Nenda kwa yaliyomo

Mkopo:Kuhajiriwa (kuhamwa) kwa Qur’ani

Kutoka wikishia

Kuhajiriwa (kuhamwa) kwa Qur’ani: Istilahi ya kuhajiriwa kwa Qur’ani inatokana na mzizi wa neno la Kiarabu linalopatikana katika Aya ya 30 ya Suratu al-Furqan. Kwa mujibu wa Aya hiyo Mtume Muhammad (s.a.w.w) anawasilisha mashtaka kwa Mola wake kuhusu umma wake kuitenga Qur'ani na kuigeuza kuwa ni kihame. Katika riwaya na tafsiri, hasa ndani ya madhehebu ya Shia, dhana hii imepewa uzito mkubwa. Haimaanishi tu kuacha kuisoma Qur'ani (tilawa), bali inajumuisha wigo mpana wa kuipuuza katika vipengele mbalimbali vya maisha ya mtu binafsi na jamii.

Wanazuoni wa tafsiri wametoa mitazamo mbalimbali kuhusu maana ya kuhajiriwa kulikotajwa katika Aya hiyo ya Suratu al-Furqan. Baadhi wameieleza kuwa maelezo ya Aya hiyo yanamaanisha kuiacha Qur’ani kabisa kabisa, kutoisikiliza, kuipa mgongo au kutoiamini. Wengine wamefafanua kwamba hata kusoma Qur’ani bila kuielewa na bila kutenda kwa mujibu wa mafundisho yake, pia ni aina ya kuihujuru (kuihama). Kwa kuzingatia Hadithi ya Thaqalain, baadhi ya wanazuoni wameona kwamba kuitenganisha Qur’ani na Ahlul-Bait — wanaotambuliwa kama wafasiri wake wakuu — ni mojawapo ya sura za kuhajiriwa na kuipa kisogo Qur’ani tukufu.

Katika miongoni mwa tafsiri za kisasa za dhana ya kuhajiriwa kwa Qur’ani, mtazamo wa Imamu Khomeini unachukua nafasi ya kipekee kwa kuunganisha uchambuzi wa kidhana na hali halisi ya kijamii. Kwa mujibu wake, Qur’ani si maandiko ya ibada binafsi pekee, bali ni mwongozo wa ujenzi wa jamii. Kwa sababu hiyo, yeye anaitafsiri dhana ya mahjuriyya (kuhajiriwa kwa Kitabu) kuwa ni kupuuzwa kwa mafundisho hayo katika nyanja mbalimbali. Kwa mtazamo wake, hali hii si tatizo la kimaadili pekee linalohusiana na mtu binafsi, bali ndiyo kiini cha changamoto zinazoikabili dunia ya Kiislamu katika nyanja za kisiasa, kijamii na kifikra.

Kutelekezwa kwa Qur'ani kunajidhihirisha katika nyanja mbalimbali kama vile usomaji, usikilizaji, uhifadhi, mazingatio, tafsiri, na utendaji. Aidha, matumizi ya Qur'ani kwa ajili ya matokeo maalumu tu kama vile khitma, au kuitafsiri kulingana na maoni binafsi ni miongoni mwa mifano ya kutengwa huku. Sababu kuu za hali hii ni pamoja na kuitenganisha Qur'ani na Ahl al-Bait (a.s), kutawala kwa mitazamo ya kijuujuu (isiyo na kina cha tafakuri), kusimama kwa ijtihad, pamoja na kuhamasisha utengano wa dini na siasa. Athari za mambo hayo ni pamoja na; kuibuka kwa makundi (umadhehebu), kurudi nyuma kimaendeleo, kuenea kwa ushirikina, umaskini, udikteta, na kupotea kwa hali ya kiroho. Wanazuoni kama Allamah Tabatabai, Imam Khomeini, na Sayyid Jamal al-Din Asadabadi walifanya jitihada kubwa kuondoa hali ya utelekezwaji wa Qur'ani.


Maana na Nafasi ya Dhana

Dhana ya kutelekezwa (kuhajiriwa) kwa Qur’ani imechimbuka kutoka katika Aya ya 30 ya Suratu al-Furqan, ambapo Mtume Muhammad (s.a.w.w) anawasilisha mashtaka yake kwa Mwenyezi Mungu akieleza jinsi watu wake walivyoipuuza Qur’ani. [1] Tahadhari dhidi ya hali hii zimejitokeza pia katika Riwaya kadhaa zilizomo katika vyanzo madhehebu ya Shia. Miongoni mwa walionukuu maonyo hayo ni Sharif Radhiy katika Nahjul Balagha [2] na Kulani katika Al-Kafi. [3]

Kwa ujumla, kutelekezwa huku hufahamika kama kushindwa kuitambua nafasi na uzito wa Qur’ani, kuacha kufuata mafundisho yake, kuipuuza kwa uzembe, na kuridhika na matumizi ya kiminasaba tu (kama vile khitmani na maharusini). [4] Kwa mujibu wa maelezo ya Sayyid Muhammad Ali Ayadhi (mtafiti wa Kishia), hali hii inabeba maana ya kuiondoa Qur’ani katika uhalisia wa maisha ya jamii ya Kiislamu. [5]

Watafiti na wanazuoni wa fani za Qur’ani wameainisha tafsiri mbalimbali kuhusu istilahi ya Mahjuriyat (Kuhujuriwa) kwa Qur’ani iliyorejelewa katika Aya ya 30 ya Surah al-Furqan:

·        Kuhajiri (Kuihama): Hii inarejelea matokeo ya kutosikiliza, kuipa kisogo, na kuachana na Qur’ani kwa namna ya dhahiri ya kutoijali [6] au kutokuwa na imani nayo. [7]

·        Dhana ya Kutengana na Qur’ani na Kuifanya Kihame: Kwa kuegemea mzizi wa neno 'Ittakhadhu' (kuchukulia/kufanya), madhumuni ya Aya iliyotangulia yatakuwa na maana ya kwamb: Licha ya Waislamu kuisoma Qur’ani, wametengana nayo na kubaki wageni kwayo kutokana na ukosefu wa ufahamu sahihi, upuuzaji wa maudhui yake makuu, na utendaji unaokinzana na mafundisho yake. [8] Katika muktadha huu, Hassan Mustafawi, ndani ya Al-Tahqiq fi Kalimat al-Qurani, anafafanua Mahjuriyat kama hali ya kuiacha Qur’ani kunakoambatana na mahusiana ya kidhahiri kati ya Waislamu na Qur’ani kama kitabu cha Mungu. [9]

·        Utenganishaji kati ya Qur’ani na Ahlul-Bait: Mtazamo huu unazingatia baadhi ya Riwaya kama vile Hadithi ya Thaqalain na kuenea kwa kauli mbiu ya 'Hasbuna Kitab Allah' (Kitabu cha Mungu kinatutosheleza) iliyoasisiwa na Khalifa wa Pili; hali iliyopelekea kuibuka kwa upotoshaji katika uelewa wa Qur’ani. [10]

Imam Khomeini, ambaye ni miongoni mwa Maraji' al-Taqlid (mafaqihi) wa Shia, ana mtazamo wa kisiasa na kijamii ulio tofauti na wengine. Yeye anaamini kuwa mafundisho ya kisiasa na kijamii yaliyomo katika Qur’ani ni mengi zaidi kuliko yale ya kiibada. [11] Kwa hiyo, kutelekezwa (kuhajiriwa) kulikotajwa ndani ya Qur’ani ni kupuuza hukumu za kisiasa na kijamii na kutosheka tu na mambo ya ibada. Akichambua tatizo hili anasema kuwa, chanzo cha matatizo ya jamii ya Kiislamu ni kutofuata hukumu hizo zilizotjwa na kusisitizwa mara kupitia Aya mbalimbali. [12]

Nyanja za Uhajiri na Utelekezaji wa Qur’ani

Watafiti wa Qur’ani wamechunguza kutelekezwa kwa Qur’ani katika vipimo na mikabala mbalimbali na wakataja nyanja kadhaa kuhusiana na suala hili. Miongoni mwa nnynja hizo ni pamoja na nynja ya tilawa, nyanja ya kusikiliza, kuhifadhi, tadaburi, fasiri, na kuitelekeza katika nyanja ya matendo. [13] Kwa mtazamo wa Makarimu Shirazi, mmoja wa wafasiri wa Qur’ani wa upande wa madhehebu ya Kishia, ni kwamba; kutelekezwa kwa Qur’ani kunajumuisha suala la kutoshka na matumizi ya Qur’ani katika harakati za kitamaduni peke yake (kama vile kutumia Aya katika mapambo ya maeneo ya kidini au matumizi ya tiba katika kuponya wagonjwa), kutanguliza mawazo ya Kimagharibi na kutojali au kuiweka nyuma misingi ya Qur’ani, na kuhukumu kupitia Qur’ani kwa kutegemea tafsiri ya rai binafsi. [14]

Wafasiri wengine pia wanataja suala la kutozingatia usomaji, kutokuwa na usikilizaji, uhifadhi, utafakari, na kutotekeleza maagizo ya Qur’ani kuwa ni dalili za kuitelekeza na kuipa kisogo Qur’ani. [15] Imam Khomeini anafasiri kutelekezwa kwa Qur’ani kama hali ya kughafilika na mafundisho yake ya msingi na kutoyafanyia kazi.[16] Kwa mtazamo wake, kujikita katika vipengele vya nje pekee kama vile Tajuidi, mijadala ya kilugha na kifasihi, au miujiza ya Qur’ani, hakutoshi kuondoa hali hiyo ya kutelekezwa. [17]

Sababu na Vyanzo Vilivyosababisha Kuihama Qur’ani

Kuna mambo kadhaa yaliyoainishwa katika kuchunguza sababu za dhana ya Mahjuriyat al-Qur’ani (Kuhajiriwa kwa Qur’ani). Miongoni mwayo ni pamoja na juhudi za kuitenganisha Qur’ani na viongozi wa upande wa Ahlul-Bait (a.s), ambao ni washereheshaji wake asili, [18] ukomo wa wafasiri katika tafsiri ya kidhahiri, kuenea kwa tafsiri za kibinafsi, ufuasi wa kichwamchungwa (mgando wa fikra) na kujitenga na mantiki za kiakili, kufungwa kwa mlango wa Ijtihadi, kushamiri kwa itikadi ya Kiikhbariyya (kushikamana na Hadithi bila ya kuzitafakari), pamoja na ulemavu wa kutafuta anasa za kidunia. Kadhalika, mambo mengine yaliyozadhaa hali ya upuuzaji wa Qur’ani ni kupatikana kwa Waislamu waliodhani kuwa Qur’ani si kitabu tosha kinachoweza kutatua matatizo mamboleo, pamoja na kupuuza mafundisho yake ya kisiasa na kijamii. [19]

Imam Khomeini anabainisha kwa kusema; ukiritimba wa kujenga ya kwamba uelewa wa Qur’ani upo mikononi mwa tabaka la wafasiri fulani tu pamoja na uharamishaji wa Tadabbur (tafakuri) kwa umma katika kuifahamu Qur’ani, jambo lililodaiwa kwa kisingizio cha kukhofia kupatikana kwa 'Tafsiri ya Rai binafsi' kumechangia kutelekezwa huku. [20] Yeye anaongeza kuwa; propaganda za kutenganisha dini na siasa (sekula) zimelenga kuifanya Qur’an ionekane haina mamlaka ya kisiasa na kijamii, ili kuhalalisha himaya ya madola makubwa katika kuutawala ulimwengu wa Kiislamu. [21]

Mwanahistoria ajulikanaye kwa jina la Rasul Jafarian anasisitiza akisema kuwa, kuanzia kipindi cha uongozi wa Safawiyya, katika masula ya maarifa ya kielemi, mrengo wa Kishia umeonekana kushikamana na kutegemea mno kwenye Hadithi na tafsiri za kiriwaya, hali iliyopelekea mpasuko mkubwa baina ya jamii na Qur’ani. [22]

Vilevile, utatu wa kiitikadi unaojumuisha Akhbariyya, Tasawwuf (Usufi), na sera za dola unatajwa kuwa ni miongoni mwa mambo yaliyochangia hali hii. Tafiti zaonesha kuwa tawala zilizoathiriwa na mikondo hii ya kiitikadi hazikuridhia, bali hata zilihisi tishio, dhidi ya kuwepo uthabiti wa Qur’ani katika nyanja za kijamii, na hivyo zikafanya jitihada mbalimbali ili kuibana Qur’ani na kuiweka mbali na jamii. [23]

Athari na Matokeo ya Kuihajiri Qur’ani

"Athari mbalimbali zitokanazo na dhana ya Mahjuriyat (Kuhujuriwa kwa Qur’an) katika jamii ya Kiislamu zimeorodheshwa, zikijumuisha:

·        Kuibuka kwa Mgawanyiko na Mparaganyiko: Kushamiri kwa mgawanyiko wa kimadhehebu na utengano wa kijamii. [24]

·        Upotoshaji wa Imani: Kuenea kwa Uislamu wa kikhurafa na Hadithi maudhui (bandia na za kupachikwa). [25]

·        Mmomonyoko na Kuporomoka kwa Hadhi: Kutoweka kwa mamlaka, hadhi, na Izza (utukufu) ya Waislamu, [26] pamoja na udumavu wa kimaendeleo;

·        Mporomoko wa Maadili: Hali ya Jamii kutengana na maisha ya kiroho na kuenea kwa mambo yaliyo kinyume na maadili na tunu za kiutu. [27]

·        Utawala Mbovu: Kupata madaraka kwa watu wasiostahiki (incompetent) na wasio na ufanisi, sambamba na kukithiri kwa ufukara. [28]

·        Ukandamizaji: Kuzaliwa kwa utawala wa kimabavu huku raia wakijitenga na nyanja za kisiasa na kijamii. [29]

·        Kuelemewa na Ghadhabu za Mungu: Kukasirikiwa na Mungu na hatari ya kupata adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. [30]

Waasisi wa Kampeni ya Kuinusuru Qur’ani

Seyyed Mohammad Ali Ayazi, mtafiti wa Qur’ani, anaeleza kuwa Allamah Tabatabai na Imamu Khomeini walikuwa na mchango mkubwa katika kuondoa hali ya utelekezwaji wa Qur’an, na walijitahidi vya kutosha ili kuhuisha mafundisho yake. Tabatabai alipambana na hali hiyo kwa kuandika Tafsir al-Mizan, na Imamu Khomeini naye kwa kuwasilisha hoja zake za kiutawala katika kulingana na mfumo wa kisiasa uendao sambamba na Uislamu. [31]

Hali kadhalika, Seyyed Jamal al-Din Asadabadi (1314 H) alikuwa mstari wa mbele katika harakati ya kuirejesha jamii katika Qur’ani. Yeye ndiye aliyehamasisha harakati za mageuzi zilizotumia mwito maalumu uliowata wanajamii kushikamana tena na Qur’ani, ambao ulizinduliwa na mwanazuoni huyo katika karne ya kumi na tano ya Hijria. [32]