Mkopo:Unywaji wa pombe
Unywaji wa pombe: Unywaji wa pombe unahusisha utumiaji wa kioevu chochote chenye asili ya kulevya, jambo ambalo katika Uislamu linatambulika kama mojawapo ya madhambi makuu. Kwa mujibu wa Qur'ani, hadithi, na mwafaka wa wanazuoni (ijmai), unywaji wa kileo cha aina yoyote ni haramu, bila kujali kama kimetengenezwa kwa zabibu, tende, zabibu kavu, au malighafi nyingine yoyote. Kisheria, wanywaji pombe wanachukuliwa kuwa ni mafasiki, hali inayopelekea kupoteza sifa ya kutoa ushahidi mahakamani na kukataliwa kwa zaka yao.
Uharamu wa kunywa ulevi (pombe) umewekwa wazi kabisa ndani ya Qur'ani, ambapo sheria ya Kiislamu imeweka adhabu ya haddi (adhabu ilioanishwa moja kwa moja na Mungu mwenyewe) ya viboko themanini kwa mwenye kutenda kuso hilo. Hata hivyo, mlango wa toba uko wazi; ikiwa mhusika atatubu kabla ya mashahidi kutoa ushahidi wao, husamehewa na kufutiwa adhabu hiyo.
Unywaji wa pombe (ulevi/mvinyo) ni kitendo cha kunywa kimiminika chochote kile chenye sifa ya kulevya [1]. Katika Uislamu, unywaji wa pombe ni haramu [2] na ni miongoni mwa madhambi makuu (Al-Kabair). [3] Uharamu wa kunywa pombe katika Uislamu ni suala lenye makubaliano ya kisheria (Ijma) miongoni mwa Waislamu wote, na linahesabika kuwa ni katika mambo ya dharura ya dini (Dharuriyyat al-Din), yeaani lenye sheria wazi isiodadisika; kiasi kwamba endapo mtu fulani atahalalisha kitendo hicho, huhesabiwa kuwa ni kafiri. [4] Katika Aya za Qur'ani, pombe imetajwa kwa jina la "Khamr", [5] aidha katika vitabu vya Fiqh pia neno hili hutumika kwa maana hiyo hiyo. [6] Baadhi ya Hukumu za Kifikihi kuhusu Unywaji wa Vileo Kwa mujibu wa fatwa za mafaqihi, vinywaji vyote vyenye kulevya—hata viwe vimetokana na malighafi gani—vina hukumu sawa kisheria na unywaji wake ni haramu. Hii inajumuisha ya ulevi iwe ni divai ya zabibu za kawaida (khamr), ya zabibu kavu (naqi’i), pombe ya tende (nabidh), ya asali (bit’), ya shayiri (mizr), mchanganyiko wa maziwa na kileo (munsif), aina fulani ya nabidhi mbichi (fadhikh), pamoja na vinywaji vingine vya mvinyo vitokanavyo na ngano na mahindi. [7] Wataalamu wa sheria za Kiislamu (Mafakihi) wanamweka mnywaji pombe katika orodha ya mafasiki (Fasiq) [8] na wanaamini kuwa hana sifa za kuaminika katika masuala yanayohitaji uadilifu, kama vile kutoa ushahidi mahakamani. [9] Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya Hadithi, unywaji wa pombe hauruhusiwi hata katika hali ya dharura ya kuficha imani (Takiya) kwa ajili ya kuepukana na hatari inayomkabili (kama vile kukhofia kwamba iwapo hatokunywa pombe basi atatambulikana msimamo wa imani yake). [10] Muhaqqiq al-Bahrani, mwanazuoni wa Kishia wa karne ya 12 (Hijri), alieleza kuwa haijuzu kumpa Zaka mnywaji wa pombe. [11] Naye Sahib al-Jawahir, mwanasheria wa karne ya 13, akirejelea Hadithi mbalimbali, [12] alisisitiza karaha ya kuoa mtu mwovu, akibainisha kuwa kwa mnywaji wa pombe, jambo hili ni zito zaidi; kwani kosa la kuoana naye ni sawa na kosa la kukata undugu na mawasiliano na jamaa wa damu. [13] Makemeo ya Unyaji Pombe Ndani ya Vyanzo vya Hadithi Unywaji wa pombe unalaaniwa vikali ndani Hadithi mbalimbali zilizonukuliwa kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w). Moja nukuu inasema kwamba, mnywaji pombe hakubaliwi Sala zake kwa muda wa siku 40, na tendo hilo ni baya mno kuliko hata kuacha Sala. Kijamii, imeagizwa kutomsalimu, kutomtembelea akiwa mgonjwa, wala kushiriki mazishi yake. [14] Halikadhalika, mnywaji wa mvinyo ameshabihishwa na Kafiri na Mwabudu masanamu), pia imetamkwa kuwa mtu huyo ameharamishwa kupata Shufaa (Uombezi) na kuingia Peponi. Katika nyanja ya mahusiano ya kijamii pia, imepokewa kuwa haijuzu kwa muumini kutolea salamu mnywaji pombe, kumdaukia (kumzuru) wakati wa kuugua, wala kushiriki katika maziko yake (kusindikiza jeneza lake). [15] Muda na Namna ya Kutangazwa Uharamu wa Mvinyo Ndani ya Uislamu Makala Asili: Kuharamishwa Unyaji Pombe Kuna mitazamo miwili tofauti kuhusu wakati na utaratibu uliotumika katika kutangaza hukumu ya uharamu wa mvinyo: "Uharamu wa Ghafla" na "Uharamu wa Hatua kwa Hatua." Kiini na nukta kuu ya tofauti hiyo inatokana na namna ya kuzitambua Aya zilizokuja kuzungumzia uharamu huo, na kwamba je Aya hizo ni za Kimakki (zilizoshuka mjini Makka) [16] au za Kimadini (zilizoshuka mjini Madina). [17] • Kwa mujibu wa maoni ya mtazamo wa kwanza, uharamu wa mvinyo ulitangazwa jijini Makka mara moja na bila ya kutumia mfumo wa hatua kwa hatua. Wanaounga mkono hoja hii wanarejelea Aya za Qur'ani zilizoshuka mjini Makka, [18] Hadithi, [19] ushahidi wa kihistoria, [20] pamoja na hoja za kimantiki (akili). [21] • Mtazamo wa pili unaeleza kuwa uharamu wa mvinyo ulifanyika kwa njia ya hatua kwa hatua na kwa awamu mbalimbali. Mtazamo huu ndiwo unakubaliwa na Ahlus-Sunnah pamoja na baadhi ya wasomi wa Kishia. [22] Katika kutetea hoja hii, Ahlus-Sunnah wanatumia Aya za Qur'ani, [23] sera ya Uislamu ya utungaji sheria kwa njia ya hatua kwa hatua, [24] na hoja ya kulinda heshima ya Masahaba. [25] Falsafa ya Uharamu wa Mvinyo kwa Mtazamo wa Kiislamu Katika kutoa jibu kwa mmoja wa madaktari kutoka Uswidi (Sweden) aliyehoji kuhusu hekima iliyojificha nyuma ya katazo la pombe, Ayatullah Borujerdi alifafanua ifuatavyo: "Tofauti ya msingi kati ya mwanadamu na mnyama ni akili, na kileo ni adui wa akili. Kwa kuwa nafsi ya mwanadamu ina tabia ya kutotosheka na kila siku kutaka ziada ya zaidi na zaidi; hivyo basi akinywa kijiko kimoja leo, kesho kiasi hicho kitaongezeka na kuwa vijiko viwili. Hatimaye, atajikuta akibugia chupa nzima." [26] Kuna Riwaya kadhaa katika vyanzo vya Kiislamu zinazotoa ufafanuzi wa kifalsafa na kibaolojia kuhusu uharamu wa kunywa pombe. Ufafanuzi huo umetolea kupitia vigezo vifuatavyo: • Athari ya Kiroho: Unywaji pombe huondoa mng'ao wa kiroho na sifa ya uungwana (muruwwa) ndani ya nafsi ya mnywaji wake. [27] • Athari ya Kifiziolojia: Hupelekea kutokea kwa maradhi ya neva yanayodhihirika kama mitetemo ya mwili. [28] • Athari ya Kisaikolojia: Huondoa vizuizi vya kimaadili, hivyo kumfanya mhusika wake kuwa na jeuri ya kukiuka miiko ya kidini na kijamii. [29] • Athari ya Kijamii: Huongeza uwezekano wa kutokea kwa jinai nzito kama mauaji na ufuska ndani ya jamii mbalimbali. [30] • Athari ya Kiakili: Husababisha mmomonyoko na kuondoa umakini wa akili (intellect), ambao ndiyo sifa kuu inayomtofautisha mwanadamu na mnyama. [31] Haddi (Adhabu) ya Kosa la Kunywa Pombe Utekelezaji wa adhabu ya unywaji pombe (Haddi) katika mfumo wa kisheria wa Kiislamu hutegemea kutimia kwa masharti mahususi kwa mhusika wa tendo hilo. Masharti msingi ya kutekeleza adhabu hiyo ni kwamba, mtendaji wake awe amefikia umri wa balehe, mwenye akili timamu, na mwenye kufahamu fika kwamba unywaji wa pombe ni haramu kisheria. [32] Kwa mujibu wa vyanzo vya kisheria, adhabu iliyowekwa kisheria kwa mhalifu huyu ni viboko themanini. [33] Muhaqqiq al-Ardabili, mwanazuoni mashuhuri wa karne ya kumi Hijiria, amebainisha kwamba, hukumu hii ni suala la mwafaka wa jumla (ijmai) miongoni mwa mafaqihi wa Kishia. [34] Kisheria (kulingana na sheria za fiqhi), kosa la unywaji pombe huthibitika kupitia njia mbili kuu: kukiri kwa mhusika mara mbili au ushahidi unaotolewa kupitia wanaume wawili waadilifu. [35] Hata hivyo, ikiwa mkosaji atatubu kabla ya mashahidi kutoa ushahidi wao, mhusika huyo hufutwa adhabu hiyo ya kisheria (haddi); ila toba inayofanyika baada ya ushahidi kutolewa, huwa haina nguvu ya kuzuia adhabu inayotaka kutolewa dhidi yake. [36] Aidha, mafaqihi wanasisitiza kuwa utekelezaji wa adhabu unabidi kusubiri hadi mhusika awe amezinduka na kuishiwa na ulevi wake. [37] Kwa upande wa wahalifu sugu, sheria inaelekeza kuwa, ikiwa mtu atapewa adhabu ya haddi mara mbili kufuatia kosa hilo alilolikariri mara mbili tofauti, katika mara ya tatu hukumu yake huwa ni kifo. [38] Hata hivyo, ikiwa mtu amekunywa pombe mara kadhaa bila kupewa adhabu katikati yake, huwa inatosha kumuadhibu kwa haddi (adhabu) moja kwa ajili ya makosa yake yote ya unywaji pombe. [39] Hatimaye, sheria inasema; hakuna adhabu inayotolewa kwa unywaji pombe uloifanyika kwa lengo la kunusuru maisha au kutibu ugonjwa sugu. [40]