Nenda kwa yaliyomo

Mkopo:Kujiua

Kutoka wikishia

Kujiua (Kiarabu: al-Intihar): ni kitendo cha kuchukua uamuzi wa makusudi wa mhusika fulani kuhitimisha maisha yake mwenyewe. Kitendo hichi ni miongoni mwa vitendo vinapingwa vikali na mafundisho ya kidini pamoja na mirengo mingi ya kimaadili na kisheria duniani. Katika muktadha wa fiqhi ya Kiislamu, kujiua ni moja ya dhambi kuu (kaba'ir) na zinazopigwa vita na Waislamu wote ulimwenguni. Pamoja na hayo, baadhi ya vyanzo vya kifiqhi vinatoa idhini ya kutenda jambo hili, iwapo kutakuwa na dharura inayokubalika kisheria au pale maslahi mapana ya jamii ya Kiislamu yanapohitajia muhanga huo. Kwa mujibu wa baadhi ya fatwa, ni halali kutekeleza operesheni za kishahidi zinazokusudia kudhoofisha maadui wa Kiislamu au zinazotekelezwa kwa ajili ya ulinzi wa jamii za Kiislamu. Hukumu za kisheria katika eneo hili zinajumuisha uwekaji wa penalti kwa wanaoshiriki kitendo hicho, pamoja na ubatilishaji wa wasia uliotolewa na mhusika wa kitendo hicho. Umuhimu wa Kadhia ya Kujiua Tendo la kujiua limetonesha na kuamsha mifumo mbalimbali ya kidini na kisheria duniani, na kufanya isimame imara katika kukabiliana na kitendo hichi. Kwa upande mwingine, baadhi ya wasomi (wananadharia) wanatetea haki ya kujiua wakiegemea misingi ya uhuru na utashi wa binadamu. [1] Hata hivyo, dini nyingi za mbinguni na mirengo ya kimaadili inapingana na kitendo hichi, huku ikiiweka dhambi ya kujiua katika orodha ya makosa jinai. [2] Kujiua ni miongoni mwa matukio mabaya na misiba mikubwa ya kijamii in inayozikumba jamii mbalimbali ulimwenguni. [3] Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani, kujiua ni miongoni mwa sababu kumi kuu za vifo ndani ya nchi mbalimbali duniani, [4] na ni sababu ya tatu ya vifo miongoni mwa vijana balehe. [5] Kukithiri kwa kujiua kunahusishwa na vyanzo mbalimbali, kama vile matatizo ya kiakili na kisaikolojia, [6] shinikizo la kutunza heshima kutokana na miiko ya kijamii na kidini, [7] migogoro ya kifamilia kama talaka, [8] changamoto za kijamii, [9] pamoja na kupungua kwa imani ya kidini na kujitenga na maisha ya kiroho. [10] Uchambuzi wa Dhana Kilugha, kujiua hufafanuliwa kama kitendo cha makusudi kinachofanywa na mtu fulani kwa nia ya kukatisha uhai wake, kitendo kinachofanywa kwa hiari pamoja na utambuzi kamili juu ya matokeo yake. [11] Kulingana na vyanzo vya sheria na fiqhi, kitendo hiki hufasiriwa kwa maana ya uamuzi wa mtu mwenye akili timamu anayejiondolea uhai wake kwa maamuzi yake mwenyewe. Hata hivyo, tofauti ya kimsingi na sifa bainifu inayotenganisha kosa la kujiua na mauaji ya kawaida (kumuua mwengine), ni muunganiko wa mtenda na mtendewa; yaani, 'mhalifu' anayetekeleza tendo la uhalifu huo ndiye yule yule anayeathirika na tendo hilo (mhanga wa tendo hilo). [12] Aina za Kujiua Kujiua kunaweza kujitokeza kwa njia mbili kuu. Njia ya kwanza ni kupitia utekelezaji wa kitendo cha moja kwa moja (mbinu tendaji/ commission), kama vile mtu kujidhuru kwa kutumia silaha kali, silaha ya moto, au kwa kunywa sumu. Njia ya pili ni njia ya kujizuia na kuepuka mahitaji muhimu yanayoendeleza maisha (mbinu zuizi / omission), kama vile kukataa kula na kunywa au kuacha kabisa matibabu fulani ambayo ni muhimu kwa maisha. [13] Vilevile, kwa kuzingatia nia ya mtendaji, kujiua—kama ilivyo kwa mauaji ya kawaida—hugawanywa katika aina mbili: kujiua kwa makusudi, ambapo tendo hilo hufanywa kwa nia na azma kamili; na kujiua kimakosa, ambapo mtu husababisha kifo chake mwenyewe kupitia tendo fulani alilolitenda bila kuwa na lengo la awali la kuhitimisha maisha yake. [14] Uharamu wa Kujiua kwa Mtazamo wa Kiislamu na Dini Nenginezo Kwa mtazamo wa wanazuoni wa Kiislamu, kujiua huorodheshwa katika orodha ya dhambi kuu (kabaira), na mtendaji wake akihisabiwa kuwa ni miongoni mwa mafasiki. [15] Mafakihi wa Kishia wamekubaliana kwa kauli moja (ijma) juu ya uharamu wa kitendo hicho. [16] Vilevile, kwa mujibu wa hukumu ya akili na mwenendo wa wenye busara (Siiratu al-Ukalaa), kujiua ni miongoni mwa matendo yanayokatazwa moja kw moja. [17] Kwa mujibu wa ufahamu wa baadhi ya wafasiri, Qur’ani imekataza kitendo cha kujiua. [18] Miongoni mwa Aya zinazotajwa kama dalili ya katazo hilo ni Aya ya 29 ya Suratu al-Nisaa, inayosema: «وَلَا تَقْتُلُواْ أَنفُسَکمْ؛» “Wala msijiue wenyewe.” Kauli hii imefasiriwa kama katazo linalopigamarufuku kitendo cha kujiua, kama ilivyobainishwa na Muhaqqiq Ardabili [19] na Naser Makarem Shirazi. [20] Aidha, kauli nyengine inayotegemewa kama ni katazo likatazalo aina na nyenendo zote za kupoteza au kuweka hatarini uhai wa binadamu, kile kifungu cha ibara kilichoko katika Aya ya 195 ya Suratu al-Baqara kisemacho: «وَ لَا تُلْقُواْ بِأَيْدِيكُمْ إِلىَ التهَّْلُكَة؛» “Wala msijiingize wenyewe katika maangamizi,”. [21] Aya nyingine zinazotumiwa kama dalili zinazoonyesha uharamu wa kujiua, ni Aya ya 84 ya Suratu al-Baqara iliyochukuwa ahadi kutoka kwa Bani Israil ya kutomwaga damu zao, pamoja na Aya ya 32 ya Suratu al-Maida inayokataza kuua nafsi zenye heshima. [22] Vyanzo vya Kiislamu vinanukuu Hadithi zenye maonyo makali dhidi ya kitendo cha kujiua. Kwa mujibu wa miongozo ya Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w), ifikapo Siku ya Kiyama, mhusika wa tendo hilo atakabiliana na adhabu itumiayo zana ileile aliyoitumia kwa ajili ya kujiua, huku akidumu motoni kwa muda usiojulikana. [23] Aidha, moja ya Hadithi za Imamu Jaʿfar al-Sadiq (a.s) inasema: “Kujiua kwa makusudi ni kushika njia ya Motoni.” [24] Kulingana na ufafanuzi wa Allama Tabatabai katika Tafsiri ya al-Mizan, kujiua ni kitendo kilichopigwa marufuku na sheria za Mwenye Ezi Mungu na kuharamishwa na dini mbalimbali ulimwenguni. [25] Katika imani ya Kiyahudi, kitendo hiki hulaaniwa, na wala wahusika hawapewi heshima ya kuzikwa pamoja na waumini wengine wa dini hiyo. [26] Vivyo hivyo, maandiko ya Kikristo yanakemea vikali kitendo kujiua [27] na kukiweka sambamba na makosa ya mauaji (jinai) ya kuwaua wengine; hivyo basi, hapewi heshima ya kuzikwa kwa taratibu za kidini. [28] Hata katika Ugiriki ya kale, kujiua kulihesabiwa kuwa ni kosa lisilokubalika kijamii. [29] Hukumu za Kifiqhi Zinazohusiana na Kujiua Katika rejea za fiqhi, masuala ya kujiua yamechambuliwa kwa upana zaidi ndani ya mijadala inayotafiti mauaji ya makusudia, sambamba na masuala yanayohusiana na wasia. Hukumu Zinazohusiana na Watoao Msaada wa Kujiua Wanazuoni na wataalamu wa sheria za Kiislamu wamegawika makundi mawili katika uangalizi wa hukumu za mwenye kushiriki na kusadia kitendo cha kujiua kwa makusudi. Kundi la kwanza linamhukumu mshiriki huyo kwa adhabu ya kisasi (qisas), ila sharti la adhabu hii, ni kupatikana malipo ya nusu ya fidia (kama gharama ya kumuua mshiriki huyo), malipo ambayo yanatakiwa kulipwa na warithi wa aliyeuliwa. [30] Kundi la pili linasema kwamba, iwapo marehemu alishiriki kikamilifu katika kusababisha kifo chake mwenyewe, mshiriki huyo hawezi kuhukumiwa kwa adhabu ya kisasi, bali atawajibika kulipa fidia ya muhanga huyo. [31] Kifo cha Kuepuka Maumivu (Euthanasia) Kwa mujibu wa fatwa za wanazuoni wa fiqhi, endapo mgonjwa fulani atatumia dawa kwa nia ya kumaliza uhai wake, tendo hilo hutambuliwa kama ni moja ya hatua na mchakato wa kujiua, tendo ambalo ni haramu kwa mujibu wa sheria za Kiislamu. [32] Miongoni mwa aina za matendo hayo (Euthanasia) ni kuwekwa dawa karibu na mgonjwa au kumkabidhi dawa hizi mikononi mwake ili azitumie kwa ajili ya kujimaliza. [33] Hukumu ya Wasia wa Mwenye Kujiua Kuna hukumu mbili tofauti kuhusiana na utekelezaji wa wasia wa wenye kujiua. Kwa mujibu wa fatwa za wanazuoni wa madhehebu ya Shia, wasia uliotolewa kabla ya maamuzi ya kujiua hutekelezwa bila matatizo, ila ule uliotolewa baada ya kujijeruhi au baada ya kitendo kilichosababisha kifo chake, haupaswi kutekelezwa. [34] Mazingira ya Kuruhusiwa Kujiua Ingawa kujiua ni haramu kisheria, ila katika baadhi ya vyanzo vya kisheria (fiqhi), kuna ibara zinazohalalisha tendo kutokana na dharura au maslahi mapana ya umma, kama vile kulinda usalama wa Waislamu. [35] Kwa mfano, wasomi kama Makarim Shirazi na Muntadhiri wanahalalisha kitendo cha mfungwa fulani cha kuchukua hatua ya kujiua mwenyewe, iwapo mfungwa huyo hataweza kuhimili mateso yanayotolewa dhidi yake. Ruhusa hii imetolewa ili kuzuia kuvuja kwa siri muhimu zitakazoweza kuwadhuru Waislamu. [36] Kadhalika, baadhi ya wanazuoni wamehalalisha mashambulizi ya kujitoa mhanga na kuyajumuisha ndani ya ruhusa hiyo, hata kama hatua hiyo inahisabiwa kuwa ni miongoni mwa hatua za kujiua. Mchakato wa kujitoa muhanga huruhusiwa chini ya dhamira ya jihadi ya kujihami, ilimradi tu lengo lake liwe ni kudhuru mipango ya adui au kutetea Uislamu. [37] Hata hivyo, wanazuoni wa fiqhi wamebainisha wakisema kwamba, mtu hapewi udhuru wa kujiua hata kama akilazimishwa kufanya hivyo, [38] na kwamba kitendo hicho huondoa (hufuta) haki ya kulipwa fidia (diya). [39]