Nenda kwa yaliyomo

Mkopo:Mwenendo wa wenye busara

Kutoka wikishia

Mwenendo wa wenye busara (Siratu al-Uqalaa/سیره العُقلاء), unaofahamika pia kama kawaida au taratibu za watu wenye akili, unarejelea tabia na makubaliano ya kivitendo ambayo watu wamezoea kuyafuata katika utendaji au kutotenda jambo fulani. Dhana hii (Siratu al-Uqalaa/سیره العُقلاء) ni istilahi maalumu inayotumika kwa upana mkubwa katika fikihi na misingi yake (Usul al-Fiqh), ambapo masuala mengi ya kisheria—hususan yale yanayohusu miamala na mahusiano ya kijamii—huthibitishwa kwayo. Ndani ya elimu ya misingi ya fikihi (Usul al-Fiqh), mjadala mkuu hujikita katika kubainisha masharti yanayofanya mwenendo huo uwe na nguvu ya kisheria na ushahidi unaokubalika (hujjiya) katika uwanja wa sheria. Kwa upande mwingine, mwenendo huu wenyewe hutumika kama dalili ya kuthibiti uhalali wa mambo mengine ya kimsingi, kama vile kukubali habari zinazoletwa na mtu mmoja mwaminifu na kutegemea maana ya nje ya maneno. Ili mwenendo huu uweze kutumika kama ushahidi kamili wa kisheria, ni sharti uambatane na kile kinachoitwa uidhinishaji wa Mwenye Sharia. Hii ina maana kuwa, ni lazima ithibitike kwamba hakuna katazo, kizuizi, wala kipingamizi chochote kilichotolewa na Mwenye Ezi Mungu au Mtume Wake dhidi ya mwenendo huo wa watu. Kimsingi ikiwa jambo fulani lilikuwa likifanyika mbele ya Macho ya Maasumu bila wao kulizuia, ukimya huo unatafsiriwa kama ridhaa na muhuri wa kisheria wa kuidhinisha. Mwenendo wa wenye busara hutumika pia katika kuchambua na kuweka wazi kiini cha maudhui ya hukumu za kisheria. Jambo hili hudhihirika pale ambapo hukumu inakuwa imeshathibiti kupitia Qur'ani, Sunna, au vyanzo vinginevyo, ilhali kile kinacholengwa na hukumu hiyo kikiwa bado kimesalia katika hali ya utatanishi au kutoonekana wazi mbele ya wahusika wanaotakiwa kuitekeleza hukumu hiyo. Katika mazingira kama haya, kawaida ya watu wenye akili huwa ndiyo nyenzo muhimu ya kupambanua na kufafanua maudhui hayo. Mathalani, sheria inapobainisha kuwa "vifaa vya kamari ni haramu," ni mwenendo wa wenye busara ama mila na desturi zao ndizo zinazotoa tafsiri ya kile kinachostahiki kuitwa kifaa cha kamari kulingana na uhalisia wa jamii zilizoishi katika zama za wafasiri wa sheria. Kwa upande wa mwenendo wa wenye busara uliozuka baada ya kupita kwa zama za Maasumu (a.s), utaratibu huo kisheria hunajulikana kama busara za mwenendo mamboleo (siratu al-mustahdatha / sira mpya zilizobuniwa). Kumekuwa na hitilafu za kimitazamo miongoni mwa wanazuoni kuhusiana na mwenendo huu kuweza kutumika kama ushahidi kamilifu katika miktadha ya kisheria. Wanazuoni wa Misingi ya Sheria (Usul al-Fiq’hi) wameainisha njia maalumu za kutambua uhalali wa desturi za wenye akili, ziwe ni zile zilizokuwepo wakati wa Maasumu au nyakati nyinginezo. Aidha, wamebainisha mbinu za kuhakikisha kuwa Mwenye Sheria (Mungu) hajakataza desturi hizo za kiakili. Dhana na Nafasi Yake Dhana ya mwenendo wa wenye busara (au Sira al-Uqalaa) inafafanuliwa kwa maana ya mazoea ya watu na makubaliano yao ya kivitendo katika kutekeleza au kuacha jambo fulani. [1] Katika taaluma ya sheria, dhana hii mara nyingine hujulikana kwa jina la "misingi ya wenye akili" (Bina al-Uqala) au "mwenendo wa watu". [2] Uhalali na nguvu ya kisheria (hujjiya) ya mwenendo wa wenye akili, ni moja ya mada muhimu na yenye uzito mkubwa mno ndani ya elimu ya misingi ya fikihi (Usul al-Fiqh). [3] Hii ni kwa sababu mwenendo wa wenye busara ni nguzo muhimu inayotumika kama kigezo cha kuthibiti na kuhalalisha misingi mbalimbali ya kisheria (fiqhi). Miongoni mwa kanuni kuu zinazotegemea mwenendo huu ni: • Kanuni ya kutodhuru (La Dharar), inayokataza madhara katika jamii. [4] • Kanuni ya kuondoa uzito na kizuizi (Nafyu al-Haraj), inayolenga kurahisisha mambo pale panapokuwa na ugumu uliopitiliza. [5] • Kanuni ya uadilifu na usawa (Adlu wa al-Insaf), inayosisitiza haki katika mahusiano ya kibinadamu. [6] • Kanuni ya kuzuia udanganyifu (Gharar), inayohakikisha uwazi katika miamala na biashara. [7] Mirza al-Na'ini anabainisha kuwa mwenendo na misingi ya watu wenye busara ni miongoni mwa dalili kuu zinazothibitisha uhalali wa ithibati inayotegemea habari ya mtu mmoja mwaminifu (Khabar Wahid). Kwa hakika, hata kama itatokea kupatikana kwa dosari au mjadala katika ushahidi mwingine unaotumika katika kutetea jambo hili (Khabar Wahid), bado hakuna nafasi ya kupinga kawaida ya wenye akili ya kutegemea habari ya mtu mmoja mwamionifu. Hii ni kwa sababu, katika mfumo wa maisha yao ya kila siku, daima watu wenye busara huonkekana kutegemea na kuamini habari zinazoletwa na watu waaminifu. [8] Tofauti Baina Mwenendo wa Wenye Busara na Urfu (Nyenendo za Jamii) Baadhi ya wanazuoni wamezifasiri istilahi za "Urfu", "Sira", na "Sira al-Uqala" zinavyotumika katika maandiko ya mafaqihi na wanazuoni wa fani ya usul al-fiqhi kwa maana moja (visawe vilivyoko chini ya dhana moja). [9] Hata hivyo, kuna kundi la wanazuoni lililotofautisha maneno hayo na kutoa maana maalumu kwa kila moja kati yake. Malezo kuhusiana na tofauti zake ni kama ifuatavyo: Makala Asili: Urfu Katika kubainisha tofauti iliyopo kati ya mila (urfu) na mwenendo wa wenye busara, baadhi ya wahakiki wameeleza kuwa mwenendo wa wenye busara unahusu tu mienendo na tabia zinazochipuka kutokana na mantiki ya kiakili. Hali ni tofauti kwa upande wa mila, kwani yenyewe haina ulazima wa kutegemea akili pekee; bali inaweza pia kupatika kutokana na mazoea ya kufuata mkumbo, kuigana, au tabia, ada na ya wanajamii. [10] Vilevile, imeelezwa kuwa mila ina upana mkubwa zaidi kuliko mwenendo wa wenye busara. Hii inatokana na ukweli kwamba, mwenendo wa wenye busara unajikita zaidi kwenye vitendo, ilhali mila inavuka mipaka hiyo na kuendelea mbele ikihusisha vitendo, kauli, pamoja na uamuzi wa kuacha kufanya jambo fulani. [11] Hata hivyo, wanazuoni wengi wa misingi ya fikihi (usulu al-fiqhi) wanaufananisha mwenendo wa wenye busara na mila ya kijumla (urfu aam), wakiamini kuwa mwenendo wa wenye busara ni sawa na ule utaratibu unaokubalika na kufuatwa na watu wote au sehemu kubwa ya jamii. [12] Akhond Khurasani anasema: Tangu asili na jadi, imekuwa ni kawaida na desturi iliyokubalika na watu wote wenye busara—wawe ni wafuasi wa dini fulani au wasio na dini—kuitegemea na kuifanyia kazi habari inayotolewa na mtu mwaminifu. Mwenendo huu haukuishia katika zama za kale tu (nyakati za kuwepo kwa Mitume na Mimamu), bali ulistawi na kuendelea tokea wakati wa uhai wa Mimamizi wa Sharia (Mitume na Maimamu) na ukadumu kwa mnyororo uleule hadi katika zama zetu hizi. Jambo la kimsingi ni kuwa, hakuna ushahidi wowote wa katazo, kizuizi, wala kipingamizi kilichowahi kutolewa na Mtume (s.a.w.w) wala Maimamu wa Ahlu al-Bait (a.s) dhidi ya utaratibu huu wa kijamii. Na lau Mwenye Sharia asingekuwa na ridhaa na kawaida hiyo, basi angepaswa kutoa katazo la wazi kabisa; na kwa kuwa mwenendo huo ulikuwa umekita mizizi katika maisha ya watu, katazo hilo lingekuwa maarufu na kuenea kwa mapana na marefu. Hivyo basi, kutokuwepo kwa pingamizi lolote dhidi yake ni thibitisho tosha kuwa Mwenye Sharia anaridhia na kukubali kikamilifu utegemeaji wa habari ya mtu mmoja mwaminifu katika kuainisha na kutekeleza mambo ya kisheria na kidini. (Kitabu: Kifayatu Al-Usul cha Akhond Kuharani, juz. 2, uk. 80). Tofauti Kati ya Mwenendo wa Wenye Busara na Hisia za Ndani za Kiakili (Irtikaz) Katika kupambanua kati ya mwenendo wa wenye busara na hisia (kanuni na hukumu) ya ndani ya kiakili (irtikaz), wasomi wanabainisha kuwa, mwenendo wa wenye busara unahusu matendo ya nje na tabia dhahiri za kufanya au kuacha jambo fulani. Kinyume chake, hisia (kanuni na hukumu) ya ndani (irtikaz) haifungamani na utekelezaji wa nje; bali ni mfumo wa kifikra na uelewa uliokita ndani ya akili za watu wenye busara, hata kama haujadhihirika kivitendo. [13] Hali kadhalika, hisia ya ndani ya kiakili inatazamwa kwa uzito na kupewa thamani kubwa zaidi kisheria kuliko mwenendo wa nje. Hii ni kwa sababu mara nyingi chimbuko la hisia hizo ni umbile asilia la mwanadamu (fitra), akili tendaji, na miongozo ya Mitume pamoja na mawasii wao. Kwa upande mwingine, wakati mwingine mwenendo wa nje wa watu, unaweza kuwa ni matokeo ya kuigana tu au kufuata mazoea ya wengine baada ya kuwashuhudia wakifanya hivyo, jambo ambalo linaweza lisiwe na misingi thabiti ya kiakili. [14]

Tofauti Kati ya Mwenendo wa Wenye Busara na Mwenendo wa Washika Dini Makala Asili: Mwenendo wa Washika Dini / Siratu Al-Mutasharri’ah Katika upambanuzi kati ya mwenendo wa washika dini na mwenendo wa wenye busara imeelezwa kwamba, mwenendo wa washika dini (Siratu al-Mutasharri’a) unatazamwa kuwa na upeo finyu na mahususi zaidi ukilinganishwa na mwenendo wa wenye busara; kwani mwendendo wa washika dini unahusiana tu na mazoea au makubaliano ya Waislamu katika kutenda au kuacha jambo fulani. [15] Kuhusu tofauti ya nguvu ya kisheria (hujjiyya) kati ya dhana mbili hizi, wasomi wanabainisha kuwa, pindi mwenendo wa washika dini unapothibiti, wenyewe huwa unatosheleza kusimama na kutumika kama dalili ya moja kwa moja ya hukumu ya kisheria. Hata hivyo, mwenendo wa wenye busara hauchukuliwi kuwa na uzito huo wa kisheria, isipokuwa tu pale unapopata uidhinishaji na baraka za Maasumu, au pindi inapothibitika kuwa hapakuwa na katazo wala kipingamizi chochote kutoka kwa viongozi hao watukufu dhidi ya mwenendo huo. [16] Hali kadhalika, mtafiti wa fikihi na mwalimu katika chuo cha Qom, Abolqasem Alidust, anafafanua kuwa, kwa kawaida pale neno "sira" linapotajwa bila kuambatanishwa na sifa nyingine, humaanisha mwenendo wa wenye busara. [17] Upeo wa Matumizi ya “Mwenendo wa Wenye Busara / Akli” Katika Fiqhi na Misingi Yake Kuna aina mbili za ufafanuzi zilizotolewa kuhusiana na upeo wa matumizi ya “mwenendo wa wenye busara” katika nyanja za fiqhi na usulu al-fiqhi. Kwanza kabisa, mwenendo huu wenyewe unatazamwa kama suala la kimsingi la kiusuli (usulu al-fiqhi); hii ni kwa sababu ya kwamba, dhana hii yenye husimama kama nguzo inayotegemewa kwa mapana katika milango mbalimbali ya fani ya fikihi, hasa ile inayohusiana na miamala na mahusiano ya kijamii. Hivyo basi, katika elimu ya misingi ya fikihi, wataalamu hujadili kwa kina kuhusu nguvu yake ya kisheria (hujjiyya) na kuainisha masharti yanayopaswa kutimia ili msingi huu uweze kutumika kama dalili ya kutegemewa katika upatuaji wa hukumu za kidini. [18] Pili, mwenendo huu hutumika kama msingi imara wa kuthibitisha uhalali wa misingi mingine muhimu ndani ya elimu ya misingi ya fikihi (usulu al-fiqhi). Mfano wa masuala hayo ni msingi wa kutegemea maana ya nje ya maneno (dhawahir), pamoja na kukubali habari ya mtu mmoja mwaminifu (khabar al-thiqa). Mambo haya yanatambulika kama viashiria vikuu vya kisheria (amara), ambavyo ni nyenzo zilizoziridhiwa na Mwenye Sharia ili kumwezesha mtafiti wa sheria kugundua na kufikia hukumu sahihi za kidini. [19]

Vigao vya Nyenendo za Wenye Busara na Vigezo vya Ukubalikaji Wake Mwenendo wa wenye busara umegawanyika katika sehemu kuu mbili, huku kila moja ikiwa na kigezo chake cha kipekee katika ukubalikaji wake kisheria. 1. Mwenendo Unaothibitisha Hukumu ya Kisheria Aina ya kwanza ya nyenendo za wenye busara, ni ule mwenendo ambao hutumika kama dalili ya kuthibitisha hukumu fulani ya kisheria. Katika aina hii ya nyenendo, tabia na makubaliano ya watu wenye akili ndiyo yanayotumika kama msingi wa kuanzisha uhalali wa jambo fulani kisheria. [21] Kwa mfano, Imam Khomeini alitegemea aina hii ya mwenendo kuthibitisha kanuni ya umiliki kupitia uwekaji mikono au ukamataji wa rasilimali (hiyazat) fulani. Akiielezea dhana hii anasema kwamba, tangu kuchomoza kwa ustaarabu wa mwanadamu, kumekuwa na mwenendo wa yakini na usiopingika kuwa, umiliki unapatikana kwa njia ya kuhuisha ardhi au kuchukua rasilimali zisizo na mmiliki na kuziingiza ndani ya milki yake. Imamu Khomeini anasisitiza kuwa, katika historia yote, hakuna Nabii, wasii, wala muumini yeyote aliyewahi kuukataa au kuuzuia utaratibu huo. [22] Hata hivyo, wanazuoni wa misingi ya fikihi (usulu al-fiqhi) wanasisitiza kuwa, ili aina hii ya mwenendo iwe na nguvu ya kisheria na iweze kutumika kama ushahidi, ni lazima ithibitike kuwa imepata uidhinishaji, na ridhaa ya Mwenye Sharia (Mungu). Bila ridhaa hiyo kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu au Mtume Wake, mazoea ya watu pekee hayawezi kugeuka kuwa hukumu ya kidini. [23] Mwenendo wa Wenye Busara Wenye Kuangaza Hukumu ya Kisheria Wakati mwengine, mwenendo wa wenye busara (akili) huwa ni kama mwanga au tochi inayowaangazo kihisikacho na hukumu fulani ya kisehria. Hii ni pale ambapo hukumu fulani huwa tayari imeshathiti kupitia Kitabu cha Mungu, Sunna au njia nyengine za kisheria. Katika hali kama hiyo, mwenendo wa wenye busara huwa ni nyenzo ng’amuzi, inayong’amua mahali na mifano ya vile vyenye kumiminikiwa (vihusikavyo) na hukumu hiyo. [24] Kwa mfano; sheria imeharamisha matumizi na mauzaji ya ala (nyenzo). Katika mfano huu, sira (mwenendo) wa wenye busara au mila za wanajamii (urfu), huwa ni tochi na mwenge wa kumurikia zile nyenzo zinazoweza kuingia ndani ya kivuli cha hukumu hiyo. Jambo ambalo hung’amua ufahamu wa jamii juu ya nyenzo hizo. [25] Pia wanazuoni wanaeleza kwamba, sira (mwenendo) wa wenye busara au mila za wanajamii (urfu), ni moja ya njia saidizi zinazoweza kuleta pamabazuko la kimaarifa katika kuelewa madhumuni na makusudio ya hukumu fulani. [26] Miongoni mwa mifano hai ya kipengele hichi, ni ile Hadithi iliyokuja kuhusiana na masuala ya mimala ya kibiashara. Hadithi hii inasema, iwapo mfanya biashara (muuzaji) atamuuzia mshitiri wake bidhaa fulani bila ya kupokea malipo ya bidhaa hiyo, na pia bila ya kuikabidhi bidhaa hiyo kwa mshitiri huyo. Katika hali hiyo, mshitiri huyo antakiwa kutoa malipo ya bidhaa hiyo kwa kipindi kisichozidi siku tatu, na kipindi hicho ndicho kinachodhamini ukamilikaji wa muamala huo, na iwapo atachelewa na kukaa zaidi siku tatu bila ya kulipa tahamani ya bidhaa hiyo, hapo hapatakuwa na muala kati yao. [27] Kidhahiri Hadithi hii inashiria kubatilika kwa muamala husika. Ila tukirudi kwenye nyenendo za wenye busara na hisia (kanuni na hukumu) za ndani za kiakili za wenye busara hao (irtikaz), tutaona kwamba, kinachokusudiwa hapo ni uwezekano wa kurefuka kwa kipindi cha muamala huo, na kuwepo kwa hiari ya wahusika hao katika kuendelea au kutoendelea na muamala wao. [28] Emeelezwa kwamba, hakuna haja ya kutafuta idhini ya Mwenye sheria (Mungu), ili kuthibitisha aina kama hii ya nyenendo za wenye busara, ambayo hutumika kama nyenzo tu ya kumurika na kuipambazua zaidi hukumu fukani ya kisheria. [29] Ufafanuzi wa Sayyid Murtadha Fiiruz-Aabaadi: Nyenendo za wenye busara, nia miongoni mwa hoja zinazotumika kama ithibati ya kuthibitisha dhana ya istishab (kuegemea kwenye welewa wa mwanzo au uliotangulia, katika hali ya kuwa na shaka juu ya kuwepo kwa hali (hukumu) mpya). Hii ni kwa maana ya kwamba; matendo yote ya wenye busara yanaonekana kutegemea kwenye welewa na hukumu zilizotangulia kabla yake…. Na kama hii haitachukua mkondo wake ndani ya jamii, mfumo wa maisha ya wanaadamu utaparaganyika na kukabiliwa na vizingiti mbalimbali. Husseini Firuza-Aabaadi, Kitabu: Ghayatu al-Usul fi Sharhi Kifayati al-Usul, juz. 5, uk. 32, mwaka 1400 Hijiria. Vigao vya Nyenendo za Wenye Busara Kwa Mujibu wa Chimbuko Lake Nyenendo za wenye busara kulingana na chimbuko lake imegawika kwa vigao vifuatavyo: [30] • Nyenendo za wenye busara zinazotokana na hukumu za kiakili za kimaadili, [31] kama vile nyenendo za kukanusha na kukataa dhulma na kuunga mkono uadilifu, au nyenendo za wenye busara katika dhana ya mjinga kumfuata mwerevu. [32] Imeelezwa kwamba, ithibati ya nyendo hizo ni zenye kujitegemea zenyewe na wala hazihitaji kuthibishwa na ridhaa ya Mwenye sharia (Mungu). Hii ni kutokana na kwamba, nyenendo hizi zinatokana na hukumu za kiakili (mantiki salama). [33] • Nyenendo za wenye busara zinazotokana na hisia, naumbile (fitra), zinazoshuhudiwa katika hali mbalimbali, zinazothibiti kupitia majaribio pamoja na zile zinazothibiti kupitia njia ya ulinganishi. [34] Nyingi miongoni mwa nyenendo za wenye busara zinahusiana na aina hii ya nyenendo. [35] Wanazuoni wanasema kwamba, ni lazima aina hii ya nyenendo ipate uhalali wake kutoka kwa Mwenye sharia mwenyewe (Mungu). [36] Nyenendo za Wenye Busara za Katika Zama za Maasumina (A.S) na Zilizozuka Baada Yao Maana ya nyenendo zilizozuka (Siratu al-Mustahdathah), ni zile zilizokuja katika kipindi cha kutowepo kwa Maasumina (a.s), ambapo kinyume chake ni zile nyenendo zilizojiri ndani ya kipindi cha Maasumina (a.s). [37] Kulingana na itikadi za wanazuoni wa fani ya misingi ya fiqhi (usulu al-fiqhi), ni kwamaba; nyenendo zote zilizotokea katika kipindi cha kutowepo kwa Maasumina, zinahitaji kupata uungwaji mkono wa Mwenye sheria (Mungu). Laa si hivyo nenendo hizo hazitaweza kupata uhalali wa kisheria wa kuweza kuthibitisha au kukanusha hukumu fulani ya kisheria. Hii inamaanisha kwamba; nyenendo hizo zinatakiwa ziwe zimepita katika zama za Maasumu huku zikipata nguvu zake kwa njia ya kutokaripiwa, au kwa kunyamaziwa bila kukatazwa wala kuungwa mkono na Maasumu huyo. [38] Wanazuoni wana mitazmo tofauti kuhusiana na nyenendo zilizotokea (kuzika) baada ya vipidi vya Maasumina (a.s). Baadhi yao wanasema kwamba; kukubalika kwa hii ya nyenendo kunahitaji dalili inayoonesha kufungamana kwake na zama za Maasumu. Na kwamba kuwepo dalili inayoonesha kwamba, nyenendo hizo pia zilikuwa zikifanyika katika za Maasumina (a.s), nao wakazinyamazia bila ya kuzikataza. [39] Baadhi ya wanazuoni hawaoni tofauti kati ya nyenendo mbili hizo. Kwa mtazamo wa wanazuoni hawa, ukubalikaji wa nyenendo za wenye busara, na ukubalikaji wake kama dalili ya kuthibitisha hukumu fulani, hauhitaji kuwepo kwa fungamno linalofungamanisha nyenendo hizo na zama za Maasumina (a.s). [40] Nija za Kuthibitisha Uwepo wa Nyenendo za Wenye Busara Zifuatazo ni miongoni mwa njia muhimu zaidi za kuthibitisha uwepo wa nyenendo za wenye busara ndani ya zama za Maasumina na nje ya zama zao: Ufafanuzi wa Imamu Khomeini: Hisia (kanuni na hukumu) za kiakili za wenye busara na nyenendo za wenye busara, ndizo dalili muhimu zaidi juu ya ulazima na wajibu wa mjinga kumfuata mwerevu na asiye na ujuzi kumfuata mwenye ujuzi. Ilimradi tu kusiwepo na makatazo ya Mwenye sheria ya kupinga nyenendo hizo. Kwa hiyo kutokuwepo kwa makaripio dhidi ya nyenendo fulani za wenye busara, kutupa welewa wa kujua kwamba nyenendo hizo ni halali na ziko chini ridhaa za Mwenye sheria (Mungu). Imamu Khomeini, Ijtihad wa Al-Taqlid, uk. 63, Chapa ya mwaka 1426 Hijiria. • Tafiti za kimeidani (Istiqraa): Wakati mwengine baada ya mtu kufuatilia na kutafiti nyenendo za wanajamii wa jamii fulani, hugundua kwamba, licha ya wao kuwa na khitilafu mbalimbali zikiwemo za kitamaduni na kimtazomo, ila bado wanaonekana kushikamana na nyenendo fulani madhubuti. Hii inaonenesha kwamba, yawezekana tukaweza kuutanua wigo wa nyenendo hizo bila ya kuweka mipaka maalumu ya wigo huo. Hivyo basi twaweza kusema kwamba, nyenendo hizo hazihusiani tu na jamii moja au mbili, bali zinahusiana na jamii zotu kwa ujumla, hata zile zilizoishi katika zama za Maasumina (a.s). [41] • Chambuzi za Kiakili (za Ndani ya Nafsi ya Mmoja Wetu): Baadhi wakati mtu hupatwa na jambo fulani ndani ya nafsi yake, na baada ya kulitafakari jambo hilo huweza kutoa hukumu fulani juu yake. Ila baada ya kutafakari zaidi, hugundua kuwa hukumu aliyoitoa ni sawa na hukumu za wanadamu wengine juu ya suala hilo, na wala haikutokana na mawazo yake yeye tu. Hapo huelewa kwamba hukumu hiyo imetoka ndani ya kiini cha akili kilichoko ndani ya kila binadamu timamu. Hii inaonesha kwamba huku aliyotoa ni kuhumu na nyenendo za wenye busara (wenye akili timamu). [42] • Dharura na Hitaji la Kijamii: Baadhi ya wakati, nyenendo za wenye busara hufungamana moja kwa moja na suala msigi ambalo miongoni mwa mahitajio ya dharura ndani ya jamii, kiasi ya kwamba kukosekana kwake hupelekea misukosuko au kupozo kwa jamii hiyo. [43] Miongoni mwa mifano yake hai, ni ule mwenendo wa kumili, unaokihisabu kilichoko mkononi mwa mtu fulani kuwa ni milki ya mtu huyo, kaida ambayo kifiqhi huitwa kaida ya Al-Yadd (Kaida ya Mkono Miliki). Na kutokuwepo kwake -hata katika zama za Maasumina- husababisha mvurugiko ndani ya jamii. [44] • Nukuu za Kihistoria: Moja ya njia za kuweza kuthibitisha kuwepo kwa nyenendo fulani za wenye busara, ni nukuu za kihistoria. [45] Tunachokusudia hapa, si kila nukuu ya kihistoria bali ni zile nukuu maalumu zenye hadhi ya kisheria, nazo ni zile zilizonukuliwa kupitia jopo kubwa la wenye kunukuu jambo hilo, au zile zilizopata msaada wa vielelezo vyengine vya kisheria vinavyoweza kuipa uzito khabari hiyo na hatimaye kujenga yakini juu ya ukweli wake. [46] Njia za Kuthibitisho Kutowepo kwa Makatazo Juu ya Nyenendo Fulani za Wenye Busara Ungiliaji wa kisheria katika kuikubali au kusimama dhidi ya nyenendo fulani za wenye busara, hutegemea uzito na umuhimu wa nyenendo hizo ndani ya jamii. [47] Hii inamaanisha kwamba, sheria inaweza kuunga mkono au kusimama dhidi ya nyenendo fulani kulingana na uzito na umuhimu wa nyenendo hizo ndani ya jamii. Zifuatazo ni njia za kuthibitisha kutowepo kwa makatazo ya kisheria dhidi ya nyenendo fulani za wenye busara: • Njia ya kwanza ya kuthibitisha kutowepo kwa katazo dhidi ya nyenendo fulani, ni kutowepo kwa Hadithi dhidi ya nyenendo hizo. Kutowepo hata Hadithi dhaifu dhidi nyenendo hizo ni dalili ya kutowepo kwa katazo dhidi yake. Pia ni dalili ya ridhaa ya Mwenye sheria ya kufikiana kwake na nyenendo hizo, kwani kama kungelikuwepo katazo fulani dhidi yake, kungeliakisiwa kupitia nukuu za watu wa jamii hizo, na hatima yake jamii zilizofuata zingeliweza kung’amua uwepo wa katazo hilo kupitia nukuu zao za kihistoria. [48] • Njia ya pili ya kuthibitisha kutowepo kwa katazo dhidi ya nyenendo fulani za wenye busara, ni kutowepo kwa njia mbadala iliyotumika katika kutatua tatizo fulani lililotatuliwa kupitia nyenendo hizo. Hii ni kuhusiana na zile nyenendo za wenye busara zilizojiri kwa ajili ya kutatua au kukabiliana na hali maalumu yenye kulazimu uwepo wa kanuni na njia ya kukabiliana na hali hiyo. Hivyo basi kutowepo kwa njia mbadala ni dalili ya kutowepo kwa katazo, kwani kama Mwenye sheria asingekubaliana na nyenendo hizo, bila shaka angeliweka njia mbadala itakayotumika kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo isiyoepupika. Hii inaonesha kwamba nyenendo hizo zilizkuwa zikiendelea bila ya pingamizi yoyote kutaka kwa Mwenye sheria (Mungu). [49] Miongoni mwa mifano hai ya nyenendo za wenye busara ulimwenguni, ni ile desturi yao ya kuyaelewa maneno na matakwa ya mtu fulani kupitia dhahiri ya maneno yake, na sio kuyapa tafsiri nyengine maneno hayo. Hili lilisimama bila kutokea njia nyengine mbadala uliotumika katika suala hilo, iliosimama dhidi ya njia hiyo ya mwanzo. Hivyo basi, kutowepo kwa njia mbadala ni picha tosha inayotupa taswira kamili ya kutowepo kwa kikwazo dhidi ya mwenendo huo ndani ya zama za Maasumina, na kwamba mwenendo huo ndiyo uliokuwa ukifuatwa hata katika zama hizo, ambazo ni zama za kuwepo kwa mawasiliano kati ya waja na Mola wao. [50]