakazi wa Makka walikuwa wakikusanyika katika kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume(s.a.w.w) mahali alipozaliwa Mtume na kujishughulisha na dua, kumdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu sambamba na kufanya tabaruku kwake. [34] Kadhalika Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mpokezi wa hadithi wa karne ya 11 Hijiria ananukuu kwamba: Katika zama zake kulikuwa na eneo lililokuwa likijulikana kwa jina hili huko Makka na watu walikuwa wakilitembelea na kwenda kufanya ziara hapo. 35]. Jengo hilo lilikuweko mpaka katika zama za kuanza utawala wa ukoo wa Aal-Saud. watawala wa ukoo wa Aal-Saud kutokana na kuwa na itikadi za kiwahabi ambazo kimsingi zinapiga marukufu kufanya tabaruku kwa athari za Mitume na waja wema wa Mwenyezi Mungu, walichukua uamuzi wa kuliharibu na kulibomoa eneo hilo. [36]

Monografia

Kuhusiana na kuthibitisha uhalali wa sherehe ya maulidi ya Mtume(s.a.w.w) kumeandikwa vitabu mbalimbali ambapo miongoni mwavyo ni:

  • Al-Bayan al-Nabawi An Fadhl al-Ihtifal Bimaulid al-Nabawi: Mwandishi wa kitabu hiki ni Mahmoud Ahmad al-Zain. Lengo la mwandishi wa kitabu hiki ni kuthibitisha kwamba, maulidi na kufanya sherehe ya maulidi ya Mtume ni halali. Katika kitabu hiki cha lugha ya kiarabu, mwandishi anatoa hoja na kuondoa baadhi ya shubha na utata kuhusiana na sherehe ya maulidi. Mwandishi wa kitabu hiki amefikia natija hii kwamba, wanazuoni na wapokezi wa hadithi wa Ahlu-Sunna wanatambua kuwa, kufanya maulidi ni mustahabu. Taasisi ya uchapishaji ya Intisharat Dar al-Buhuth Lidirasat al-Islamiyah ya Dubai ilichapisha kitabu hiki 1426 Hijiria. [37].
  • Jashn Payambar (s.a.w.w) yaani “Sherehe ya Maulidi ya Mtume” cha lugha ya kifarsi, kimeandika na Abdul-Rahim Mousawi kwa lengo la kuthibitisha uhalali wa kufanya sherehe ya maulidi ya Mtume ambapo anakosoa mitazamo ya wanaopinga sherehe ya maulidi. Kwa mtazamo wa mwandishi ni kuwa, kufanya sherehe ya maulidi ya Mtume ni moja ya vielelezo na mifano ya wazi ya wajibu wa kuonyesha heshima kwa Mtume. Kitabu hiki ni katika majimui ya kitabu cha “Katika Maktaba ya Ahlul-Baiti Juzuu 25” kilichochapishwa na jumuiya ya kimataifa ya Ahlul-Baiti 1390 Hijiria Shamsia kikiwa na kurasa 57. [38]


Rejea

  1. Al-Daweish, Fatāwa al-Lajnah ad-Dā'imah, juz. 3, uk. 29.
  2. Muqrizi, al-Mawaidhwa wal-iitba'ar, 1418 AH. juz. 2, uk. 436.
  3. Ibn Kathir, al-Badaiya wa al-Nahiya, 1407 AH, juz. 13, uk. 137; Muqrizi, Al-suluk limaarifat dual al-muluk, 1418 AH, juz. 1, uk. 368.
  4. Al-Daweish, Fata'wa al-jannat al-Daimmah, Riyadh, juz. 3, uk. 29
  5. Shahata, Maulid al-Nabawi..., Iskandriye, uk. 116.
  6. Dabirii, Jashni milad al-nabii(s.a.w.w), 1437 AH, uk. 9.

Vyanzo

  • Āmilī, al-Sayyid Jaʿfar al-Murtaḍā al-. Al-Ṣaḥīḥ min sīrat al-nabīyy al-aʿẓam. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1426 AH.
  • Āl al-Shaykh, ʿAbd al-Laṭīf b. ʿAbd al-Raḥmān. ʿUyūn al-rasāʾil wa al-ajwabat ʿalā al-masāʾil. Edited by Ḥusayn Muḥammad Bawā. Riyadh: [n.n], [n.d].
  • Baḥraq, Muḥammad b. ʿUmar. Ḥadāʾiq al-anwār wa maṭāliʿ al-asrār fī sīrat al-Nabī al-mukhtār. Edited by Muḥammad Ghasāq Naṣūḥ Azqūl. Jeddah: Dār al-Minhāj, 1419 AH.
  • Dawīsh, Aḥmad b. ʿAbd al-Razzāq. Fatāwā al-lujnat al-dāʾima. Riyadh: Riʾāsat Idārat al-Buḥūth al-ʿIlmiyya wa al-Iftāʾ. [n.p], [n.d].
  • Dabīrī, Ishāq. Jashn-i mīlād-i Rasūl Allāh (a). [n.p]: Kitābkhāna-yi ʿAqīda, 1437 AH.
  • Ibn Kathīr al-Dimashqī, Ismāʿīl b. ʿUmar. Al-Bidāya wa l-nihāya. Beirut: Dār al-Fikr, 1407 AH.
  • Imām Khomeinī, Sayyid Rūḥ Allāh. Ṣaḥīfa-yi Imām. Muʾassisa-yi Tanẓīm wa Nashr-i Āthār-i Imām Khomeini, 1378 SH.
  • Ibn Ṭāwūs, ʿAlī b. Mūsā. Al-Iqbāl bi-l-aʿmāl al-ḥasana. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1409 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Second edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Mirʾāt al-ʿuqūl fī sharḥ akhbar Āl al-Rasūl. Edited by Sayyid Hashim Rasūlī Maḥallātī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1404 AH.
  • Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Murūj al-dhahab wa maʿadin al-jawhar. Edited by Asʿad Dāghir. Qom: Dār al-Hijra, 1409 AH.
  • Maqrizī, Aḥmad b. ʿAlī. Imtāʿ al-asmāʾ bimā li-Nabī min al-aḥwāl wa al-amwāl wa al-ḥafda wa al-matāʾ. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Ḥamīd al-Namīsī. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1420 AH.
  • Maqrizī, Aḥmad b. ʿAlī. Al-Sulūk li maʾrifa dūn al-mulūk. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1420 AH.
  • Maqrīzī, Taqī al-Dīn. Al-Mawāʿiz wa al-iʿtibār bi dhikr al-khiṭaṭ wa al-āthār. Edited by Khalīl al-Manṣūr. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1418 AH.
  • Qādirī, Muḥammad Ṭāhir. Kiyā mīlād al-Nabī manānā bidʾat hi. Laura: Minhāj al-Qurān, 2008.
  • Subḥānī, Jaʿfar. Furūgh-i abadīyyat. Qom: Būstān-i Kitāb, 1380 Sh.
  • Shaḥāta, Muḥammad Ṣaqar. Al-Mawlid al-nabawī; hal naḥtafil?. Alexandria: Dār al-Khulafā al-Rāshidīn, [n.d].
  • Ṭūsī, Muḥamamd b. al-Ḥasan al-. Miṣbāḥ al-mutahajjid wa silāḥ al-mutaʿabbid. Tehran: Maktabat al-Islāmiyya, [n.d].
  • Celebration of the birth of the Prophet and Islamic events (Arabic). Official Website of Sheikh Yusuf al-Qaradawi. Accessed: 2023/01/02.
  • Imam Ibn Taymiyyah did not approve of celebrating the Prophet's birthday (Arabic). Official Website of Abdullah Binbaz. Accessed: 2023/01/02.
  • Celebrating the birthday of the Prophet of Islam (s) is an act of love for him and fulfilling the instructions of the Quran (Persian). Shafaqna Website. Accessed: 2023/01/02.
  • In the School of Ahl al-Bayt (a), vol. 25; Celebration of the birth of the Prophet (s) (Persian). Accessed: 2023/01/02.
  • The Eid of the Prophet's birthday (Arabic). Accessed: 2023/01/02.
  • Al-Qaradawi: Celebrating the Prophet’s birthday is not an innovation (Arabic). Accessed: 2023/01/02.
  • Mawlid al-Nabi, Al-Azhar website (Arabic). Accessed: 2023/01/02.
  • Public Holidays in Pakistan 2018. Accessed: 2023/01/02.