Mkopo:Mtetenda Madhambi Makuu
Mtetenda Madhambi Makuu: Dhana ya mtenda dhabi kuu inamrejea yeyote yule aliyefanya kosa lililomo ndani ya orodha ya yale madhambi yanayochukuliwa kuwa ni makubwa katika sheria ya Kiislamu. Mzozo juu ya usalama wa imani ya mtu huyu ni miongoni mwa mivutano ya kwanza kabisa iliyojitokeza katika historia ya Kiislamu. Wanazuoni wengi wa madhehebu ya Shia Imamiyyah, kwa kuegemea ushahidi wa Qur’ani na mapokezi ya Maimamu wa Ahlul-Bait, wanaamini kuwa bado mtenda dhambi hubaki katika imani ya Kiislamu, ingawaje kisheria huhisabiwa kuwa ni miongoni mwa mafasiki (watu waovo). Aidha wanazuoni wanasisitiza kuwa kwa kuwa mhusika na muumini wa imani ya Kiislamu, hivyo basi adhabu atakayopata itakuwa ni ya muda fulani inayolingana na kosa lake, na wala hatasalia motoni milele. Kuna mgawanyiko wa kifikra katika historia ya teolojia ya Kiislamu kuhusu athari za dhambi kuu katika kuathiri na kuharibu imani ya muumini atendaye dhambi hizo. Mijadala hii imezaa misimamo tofauti ya kimadhehebu, huku kila mmoja ukiakisi mtazamo wake kuhusu uhusiano kati ya imani na matendo ya muuni fulani. Khawarij walimchukulia mtenda dhambi kubwa kuwa tayari ameshatoka katika imani ya Kiislamu na kuingia katika ukafiri, na hivyo kustahili adhabu ya milele. Kwa upande wa Muutazila, wao walitoa nadharia ya kati na kati inayojulikana kama Manzila bayna al-Manzilatain (daraja kati ya daraja mbili). Ila kwa mtazamo wa Ahl al-Hadith, humuhisabu mhusika wa matendo ya dhambi kuu kuwa ni miongoni wa watu wenye imani dhaifu. Nadharia za madhehebu ya Kiash’ari na Kimaturidi zinaelekea katika mwelekeo unaokaribiana kwa kiasi fulani. Nadharia za madhehebu haya zikisisitiza kuwa; kiini cha imani ni usadikisho wa moyoni (tasdiq), kwa msingi huo, madhambi makuu hayaibatilishi imani ya kimsingi iliyomo ndani ya moyo wa muumini fulani, hata kama yanaathiri ukamilifu wa hali ya kiimani ya mhusika wake. Kwa mujibu wa fatwa zilizomo ndani ya vyanzo vya fiqhi, utendaji wa madhambi makuu una athari za moja kwa moja katika hadhi ya kisheria inayohusiana na muumini wa imani ya Kiislamu. Miongoni mwa athari hizo ni kupotea kwa sifa ya uadilifu wa kibinafsi. Hii ni kwa kutokana na kwamba, kuepuka madhambi makuu ni sharti la msingi linalomfanya mtu ahesabiwe kuwa ni mwadilifu kisheria. Hivyo basi pale mtu anapotenda dhambi kubwa, hadhi yake ya kisheria hushuka, jambo linayoweza kumwondolea uwezo wa kukubalika kama shahidi katika mahakama au pia kumyima uwezo wa kushika majukumu ya uongozi wa kidini yanayohitaji uadilifu uliothibitishwa kisheria. Aidha, sheria ya Kiislamu inampa mtawala jukumu la kusimamia utekelezaji wa adhabu zinazohusiana na madhambi makuu, ili kudhamini maadili mema ndani ya jamii. Uchambuzi wa Mtenda Dhambi Kubwa na Nafasi Yake Mwanateolojia wa Kishia, Ja'far Subhani, anaeleza kuwa; baada ya suala la imama (uimamu na uongozi wa kidini), mjadala kuhusu mtenda dhambi kubwa ulikuwa ni miongoni mwa masuala ya mwanzo kabisa katika uwanja wa elimu ya kalamu ya Kiislamu. Na kwamba suala hilo ndilo lililochangia kwa kiasi kikubwa kabisa kugawanyika kwa Waislamu katika mikondo tofauti ya kimafundisho (kimadhehebu). [1] Kwa mujibu wa uchambuzi wake, mjadala huo ulijikita katika maswali matatu ya msingi yafuatayo: 1. Je, mtenda dhambi kubwa anabaki muumini au anahesabiwa mshirikina? 2. Je, anahukumiwa kuwa muumini au kafiri? 3. Je, anastahili adhabu ya milele au la? [2] Kiini cha mjadala huu kinarejea kwenye uhusiano kati ya matendo na imani, [3] mjadala unaoonesha kuwa, iwapo matendo yatachukuliwa kuwa ni sehemu ya kiini cha imani, basi mtenda dhambi kuu atahisabiwa kuwa ametoka katika duara la imani. Lakini ikiwa imani itafasiliwa kuwa ni kitu tofauti na matendo ya muumini mwenyewe, basi mwenye mtendaji dhambi kuu bado ataendelea kubaki ndani ya imani huku akihesabiwa kuwa ni muumini mwenye sifa ya ufasiki. [4] Kwa upande mwingine, Sayyid Abdolhossein Dastghaib akiifafanua dhambi kubwa anasema kuwa; dhambu kubwa ni ile iliyotambuliwa na Qur’ani au Riwaya huku ikitajwa wazi kuwa ni kubwa, au ambayo mtenda wake ameahidiwa kupata adhabu ya Moto kutokana na dhambi hiyo. [5] Pia tazama: Maedhambi Makubwa Kauli ya Imamu Jaafar al-Sadiq (A.S) kuhusu Athari za Dhambi Jaafar al-Sadiq (a.s) amenukuliwa akifafanua hali ya kiimani ya mtu anayetenda dhambi kwa kusema kwamba; pale mja anapofanya dhambi iliyokatazwa na Mungu —iwe kubwa au ndogo—hutoka katika hadhi ya imani, hali inayomuondolea sifa ya imani, huku akiendelea kubaki ndani ya Uislamu. Endapo atatubia na kuomba msamaha, basi hurudi tena katika nyumba ya imani. Hata hivyo, ikiwa atafikia hatua ya kukanusha halali au haramu fulani, au kubadilisha halali kuwa haramu na haramu kuwa halali kisha akaamini hivyo, basi si kwamba tu yeye atakuwa ametoka katika imani, bali pia atakuwa ameingia katika upeo wa ukafiri. Imenukuliwa na Kulaini katika kitabu chake cha Al-Kafi, Uk. 27-28, Juz. 2. Toleo la Mwaka 1407 Hijiria. Mtazamo wa Wanazuoni wa Kishia kuhusu Mtenda Dhambi Kubwa Licha ya wanazuoni wa Kishia, kuwa na tofauti katika kufasili dhana ya imani, ila bado wa wanaafikiana kuwa mtenda dhambi kubwa hahesabiwi kuwa ni kafiri wala mshirikina, bali hubaki ndani ya Uislamu na kama walivyo wengine. Aidha, wanashikilia kuwa hatima ya adhabu yake iko chini ya mamlaka ya Mungu mwenyewe, ambaye anaweza kumsamehe kwa rehema na fadhila Zake.
Shaykh al-Saduq, akitegemea baadhi ya Riwaya, anaeleza wake akisema kwamba; imani hujengeka kupitia nguzo tatu, nazo ni: kukiri kwa ulimi, kusadiki kwa moyo, na utekelezaji wa matendo kupitia viungo. [6] Kwa msingi huu yeye hutofautisha kati ya Uislamu na imani, akichukulia matendo kuwa ni sehemu na dalili ya ukamilifu wa imani. [7] Aidha kwa mujibu wa ufafanuzi wake wa Qur’ani wa Aya ya 49 ya Suratu al-Nisaa, Mungu ana hiari katika kumuadhibu au kumsamehe mtenda dhambi fulani; na msamaha wake unatokana na fadhila Zake, si wajibu wa lazima unaomlazimisha kufanya hivyo. [8] Katika kufafanua hadhi ya mtu anayetenda dhambi kubwa, Shaykh al-Mufid anaweka wazi tofauti kati ya dhana ya Uislamu na imani, huku akiona kuwa Uislamu kama Uislamu, ni wigo mpana zaidi kuliko dhana ya imani. [9] Kwa mujibu wa mtazamo wake, mtenda dhambi kubwa hawezi kuingia kikamilifu katika dhana ya muumini kamili, wala haingii katika hukumu ya ukafiri (ufasiki kamili); istilahi sahihi ya kisheria ya kumtambua mtu kama huyu, ni kumtaja tu Mwislamu wa kawaida. [10] Sheikh Mufid pia ananukuu kuwepo kwa mwafaka (ijmai) kamili miongoni mwa wanazuoni wa madhehebu ya Shia Imamiyyah ya kwamba, watenda dhambi kubwa hawakatishwi kabisa matumaini ya kupata rehema za Mwenye Ezi Mungu. Kwa mujibu wa mafundisho hayo, wanaweza kunufaika na uombezi (shufaa) na kuokolewa kutokana na adhabu ya Mungu. [11] Sayyid Murtadha akitoa maoni yake anasema kwamba; imani ni jambo linalostahili thawabu za milele na wali haiyumkiniki kupotea kwa sababu ya mhusika wake kufanya madhambi makuu yenye kustahiki adhabu ya muda mfupi (ilinganayo na uovu wake). [12] Akiendelea na uchambuzi wake anasema kuwa; mtu anayefanya madhambi makuu atahesabiwa kuwa kafiri pale tu atakapokanusha dhambi na uharamu wa tendo hilo; ila kama atatenda dhambi kubwa huku akikubali kwamba tendo hilo ni la haramu, basi atabaki kuwa muumini kama ilivyo hapo awali kabla ya utendaji wa dhambi hizo. [13] Kulingana na mtazamo wa Sheikh Tusi ni kwamba; imani ni usadikisho wa ndani wa moyo (tasdiq), na wala dhana ya imani hailazimiani na kuwepo kwa tamko la ulimi katika ili kuhakikisha uwepo wa uumini juu ya imani fulani. [14] Anapojadili hali ya mtetenda madhambi makuu kupitia lenzi ya madhehebu mbalimbali, Sheikh Tusi ansema kwamba; kukithiri kwa madhambi au uzito wa makosa hakuondoi msingi wa imani ya moyoni, hali inayomfanya mhusika kubaki katika hadhi ya ufasiqi tu bila ya kumtoa katika imani ya dini. [15] Aidha, mtazamo wa Khaje Nasiruddin Tusi ambaye ni mwanatheolojia shupavu wa Kishia, ni wenye kuendana sambamba na mtazamo wa Sheikh Tusi. Yeye anaamini kwamba; Mtenda dhambi kuu si mwenye kustahiki kupata adhabu ya kudumu, bali adhabu hii stahikia kafiri peke yake. Akibainisha mawazo yake anasema kuwa; kwa vile mtenda dhambi ni mwenye imani juu ya Uislamu, basi hatoacha kustahili kupata thawabu, jambo ambalo kiakili linaifanya adhabu yake iwe ya muda mfupi ili kutoa nafasi ya kupata malipo ya imani yake juu Uislamu. [16]
Allamah Hilli naye anaonekana kuafikiana na rai ya Khawaja Nasir al-Din Tusi, kwani naye amesimamia kwenye hoja ile ile isemayo kwamba; maasi na madhambi ya mja fulani, hayawezi kumtoa na kumweka nje ya ngoni ya Imani. [17] Yeye amekuja na hoja mbili za kimantiki ili kuthibitisha kuwa, haiyumkini kwa mtenda dhambi (Fasiki) kupewa adhabu ya milele na isio na kikomo. Hoja mbili hizi zimefafanuliwa kama ifuatavyo: 1. Hoja ya kwanza imesimama juu ya msingi wa istihqaq (ustahiki), nayo inasema kwamba; Bila shaka uumini anastahili thawabu kutokana na imani yake, na pia anasihiki kupata adhabu kutokana na kosa lake. Na kwa kuzingatia kuwa, adhabu hutangulia kabla ya malipo, hivyo basi kama ataingia kwenye adhabu ya milele, adhabu hiyo itambatilishia yeye kupata haki yake ya thawabu juu ya imani yake; jambo ambalo ni batili katika vipimo vya mizani ya sheria. [18] 2. Hoja ya pili iliosimama kwenye msingi wa akili (mantiki) inasema kwamba; Ni jambo lililo Muhali (lisilowezekana kimantiki) kwa mtu aliyedumu katika utii na imani umri wake wote, kuhukumiwa kupitia adhabu ya milele kutokana na dhambi aliyoitenda ukingoni mwa uhai wake. Akili salama inakataa uwezekano wa kufanyika dhulma kama hiyo. [19] Mitazamo ya Makundi Mbalimbali ya Waislamu Wengine Wasio Mashia Khawarij Kuhukumu ukafiri kwa mtu aliyetenda dhambi kubwa kumechukuliwa kuwa ndiyo hoja ya kwanza iliyokubaliwa kwa pamoja na madhehebu ya Makhawarij duniani. [20] Kundi mojawapo miongoni mwao lililojulikana kwa jina la Azaariqa lilionekana kushika msimamo usemao kwamba; mtenda dhambi kubwa ni murtadi na atadumu milele katika moto wa Jahannam, na wala mtu huyo hana uweze wa kurejea tena katika imani, na anapaswa kuchomwa moto yeye pamoja na watoto wake. [21] Muutazila Kwa mujibu wa msimamo wa madhehebu ya Muutazila ni kwamba; mtu anayefanya madhambi makuu hahesabiwi kuwa ni kafiri, ila hutoka na kukaa nje ya duara la imani. [22] Kwa mtazo wao, mtu kama huyo huwa si muumini wala si kafiri; bali huitwa fasiq (mwovu), na hali hiyo ya ufasiqi huchukuliwa kuwa ni hali au sifa ya daraja ya kati na kati iliopo baina ya imani na ukafiri. [23]
Kulingana na hoja ya Qadhi Abd al-Jabbar al-Muutazilī, mtenda dhambi kubwa hawezi kuitwa muumini, hii kutokana na kwamba; muumini hustahili kusifiwa kwa sifa ya imani yake aliyonayo, ilhali fasiqi hustahili kulaumiwa kwa sababu ya dhambi zake. Wakati huohuo, mtu huyo hawezi kuhesabiwa kuwa ni kafiri, hii ni kwa sababu ya kwamba; kafiri hukabiliwa na hukumu mahsusi za kisheria — kama vile kuchukuliwa kuwa najisi — ilhali hukumu hizo hazimhusu mtu aliyevaa sifa ya ufasiki. [25] Murji'ah Msimamo wa Murjiʾa umefafanuliwa kuwa ni mkondo maalumu wa kifikra uliosimama kinyume na dhidi ya nadharia ya Makhawarij inayomhukumu mtenda dhambi kubwa kuwa kafiri. [26] Kwa mujibu wa maelezo ya Jaʿfar Subhani ni kwamba, tofauti kuu ya kundi hili na Waislamu wengine iko katika ufafanuzi wa hakika ya imani na uhusiano wake na matendo ya mja; Murjiʾa hutenganisha kati ya imani na amali, wakiona kuwa matendo si sehemu ya kiini cha imani. [27] Kwa mtazamo wao, imani ni tasdiq ambayo ni usadikisho uliomo moyoni au inayodhihiri kwa njia ya kukiri kwa ulimi, na wala haina uwezekano wa kuongezeka wala kupungua. [28] Hivyo, mtenda dhambi kubwa hubaki na imani hiyo iliyofungamana naye moyoni mwake, na kwa msingi huo huhesabiwa kuwa ni muumini. [29] Kutokana na uwepo wa imani hiyo, Murjiʾa hushikilia kwamba mtenda dhambi kubwa, hata asipotubu, hatadumu milele Motoni, na wala hastahiki kupata adhabu (hii inaonesha kwamba wao wanatosheka na imani tu bila ya matendo). [30] Ahlu Al-Hadith Kinyume na Murjiʾa na Khawarij Ahl al-Hadith wanaitakidi kuwa, imani ni tunu inayokubali mabadiliko kupata mabadiliko ya viwango mbalimbali (intensity and weakness). [31] Wao wanafafanua dhana ya imani kama muundo unaojumuisha tamko (qawl) pamoja na utendaji wa kivitendo (amal). [32] Kwa mtazamo huu, mhusika anayetenda madhambi makuu (Mortakib al Kabair) anatazamwa kama ni muumini aliyedhoofika kifikra na kivitendo, anayejulikana kama "muumini fasiqi". Hoja yao ya msingi juu ya hili ni kwamba, dhambi kuu haimtoi mtu katika dini, bali humvua tu sifa ya ukamilifu wa imani, hali inayomfanya achukuliwe kuwa ni muumini mwenye imani duni au pungufu. [33]
Ashʿariyya na Maturidiyya Kwa mujibu wa mtazamo wa Ashʿariyya, imani ni sifa na hali iliyomo moyoni mwa muumini, ingawa imani imani yake inabaki kuwa ndiyo sharti msingi la kukubalika kwa matendo mema. [34] Kwa msingi huo, wafwasi wa madhehebu haya humhisabu mwenye kutenda dhambi kubwa (kabair) kuwa ni muumini mwenye kustahiki adhabu ya mpito, na namna ya adhabu hiyo imo katika elimu ya Mwenyezi Mungu, wala haijabainishwa kwa wanadamu. [35] Aidha kwa mtazamo wa Maturidiyya, mtenda dhambi kubwa hahukumiwi kuwa ni kafiri na adhabu yake itakuwa ni kwa kadiri ya makosa yake yalivyo. [36] Kwa mujibu wa mtazamo wa Abu Mansur al-Maturidi, imani ni kusadiki kwa moyo, na maana ya ukafiri ni kukanusha. [37] Mtenda Dhambi Kubwa katika Fiqhi ya Shia Kwa mujibu wa fatwa za mafaqihi wa Shia, kuepuka na kuacha madhambi makubwa ndiyo sharti msingi la kuthibiti kwa uadilifu wa mtu fulani. Endapo mtu atatenda dhambi kubwa, sifa ya uadilifu wake hupotea moja kwa moja na kumvika sifa nyengine iitwayo ufasiki. [38] Aidha, imeelezwa kwamba, iwapo dhambi hiyo itakuwa ni miongoni mwa zile ambazo zimewekewa adhabu mahsusi (hadd) katika sheria za dini, basi adhabu hiyo itabidi tekelezwa kwa mujibu wa masharti yake kama ilivyoelezwa katika kifiqhi. Na ikiwa haijawekewa hadd (hukumu) maalumu, basi mtawala wa Kiislamu (hakim al-sharʿi) ndiye atakayekuwa na jukumu la kumwadhibu mhusika kwa adhabu ya kinidhamu (taazir) kwa kuzingatia mizani ya sheria na maslahi ya jamii. [39]