Mkopo:Tajwidi
Tajwidi: ni taaluma maalumu inayoshughulikia matamshi sahihi ya herufi za Qur’ani. Lengo la fani hii ni kuhakikisha kuwa kila herufi inatamkwa kwa ukamilifu wake, na kwa kuzingatia makhraj yake (eneo la kinya itokako herufi hiyo), pamoja na sifa zake maalumu. Istilahi ya “tajwidi” haikuwepo katika maandiko ya awali ya elimu hii, na matumizi yake yalijitokeza baadaye katika baadhi ya kazi za kielimu za fani hiyo. Miongoni mwa kazi andishi zilizotumia istilahi hii, ni kitabu kiitwacho as-Sab‘atu fi al-Qiraa’aat cha Ibn Mujaahid na at-Tanbīh cha Ali bin Ja‘far Sa‘idi. Pamoja na kwamba elimu ya tajwidi hapo awali ilijitokeza kwa namna iliyotawanyika ndani ya maandiko ya vitabu vya fani ya qiraa’at (elimu ya usomaji wa Qur’ani), ila kuanzia karne ya nne Hijria elimu hii ilianza kujengeka na kutambuliwa kama fani kamili inayojitegemea kielimu. Kuna mada kuu kadhaa zinazojadiliwa dani ya taaluma hii, ikiwemo; uchambuzi wa makhraj (eneo la kinywa zitokapo herufi za Qur’ani), sifa za herufi, hukumu za nuni saakina na miim saakina, hukumu zinazohusiana na laam, masuala ya madd na qasr (uvutaji na ukataji wa herufi), kanuni za waqfu na ibtidaa (namna ya kuanza na kusimama), pamoja na vipengele vya ghunna (naghama) na qalqala (ugongaji unaohusiana na baadhi ya herufi). Kazi za mwanzo kabisa zilizoandikwa kwa namna ya kujitegemea kuhusiana na fani ya tajwidi ni; shairi la Abu Muzahim Khaqani, kitabu ar-Riaa’ya li-Tajwīd al-Qiraa’a cha Makki bin Abi Talib, pamoja na at-Tahdiid cha Abu Amr al-Dani. Kwa mujibu wa misingi ya fiqhi ya ibada, wajibu wa kuzingatia tajwidi katika Sala unategemea athari ya kimaana inayotokana na matamshi na lafudhi ya kisomo cha Qur’ani kisomwacho ndani ya Sala. Kwa msingi huo, endapo kutozingatia baadhi ya hukumu za tajwidi hakutabadilishi maana ya matamshi ya Akisomo hicho, basi hakutakuwa na ulazima wa kisheria wa kuizingatia kanuni hizo za elimu ya tajwidi. Aidha, wanazuoni wametoa fatwa ya ulazima wa kufwata misingi ya tajwidi katika dhikri zinazohusiana na ibada ya hija, hasa katika talbiya. Ufafanuzi na Umuhimu wa Fani ya Tajwidi Kwa mujibu wa istilahi za taaluma ya Qurani, tajwidi ni nidhamu inayohusiana na utamkaji sahihi wa herufi za Qurani kwa misingi ya kifonolojia uhalisia wake, kwa kuzingatia mahali pa kutokea herufi (makhraj) na sifa zake za matamshi yake. Aidha, utekelezaji wa tajwidi unasisitizwa kufanywa kwa kiwango cha wastani, bila kupindukia, ili kuhakikisha usomaji ulio sahihi, fasaha, na wenye mvuto wa kisanaa. [1] Kwa mujibu wa tafiti zilizopo, yaonekana kwamba hakuna neno hata moja lenye mizizi ya neno tajwidi lililotumika katika shairi la Khaqaaniyya linalohusishwa na Abu Muzahim (aliyefariki mwaka 325 H). Kazi ambayo hutambuliwa kama kazi ya kwanza huru katika taaluma ya tajwidi. Neno la kwanza kabisa kutumika kwa maana inayojulikana leo, lilionekana katika kitabu kiitwacho Al-Sabʿatu fī al-Qiraaʾāt, kilichoandikwa na Ibn Mujahid (aliyefariki mwaka 324 H). Baada yake, mtu wa pili kutumia neno tajwidi kwa maana ya kiistilahi kama ilivyo hivi sasa, ni Ali ibn Jaʿfar Saʿidi (aliyefariki takriban mwaka 410 H), ambaye alitumia istilahi hiyo katika kitabu chake Al-Tanbih Alaa al-Lahni al-Jaliyyi wa al-Lahni al-Fakhiyyi. [2] Kabla ya fani ya tajwidi kutambulika kama elimu inayojitegemea, wakati mwingine maudhui zake zilielezwa na kufafanuliwa katika elimu ya qiraaʾaat (fani ya visomo), na wakati mwingine katika vitabu vya lugha. Pamoja na hayo, kuanzia karne ya nne Hijria, fani ya tajwidi ilitambuliwa kama elimu huru ianyojitegemea. [3] Baadhi ya mada zinazojadiliwa katika elimu ya tajwidi ni: mahali pa kutokea herufi na sifa zake, kanuni za nuun saakina na tanwini, kanuni za miim saakina, kanuni za laam, madd (uvutaji wa herufi) na qasr (ukataji wa herufi), waqf (vituo vya kusimama na kupumzika katika kisomo) na ibtidaa (vituo vya kuanzia kisomo), pamoja na ghunna (naghama) na qalqala (ugongaji wa herufi). [4] Vitabu vya Mwanzo vya Elimu ya Tajwidi Kabla ya kuibuka kwa vitabu huru vinavyoshughulikia tajwidi ya Qurani, maudhui za elimu hii zilijitokeza kwa njia isiyo ya moja kwa moja ndani ya vitabu vya elimu ya qiraa’aat (elimu ya visomo vya Qur’ani). [5] Hata hivyo, katika hatua za baadaye, kazi mahsusi katika taaluma ya tajwidi zilianza kuandikwa, zikiwemo: 1. Shairi la Abu Muzahim al-Khaaqaani la Abu Muzahim al-Khaaqaani (Aliyefariki mwaka 325 H). Kwa mujibu wa Abdulaziz Abdulfattah shairi hili hutajwa kuwa maandishi ya kwanza huru na ya kale zaidi kuhusu fani ya tajwidi, yaliyotungwa katika karne ya nne Hijria. [6] 2. Umdat al‑Mufid wa Uddat al‑Majid fi Maʿarifat al‑Tajwid, shairi la Ilmu al‑Dīn al‑Sakhawi (w. 643 H). [7] 3. Al‑Riʿayatu li‑Tajwid al‑Qiraʾa wa Tahqiq Lafdh al‑Tilawa, cha Makki ibn Abi Talib al‑Qaysi al-Qayrawani al-Qurtubi (aliyefariki 437 H), ambacho kinahesabiwa kuwa ni rejea kuu miongoni mwa kazi za wanazuoni wa awali na miongoni mwa vitabu vya kina zaidi katika taaluma ya tajwidi. [8] 4. Al‑Tahdīid fī al‑Itqan wa al‑Tajwīd cha Abu Amr al‑Dani (aliyefariki 444 H), kilichoandikwa karibu na kipindi cha kitabu kilichotangulia, cha Makki ibn Abi Talib vitabu viwili hivi vinachukuliwa kuwa ni miongoni mwa vitabu vya kale zaidi vya fani ya tajwidi. [9] Mizatamo ya Kifiqhi Kuhusu Fani ya Tajwidi Kwa maoni ya wanazuoni, ni lazima (wajibu) Sala kusaliwa kwa kutumia lugha sahihi ya Kiarabu kilicho fasaha. [10] Hata hivyo, kiwango tosha kinachozingatiwa kuhusiana na utumiaji wa fani ya tajwidi, ni kile kiwango kichadhamini usalama wa maana za lafudhi zitamkwazo ndani ya Sala, hii ina maana ya kwamba, si lazima mtu kuchunga sheria za tajwidi kiukamilifu kama ilivyo katika sheria zinazozingatiwa na wasomaji wa Qur’ani duniani. [11] Kwa mtazamo wa wanazuoni wa madhehebu ya Ahlu al-Sunna, si wajibu mtu kuchunga hukumu za tajwidi katika Sala, iwapo jambo litamsababishia mwenye kusali ugumu wa kutekeleza Sala zake. Hii inamaanisha kwamba, kufanya hivyo huwa ni wajibu wa yule mwenye uwezo kamili wa kuchunga sheria za tajwidi bila ya vikwazo. Kwa hiyo wanazuoni wa Kisunni hawaoni kuwepo ulazima (wajibu) wa kuchunga sheria za matamshi pambanuzi yanayopambanua dhaad (ض) na dhee (ظ). [12] Kwa mujibu wa fatwa za wanazuoni, hata talbya (labbaika Allaahuma labbaika), ambayo ni moja ya amali za hija, pia nayo yatakiwa (ni wajibu) kusomwa kwa ushahihi au kwa kuzingwatia sheria za fani ya tajwidi. [13] Mada zinazofungamana: • Elmu al-Qira’aat • Kisomo cha Sala