Nenda kwa yaliyomo

Mkopo:Hukumu ya Ndoa kati ya Mwislamu na Asiye Mwislamu

Kutoka wikishia

Hukumu ya Ndoa kati ya Mwislamu na Asiye Mwislamu: Ndoa kati ya Mwislamu na asiye Mwislamu ni suala linalohusiana na kisheria (kifiqhi) ambalo limeonekana kujajadiliwa kwa muda mrefu katika ndani ya vyanzo vya fiqhi vya pande zote mbili za Kishia pamoja na Kisunni. Suala limegawanyika katika masuala mengi madogo madogo. Kulingana na fatwa (uamuzi wa kisheria za fiqhi) za wanazuoni wote wa Kishia na wa Kisunni nikwamba; hairuhusiwi na haramu kwa mwanamke wa Kiislamu kuolewa na mwanamume asiye Mwislamu. Uamuzi huu unajumuisha hata kama mwanamume huyo ni Ahlu al-Kitab (mtu mwenye imani ianyofuata Kitabu cha mbinguni) au Kafiri Dhimmi (kafiri anayeishi chini ya dhamana ya dola ya Kiismau ambaye si audi wa Uislamu), na bila kujali kama ndoa hiyo ni ya kudumu au ya muda mfupi. Aidha, ni haramu kwa mwanamme wa Kiislamu kuoana na mwanamke kafiri asiyeamini kuwepo kwa Mungu.


kuna tofauti za kifiqhi (ikhtilaf) za maoni katika uwanja wa shiria za fiqhi miongoni mwa wanazuoni wa kishia, kuhusiana na uhalali wa ndoa ya mwanamme wa Kiislamu na ahlu al-kitab. Mtazamo wenye nguvu zaidi kati yao ni ule unaosisitiza kwamba uharamu wa ndoa ya kudumu (ziwaju al-dā'im) kati ya wawili hao, kinyume na ndoa ya muda (ziwaju al-muwaqqat) ambayo inaruhusiwa bila ya kupewa vikwazo maalumu ndani yake. Kwa upande wa wanazuoni wa Kisunni, wao wanatoa idhini ya kisheria kwa ndoa ya kudumu baina ya mwanamme Kiislamu na mwanamke wa upande wa Ahlu al-Kitabu.

Umuhimu

Suala la ndoa baina ya Mwislamu na asiye Mwislamu ni mada ya kifiqhi iliyojadiliwa kwa mapana kabisa ndani ya jamvi la sheria ya Kiislamu. Mada hii hakuwa ni kitendawili cha kifiqhi upande wa wnazuoni wa Kishia peke yao, bali pia hata ndani ya Fiqhi ya madhehebu ya Kisunni. [1] Mada hii hugawanyika katika matawi makuu kadhaa, kama vile:

·           Ndoa ya mwanamke Mwislamu na mwanamume asiye Mwislamu.

·           Ndoa ya kudumu ya mwanamume Mwislamu na mwanamke asiye Mwislamu.

·           Ndoa ya muda (au ndoa ya Mut’ah) ya mwanamume Mwislamu na mwanamke asiye Mwislamu.

Zaidi ya hayo, utata wa suala hili pia umezingatiwa na kutengewa vipengele maalumu vya kanuni ndani ya Sheria za Kiraia za Iran. [2]


Ndoa ya Mwanamke Mwislamu na Mwanamme Asiye Mwislamu

Kuna makubaliano na ijma kamili (utangamano wa maoni) Katika Fiqhi ya Kishia na Kisunni, kwamba; hairuhusiwi (si halali) kwa mwanamke wa kiislamu kuolewa na mwanamme asiye Mwislamu, na wala hakujawahi kutokea ndoa ya aina kama hiyo iliyotambuliwa kisheria katika historia ya Uislamu, hii inajumuisha hata kama mwanamme huyo ni muumini wa moja ya vitabu vya mbinguni (Ahl al-Kitab). [3]

Hukumu hii haitofautishwi kati ya yule anayehesabiwa kuwa ni kafiri dhimmi (anayeishi chini ya mkataba wa kupewa himaya na dola ya Kiisalmu), kafiri harbi (mwenye uadui dhidi ya Uislamu ambaye yupo nje ya mkataba wa kupewa himaya), au muasi (Muislamu aliyeritadi). Vilevile, hukumu hii inasimama bila kujali kama ndoa hiyo ni ya muda (mut’a) au ni ya kudumu. [4] Hukumu hii pia imefafanuliwa kwenye kifungu cha sheria nambari 1059 cha Sheria za Kiraia za Iran. [5]


Mwanamume Mwislamu Kuwaoa Wanawake wa Kitabu (Ahl al-Kitab)

Madhehebu yote ya Kisunni yanaafiki (yanahalalisha) mwanamme wa Kiislamu kumuoa mwanamke anayetokea moja ya upande wa waumini wa kitabu cha mbinguni (Ahlu al-Kitab), ambao ni Mayahudi na Wakristo. [6] Hata hivyo, mafaqihi (wanazuoni wa sheria) wa Kishia wanatofautisha kati ya ndoa ya muda (Mut’ah) na ndoa ya kudumu, hii ni kwa mwanamme Mwislamu anayeoana na mwanamke wa upande wa waumini wa Kitabu (Ahlu al-Kitab). Ila ruhusa hiyo imetolewa kwa ajili wale wanaooana kwa mkataba wa ndoa ya muda peke yake, na si halali (ni haramu) kwa mwanamme wa Kiislamu kuoana na mwanamke wa upande wa “Ahl al-Kitab” kupitia mkataba wa ndoa ya kudumu. [7]

Muhaqqiq Hilli na Faidhu Kashani walibainisha wakisema kwamba; hii ndiyo ilikuwa hukumu yenye umashuhuri zaidi miongoni mwa wanazuoni wa Kishia. [8] Kwa kuongezea, pia Ibn Said Hilli alisisitiza kuwa, maoni haya ni miongoni mwa nadharia zenye ijma (utangamano wa maoni) miongoni mwa wanazuoni wote wa Kishia. [9]

Mitazamo Tofauti Katika Fiqhi ya Kishia

Licha ya hayo, kuna ripoti isemayo kwamba; mtazamo ulioshikiliwa na wanazuoni wa zamani (kabla ya zama za Muhaqqiq Hilli), ni msimamo wa kukataza na kuharamisha moja kwa moja suala Muilamu wa kiume kufunga ndoa na watu wa kitabu (Ahlu al-Kitab). [10] Wale walioshikilia mtazamo huu ni pamoja na Sheikh Mufid, [11] Sheikh Tusi, [12] Sayyid Murtadha, [13] na Tabarsi. [14] Hawa ndio wale wanazuoni walioshikilia nadharia ya uharamu wa mwanmme wa Kiislamu kuoana na mwanamke wa upande wa (Ahlu al-Kitab), bila ya kutofautisha baina ya ndoa ya mut’a (ya mpitia au ya muda mfupi) na ndoa ya kudumu. [15]

Kinyume na mtazamo wa wanazuoni hao, pia kuna mafaqihi wengine waliokwenda kinyuma na nadharia hiyo. Miongoni mwa wanazuoni hao ni kama vile Sheikh Sadduq, [15] Shahid Thani, [17] Faidhu Kashani, [18] na Sahib Jawahir. [19] Hawa ni miongoni mwa wale walioruhusu na kuhalalisha hata ndoa ya kudumu na mwanamke wa upande wa (Ahlu al-Kitab). [20] Aidha, Sahib Jawahir alimnukuu Sheikh Tusi akieleza kwamba; kulikuwa na ijma kamili (utangamano wa maoni) miongoni mwa mafaqihi wa Shia Imamiyya (Ithna-ashariyya), juu ya uhalali wa mwanamme wa Kiislamu kufunga ndoa ya muda (Mut’a) na mwanamke wa upande wa (Ahlu al-Kitab). [21]

Mtazamo wa Zama za Kisasa

Kama ishara ya mabadiliko ya kihistoria na maendeleo ya kifiqhi, Mohammad Jawad Mughniyya, mwanazuoni mashuhuri wa Kishia kutoka Lebanoni, aliandika akisema kwamba; mafaqihi wengi wa Kishia wa zama za hizi sasa (Karne ya 14 Hijiria), wameonekana kuruhusu ndoa ya kudumu na wanawake atokeaye upande wa waumini kitabu cha mbinguni (Ahlu al-Kitab). Pia, Mahakama za Kija’afari (Shia Ithna-asharia) nchini Lebanoni zinaidhinisha (zinahalalisha) mikataba ya ndoa ya aina kama hiyo. [22]


Ndoa ya Mwanamme wa Kiislamu na Mwanamke wa Kizoroastria (Mmajusi)

Miongoni mwa mada tatanishi zenye khitilafu miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu, ni ile ndoa kati ya mwanmme wa Kiislamu na mwanamke wa Kizoroastria (Kimajusi). [23] Kuna mitazamo tofauti miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu juu ya hukumu ya ndoa hii. Yasemekana kwamba; kuna baadhi ya mafaqihi wa Kishia walioruhusu ndoa ya muda (Mut’ah) ya kuoana na wanawake wa Kizoroastria, [24] ilhali, Sheikh al-Saduq ni miongoni mwa wanazuoni wa Kishia walioharamisha ndoa hii. [25] Kwa upande mwingine, Muhaqqiq al-Hilli anawahisabu Wazoroastria sawa na Watu wa Kitabu (Ahl al-Kitab), na hivyo anaruhusu wanaume wa Kiislamu kuoana nao kwa mkataba wa ndoa ya muda (Mut’ah). [26]


Hukumu ya Ndoa kati ya Mwanamme wa Kiislamu na Mwanamke Asiye Mwislamu

Katika misingi ya fiqhi ya Kishia, mwanaume wa Kiislamu hapaswi wala haruhusiwi kufunga ndoa na mwanamke asiyeamini uwepo wa Mungu wala Siku ya Marejeo (Kiama). [27] Hukumu hii ni thabiti katika hali zote mbili, iwe ni ndoa ya kudumu au ya muda mfupi. [28] Wanazuoni wote wa fiqhi, kwa sauti moja, wameafikiana juu ya msimamo huo, yaani kuna ijma kamili (utangamano wa maoni) ya wanazuoni wa Kiislamu juu ya hukumu hiyo. [29] Aidha, imekatazwa na kuharamishwa moja kwa moja Mwislamu wa kiume kuoana na mwanamke wa madhehebu ya Baha’i (Bahaa’iyya). [30]