Qawaid al-Ahkam (Kitabu)

Kutoka wikishia

Qawaid al-Ahkam fi M’arifat al-Halal wal-Haram mashuhuri zaidi kwa jina la Qawaid al-Ahkam ni kitabu kilichoandikwa kwa lugha ya Kiarabu na Allama Hilli (aliyeaga dunia 726 Hijria). Kitabu hiki maudhui yake ni ya fat’wa (za Kifiq’h). Miongoni mwa sifa maalumu za kitabu hiki ni kujikita katika maudhui, umakini katika kugawa makundi na kuweka migawanyiko ya masuala ya kisheria, ubainishaji mwepesi na usio na ugumu na kuzingatia milango yote ya fiq’h. Kitabu cha Qawaid al-Fiq’h kiliandikwa kwa ombi la Fakhr al-Muhaqiqin (aliyeaga dunia 771 Hijria) mtoto wa Allama Hilli. Mwishoni mwa kitabu hiki pia kuna wasia wa mwandishi wa kitabu kwa mwanawe. Katika zama za utawala wa Safaviyah, kitabu hiki kilikuwa msingi wa sheria za kuongoza nchi. Kumeandikwa maelezo na ufafanuzi (sharh) na makala mbalimbali kuhusiana na kitabu hiki. Kadhalika kutarjumiwa duru kamili ya Kifarsi kunahesabiwa kuwa moja ya sifa maalumu za kitabu hiki.

Nafasi na Umuhimu

Qawaid al-Ahkam fi M’arifat al-Halal wal-Haram mashuhuri zaidi kwa jina la Qawaid al-Ahkam ni miongoni mwa vitabu vya fiq’h vya fat’wa [1] vya Kishia ambacho kinajumuisha milango yote ya fiq’h kuanzia tohara mpaka dia. Kwa mujibu wa Agha Bozorg Tehrani, kitabu hiki ni chenye thamani sana miongoni mwa vitabu vya Fiq’h baada ya kitabu cha Shara’i al-Islam cha Muhaqqiq Hili (aliyeaga dunia 676 Hijria). [2] Allama Hilli alikiandika kitabu hiki kwa muda wa miaka 10 na akakifanya kuwa mhimili wake wa kufundishia katika Chuo Kikuu cha Kiislamu (Hawza) cha Baghdad. [3] Katika zama na duru mbalimbali kitabu cha Qawaid al-Ahkam kilizingatiwa na Maulamaa na shakhsia wakubwa wa Hawza mbalimbali. [4] Muhaqqiq Karaki amekitambua kitabu hiki kuwa kisicho na mithili katika upande wa namna kilivyotungwa na katika uandishi wake. [5] Kadhalika kwa mujibu wa nukuu za vyanzo vya historia, kitabu cha Qawaid al-Ahkam kiliteuliwa na Shah Ismail katika zama za utawala wa Safaviyah kuwa sheria (katiba) ya utatuzi wa masuala mbalimbali ya kiutawala na kidini. [6] Qawaid al-Ahkam ni katika vitabu vyenye itibari na mashuhuri vya Kifiq’h vya Shia Imamiyyah ambacho kinajumuisha duru kamili ya fiq’h kuanzia mlango wa tohara mpaka dia. [7]

Mwandishi

Makala kuu: Allama Hilli na orodha ya athari za Allama Hili

Ibn Mansur Hassan bin Yusuf bin al-Mutahhar mashuhuri zaidi kwa jina la Allama Hilli, ni katika Maulamaa wa karne ya 8 Hijria ambapo kwa mujibu wa ungamo la akthari ya Maulamaa ni kwamba, alikuwa na nadharia na mtazamo katika elimu za akili na nakili na ameacha athari mbalimbali za kielimu ambapo miongoni mwazo tunazoweza kuziashiria ni: Al-Mukhtalifah Wal-tadhikrah na Muntaha al-Matlab. [8] Inaelezwa kuwa, hakuwa na mfano wake katika fadhila, ukamilifu na kuchunga adabu na maadili. [9]

Muundo na maudhui

Kitabu cha Qawaid al-Ahkam kinajumuisha milango 21 vya fiq’h na kimeandikwa na kuchapishwa katika juzuu tatu [10] ambapo kimejumuisha humo mas’ala 6,600. [11]

• Juzuu ya kwanza inajumuishwa milango ya: Tohara, Sala, Zaka, Saumu na Hija;

• Juzuu ya Pili inajumuisha milango ya: Biashara, dini na vinavyohusiana navyo, amana na vinavyohusiana navyo, ghasb (unyang’anyi) na vinavyohusiana nao, ukodishaji na vinavyohusiana nao, waqf na zawadi;

• Juzuu ya tatu inajumuisha milango ya: Ndoa, talaka, kumuachilia huru mtumwa na vinavyohusiana navyo, viapo na yanayohusiana navyo, uvuvi, vichinjwa, faradhi, kadha, adhabu na dia;

Mwishoni mwa kitabu, kuna wasia kamili na muhimu wa mwandishi kwa ajili ya mwanawe Fakhr al-Muhaqiqin. [12]

Sharh (ufafanuzi) na maelezo

Makala asili: Orodha ya sharh (ufafanuzi) na maelezo ya Qawaid al-Ahkam

Agha Bozorg Tehrani ametaja na kutambulisha katika kitabu chake cha al-Dharia’ vitabu 35 vilivyoandikwa kwa ajili ya kutoa sharh (ufafanuzi) wa kitabu cha Qawaid al-Ahkam [13] ambapo baadhi yavyo ni:

• Idhah al-Fawaid, mwandishi: Fakhr al-Muhaqiqin mtoto wa Allama Hili (aliaga dunia 771 Hijria).

• Sharh Qawaid al-Ahkam, mwandishi: Kashif al-Ghitaa (aliaga dunia 1228 Hijria).

• Sharh Qawaid al-Ahkam, mwandishi: Shahid al-Thani (aliaga dunia 911 Hijria).

• Jamiu al-Maqaasid, mwandishi: Muhaqqiq Karaki (aliaga dunia 940 Hijria).

• Kashf al-Litham, mwandishi: Fadhil Hindi (aliaga dunia 1137).


Tarjumi na ukosoaji

Kitabu cha Qawaid al-Ahkam kimetarjumiwa kwa lugha ya Kifarsi na Muhammad bin Abi Abdillah mashuhuri kama Haji (aliaga dunia 732). [14] Ali bin Muhammad Qashi (Kashi) Hilli, mwenye lakabu ya Nasir al-Din, ameandika katika kitabu chake cha Risalat al-Fiq’h nukta 20 kama upinzani na ukosoaji wake kwa Qawaid al-Ahkam cha Allama Hilli ambacho ni mashuhuri kwa risala ya upinzani. Hata hivyo ni sehemu tu ya kitabu hiki ambayo ipo miongoni mwa vitabu vya fiq’h. [15]

Nakala • Kuna nakala ya kitabu hiki inayopatikana katika maktaba ya Sayyid Hussein Sadr huko Kadhmiya Iraq: Nakala hii iliandikwa na Muhammad bin Ismail Harqali mwaka 706 Hijria. Kitabu hiki alisomewa Allama na akakiunga mkono.

• Nakala iliyoko katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Tehran, Iran: Nakala hii iliandikwa na Ali bin Muhammad Neili mwaka 709 Hijria.

• Nakala iliyoko katika maktaba ya Madinat al-Ilm Kadhimiya, Iraq: Nakala hii iliandikwa na Muhammad Mohsin Saruqi mwaka 713 Hijria.

• Nakala iliyoko katika maktaba ya Feyziyeh Qom, Iran: Juzuu ya kwanza ya nakala hii iliandikwa na Muhammad bin Bani Nasr mwaka 717 Hijria na juzuu ya pili ikaandikwa mwaka huo huo na Muhammad bin Muhammad, [16].